|
Na. 049 Jumatano Mei 24 - 30, 2000 |
|
|
|
|
|
Afande Mahita, wananchi hatutaki Dola ya kipolisi Na Mwinjilisti Kamara Kusupa Kazi kuu ya Polisi ni kulinda usalama wa raia. Hii ni kazi njema maana hakuna raia asiyetaka usalama wa nafsi yake na mali zake. Lakini polisi wa Tanzania chini ya Inspekta wao Mkuu Omari Mahita sasa wamechukua mwelekeo mwingine kiasi kwamba kwa mwelekeo huu potofu, wananchi watafikia hatua ya kuhoji jeshi la aina hii lina faida gani kwao? Kazi nyingine ya Polisi, ni kuhakikisha siasa ya nchi haikorofishwi. Si jukumu la Polisi kuhakikisha kwamba siasa ya nchi haipingwi, maana kuna tofauti kubwa kati ya kuipinga siasa ya nchi na kuikorofisha. Mpinzani na mkorofi ni watu wawili tofauti. "Upinzani" na "ukorofi" ni vitu viwili tofauti. Tatizo kuu la Polisi wetu hawatofautishi kati ya mambo hayo mawili, kwao upinzani ni sawa na ukorofi, ndiyo maana wako tayari kupambana na upinzani kwa gharama zozote zile hata ikibidi kutumia risasi za moto dhidi ya raia wema, huku wakiwaachia wevi wa mali ya umma kufanya vitu vyao. Wala si jukumu la Polisi kuhakikisha wale walioko madarakani hawaondoshwi bali jukumu lao ni kuitii Serikali iliyoko madarakani katika misingi ya kikatiba na kisheria. Kutii serikali na kuhami wale walioko madarakani ili wasiondoshwe pia ni na mambo mawili tofuati. Mfumo wa Polisi katika nchi hii tumeurithi kwa Waingereza na kwahiyo Polisi wetu kwa vyovyote vile walistahili kufanana na Polisi wa Malkia. Polisi wa Malkia ni mwiko kumpiga mtu. Pia Polisi wa Malkia hawako kwa ajili ya chama chochote bali wako kama walivyo wanataaluma wengine, yaani wako kwa ajili ya taaluma yao tu. Hapa kwetu Tanzania "Upolisi" siyo taaluma tena bali ni "ukada" nambari wani wa chama tawala. Kisa cha mapolisi kugeuka kuwa makada wa CCM ndiyo kiini cha mada hii. Enzi za mfumo wa chama kimoja ilikuwa halali kwa polisi kuwa mtetezi mkubwa wa siasa ya nchi kwani huo ulikuwa ni sehemu ya uzalendo lakini enzi hizi za mfumo wa vyama vingi Polisi kuwa mtetezi wa siasa ya chama ni kosa la jinai kwani atatetea siasa ya chama kipi? Kwa jinsi mambo yanayokwenda kinyume Polisi wa Tanzania ni makada wa CCM. Wako ili kuhakikisha CCM HAIKOROFISHWI. Makada halisi wa CCM hawana kazi kwani hawana hoja yoyote yenye nguvu ya kuwafanya kusimama nayo aidha kunena hadharani na wananchi ama kuitetea dhidi ya mashambulizi ya kihoja kutoka upande wa upinzani. Tangu walipoiua itikadi ya ujamaa na kujitegemea sasa CCM hawana chochote kilicho "mbadala" na kuwa hiyo hawana lolote la maana la kusema, kunadi au kulitetea hadharani. Hawana sera, hawana lengo, wala mwelekeo, walicho nacho wao mikoni mwao ni madaraka tu. Kushika madaraka bila ya lengo ni tatizo. Nadhani CCM hawatalitambua tatizo lao la awali kwamba ni kule kukusa lengo. Kutokana na hali yao ya kukosa lengo mara wanapokutana na wananchi wenye lengo basi moja kwa moja wanajikuta katika mgongano wa kimaslahi, dhidi ya wananchi. Wakitokea watu wenye lengo na chochote kilicho katika nchi hii ni lazima watagongana tu na CCM, kwa kuwa CCM iko madarakani kwa ajili ya maslahi binafsi na kwa kuwa ndiyo inayotawala nchi na vyote viko chini yake. Wakitokea wenye lengo kuhusiana na rasilimali za nchi, au wenye lengo na vijana, au wenye lengo na wasomi au wafanyibiashara, au wastaafu n.k. lazima watagongana na CCM. Mfano hai ni mgongano kati ya utawala wa CCM na BAWATA, hii Bawata ama kwa kirefu Baraza la Wanawake Tanzania, ilikuwa na lengo lililo kamilika kuhusiana na wanawake wa nchi hii. Sasa kwakuwa CCM haina lengo ikahesabu kwamba BAWATA ni chombo cha kuipiku UWT, na kwahiyo wakaamua kuifuta kwa kisingizio kwamba mtandao wake wa kuwa na matawi hata vijijini unafanana na chama cha siasa. Hizi ndizo gharama za KUWA NA WATU WASIO NA LENGO MADARAKANI. Watu ambao kwa hakika wamekuwa mzigo. Kukaa madarakani bila lengo ni dhambi, na dhambi ya CCM itaendelea kutesa wananchi kutokana na ukweli huu. Kwa chama cha siasa ambacho kiko makini ni lazima kiwe na lengo lililo kamilika kuelekea nchi na watu wake, na kwa mantiki hiyo ni lazima chama hicho kijikute kwenye migongano na CCM, ndiyo maana CCM wakaweka sheria mbovu kwamba chama cha sisasa kikitaka kufanya mkutano wa hadhara wa kujinadi au kutangaza sera zake basi ni lazima kipate kibali cha Polisi. Katiba haisemi hivyo lakini kaida ni kama sheria. Nia ya kuweka mizengwe ya aina hii ni kuzuia watu wasishirikishwe katika lengo lolote maana wasije wakafikia uamuzi wa kuwaondoa wao madarakani. Watawala wana hofu inayotokana na wao wenyewe kutojiamini, wanashikilia madaraka sawa na mtu anavyoshikilia mali ya wizi ambaye anaogopa kukamatwa wakati wowote. Hapa ndipo Polisi wa Tanzania wanapoingia kufanya kazi mbovu, kwanza wanashirikishwa kwenye hofu ya CCM pasipo wao wenyewe kutambua, na baadaye wanabebeshwa hofu ambayo si yao, na mwisho wanatwishwa mzigo ambao si wao. Baya kuliko yote ni kwamba hawapati faida yoyote kutokana na kuubeba mzigo huo wa CCM. Labda kama iko faidi yoyote ni kwa Mahita binafsi na Makamanda wa Mikoa na Wilaya. Tuchukulie kwa mfano BAWATA wangefanya ukaidi wa kusema sisi tutaendelea kuhamasisha wanawake kwa ajili ya maendeleo yao kwa sababu hatuoni uhalali wowote wa kusikiliza onyo la CCM la kuikataa BAWATA hadi kuifuta, ni wazi kwamba wangeitiwa polisi kuja kuwapiga BAWATA na wakaamua kuchukua njia ya ustaarabu wakashitaki mahakamani. Sasa kwa bahati mbaya si taasisi zote za nchi hii ambazo ziko tayari kufuata njia kama ya BAWATA, badala yake wengi wanaona ni heri wakaidi mambo yasiyofaa ya CCM kuliko kuyatii kwani hata ukiyatii bado utapata hasara ile ile sawa na yule aliye asi. Kwa nini Polisi wako upande wa CCM Suala la mapolisi kugeuzwa makada wa kuipigania CCM chimbuko lake ni katiba ya nchi. Kulingana na Katiba bomu iliyopo, Rais ndiye anayemteua IGP (Mkuu wa Polisi) na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na kwa hiyo anaweza kutengua uteuzi wao wakati wowote anaotaka yeye, na kwa ajili hiyo ili Polisi walinde ajira zao inabidi wajisalimishe kwa Rais kama mateka. Hali hiyo inawafanya Mapolisi badala ya kuwa na "obedience" wawe na "Loyality". Mtu anapogeuka kuwa Loyalist kwa mtu fulani inabidi asitazame sheria, kanuni, wala fahamu za kawaida badala yake hata akitumwa kufanya kosa la wazi wazi basi atafanya kwa sababu huyu hana nidhamu ya kazi bali ana nidhamu ya "kitumwa". Badala ya nidhamu ya "utumishi", au Service ana kile tuwezacho kuita "slavish altitude". Mtu aliyefikia kiwango hichi ni sawa na "robbot". Nawashangaa CCM wanapomlaani Kibwetere wakati wao ndio "Kibwetere" nambari wani wa Tanzania ambao wamewafanya Mapolisi na Watumishi wengine wa vyombo vya dola wawe sawa na "ndondocha". Polisi wa Tanzania hata akiambiwa aue hawezi kuuliza ni kwanini niue? Badala yake atammiminia huyo aliyekusudiwa hata risasi sita kifuani na baadaye akifikishwa mahakamani ndipo atawauliza waliomtuma "niende kusema nini huko mahakamani". Utumwa wa Mapolisi kwa chama tawala umeua na kuharibu kabisa taaluma yao. Hivi sasa mwanchi amefikia hatua ya kusema ni heri akutane na jambazi kuliko akutane na Polisi kwa sabbu jambazi akisha kukupora, au kunyang’anya mambo yanaisha, kinyume na Polisi ambao raia akikutana nao ni lazima wampige, wadai rushwa na mwisho wamweke mwananchi huyo rumande na baadaye abambikiziwe kesi ambayo hakuwahi kukosa maishani mwake na hatimaye anyimwe dhamana mahakamani. Kuishi kama mahabusu kwa muda mrefu ni heri yule anayeuawa na majambazi maana hapati mateso ya muda mrefu kuliko hayo anayeishi miaka 10 hadi 20 kama mahabusu, wala kesi yake haina hata tumaini la kusikilizwa. Polisi wa Tanzania na Rushwa Mapolisi wa Tanzania ni walaji rushwa mahili, hili halinakificho, kwani ulaji rushwa wa mapolisi ni wa kulazimishwa. Hata angechukuliwa malaika toka mbinguni kisha akapewa kazi ya upolisi ni lazima ghafla angegeuka kuwa "Pepo" na kuanza kula rushwa ama kazi ya upolisi ingemshinda na kuiacha. Polisi wa nchi hii hasa wale wa vyeo vya kati na wasiokuwa na vyeo wako kama walivyo walalahoi wengine wa nchi hii, ni watu wenye kipato duni na baya zaidi mazingira yao ya kazi ni magumu sana kuliko ya mfanyakazi yoyote yule wa nchi hii. Mwananchi wa kawaida hawezi kujua machungu aliyo nayo polisi kwa sababu yuko nje ya mfumo wa Polisi na kila kitu anakiona kwa nje na siyo kwa ndani. Polisi wa nchi hii kwanza anakabiliwa na tatizo la kuchukiwa. Hata pale anapooneshwa kuthaminiwa si kwa sababu anapendwa bali kwasababu anaogopwa, ngoja siku aachishwe kazi ndipo atatambua ni kiasi gani hatakiwi. Pili, Polisi wa nchi hii hathaminiwi hata na Jamhuri. Kiongozi wao mkuu Omari Mahita ndiye anayeongoza kwa kutojali maslahi ya vijana wake. Mapolisi waandamizi hawaonji dhiki anayoipata Polisi wa kawaida kwa sababu wengi wao kama si wote wameingizwa kwenye "Pay roll" za matajiri wanaoishika nchi (Kiuchumi) wanaoshika mikoa, na wanaozishika wilaya. Hawa vigogo wa Jeshi la Polisi mara wanapoishiwa au kuchacha, wanachokifanya ni kuandika "Vimemo" tu na kumtuma kijana kwenda kuchukua fedha. Kwa ajili hiyo hawaoni hata ulazima wa kupigania maslahi ya jeshi la polisi badala yake na wao wanakuwa kama walivyo viongozi wa CCM wapo kupigania maslahi yao binafsi na zaidi kuhami nafasi zao zinazowapa ulaji ili wasije kuzidondosha maana siku watakapoziacha nafasi zao itakuwa ni sawa na kudondokea kwenye makaa ya moto Kwa ajili hiyo Polisi wa kawaida ni sawa na yatima anayetunzwa na Baba au mama wa kambo, ana wakubwa lakini wasiojali matatizo yake, ana kazi isiyomwezesha kupata kipato kizuri na kuishi maisha mazuri, ana mamlaka na amri lakini haheshimiki, wakati wote ni mtu wa mapambano kama vile yuko vitani. Asipokerwa na raia ni lazima akerwe na bosi wake au akerwe na umaskini unaowakera walalahoi wengine. Kwahiyo kisaikolojia Polisi wa Tanzania anatatizo la ugiligili hana amani, kichwa chake kinawaka moto kwa wakati wote ndiyo maana ametanguliza mbele kipigo kabla ya mbinu zingine zote wakati wa kutekeleza majukumu yake. Katika hili inabid imkuu wa Polisi (IGP) na viongozi wengine waandamizi ndio walaumiwe kwa sababu wameshindwa kabisa kuboresha mazingira ya kazi ya "upolisi", na pia wameshindwa kabisa kuboresha maisha ya Mapolisi wa kawaida na wameachia kila Polisi ajipiganie kivyake kuboresha maisha yake au kukabili hali ngumu ya maisha. Sasa wananchi watarajie nini kutoka kwa Polisi ambao tayari ni "frustrated" katika ujumla wao? Ni wazi kwamba tusitarajie mema kutoka kwa watu ambao wamezingirwa na mabaya kuanzi anyumbani wanakoishi hadi kazini wanakaofanyia kazi. Polisi anaenyanyasika kila siku hawezi kuwa "fair" hata siku moja na eti akajali haki za watu asiowafahamu au haki za wengine wakati yeye binafsi haki zake hazithaminiwi, ni lazima atalipiza kisasi cha kunyanyaswa kwake, na kuonewa kwake kwa wengine. Ikumbukwe kwamba Polisi wa Tanzania , na askari wengine wa majeshi yetu (Magereza, JWTZ na Uhamiaji) hata wakikabiliwa na ugumu unaozidi kawaida, ama uonezi au dhuluma zinazozidi kawaida, ambazo kwa raia wa kawaida zitawafanya kuandamana kuipinga serikali au kupiga kelele za aina yoyote kuiarifu, kwao upande wa Polisi hawana nafasi ya kuandamana, wala kulalamika popote pale. Zamani enzi za mfumo wa chama kimoja walitumia chama kama jukwaa la kusemea maovu yanayowaumiza ama yale yanayowakera lakini sasa hawana "forum". Kwahiyo malimbikizo yote ya uchungu wao huamua kuyamalizia kwetu sisi raia na hasa wanasiasa. Mikong’oto na vipigo vingine wanavyotushushia (hasa wapinzani) huwa ni matokeo ya dhiki na "frustrations" zao baada ya kukosa namna ya kuziondoa katika maisha yao. Tahadhari kwa Afande Mahita Afande Mahita ametoa mwito wa Polisi kurejesha heshima yao, mwito unaoashiria kwamba Polisi watakuwa wakali na wakatili zaidi. Mahita haangalii heshima ya Polisi katika misingi ya kuwa na maisha bora, nyumba bora, mavazi mazuri, elimu nzuri, afya au lishe nzuri (maana siku hizi mapolisi wengi wanaonesha kuwa na njaa ya muda mrefu, kula vitu vidogo vidogo ovyo njiani na wakati mwingine kuomba omba hela ya kula kwa raia) wala Mahita haiangalii heshima ya Polisi katika msingi wa kipato bora. Mahita haoni kwamba maisha duni ya vijana wake ni aibu na fedheha ambayo kwa kiasi kikubwa inalipunguzia heshima jeshi la Polisi badala yake yeye anachokiona cha aibu eti ni kule kuzidiwa nguvu na raia wakati wa mapambano kama ilivotokea huko Zanzibar ambao baadhi ya Polisi walipigwa na kuumizwa na wafuasi wa CUF. Kwahiyo tutarajie "ukali" zaidi, na "Ukatili" zaidi hali hiyo kwake Mahita itakuwa sawa na "Upolisi" zaidi. Mahita haoni kwamba upolisi ni utaalamu kama ulivyo udaktari, ualimu n.k. bali anaona "upolisi" ni "Ukali na Ukatili". Onyo la msingi ni kwamba akiileta tafsiri hiyo ya upolisi kuwa sana na ukali na ukatili ataiponza nchi, na pia ataiponza serikali iliyoko sasa madarakani kwa sababu idadi ya Polisi kwa nchi nzima wako 60,000 (sitini elfu) endapo wananchi 1,000,000 (milioni moja tu) wakaamua kupambana na polisi ana kwa ana ama jicho kwa jicho ni wazi kwamba polisi sitini elfu watasambaratishwa ndani ya wiki moja tu. Hakuna lisilowezekana kwa watu walioamua na waliodhamiria. Wananchi wa Afrika Kusini waliamua kupambana na Polisi wa Makaburu sawa na mtu anavyopambana na nyoka mwisho wa yote utawala wa Makaburu ukaanguka. Mahita inabidi atambue kwamba kwa sasa vijana wengi (wenye nguvu) wako "vijiweni", hawana makasri huko Masaki, Mbezi Beach, Mikocheni na kwingineko, hawana mali kama walizo nazo watawala na viongozi wengine wa CCM, na kwahiyo hawana chochote cha kupoteza hata kama inatokea "jihad" kati yao na Polisi. Kisha, vijana hao walioko vijiweni ndio walio wengi. Kulingana na data za UNDP theluthi mbili au asilimia 67 ya Watanzania ni vijana kati ya miaka 25 kwenda chini. Hawa wanachokihitaji ni kitu kidogo tu nacho ni kuhamasishwa na kuunganishwa pamoja tayari. Aidha, kufanya lililo jema kwa taifa ama baya, na kwahiyo hakuna ugumu wowote wa kuwafanya kupambana na dola ya kipolisi kufa na kupona. Endapo hiyo ya mapambano itatokea ama itakaribishwa basi mwisho wake Polisi watashindwa kudhibiti mambo na hivyo italazimu Jeshi kuu kuingia mitaani kufanya kazi ya Polisi. Sasa Jeshi litakapolazimika kuinuka na kuingia mitaani, ieleweke wazi kwamba lolote linaweza kutokea, hakuna haja ya kuficha kwani wanaweza kuamua kuzimisha fujo na papo hapo kuuzimisha utawala wa CCM uliopelekea nchi kwenye vurugu. Hivyo basi, kwa nia njema tunaonya kwamba Afande Mahita sisi wananchi hatutaki dola ya kipolisi, hatutaki mapambano na watoto wetu, na pia hatutaki Polisi ambao ni vijana wetu watumike kwa manufaa ya CCM, wala sisi hatufurahii kabisa kuona Polisi wenye dhiki, wanaokula ovyo barabarani kutokana na njaa kali na ya muda mrefu, Polisi ambao wanalazimisha kupanda daladala bure wakati nchi ingeweza kuwanunulia "mini-bus" zao na magari mengine ya kufanyia kazi. Mbona serikali hii inaweza kuwanunulia wabunge mashangingi ya milioni mia, wakuu wa mikoa na maafisa wengine waandamizi mabenzi ya milioni sitini hadi themanini, Je, inashindwa nini kuwanunulia Polisi wake Landrover za milioni kumi na nane tu hadi kusababisha mapolisi na maaskari wengine wawe mzigo kwa bishara ya daladala? Endapo utalipuuza onyo hili ujue
wazi kwamba unautengenezea jeneza utawala wa CCM yenu kwasababu hatutakubali
kufa kikondoo badala yake tutahakikisha kama ni kufa, basi tunakufa wote
na dola, kama ni kukosa basi tunakosa wote, yaani sisi wapinzania na hiyo
CCM yako unayojaribu kuihami na kuitetea. Usiwashe moto wakati umezungukwa
na petroli!!
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Chuo Kikuu Dar wafanya mitihani katika Bwalo la chakula Udini wa CCM utaisambaratisha nchi -Tambwe ‘Kutoweka’ kanda ya Kakobe: CCM yatuhumiwa Maalim Seif awaambia Wazanzibari: Wenye mamlaka ya kumuweka mtu Ikulu ni wananchi Mkapa afurahia maendeleo Pwani ‘Zawadi’ ya Uchaguzi yatishia kusambaratisha taasisi ya Kiislam Tanga Serikali yakemea mwanamke kudhalilishwa Ushauri Nasaha
MAKALA
Makala
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Makala
Makala
RIWAYA
Lishe
|
|
|
|
|