NASAHA
Na. 049 Jumatano Mei 24 - 30, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Kalamu ya Mwandishi

Makubaliano kwa vitendo Z'bar

NA MAALIM BASSALEH

Waswahili wamesema, "mwenye macho haambiwi tazama!". Lakini kwa jinsi hali ilivyo, hivi sasa huko Zanzibar, hata kipofu, asiyekuwa na macho, kwa kupapasa papasa tu, anaweza kuhisi hatari inayovikabili visiwa hivyo. Tukitaka tusitake, Zanzibar imo katika mgogoro mkubwa uliokwishavunja umoja wa Kitaifa, na unaotishia kuhatarisha amani."

Jambo hilo linaonekana waziwazi. Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Omar Ali Juma, juzi alipokuwa akihojiwa na shirika la utangazaji la BBC, alisema kuwa katika kipindi hiki cha kutafuta mgombea wa kiti cha Urais, kwa tiketi ya chama chake, cha CCM, inataka apatikane mgombea atakayekuwa na uwezo wa kuondoa siasa za chuki, uhasama na ugomvi, ambazo zimepoteza kabisa umoja wa kitaifa visiwani humo.

Kwa kauli yake hiyo ni wazi kuwa Dkt. Omar anakiri kuwa hali ya kisiasa katika visiwa hivyo si ya kuridhisha hata kidogo. Ni lazima basi upatikane ufumbuzi. Na ufumbuzi si kupatikana tu kwa mgombea anayekubalika kutoka chama cho chote kile, iwe kutoka chama cha CCM au CUF, bali jambo linalohitajika lililotanda hivi sasa kwenye anga ya visiwa vya Zanzibar, ni kuandaa mazingira mazuri yatakayopelekea uchaguzi mkuu ujao, wa Oktoba 2000, uonekane kuwa ni wa haki na huru. Vinginevyo, migogoro haitamalizika.

Hali hii ya sasa ya mgogoro, huko Zanzibar, ilisabishwa na mazingira mabaya yaliyotawala uchaguzi Mkuu uliopita, ambao ulileta utata wa matokeo ya kura zilizopigwa. Na kwa vyo vyote vile, mazingira mazuri ya uchaguzi hayatakuwepo mpaka kwanza upatikane mwafaka wa kweli, baina ya pande mbili zinazozozana, pamoja na kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi itakayopata ridhaa ya pande zote zinazohusika.

Inaposemwa mwafaka, inakusudiwa suluhu baina ya CCM na CUF. Basi ni nani atakayeileta suluhuu hiyo, hapana shaka ni Wazanzibari wenyewe. Watu wengine wanaweza kusaidia tu katika kuzikutanisha pande mbili zinazotofautiana ili zizungumze juu ya hizo tofauti zao. Lakini kamwe hawawezi kuleta suluhu, kama Wazanzibari wenyewe hawataki. Ni lazima Wazanzibari wenyewe wawe tayari kusahau tofauti zao na kutaka kupatana.

Kurani Tukufu inasema, "Wakitaka suluhu Mwenyezi Mungu atawawezesha." (An Nisai 4:35) kwa hivyo, kama CCM na CUF, Zanzibar, wana nia ya kusuluhiana basi Mwenyezi Mungu atawawezesha kufikia suluhu hiyo. Lakini lazima wawe na nia hiyo!

Kwa nini juu ya kutiwa saini mkataba wa mwafaka na mpaka hii leo suluhu bado haijapatikana? Ni kwa sababu kama kuna upande unaotaka suluhu basi upande mwingine hautaki! Kwa hali hiyo suluhu haitaweza kupatikana. Na kwa sababu hakuna nia ya suluhu!

Jumuiya ya Madola kwa kupitia kwa aliyekuwa Katibu wake Mkuu, Chifu Emeka Anyauko, pamoja na msaidizi wake Dkt. Moses Anafu, imefanya juhudi kubwa sana ya kuzikutanisha pande mbili zinazovutana, CCM na CUF, kuzungumzia juu ya tofauti zao na hatimaye kufanikisha kutiwa saini kwa mkataba wa makubaliano ya mwafaka, baina ya pande mbili hizo.

Lakini, inafaa ieleweke kuwa kutiwa saini mkataba wa mwafaka si kigezo cha kupatikana suluhu ya kweli. Ili suluhu ya kweli ipatikane inabidi pande zote zinazohusika zitekeleze kwa vitendo makubaliano yaliyofikiwa katika waraka wa mkataba huo. Aidha inabidi kuwepo na ufatilizi kuona jinsi kila upande unavyotekeleza vipengele hivyo vya mwafaka.

Wiki iliyopita Dkt. Moses Anafu amewasihi nchini kwa lengo hilo. Amekuja kufuatilia utekelezaji wa mwafaka. Kwa mujibu wa habari za kuaminika, kwanza ataonana na Mheshimiwa William Benjamin Mkapa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Taifa; na kisha atakwenda Zanzibar kuonana na Mheshimiwa Dkt. Salmin Amour Jumaa, Rais wa Serikali ya Zanzibar na Makamo Mwenyekiti wa CCM, Visiwani. Hapana shaka baadaye pia, ataonana na viongozi wa upande wa pili wa chama cha CUF pamoja na kamati ya IPC.

Jambo linalosikitisha na kukatisha tamaa ni kuwa hata kabla ya kuonana na viongozi wa pande zinazohusika, Dkt. Anafu, ambaye ndiye msuluhishi wa mgogoro huo, amesema kuwa amechoshwa na mgogoro huo wa Zanzibar usiomalizika.

Kauli hiyo ya Dkt. Anafu inadhihirisha vipi Jumuiya ya Madola ilivyovunjika moyo na jinsi utekelezaji wa makubaliano ya mwafaka yanavyotekelezwa. Utekelezaji wake umekuwa ama wa pole pole sana, au vipengele vingine kutotekelezwa kabisa.

Wamekwisha sikika baadhi ya viongozi wa upande mmoja wakisema kuwa mwafaka ule ulikuwa ni geresha tu. Kama mtu atasema kuwa Zanzibar hakuna kitu kinachoitwa mwafaka, hatakosea!

Wiki iliyopita ujumbe mzito kutoka serikali ya Zanzibar ukiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Zanzibar, Mheshimiwa Mohammed Ramia, ulifika Dar es Salaam na kufanya mkutano na waandishi wa habari.

Ujumbe huo ulizindua kitabu kinachokishutumu chama cha CUF pamoja na uongozi wake kwa kufanya vitendo vya hujuma kabla na baada ya uchaguzi wa mwaka 1995. Aidha kitabu hicho kimedai kuwa chama cha CUF ndicho kinachofaa kilaumiwe kwa kukwamisha utekelezaji wa mwafaka kutokana na kukataa kuunga mkono mswada wa mabadiliko ya nane ya katiba ya Zanzibar.

Inaonekana lengo la kujitabu hicho ni kukipaka matope chama cha CUF mbele ya Wantanzania na jumuiya ya kimataifa, kuwa chama hicho ndicho kikorofi na ndicho kinachoendeleza mgogoro Zanzibar.

Lakini waandishi wa habari waliokuwa wakisikiliza maelezo ya kitabu hicho kutoka kwa ujumbe huo wa serikali ya Zanzibar inaonekana wameshindwa kukubaliana na maelezo hayo. Wao waliona ni CCM ndiyo inayokwamisha mwafaka! Waandishi hao walitaka waelezwe kwa nini Rais wa Zanzibar hajateua wajumbe wawili wa CUF kuingia katika Baraza la Wawakilishi, au kwa nini hakuifanyia marekebisho Tume ya Uchaguzi, kama makubaliano ya mwafaka yanavyosema?

Kwa jinsi hali ilivyo hakunasababu, hivi sasa ya kutafuta nani ni mchawi! kinachohitajika ni kwa kila upande kutekeleza yale yaliyokubaliwa katika mwafaka huo. Hakuna haja ya kukisakama chama cho chote. Faida au hasara itakayopatikana kwa kutekeleza au kutotekeleza mwafaka itakuwa kwa Wazanzibari wote pamoja na visiwa vyao; na siyo kwa chama fulani tu.

Habari zilizotufikia wakati tukiwa mbioni kukamilisha kuandika makala haya ni kuwa yule msuluhishi wa mgogoro wa Zanzibar, Dkt. Moses Anafu, tayari amekwisha wasili visiwani humo kwa ajili ya kukutana na viongozi wa huko.

Amekwisha kutana na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mheshimiwa Ameir Kificho; na leo anatazamiwa kukutana na Rais wa Zanzibar, Dkt. Salmin Amour.

Katika mazungumzo yake na Spika, Dkt. Anafu amesema ingawa inaonekana utekelezaji wa mwafaka umesita; lakini bado upo muda wa kutosha wa kutekeleza mwafaka huo.

Kuhusu madai kwamba chama cha CUF kinakwamisha utekelezaji wa mwafaka huo kwa kukataa kuunga mkono mswada wa mabadiliko ya nane ya katiba ya Zanzibar, Dkt. Anafu amesema yapo mengi ndani ya mkataba wa makubaliano ya mwafaka ambayo yanaweza kutekelezwa hata bila ya kupelekwa kujadiliwa katika Baraza la Wawakilishi.

Akieleza juu ya umuhimu wa kuwa na tume huru ya uchaguzi, amefafanua kuwa yeye hakusema kuwa lazima tume hiyo iwe na wajumbe kutoka vyama vya siasa. Amesema kuwa tume hiyo inaweza kuundwa kwa kushauriana na viongozi wa vyama vya siasa. Kwa mfano amesema wakuu wa vyama vya siasa wanaweza kupewa fursa ya kupendekeza majina ya wajumbe watakaounda tume hiyo. Kisha serikali ikateua wale inaowaona wanafaa.

Ameeleza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kupata tume yenye wajumbe waadilifu na pia tume yenyewe iwe ni yenye kukubalika na pande zote.

Kiini cha mgogoro wa Zanzibar kinatokana na utendaji mbovu wa tume ya uchaguzi iliyopo. Wakati chama tawala kinaikubali tume hiyo, wapinzani wanaikataa, kwa madai kwamba inakipendelea chama tawala.

Na kwa kweli, kwa jinsi hali ilivyo, uwezekano wa tume hiyo kufanya hivyo ni mkubwa sana; hasa ukitilia maanani kuwa tume hiyo iliteuliwa na kiongozi wa serikali inayoongozwa na chama hicho.

Dkt. Anafu amesisitiza kuwa tume itakayokubalika na pande zote itaondoa malalamiko. Mwisho, Dkt Anafu amekanusha habari kuwa amekuja kuifunga IPC, yaani kamati ya kusimamia mwafaka inayoundwa na wawakilishi kutoka CCM na CUF; bali amesema kuwa amekuja kuona vipi mwafaka huo unavyotekelezwa, ili uchaguzi ujao uwe ni wa haki na huru.

Kutupiana lawama katika vyombo vya habari, kwa wakati huu, hakutasaidia cho chote katika kurejesha utulivu Zanzibar. Inafaa ieleweke kuwa bila ya kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi kamwe Zanzibar haitakuwa na utulivu wa kisiasa!
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
KERO katika Elimu ziondolewe haraka

Chuo Kikuu Dar wafanya mitihani katika Bwalo la chakula

Udini wa CCM utaisambaratisha nchi -Tambwe

‘Kutoweka’ kanda ya Kakobe: CCM yatuhumiwa

Maalim Seif awaambia Wazanzibari: Wenye mamlaka ya kumuweka mtu Ikulu ni wananchi

Mkapa afurahia maendeleo Pwani

Wapinzani wajiimarisha Moro

‘Zawadi’ ya Uchaguzi yatishia kusambaratisha taasisi ya Kiislam Tanga

Serikali yakemea mwanamke kudhalilishwa

Ushauri Nasaha
Umuhimu wa kushirikiana na majirani katika malezi ya watoto

MAKALA
Afande Mahita, wananchi hatutaki Dola ya kipolisi

Makala
CCM hawawezi kuondoa umasikini, ndio tegemeo lao

Kalamu ya Mwandishi
Makubaliano kwa vitendo Z'bar

MAKALA
CCM na sera za maendeleo (5)

Makala
Wanawake na maendeleo: Je ni wimbo wa kuchaguliwa?

Makala
CCM inatawala badala ya kuongoza

Habari za Kimataifa

RIWAYA
Mapinduzi ya fikra -4

Lishe
Unachotakiwa kufanya kabla ya kuweka chakula kwenye jokofu

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Raza kufungua mashindano ya Wavu Zanzibar
  • Real Madrid yaota Ubingwa  leo
  • Kajumulo asema Yanga timu ya Wananchi

  •  


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita