|
Na. 036 Jumatano Februari 23 - 29, 2000 |
|
|
|
|
|
Ndoto ya mafanikio - 2 MTUNZI: Abu Firdaus Aliyavumilia yote haya kwa kuthamini elimu ya mwanae Hidaya. Huduma alizozitoa Mzee Faida kwa Hidaya kwa mwaka hazikulingana na wingi wa kazi alizozifanya Mzee Yassini. Mzee Faida alifurahi sana kwani aliona amepata mtu ambaye anafanya kazi iliyostahili kufanywa na wafanyakazi takribani wasiopungua watatu. Hakuona vibaya kabisa kumnyonya Mzee Yassini kwa vile tu Mzee Yassin asingeweza kukataa ili hali yeye ana anashida. Jioni moja mkewe Mzee Faida alikaa na mume wake wakibadilishana mawazo. Mama Rashid, mkewe Mzee Faida, aliamua kumshawishi mumewe kuangalia upya mkataba wake na Mzee Yassini. "Mimi nafikiri ni bora Mzee Yassin tukiwa tunampa hela ya sabuni kila mwisho wa mwezi pamoja na kuwa sio mapatano yetu," alishauri Mama Rashid. "Kwanini tumpe hela tena wakati si makubaliano yetu?" aliuliza Mzee Faida." Tazama jinsi Mzee yule anavyojituma katika kazi kila siku bila kutega, kazi anazozifanya vilevile ni nyingi kuliko huduma anazotakiwa kupewa Hidaya," alifafanua mama Rashid. "Lakini aliomba yeye mwenyewe na wala sio mimi niliyempa masharti haya," alidai Mzee Faida. Pamoja na hayo, hiyo ilikuwa kwasababu ya shida aliyokuwa nayo na ambayo mpaka sasa anayo, ambayo ni kumsomesha mtoto wake. Kibinadamu inabidi tufahamu kuwa shida haina wakati wala haiangalii mtu. Tungeweza kumsaidia kumsomesha Hidaya bure. Hivyo kwa kumpa hela ya sabuni itajenga mahusiano mazuri kati yao na sisi. Pili itamfanya aongeze ubora wa utendaji wake." alifafanua Mama Rashid. ok! Sasa tumpe kiasi gani? Alikubali na kuuliza Mzee Faida. "Tumpe kama shilingi elfu kumi hivi" alishauri Mama Rashid. "Hapana tutampa shilingi elfu tano kwanza."alipinga mzee Faida. "Sawa", alikubali Mama Rashid. Siku nne baadaye mwisho wa mwezi ulifika. Baada ya kazi za mchana kutwa Mzee Yassini aliaga ili arejeee nyumbani. Aliitwa na Mzee Faida na kuambiwa "chukua fedha hizi zikusaidie kwa sabuni". Alisema Mzee Faida huku akimkabidhi fedha zile Mzee Yassini. Mzee Yassin alisita kuzipokea kwa kuhofia labda umevunjika mkataba wao. Lakini Mzee Faida alimuondoa wasiwasi kuwa hiyo ilikuwa nje ya makubaliano yao , mkataba wao unaendelea kama ulivyokuwa. Mzee Yassini alishukuru sana. Aliondoka kwa furaha na kurejea nyumbani. Jioni ile alimwita mkewe Mama Mussa na kumueleza tukio lile la "kihistoria". Walifurahi na kumuona Mzee Faida kama mtu mwenye kuwajali watu wenye shida. Kitendo kile kiliongeza uhusiano katika familia zao. Sasa Mama Mussa aliweza kutembeleana na Mama Rashid na kusaidiana katika baadhi ya majukumu ya nyumbani. Ni miaka minne sasa tangu Hidaya aanze kidato cha kwanza pale Jangwani sekondari. Mama Rashid alimuomba mumewe wamruhusu Hidaya aishi nao pale nyumbani kwa miezi michache iliyobaki ili aweze kusoma vizuri kwa kuwa pale nyumbani kuna maji, umeme na nafasi ya kutosha, Mzee Faida hakusita kukubali wazo hili. Siku inayofuata jioni Mama Rashid alimtembea Mama Mussa nyumbani kwake alimkuta akiendelea kuuza karanga na ubuyu wake. Zaidi ya yote sasa alikuwa anauza bamia, nyanya chungu na pilipili. Walikaa pamoja na kuzungumza kwa muda takriban masaa matatu na nusu. Mwisho Mama Rashid alitumia nafasi ile kumueleza Mama Mussa wazo lao la kumuomba Hidaya akaishi kwao ili aweze kusoma vizuri katika muda uliobaki. Mama Mussa alilikubali wazo lile binafsi na kuahidi kuwa atamueleza mume wake ili wafikie uamuzi wa pamoja. Mama Rashid aliaga na Mama Mussa aliinuka na kumsindikiza shoga yake huyo kwa kitambo kirefu kisha alirejea nyumbani na kumkuta Hidaya tayari amesharejea kutoka shuleni. Yapata saa kumi na mbili na nusu, Mzee Yassin alirejea nyumbani kutoka kibaruani. Baada ya kusabahiana, Mzee Yassini alielekea chumbani na kujitupa kitandani. Kutokana na uchovu aliokuwa nao, haikumchukua muda mrefu alijikuta amepitiwa na usingizi. Aliamshwa na Mama Mussa yapata saa mbili kasorobo ili aende msikitini kwani muda tayari ulikuwa umewadia. Aliporejea, alikuta chakula tayari, walikaa pamoja na kuanza kunawa kisha wakala chakula. Baada ya mlo huo, Mama Mussa alimkabili Mzee Yassin (Baba Hidaya) na kumueleza ushauri aliouleta Mama Rashid juu ya mtoto wao Hidaya. Mzee Yassin alifurahi sana na kuona kuwa si tu kwamba Mzee Faida anamsaidia kumsomeshea mwanae, bali pia alipenda maendeleo na mafanikio ya Mzee Yassin. Walimwita Hidaya na kumueleza juu ya suala hili ili kujua mtazamo wake. Hidaya hakuonyesha japo chembe ya upinzani. "Ikiwa ninyi wazazi wangu mnaona ni kheri kwangu, bila shaka mimi niko radhi", haya ndio yalikuwa majibu ya Hidaya. Walifunga mjadala wao na Mama Mussa akapewa jukumu la kufikisha salamu zile kwa Mama Rashid. Siku iliyofuata asubuhi yapata saa nne, Mama Mussa alifika nyumbani kwa Mama Rashid. Pamoja na mazungumzo yao mengi pia Mama Mussa alimfahamisha Mama Rashid kuwa wazo lao limepokelewa kwa furaha katika familia ya Mzee Yassin. Waliagana na Mama Rashid alimuomba Mama Mussa kuwa siku hiyo hiyo jioni Hidaya ahamie nyumbani kwa Mzee Faida. Na Mama Mussa alikubali. Baada ya Hidaya kuhamia nyumbani kwa Mzee Faida, alijihisi kuwa na muda na nafasi nzuri ya kujiandaa na mtihani wake wa mwisho. Sasa alikuwa na nafasi nzuri zaidi ya kujisomea usiku. Aliongeza bidii huku akiyaelekeza matarajio yake kwa Mwenyezi Mungu. Muda wa mtihani uliwadia na Hidaya alikuwa miongoni mwa wahitimu waliotarajiwa kufanya vizuri. Katika hafla ya kuwaaga, Hidaya alikuwa miongoni mwa wahitimu waliopewa zawadi ya wanataaluma bora shuleni. Alipewa zawadi ya vitabu, madaftari na fedha taslim kiasi cha shilingi elfu tano. Fedha ambazo kwa wakati huo zilikuwa nyingi za kutosha. Wakati huo ada ya shule kwa mwaka ilikuwa shilingi elfu mbili na mia tano. Baada ya hapo Hidaya aliendelea kukaa nyumbani kwa Mzee Faida kwa muda wa wiki mmoja. Kisha aliomba aruhusiwe arejeee nyumbani kushirikiana na Mama yake katika kazi za nyumbani. Alirejea nyumbani na kushirikiana na wazazi wake katika shughuli mbalimbali. Mussa, kaka yake Hidaya, mbali ya kazi yake ile ya uchotaji maji, sasa alikuwa ameajiriwa katika kampuni moja kama mlinzi. Hali ilianza kuridhisha pale nyumbani. Kidogo vyanzo vya fedha viliongezeka. Baada ya miezi miwili na siku kumi na tatu tangu Hidaya alipomaliza shule, Mussa, kaka yake Hidaya alimposa na kufunga ndoa na binti mmoja aitwae Mariam mtoto wa Mzee Ali Matola. Kupata jiko kwa Mussa, kuliifanya familia ya Mzee Yassin kuwa moja lakini yenye tofauti. Baada ya Mussa kuishi na mkewe kwa takriban miezi minane, mgogoro ulianza huku mkewe binti Mariam akipigia kelele japo matembele yatakayopelekwa kwa Mama Mussa. Kutokana na hali hiyo Mussa alijikuta akitoa huduma zaidi kwa mkewe na wala hakuwakumbuka wazee wake. Hivyo uangalizi wa familia ya Mzee Yassin ukabaki unamgharimu yeye mwenyewe na mkewe. Kwa upande mwingine vijana kadhaa walijitokeza kumposa Hidaya. Hidaya ambaye sasa alikuwa na umri wa miaka kumi na saba, alijengeka kwa huba nzuri na yenye kuvutia japo alitoka katika familia duni na hivyo kukosa baadhi ya vitu muhimu. Pamoja na vijana hao kujitokeza kutaka kumuoa Hidaya, bado Hidaya hakuona kama ni jambo la busara kufanya hivyo. Alihisi kwa kufanya hivyo itakuwa kama kuitelekeza familia ya Mzee Yassin ambayo mbali na baba na mama ilikuwa na wadogo zake wanne. Jibu pekee alikuwa akilitoa Hidaya ni" Mimi bado nahitaji kujielimisha zaidi ili niweze kutoa msaada wa kutosha katika familia yetu na kuilea vizuri familia yangu pale itakapokuwa imefikia wakati wa kufanya hivyo. Nahisi kusoma hali yakuwa nimeolewa itaniathiri kisaikolojia na hivyo kutofanya vizuri." Pamoja na viswahili virefu walivyokuja navyo, bado Hidaya alishikilia msimamo wake. Miezi ilikwenda na hatimae muda wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliwadia matokeo yalibandikwa, Hidaya alishindwa kabisa kufika mwenyewe kuangalia matokeo. Alihisi kuishiwa nguvu. Baba yake na Mama yake nao walishindwa kwenda kuangalia mtokeo kwani hakuna hata mmoja kati yao aliyefahamu kusoma wala kuandika. Walimtegemea Hidaya na Mussa kuwasomea kila waraka uliofika pale nyumbani. Jioni ya siku ya pili baada ya matokeo, Mama Rashid mkewe Mzee Faida alifika nyumbani kuwasabahi. Baada ya mazungumzo marefu na Mama Mussa. Mama Mussa alimuomba Mama Rashid amsaidie kwenda kuangalia matokeo ya Hidaya kisha aje awafahamishe. Mama Rashid hakusita alilikubali ombi la Mama Mussa waliagana na Mama Rashid aliondoka. Siku inayofuata, Mama Rashid alifika nyumbani kwa Mzee Yassin yapata saa kumi na moja jioni. Baada ya kubisha hodi, alipokewa na Hidaya ambaye alikuwa anafanya usafi barazani. Mama Rashid alimkumbatia Hidya na kuanza kumpongeza kabla hata hajataja matokeo yake. Mama Mussa alikuja kuungana nao pale barazani, lakini alishindwa kutoa pongezi kwakuwa haelewi lolote juu ya matokeo ya Hidaya. Waliketi kwenye mkeka ambao alimtandikia chini Hidya. Mama Rashid alimueleza Mama Hidaya na Hidaya kuwa Hidaya alikuwa amefanya vizuri katika mitihani yake. Alipata daraja la kwanza pointi kumi. Hivyo atapata nafasi ya kuendelea na masomo ya elimu ya kidato cha tano na sita. Mama Hidaya alimkumbatia Mwanae na kumbusu, alifurahi kuona mwanae Hidaya amefanikiwa. Alimshukuru sana Mama Rashid kwa taarifa ile waliagana na Mama Mussa alimsindikiza kidogo Mama Rashid kisha alirejea. Baada ya sala ya Magharibi yapata saa moja, Mzee Yassin alirejea nyumbani. Alifahamishwa matokeo ya Hidaya naye ghafla alijikuta akiungana nao katika furaha na shamrashamra. Alimpongeza sana Hidaya na kumwambia kuwa kwa matokeo yake mazuri kunaonyesha jinsi gani Hidaya anajali mchango wa familia yake. Hidaya kwa upande wake alifurahi sana, zaidi ya hayo alifikiri ni jinsi gani anapaswa kumshukuru Mungu kwa kufaulu kwake. Aliamua afunge siku tatu. Alifunga kuanzia siku ya Jumanne mapaka Alhamisi na usiku wa kuamkia Ijumaa aliamka usiku yapata saa nane usiku na kuanza kufanya ibada mbalimbali. Hii ndio njia pekee aliyoichagua Hidaya kusherehekea na kushukuru kwa kufaulu mitihani yake. Alitumia fursa hii pia kumuomba Mwenyezi Mungu amuhifadhi na afanye vizuri zaidi huko atakapopangiwa kwenda kusoma tena. Siku, mwezi, miezi ilipita, hatimaye Mzee Yassin alipokea barua ya kumwita Hidaya shuleni. Hidaya aliitwa jioni ile na kukabidhiwa barua ile aisome ili wafahamu nini kinatakiwa. Hidaya alichaguliwa kujiunga na Shule ya Wasichana ya Tabora. Alitakiwa aripoti shuleni mapema mwezi wa saba. Mzee Yassin pamoja na furaha aliyokuwa nayo, ilimpasa aende kuwasiliana na Mzee Faida ili aendelee na mkataba wake. Mzee Faida hakuonesha ugumu wowote juu ya hilo. Hivyo Mzee Faida alikuwa tayari kumsomesha Hidaya. Wakati wa Hidya kuondoka kuelekea masomoni uliwadia. Mzee Faida alimgharimia kila lililohitajika pamoja na ada. Jioni ya mwisho kabla Hidaya hajaondoka, Mzee Yassin aliona ni bora achukua fursa hii kumhusia mwanae. Baada ya chakula cha jioni siku ile, Mzee Yassin alimwita mwanae Hidaya na Mama Mussa. Waliketi pamoja na kisha Mzee Yassin alianza kumuusia mwanae, "Mwanangu Hidaya, hali zetu wazijua, hatuna na kukuficha kila kitu wakijua. Mkombozi wetu na wadogo zako ni wewe. Tunakubali kulala njaa, kula matembele bwawa ilimradi mwanetu usome. Tunashukuru umeonyesha kuthamini mchango wetu kwa kufanya vizuri mtihani wako uliopita. Nenda mwanangu, kasome kwa bidii, jitenge mbali na anasa. Zingatia kile kilichokupeleka pale shuleni. Zaidi ya yote mwanangu, ngao pekee ya kukusaidia huko ni maadili ya dini yako. Ifanye dini yako kuwa mshauri juu ya kila jambo. Ujihifadhi kama ulivyo sasa. Kila mara ukumbuke hali ngumu tuliyonayao hapa nyumbani", alimaliza usia nyumbani isingekuwa duni kiasi kile. Kwanini lakini watu wabaguliwe? Kwanini watu wadhulumiwe? Alijikuta akibubujikwa na machozi. Kwa mara ya kwanza alifahamu sababu ya wazazi wao kutosoma. Alihisi uchungu wa hali ya juu. Sasa nitahakikisha.... Aliwaza Hidaya huku akibubujikwa na machozi. Asubuhi na mapema Hidaya alikuwa wa kwanza kuamka baada ya kusikia tu adhana. Kwa sababu hakusinzia kabisa siku ile. Aliwaamsha wote ndani ya nyumba ya nyumba ya Mzee Yssin ili waianze siku vyema kwa ibada ya sala ya asubuhi. Baada ya hapo kila mmoja alielekea kwenye shughuli zake wakimuacha Hidaya pale nyumbani na wadogo zake. Hidaya aliendelea na kazi za pale nyumbani mpaka yapata saa tisa alasiri. Walirejea nyumbani Mama Mussa na Baba Mussa, walijiandaa tayari kumsindikiza mwanao kituo cha gari moshi. Walikuwa tayari wamebeba mizigo yao tayari kwa safari kuelekea kituo cha gari moshi, alifika Mama Rashid. Rashid na Mzee Faida kuungana nao kumsindikiza Hidaya. Walielekea kituoni na kufika saa kumi na robo jioni. Walikaa wakizingumza pale nje baada ya kuwa wamepanga mizigo yao ndani ya gari. Ilipofika saa kumi na moja kasoro dakika tano, wasafiri wote walitangaziwa kuingia ndani ya gari. Waliagana kwa furaha iliyoambatana na majonzi. Hidaya aliingia garini, na mara safari ilianza. Hidaya aliendelea kuwaangalia wazazi wake huku akiwapungia mkono mpaka alipofikia sasa hawaoni tena kisha alikaa kwenye kiti. Hidaya ambaye hajawahi kukaa mbali na wazazi wake kwa kipindi kisichozidi mwezi mmoja. Hajawahi kusoma shule ya bweni, alijikuta akibeba mzigo wa maswali mengi kichwani. Alijiuliza atafikaje shuleni kwake Tabora, sehemu yenyewe hajawahi kufika hata siku moja. Na sasa atafika hapo Tabora usiku. Alijiuliza vipi ataanza maisha mapya ya bweni akiishi na watu wenye tabia na mienendo tofuati na ule aliolelewa. Ni hali gani waliyobaki nayo wazazi wake na wadogo zake ambao yeye ndiye alikuwa muangalizi pale nyumbani. Alijikuta akibubujikwa na machozi hasa alipowafikiria wadogo zako. Baaada ya mwendo mrefu wa takribani masaa ishirini na nane, Hidaya alifika mwisho wa safari yake ambayo ilikuwa Tabora. Swali ilikuwa ni jinsi gani atafika shuleni. Aliinua mfuko wake na kushuka chini. Baada ya kutembea hatua kadhaa, alisikia sauti ikiita kupitia kipaza sauti "wanafunzi wote wa Tabora Girls mnaombwa kuja hapa ili muelekezwe la kufanya" alinadi mtu mmoja aliyesimama sehemu iliyojitenga. Hidaya bila kusita, alienda eneo alilosimama mtangazaji. Alielekezwa gari ambalo alitakiwa kupanda. Moja kwa moja aliingia ndani ya gari hilo. Alikuta tayari kuna wanafunzi wachache wameisha panda na kukaa. Hidaya nae alichagua kiti na kukaa. Hakuna aliyemfahamu Hidaya wala Hidaya hakumfahamu yeyote. Wanafunzi wengine waliendelea kuingia ndani ya gari. Baadhi ya wanafunzi walionekana kufuhamiana kabla. Walikumbatiana kwa furaha walipoonana. Baada ya takriban dakika ishirini au nusu saa, gari liliondoka kuelekea shuleni Tabora girls. Walifika shuleni usiku ule na kupokelewa vizuri. Kila mmoja alionyeshwa sehemu yake ya kutunza vitu vyake na shemu ya kulala. Asubuhi ya siku iliyofuata walipewa maelekezo mbalimbali yahusuyo taratibu za maisha na masomo pale shuleni. Baada ya hapo masomo yalianza kama kawaida. Hidaya alipangiwa kusoma uchumi, jiongrafia na Hesabu (EGM) masomo ambayo aliyapenda mno. Siku, wiki, miezi, mwaka hatimaye ilipita huku ikipunguzwa makali na likizo alizopewa kila mwisho wa muhula. Sasa Hidaya alitakiwa kuukabili mtihani wa kidato cha sita. Hidaya ambaye katu hakuutunuku usingizi wala kujihusisha na mambo ya anasa. Alijisomea kwa bidii sana, bila kujali kejeli na majina aliyopewa. Wapo waliomwita "msongo" wengine wakadai "katumwa na kijiji" ili mradi kila mtu alitafuta namna ya kumuathiri kisaikolojia ili apunguze muda wa kusoma. Hidaya kwa kuzingatia hali ngumu aliyoiacha nyumbani, alijisemea moyoni "bora lawama kuliko fedheha". "Hapa nilikuja peke yangu na nitaondoka peke yangu." Tarehe ya mtihani ilifika na Hidaya akawa miongoni mwa watahiniwa. Alifanya mitihani kwa kujiamini huku akitegemea msaada wa Mwenyezi Mungu. Baada ya mitihani kumalizika, shule iliwaandalia sherehe ya kuwaaga ambayo mbali ya vyakula na vinywaji, pia liliandaliwa disko ambapo wavulana na wa Mirambo Sekondari, Kazima na Tabora wavulana nao walihudhuria katika ukumbi wa mziki. Baada ya chakula "maalumu" cha siku hiyo kwa waagwa, Hidaya aliingia maliwatoni na kuoga vizuri kisha alirejea chumbani. Alikaa na kuzungumza na wenzake na kupeana anuani. Hidaya ambaye kwao hawana sanduku la posta, aliwapa anuani kupitia kwa Mzee Faida. Ilipofika muda wa kuelekea kwenye ukumbi wa mziki, Hidaya aliona hili kwake linakwenda kinyume na maadili aliyolelewa, aliamua kujilaza kitandani na kujisomea kitabu cha hadithi ili kujiongezea maarifa. Wenzake walimsihi wajumuike pamoja, japo asicheze aingia akae tu pembeni lakini alikataa. Wapo waliomcheka kwa kumuona mshamba lakini Hidaya hakujali. Aliamua "kutia pamba masikio." Siku iliyofuata wanafaunzi walibebwa kwenye gari la shule kupelekwa kwenye kituo cha gari moshi tayari kwa safari kurejea makwao. Walipanda gari moshi na safari ya kurejea Dar es Salaam ilianza. Hidaya alikuwa na hamu na furaha kukutana na wazazi wake nyumbani akiwa amemaliza masomo salama pale shuleni. Shule ya kijeshi, kila jambo lilipelekwa kijeshi. Kitu ambacho kilimfanya Hidaya kuwa mkakamavu. Waliwasili Dar es Salaam yapata saa nne asubuhi, Hidaya aliagana na wenzake na kupanda daladala ziendazo Ubungo na kutelemkia Manzese. Alitembea kwa miguu kitambo cha takriban daika arobaini na tano au hamsini, akawasili kwa wazazi wake walikuwa hapo nyumbani saa ile. Hidaya alipumzika kwa msaa machache kabala ya kuanza kushughulika na kazi za pale nyumbani. Saa nane mchana wazazi wa Hidaya karibu wote walikuwa wamerudi nyumbani ili kujipatia chakula cha mchana. Walifurahi sana kumkuta Hidaya nyumbani. Walimpongeza kwa kumaliza masomo na kurejea nyumbani salama. Baada ya chakula, waliendelea kuzungumza hili na lile kwa furha. Jioni ile Hidaya alimchukua mdogowake wa mwisho Ayub na kuelekea naye kwa Mzee Faida kuwasabahi. Alifika kwa Mzee Faida yapata saa kumi na moja na robo. Alipokewa na Mama Rashid aliyekuwa akifuma shuka ukumbini "karibu mwanangu Hidaya karibu sana kipenzi changu" alisikika Mama Rashid akimkaribisha Hidaya kwa sauti iliyojua upendo. Aliinuka na kumkumbatia kisha kumkaribisha kwenye jamvi zuri la maua. Aliinuka na kuelekea mekoni, na huko alitoka na bilauri iliyojaa maziwa na kumkaribisha. Hidaya alipokea maziwa yale na kushukuru. Alikunywa maziwa yale taratibu huku wakizungumza. Mazungumzo yao yalichukua takriban masaa mawili Hidaya aliaga na huku Mama Rashid akiomba siku ile Hidaya alale pale nyumbani. Hidaya alishauri ombi hilo lipelekwe kwa wazazi wake kwa kuwa yeye bado ni mgeni na ni mtoto anapewa uangalizi wa wazazi wake. |
YALIYOMO
Tahariri:
‘CUF tumejiandaa kuchukua serikali' Suala la Mwembechai lazua mtafaruku Mabadiliko ya katiba ya Zanzibar: CCM Z'bar ina nafasi ya ushindi MPASHO
NASAHA
Habari
za ndani
Ushauri
Nasaha
MAKALA
WAZO
LA WIKI
Makala
ya Kimataifa
Kalamu
ya Mwandishi
MAKALA
LISHE
|
|
|
|
|