NASAHA
Na. 036 Jumatano Februari 23 - 29, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MICHEZO
 
 

BAADA YA KUFUNGIWA KUCHEZA SOKA
Makoye, Mapunda wateta Dar

  • Mapunda asema huenda Makoye 'akachomoa'
  • Azzan asema Tauzany kujinga na kambi ya Simba wiki ijayo
Na Hamis Kasabe

WASHAMBULIAJI wa Kimataifa wa Tanzania Ephraim Makoye na Steven Mapunda 'Garincha' waliotangazwa kufungiwa kucheza soka kwa mwaka mmoja na chama cha soka nchini (FAT) wamekutana jijini na kufanya mazungomzo yasiyo rasmi.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana Jijini na kuthibitishwa na mmoja wa wachezaji wa klabu ya Yanga, ajenda kubwa katika mazungumzo hayo ilikuwa jinsi ya kukabiliana na adhabu waliyopewa.

Mchezaji huyo ambaye hakutaka jina lake lianikwe gazetini kwa sababu si msemaji wa Makoye wala Mapunda, alisema kuwa Mapunda alimuomba ushauri Makoye nini afanye wakati akitumikia kifungo.

"Makoye alimwambia kwamba kitu cha msingi anachotakiwa kufanya sasa hivi ni kuendelea kufanya mazoezi kwa kujituma zaidi ili kiwango cha uchezaji kisishuke", ameeleza mpashaji huyo.

Katika mazungumzo hayo, mpashaji wetu amethitibisha Makoye alimuhakikishia Mapunda kuwa hakusaini kabisa fomu za usajili wa klabu ya Simba zaidi ya kujaza mkataba wa klabu hiyo.

Hata hivyo, imedaiwa kuwa Makoye alipatwa na kigugumizi cha ukubwani baada ya Mapunda kumuuliza kwamba alijaza mkataba wa Simba ili aifanyie nini klabu hiyo kama si kuichezea.

Katika maongezi ya wanandinga hao, habari zaidi zimedai Mapunda alitamka kuwa huenda Makoye akafunguliwa kama anachodai ni sahihi.

Kwa mujibu wa FAT, Mapunda na Makoye wamefungiwa baada ya kubainika kujisajili Yanga na Simba katika msimu mmoja wa ligi.

Naye kocha mkuu wa klabu ya Simba, Nzoyisaba Tauzany amesema ana hakika Mapunda atafunguliwa na kuchezea Simba katika kikao kijacho baina ya vilabu vya Ligi Kuu na FAT.

Wakati huo huo mwandishi wetu wa Morogoro RAJABU RAJABU anaripoti kuwa, klabu ya Simba ya jijini iliyopo Morogoro inatarajiwa kuondoka mjini hapa keshokutwa kuelekea Arusha kwa ajili ya mechi za kirafiki.

Hata hivyo, meneja wa klabu hiyo Idd Azzan hakuzitaja timu watakazopambana nazo kwa madai kuwa hazijafahamika.

Aidha, Azzan amewalaumu viongozi wa klabu yake kwa kuzembea kumtafutia kocha wa klabu hiyo Tauzany kibali cha kufanyia kazi wakati walijua mapema kuwa kimekwisha.

Azzan amewatoa wasiwasi wanachama na wapenzi wa Simba kuhusu hatima ya kocha wao kwa madai kuwa mipango inafanywa ili wiki ijayo ajiunge na wachezaji.


Tino, Katolila, Omar 'wautwaa' ukocha
  • Wapania kuinua kiwango cha soka nchini
Na Mwandishi Wetu

WASHAMBULIAJI wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Peter Tino, Ally Katolila na Omar Hussein "Keagan" ni miongoni mwa wachezaji 25 wa zamani wanaochukua mafunzo ya ukocha.

Wakufunzi hao wako chini ya Mkufunzi na Katibu Mkuu wa chama cha makocha nchini Idd Machupa kwa kozi ya awali ya ukocha itakayowachukua mwezi mmoja kuhitimu.

Wakiongea na mwandishi wa habari hizi jana Jijini katika uwanja wa Karume, wachezaji hao wameahidi kutumia taaluma yao kuinua kiwango cha soka nchini.

"Unajua nilipokuwa mchezaji nilililetea sifa kubwa Taifa hili na kila mmoja anajua, sasa nataka pia nilitumikie taifa hili kama kocha", alisema Tino.

"Kwa kuwa mimi nilifundishwa nikawa mchezaji mzuri, nataka sasa nirithishe kipaji changu kwa vijana wa sasa kupitia taaluma hii ili wacheze kama mimi na ikibidi zaidi yangu", Katolila aliliambia NASAHA.

Kwa upande wake, Omar Hussein amesema soka ya Tanzania imeporomoka kutokana na kufundishwa na watu wengi ambao hawakucheza kabisa mpira zaidi ya kuwa watazamaji.

"Kwa hiyo naamini kabisa baada ya sisi kuhitimu soka ya Tanzania itapata mabadiliko kwa sababu itafundishwa na watu ambao wanafahamu mazingira ya mchezo Practically", ameongeza.

Baadhi ya wachezaji wengine wanaoshiriki kozi hiyo ni Adolf Rishard, Mbwana Makata, Muhidin Sisso na James Kisaka.


Tuna mashaka na Shungu - Yanga



Na Mwandishi Wetu

WANACHAMA na wapenzi wa klabu ya Yanga ya Tanzania wamesema kwamba wana mashaka na kauli ya kocha mkuu wa klabu hiyo Roul Shungu kwamba wachezaji wa Yanga waliokuwa nje ya nchi viwango vyao vimeshuka.

Akinukuliwa na vyombo vya habari nchini, Shungu alisema viwango hivyo vimeshuka kutokana na kutofanya mazoezi na kucheza mechi mara kwa mara.

Wachezaji waliolengwa katika kauli ya Shungu ni Edibily Lunyamila, Ephraim Makoye na Ally Mayai Tembele waliokuwa nchini Chile.

Wengine ni Mohammed Hussein Daima na Idd "Mnyamwezi" Moshi ambao walikuwa nchi za Falme ya Kiarabu.

Wakiongea kwa nyakati tofauti na NASAHA katika makao makuu ya klabu yao mtaa wa Jangwani na Twiga Jijini, wakereketwa hao wamesema bado viwango vya wachezaji hao ni vizuri kama wakati wanaondoka.

"Mimi nina wasiwasi kwamba kauli ya Shungu ililenga kuwafanya kina Lunyamila kuongeza juhudi ya mazoezi lakini kwa viwango vyao badso ni vizuri", amesema mwanachama Selemani Kato, kadi namba 0445.

Kato ameungwa mkono na shabiki Iddi Mipata wa Jijini, lakini akaongeza kwamba matamshi ya Shungu yanamtia mashaka kwani yanaweza kuvunja moyo wachezaji.

Juu

YALIYOMO
 

Tahariri:
Katiba ya Zanzibar ni ya Wazanzibari

‘CUF tumejiandaa kuchukua serikali'

Suala la Mwembechai lazua mtafaruku

Mabadiliko ya katiba ya Zanzibar: CCM Z'bar ina nafasi ya ushindi

MPASHO NASAHA
Ulimbukeni wa siku ya Valentino

Habari za ndani
NCCR-Mageuzi wamkataa Msimamizi wa Uchaguzi

Ushauri Nasaha
Nafasi ya familia katika makuzi ya mtoto

MAKALA
CCM imepindua nini?

WAZO  LA  WIKI
Vitisho vya kikachero visihamishiwe mashuleni

Makala ya Kimataifa
Mtazamo wa maadui wa Uislamu juu ya Uislamu

Kalamu ya Mwandishi
Katiba irekebishwe, lakini kwa maslahi ya wananchi

MAKALA
MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA  JAMHURI YA MUUNGANO -2
Vita dhidi ya demokra

HABARI ZA KIMATAIFA

  • Clinton kusaidia  amani Burundi
  • Nigeria yaazimia kuwa taifa la Kiislamu
  • n.k

  • Riwaya 
    Ndoto ya mafanikio - 2

    LISHE 
    Madhara ya mafuta mwilini

    Barua/Maoni

    MASHAIRI

    MICHEZO

  • Makoye, Mapunda wateta Dar 
  • Tino, Katolila, Omar 'wautwaa' ukocha 
  • Tuna mashaka na Shungu - Yanga

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita