NASAHA
Na. 036 Jumatano Februari 23 - 29, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Kalamu ya Mwandishi
 
 

Katiba irekebishwe, lakini kwa maslahi ya wananchi





NA MAALIM BASSALEH 

MSAHAFUNI maneno ya Mungu, hayabadilishwi na wala hayafutwi. Ndani ya msahafu mna sheria na amri ambazo Mungu amewapangia wanadamu wazifuate. Muumini wa dini hutakiwa ayafuate yaliyomo katika msahafu wa dini husika bila ya kupunguza au kuongeza chochote. Kuongeza au kupunguza neno katika msahafu ni mwiko na ni dhambi isiyosameheka.

Kwa upande mwingine, katiba ya nchi huitwa sheria mama, kwa maana ya kwamba sheria zote zinazotungwa hutokana ndani ya katiba hiyo. Sheria yoyote itakayotungwa, lakini ikaenda kinyume na katiba ya nchi, huhesabiwa kuwa ni batili. Lakini hiyo haimaanishi kuwa katiba nayo ni kama msahafu, yaani yaliyomo katika katiba hayabadiliki. 

Katiba inaweza kubadilishwa, au inapobidi, hata kufutwa kabisa na kuandikwa nyingine mpya itakayokidhi matakwa ya wananchi kwa mujibu wa mazingira na zama zinazohusika. 

Mara nyingi tumekuwa tukiwasikia wanasheria pamoja na wanasiasa wakisema kuwa katiba si msahafu! Na hilo nikweli. 

Msahafu ni matakwa ya Mungu kwa wanadamu. Mungu akiwa ndiye Muumba anayajua yale yote yenye manufaa na madhara kwa viumbe wake. Ndiyo akawapangia sheria na desturi ili wazifuate wapate mafanikio katika maisha yao ya hapa duniani na kesho akhera. 

Kama Mungu, katika msahafu, alimkataza mwanadamu asilewe, asizini au asiibe, basi makatazo hayo yatamhusu kila binadamu, popote alipo, na katika zama zozote ziwazo. Mwanadamu atakayejaribu kubadilisha maneno hayo ya msahafu na kutenda yale yaliyokatazwa na Mungu basi kwanza ataidhuru nafsi yake kabla hajapata laana na adhabu kutoka kwa Mola wake. Kwa hivyo, msahafu hauna sababu ya kutaka kubadilishwa. Msahafu unaobadilishwa badilishwa hupoteza ile sifa yake ya kuwa ni neno la Mungu! 

Lakini katiba, kwa vile si neneo la Mungu, hubadilishwa, kila pale inapotokea haja ya kufanya hivyo. Katiba ni matakwa ya wanadamu wenyewe. Katiba ya nchi ni matakwa yaraia kwa serikali yao, juu ya jinsi vile wanavyotaka serikali hiyo iendeshe utawala wake. Ndiyo maana wanasheria wakasema, "Katiba ya nchi ni mkataba baina ya watawaliwa, yaani raia, na watawala, yaani serikali, namna vile raia hao wanavyotaka watawaliwe na hiyo serikali yao." 

Tukiyazingatia maneno hayo tutaona kuwa wanasheria wanataka kutwambia kuwa katiba ya nchi yoyote, ni lazima itokane na matakwa ya wananchi wenyewe, siyo na serikali. Serikali hubidi kufuata vile wananchi wanavyotaka. Kwa maana nyingine, ingawa katiba inaweza kufanyiwa marekebisho, lakini kama serikali ina nia ya kufanya hivyo, inabidi isikilize na kuyatilia maanani,maoni ya raia wake wote; na siyo baadhi tu ya raia, au wanachama wa chama tawala tu. 

Nchi nyingi za Kiafrika, yaonekana, haziijali kanuni hii. Mara nyingi serikali zilizo madarakani, katika nchi kama hizo, huiteka nyara katiba ya nchi na kuifanya ni mali yao. Wengine wote huwa hawana hakinayo. Serikali za aina hiyo huwa hazijali kabisa matakwa au maslahi ya wananchi. Zinajali maslahi ya wale waliopo madarakani. 

Pale serikali inapoona inamaslahi huwa iko tayari kurekebisha katiba; lakini pale inapoona kifungu au ibara inayotaka kubadilishwa itaibana serikali basi, mara nyingi, serikali huwa haiko tayari kukifanyia marekebisho kifungu kama hicho. 

Viongozi wengi wa serikali za Kiafrika wanapokuwapo madarakani huwa hawashughulishwi zaidi na maendeleo ya nchi zao au uhuru wa raia zao bali hushughulishwa na kutafuta mbinu mpya za kuendeleza tawala zao. Haidhuru uchumi wa nchi uanguke na maendeleo ya watu wake yadumae, madamu yeye kiongozi atabaki madarakani, basi kwake hayo, yanatosha kuwa ndiyo mafanikio ya utawala wake. 

Na wapinzani nao,inaonekana linalowashughulisha zaidi ni lile la kutafuta njia ya kuingia Ikulu. Hawaoni sababu ya kuungana pamoja na kuiangalia katiba iliyopo hivi sasa inavyowakwamisha katika juhudi zao hizo. 

CUF, Zanzibar,ilikubali kuingia katika uchaguzi mkuu wa 1995 huku ikijua kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ndiyo yenye kauli ya mwisho katika kutangaza matokeo ya uchaguzi. Katiba ndivyo inavyoeleza. Tume ikisha tangaza jina la mshindi, mgombea aliyeshinda hata kama hakuridhika na matokeo hayo hataweza kulalamika pahali po pote. Mgombea anayeikubali ibara hiyo ni sawa na aliyekubali kujitia kitanzi mwenyewe. 

Wapinzani wa bara nao walikubali kuingia katika uchaguzi mkuu wa 19995 hali wakielewa kuwa katiba inasema kuwa Tume ya uchaguzi itateuliwa na Rais ambaye yeye mwenyewe ni miongoni mwa wagombea katika uchaguzi huo huo. Halafu baada ya uchaguzi wanakuja kulalamika kuwa Tume ya uchaguzi imekipendelea chama tawala. Wao walitarajia nini? Walitaka tume iliyoteuliwa na chama tawala iwapendelee wao? 

Ilikuwa ni wajibu wa vyama vya upinzani kushikamana na kudai kuandikwa katiba mpya inayolingana na mfumo mzima wa vyama vingi. Na hata kama hilo lisinge wezekana basi wangali ishinikiza serikali angalau ikavifuata vile vipengele viwili kile kinachoipa Tume ya uchaguzi ya Zanzibar mamlaka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi bila ya kuhojiwa na yeyote. Na kile kipengele kinachompa Rais uwezo wa kuteua Tume ya uchaguzi, pekeyake, bila ya kuingiliwa na yeyote. 

Hata hili jambo la wabunge wa chama kimoja, kiwe ni chama tawala au chama cha upinzani, kila wakati kuingia bungeni, wakiwa na msimamo mmoja wakati wa kujadili hoja fulani si kitendo cha kukuza demokrasia. Kwa vyovyote ni jambo lenye kumpunguzia mbunge uhuru wa kutoa maamuzi ambayo anaamini ndiyo yangalipendelewa na wale waliompigia kura na kamchagua. 

Si kila wakati wabunge wa chama tawala wanapotakiwa waiunge hoja inayotolewa na serikali kwa sababu tu hoja hiyo imetoka chama chao. Ni wajibu wa wabunge kukitazama kwa makini kila kipengele kinachotaka kujadiliwa, iwe kwa kutaka kufutwa au kuongezwa kingine kipya. Jee! Kipengele kama hicho kina manufaa au madhara gani na wananchi? 

Wabunge wasikubali kabisa kuiunga mkono hoja yoyote inayowapungizia uhuru wao raia, au inayoididimiza demokrasia katika nchi. Kwa mfano mbunge anapoiunga mkono hoja inayompa Rais uwezo wa kumweka raia yeyote ndani, bila ya kuhojiwa na chombo cho chote kile, haoni kuwa badala ya kumsaidia raia yeye anamwingiza katika matatizo? 

Ni kweli kuwa wanaweza kutokea wakorofi wanaotaka kuchafua amani ya nchi ambao inabidi wadhibitiwe. Lakini hilo lisiwe ndiyo sababu ya kuwapunguzia raia uhuru wao wa kusema au kuibana demokrasia nchini. Rais, kwa vyovyote, ni binadamu anaweza kukosea au hata kumchukia mtu, hasa mpinzani wake, akautumia mwanya huo kumweka kizuizini mtu asiyekuwa na hatia yoyote, isipokuwa kutofautiana na mawazo ya Rais kama huyo.

Kama hivi sasa bado hatujapata Rais mwenye kutumia madaraka yake vibaya kuna siku tunaweza kuwa naye Rais kama huyo. Kwa hivyo hao hao wanaoiunga mkono hoja hiyo ya kutaka Rais apewe mamlaka ya kumweka raia yeyote anayehisi ni mkorofi kizuizini, si ajabu siku moja wakajikuta wao wenyewe ndio waliowekwa kizuizini, si kwa jambo jingine lo lote, bali kwa kutokubaliana na rai ya Rais huyo. 

Katika nchi moja ya Kiafrika, iliyo jirani na sisi jambo kama hilo lilikwishatokea. Rais wa nchi hiyo alitaka apewe mamlaka ya kuwaweka kizuizini raia anaowahisi kuwa ni wakorofi bila ya kufikishwa mbele yavyombo vyasheria. Waziri mmoja, wakati huo akiwa na uhusiano mzuri na Rais huyo aliipigia sana debe hoja hiyo mpaka ikapitishwa bungeni na kuwa ni sheria. 

Baadaye waziri huyo, alikuja kukosana na Rais wake huyo ikambidi aikimbie nchi kwa kuiogopa sheria ile ile aliyoipigia debe yeye mwenyewe. Baada ya kupita muda akasikia kuwa mambo yameanza kubadilika katika nchi yake. Watu wameanza kujitokeza na kudai haki zao waziwazi. Akaona bora na yeye arudi nchini kwake. 

Masikini roho yake, alisahau ile sheria aliyosaidia mwenyewe kuitunga. Alipofika huko Rais aliamrisha akamatwe na kuwekwa kizuizini. Waziri huyo alifia huko huko gerezani. Ni sheria ile ile aliyosaidia kuipitisha bungeni ndiyo iliyokuja kuyadhulumu maisha yake! 

Pili, ikiwa serikali imekubali kuanzisha mfumo wa vyama vingi ili kukuza demokrasia katika nchi, vipi wabunge wanao amini juu ya demokrasia wakubali kumpa uwezo Rais kuteuwa wabunge kumi wasiochaguliwa na wananchi? Kama kuna ulazima wa kufanya hivyo basi angalipewa uwezo wa kuteua mbunge mmoja, au wawili au hata watatu. Lakini kumi! Masalale! Jee! Hilo linaikuza demokrasia au linaidumaza? 

Mwisho, hivi juzi tumeshuhudia mvutano baina ya wabunge wa chama tawala na wale wa vyama vya upinzani juu ya kifungu kipi kitumike katika kupitisha marekebisho ya 13 yakatiba. Vifungu viko viwili, nambari 91(a) na nambari 91(b). 

Kifungu kimoja kinatamka kuwa ili marekebisho ya katiba ya Jamhuri ya Muungano yapite lazima yakubaliwe na theluthi mbili ya wabunge wa Bara na pia, theluthi mbili ya wabunge wa Zanzibar. Na kile kifungu cha pili kinasema kuwa katiba inaweza kubadilishwa kwa kupata ridhaa yatheluthi mbili ya wabunge wote. 

Bila ya shaka yoyote vifungu hivyo viwili vyenye kupinzana vimeiletea utata katiba. Haiyumkiniki vifungu vyote hivyo viwili vikawamo katika katiba moja. Lakini badala ya wabunge wote wa Zanzibar wa CCM na CUF, kushirikiana kwa pamoja na kutangaza kuwa katiba ya Muungano ina utata, wakaomba wapewe ufafanuzi. Wabunge wa CCM Zanzibar walishirikiana na wabunge wanzao wa CCM-Bara na kuyapitisha marekebisho hayo ya 13 ya katiba. 

Baadaye tutakuja kusikia wana-CCM Zanzibar wakilalamika kuwa Zanzibar inaburuzwa na Bara! Lakini wanaotoa kibali hicho cha kuburuzwa ni nani? Hivyo hawaelewi kuwa kwa kukiafiki kile kifungu kinachotaka marekebisho ya katiba ya Muungano yapitishwe yanapoungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wanainyima kauli Zanzibar? 

Kwa kutumia kipengele hicho, wabunge wa Zanzibar, wanadhani lini wataweza kupinga mabadiliko yoyote wanayohisi yatawakandamiza Wazanzibari! Kwa hivyo wakati wa kutaka kuifanyia marekebisho katiba jambo kubwa la kuzingatia ni maslahi ya wananchi na siyo maslahi ya chama cho chote cha siasa! 

Juu

YALIYOMO
 

Tahariri:
Katiba ya Zanzibar ni ya Wazanzibari

‘CUF tumejiandaa kuchukua serikali'

Suala la Mwembechai lazua mtafaruku

Mabadiliko ya katiba ya Zanzibar: CCM Z'bar ina nafasi ya ushindi

MPASHO NASAHA
Ulimbukeni wa siku ya Valentino

Habari za ndani
NCCR-Mageuzi wamkataa Msimamizi wa Uchaguzi

Ushauri Nasaha
Nafasi ya familia katika makuzi ya mtoto

MAKALA
CCM imepindua nini?

WAZO  LA  WIKI
Vitisho vya kikachero visihamishiwe mashuleni

Makala ya Kimataifa
Mtazamo wa maadui wa Uislamu juu ya Uislamu

Kalamu ya Mwandishi
Katiba irekebishwe, lakini kwa maslahi ya wananchi

MAKALA
MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA  JAMHURI YA MUUNGANO -2
Vita dhidi ya demokra

HABARI ZA KIMATAIFA

  • Clinton kusaidia  amani Burundi
  • Nigeria yaazimia kuwa taifa la Kiislamu
  • n.k

  • Riwaya 
    Ndoto ya mafanikio - 2

    LISHE
    Madhara ya mafuta mwilini

    Barua/Maoni

    MASHAIRI

    MICHEZO

  • Makoye, Mapunda wateta Dar 
  • Tino, Katolila, Omar 'wautwaa' ukocha 
  • Tuna mashaka na Shungu - Yanga

  •  

     
     
     

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita