NASAHA
Na. 036 Jumatano Februari 23 - 29, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA
 
 

MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO -2

Vita dhidi ya demokrasia 

KINYUME na matarajio ya wananchi walio wengi, marekebisho ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yamedhihirisha tena yale madai ya wananchi kwamba Chama Cha Mapinduzi na serikali yake, wamedhamiria kutokuheshimu matakwa ya wananchi katika kuilea na hatimae kuikuza demokrasia ya kweli nchini.

TUNAENDELEZA madai haya, kwa sababu, katiba ndio dira na pia ndio sheria kuu ya nchi, kwa mantiki hiyo, kigezo cha kwanza cha kuonesha kama kweli nchi ina muelekeo wa kidemokrasia ni kuonekana kwa misingi ya demokrasia ndani ya katiba ya nchi. 

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haina sifa tuliyotaja. 

Wananchi wengi walitegemea kuona mabadiliko yenye manufaa kwa taifa katika muswada huu wa marekebisho ya 13, hasa tukizingatia kwamba uchaguzi mkuu wa pili wa vyama vingi vya siasa nchini umekaribia. 

Mambo yamekuwa ni kinyume chake, sote tumeshuhudia jinsi serikali ilivyowakokota wananchi kwa kusaidiwa na wabunge wake kuendeleza ule utamaduni waliourithi kutoka katika utawala wa Awamu ya Kwanza wa kulitumia Bunge kama chombo tu cha kuhalalisha yaliyokwisha kuamuliwa na serikali na kwa hivyo kuwatumia wananchi kama ngazi tu ya kufikiria malengo yao ya kisiasa. 

Masuala ya msingi, ambayo wananchi walitegemea kwamba yangeshughulikiwa kama vile, Tume huru ya Uchaguzi. Kupunguzwa kwa madaraka ya Rais suala linalohusu uwakilishi wa uwiano ndani ya bunge na kuundwa kwa Tume ya Haki za Binaadamu na utawala bora iliyo huru na yenye madaraka ya kufanya kazizake bila ya vikwazo au kuingiliwa yakiwa ndio misingi ya demokrasia ndani ya katiba yameachwa bila ya kutolewa maelezo ya kuridhisha. 

Katika marekebisho hayo ya 13, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepewa madaraka makubwa mno dhidi ya Tume ya Hak za Binaadamu na Utawala bora. 

Katika muswada huo, Rais amepewa uwezo wa kuiagiza tume au kuizuia tume isifanye uchunguzi, hii ni pamoja na kupewa madaraka ya kuteua makamishna wote, badala ya Bunge. 

Katika Ibara ya 130 (4) ya muswada huo, Rais amepewa uwezo wa kumwachisha kazi kamishna wa Tume hiyo kwa sababu yoyote ile. 

Madaraka haya ni kinyume kabisa na utawala wa kidemokrasia, hasa tukizingatia kwamba sababu za kumuwezesha Rai skumfukuza kazi Kamishna wa Tume hazikuainishwa. 

Katika muswada huo, Ibara ya 129 (4) inaeleza kwamba tume haitakuwa na uwezo wa kufanya uchunguzi dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kiongozi wa serikali ya Zanzibar. 

Kinachowatia wasiwasi wananchi wengini hii tabia ya viongozi wa ngaziza juu kujiwekea kinga dhidi ya kuchunguzwa hata kabla hawajatenda makosa yenyewe. 

Kwa ujumla Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala bora inayokusudiwa kuundwa nchini itakuwa tofauti kabisa na tume za aina hiyo katika nchi nyingine duniani mambo mengi yanayohusu haki za Binaadamu hayamo. 

Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imeamua kuendeleza dhana iliyotolewa na Mheshimiwa Rashid Kawawa wakati akiwa Waziri Mkuu mwaka 1962 pale aliposema "Muswada wa Haki za Binaadamu utakaribisha madai ya mambo ya anasa ambayo kamwe hatutaweza kuyavumilia." 

Huu ndio msimamo ambao baadae ulikuja kuhalalisha mfumo wa chama kimoja cha siasa nchini na baadae chama kushika hatamu. 

Mfumo ambao ulivigeuza vyombo vyote vya dola yaani bunge, serikali na mahakama kuwa mateka wa fikra za mwenyekiti wa chama ambaye pia katika mfumo huo anakuwa ndiye Rais wa nchi. 

Kwa lengo la kuendelea kushika hatamu, serikali ya Chama Cha Mapinduzi ilikubali kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, bila ya kuweka ratiba ya kufanya mabadiliko ya msingi katika uwanja wa kisiasa kwa lengo la kuondoa athari za ukiritimba uliokithiri ndani ya vyombo vya dola uliokuwa unastawishwa na mfumo wa chama kimoja cha siasa. 

Nchi ikaingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, huku viongozi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi wamepania kuhakikisha kwamba vyama vya upinzani havifanikiwi katika dhamira yao ya kuwaondoa madarakani. 

Haya madai tunayoyasikia kuwa vyama vya upinzani vinawagawa wananchi katika makundi ya kikabila na wakati mwingine makundi ya kidini ni mbimu tu inayotumiwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na vibaraka wao waliopandikizwa katika vyama fulani fulani kwa lengo la kuchafua mawazo ya wananchi. 

Lengo jingine ni kuwagawa na pia kuwatisha wananchi wasiviunge mkono vyama hivyo ili wavidhoofishe visipate nguvu na hatimaye kuwang'oa madarakani. 

Mbinu nyingine inayotumiwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzina serikali yake ni kwa viongozi hao kupanda majukwaani na kudai kwamba wapinzani wote kwa ujumla wao ni watu wenye uchu wa madaraka tu na kwamba wakipata nafasi ya kushika nafasi ya kuongoza nchi hawawezi kuleta mabadiliko yoyote. 

Haya ni madai ya uongo yasiyo na ushahidi, ambayo kwa kweli yamekusudiwa kuwalaghai wananchi. 

Tunasema hivi kwa sababu sote tunakubaliana kwamba hakuna mwanaadamu yoyote, kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi au serikali yake ambaye anaweza kututhibitishia kwamba yeye anao uwezo wa kupiga ramli ya kufahamu mambo yatakayotokea siku za usoni, huu utabiri wanaotoa kuhusu uwezo wa viongozi wa vyama vya upinzani kutokuweza kuleta mabadiliko wanautoa wapi? 

Wananchi tusikubali kupumbazwa, wakati wa kupambanua mchele na chuya umekaribia, ni lazima sasa tuwe macho na ambao bado wanadhani kuwa maneno yao ya kwenye majukwaa bado ni turufu tosha ya kuzoa kura za wananchi. 

Uwezo wa Tanu na sasa Chama Cha Mapinduzi kuwaletea wananchi maendeleo tumeuona bayana na wala sio suala la utabiri wa sangoma (mganga wa kienyeji). 

Umaskini umekithiri, ujinga unaongezeka, na maradhi tele, hata yale yanayoweza kuzuilika kama kipindupindu na malaria, maradhi ambayo sote tunafahamu kuwa husababishwa na maji machafu yanayoegama na yale yanayonywewa na watu kwa sababu ya ukosefu wa maji safi na salama. 

Lawama wanazotoa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake kwamba matatizo hayo yanasababishwa kwa kiwango kikubwa na wananchi wenyewe, si ya kweli. 

Kwa sababu hiyo kukusanya kodi mbali mbali kutoka kwa wananchi, ni wajibu na ni jukumu la serikali kutoa huduma zote muhimu za jamii, kuhakikisha usafi wa mazingira pamoja na kuhakikisha kunakuwepo na urahisi wa kupatikana kwa madawa ya kutosha pale inapotokea dharura ya magongwa ya kulipuka, ukiachilia mbali dharura ya njaa. 

Wananchi, kwa vile nchini mwetu tunatumia demokrasia ya uwakilishi kwa kuwachagua wabunge kama wawakilishi wetu, katika chombo cha kutunga sheria na kusimamia maendeleo na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma yaani Bunge, ni muhimu sana katika uchaguzi mkuu ujao tuwe makini na kuhakikisha kwamba tunachagua wabunge ambao watawakilisha matakwa yetu kweli, badala ya matakwa yao binafsi. 

Tunachohitaji kutoka kwa viongozi wa vyama vya upinzani ni orodha ya mambo waliyoyapata kipaumbele katika utekelezaji, kwa sababu ya umuhimu wake, waahidi kutekeleza tukiwapa kura zetu, ambayo na wao pia tutakuja kuwauliza baada ya miaka mitano, watakapokuja tena kutuomba kura. 

Huu ndio utakuwa utamaduni mpya wa wananchi maana sasa tumechoka na ahadi za kutapeli kura zetu. 

Juu

YALIYOMO
 

Tahariri:
Katiba ya Zanzibar ni ya Wazanzibari

‘CUF tumejiandaa kuchukua serikali'

Suala la Mwembechai lazua mtafaruku

Mabadiliko ya katiba ya Zanzibar: CCM Z'bar ina nafasi ya ushindi

MPASHO NASAHA
Ulimbukeni wa siku ya Valentino

Habari za ndani
NCCR-Mageuzi wamkataa Msimamizi wa Uchaguzi

Ushauri Nasaha
Nafasi ya familia katika makuzi ya mtoto

MAKALA
CCM imepindua nini?

WAZO  LA  WIKI
Vitisho vya kikachero visihamishiwe mashuleni

Makala ya Kimataifa
Mtazamo wa maadui wa Uislamu juu ya Uislamu

Kalamu ya Mwandishi
Katiba irekebishwe, lakini kwa maslahi ya wananchi

MAKALA
MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA  JAMHURI YA MUUNGANO -2
Vita dhidi ya demokra

HABARI ZA KIMATAIFA

  • Clinton kusaidia  amani Burundi
  • Nigeria yaazimia kuwa taifa la Kiislamu
  • n.k

  • Riwaya 
    Ndoto ya mafanikio - 2

    LISHE
    Madhara ya mafuta mwilini

    Barua/Maoni

    MASHAIRI

    MICHEZO

  • Makoye, Mapunda wateta Dar 
  • Tino, Katolila, Omar 'wautwaa' ukocha 
  • Tuna mashaka na Shungu - Yanga

  •  

     

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita