AN-NUUR 
Na.173 Rajab 1419, Oktoba 30 - Novemba 6, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Barua 

 

Kufuata mwongozo wa Allah tu, ndiyo tiba ya ukimwi 

Ndugu Mhariri 

UKIMWI limekuwa ni tatizo sugu ambalo kila kukicha linazungumziwa katika vyombo vya habari. Limekuwa likijadiliwa katika vipindi mbalimbali kama KULIKONI, Ukimwi na Jamii n.k. 

Wamekuwa wakihojiana na watu mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa shule za sekondari ili kutafuta ni njia gani zitumiwe ili kudhibiti hilo janga lisiendelee. Wakataja njia mbalimbali baadhi yake zikiwa ni kutumia uzazi wa mpango, kutumia kondomu na kuwa na mpenzi mmoja. 

Hebu tuangalie njia hizi kwa undani udhaifu wake tukianza na dai la kutumia uzazi wa mpango. Imedaiwa itumike hii ili kuwe na idadi sawa kati ya wanaume na wanawake kwa kutumia kiwango ambacho watakuwa wamekiweka wao bila kuzingatia kuwa Muumbaji ni sifa ya Allah (s.w.) peke yake. Je, ikitokea hao wazazi watoto wao wakawa ni wa jinsia moja au jinsia mmoka ikazidi nyingine ikarudi kama ilivyokuwa mwanzo wanawake ni wengi kuliko wanaume hapo tatizo hilo limetatuliwa ? 

Njia hii ya kutumia kondomu, wataalamu wanasema kuwa kuna vitundu ambavyo hivyo Virusi vya Ukimwi vinaweza kujipenyeza. Na kama utaendelea kuitumia kwa mrefu matokeo yake ni yapi ? Nadhani hao usalama ni mdogo mno, hivyo hatuwezi kuiamini sana tayari tumekuwa na wasiwasi. 

Na hii nyingine isemayo kuwa kila mtu awe na mpenzi mmoja. Hii ina maana kuwa ni mopenzi tu sio mke wala mme unaweza kuamua baadae kuwa naye au ukamwacha ukatafuta mwingine endapo uligundua kuwa tabia yake haifaai kukaa ndani akatulia yeye kila kukicha ni madisko tu watoto atawalea lini ! 

Na hili limejengwa kutokana na hoja isemayo haiwezekani mtu kukaa bila kufanya mapenzi. Sasa wewe uliyeamua kuoa au kuolewa ukamtafuta mwingine ukamuacha huyo wa kwanza uliyemtafuta si na yeye alikuwa na mpenzi wake; huoni kuwa hapo kumekuwa na mchanganyiko wa watu kama wanne. 

Na je, suala la mpenzi mmoja bado lipo ? Manake na huyo wa pili ni mpenzi wako vile vile. Hapo na rudi kwa Bi. Rahma Salum (AN-NUUR No. 169 Kwa nini iwe Boy friend na isiwe husband?) Manake ukishaoa unakuwa na uhakika kuwa huyo ni wa kwako tu tena wa uhakika hakuna mwingiliano na watu wengine. 

Mtu mwingine anaweza kuamua kila mwezi anabadilisha mpenzi ili mradi akiwa naye ni huyo mmoja tu. Manake hoja ni mpenzi mmoja kwa wakati mmoja, hivyo kwa mwaka wapenzi kumi na mbili. Vipi hapo ! 

Tatizo hili limekuwa sugu kutokana na kukiukwa maadili ya Allah (s.w.) anaposema kuwa ‘wala msikaribie zinaa’ natumai singesema haya akiwa anafahamu kuwa haiwezekani mtu kukaa bila kufanya mapenzi na wakati anasema tena ‘haikalifishi nafsi yoyte ile yaliyo sawa na uweza wake’. Kila gonjwa linatiba yake. Kwa asiyeoa au kuolewa awe ni mewnye kufunga (swaumu) na kumkaribia sana Mola wake atamjaalia Inshaallah, kuvaa mavazi ya stara, kujiepusha na michanganyiko isiyo ya lazima na wataalamu wanaongezea kwamba afanye mazoezi ya viungo vya mwili, aepuke picha za kimapenzi mfano EGOL – ITV, usisome Novel zinazohusiana na mapenzi, vile vile na gumzo za mambo ya mapenzi katika vikundi. 

Sio unashinda na mabinti walo uchi mbele yako, unaenda video za X kwenye michanganyiko ya watu halafu unasema haiwezekani kukaa bila kufanya mapenzi. Mnayataka wenyewe ! 

Inawezekana kukaa bila kufanya mapenzi tena sana endapo tutafuata maamrisho ya Allah (s.w.) ya kukatazana maovu na kuamrishana mema na hii ndio tiba pekee ya ukimwi. Kwa kufuata mwongozo wa Allah (s.w) nadhani licha ya kupunguza kasi ya uenezaji kama wanavyodai wao, Ukimwi utaisha kabisa. 

Aula Tinda, 
Dar es Salaam. 



Bakwata acheni vurugu 

Ndugu Mhariri 

Mimi binafsi ninapenda kutoa dukuduku langu katika gazeti letu la Kiislamu, dukuduku lenyewe ni kuhusu Waislamu wa Mtaa wa Bakwata Mlangarini Wilaya ya Arumeru kuhujumiwa haki yao ya uchaguzi. 

Hivi karibu kulifanyika uchaguzi wa viongozi wa Kiislamu kuanzia ngazi ya Sheikh wa Mtaa, Imamu wa Msikiti, Katibu wa Mtaa, na viongozi wengine, katika mtaa huu wa Mlangarini, lakini kufuatana na uchaguzi uliofanyika, ule uongozi wa nyuma kuanzia Sheikh wa Mtaa, pamoja na Imamu wa Msikiti hawakubahatika kuchaguliwa katika kipindi hiki, ila walichaguliwa viongozi wengine wa ngazi hizo. Sasa kufuatana na njama za uongozi wa Wilaya Bakwata Arumeru (Sheikh wa Wilaya pamoja na katibu wake, pamoja na huo uongozi uliomwagwa, walikutana wakauvunja ule uongozi wote uliochaguliwa na Waislamu wa Mtaa wa Mlangarini, BAKWATA. Katika uchaguzi huo hapajavunjwa kanuni yeyote ya katiba, hivyo Waislamu wa Mlangarini wamepatwa na mshangao mkubwa. 

Hivyo nasaha zangu ni kwamba, inatakiwa uongozi wa Kiislamu Wilaya ya Arumeru utoe uamuzi wa vitabu sio wa vichwa vyao. Uongozi wa Bakwata Wilaya ya Arumeru bado unayumbayumba. 

Ustadh Adamu Ramadhani, 
S.L.Posta, 
MLANGARINI, 
ARUSHA. 


Ujenzi wa shule ya sekondari Maere – Tanga 

Ndugu Mhariri 

KWANZA kabisa ningependa kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia sisi Wanamtang’ata kuamka kutoka katika usingizi mzito tuliokuwa tumelala kuhusu maendeleo ya kwetu Matang’ata. 

Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu sasa nawashukuru wale Wanamtang’ata wote waliokaa pamoja kule Tanga na kufikiria wazo hili la ujenzi wa shule ya sekondari Maere. Wakaweza kutoa tangazo kupitia katika gazeti la AN-NUUR lililotolewa na Sheikh Hussein Abdallah ili wakutane. 

Na wakakutana na kutueleza kwa ufupi kupitia katika gazeti hili hili la AN-NUUR mambo waliyoafikiana juu ya ujenzi wa shule hiyo. 

Mimi nikiwa mmoja wa Wanamtang’ata wazo walilolitoa wenzetu kwetu sisi Wanamtang’ata wengine popote tulipo ikiwa ni Dar es Salaam ambapo naamini ndipo walipo wengi sana, mikoa mingine ya Tanzania Bara hadi Visiwani, nchi za jirani hadi za dunia nzima ili mradi mnajijua kuwa ninyi ni Wanamtang’ata, basi wazo hilo ni changamoto kubwa sana kwetu sisi. 

Kama nilivyosema hapo awali kwa vile Mwenyezi Mungu (s.w.) katuamsha, basi tusikubali tena kupata hata lepe kidogo la usingizi kuhusu suala hili. 

Kule Dar es Salaam kuna Umoja wa Vijana wa Darigube ambao hukutana takriban kila baada ya miezi miwili chini ya Uenyekiti wa Abdallah A.A. Makame na Katibu wake Abdulrahman Aziz, na kwa vile Darugube ni miongoni mwa vijiji vya Mtang’ata, ninawashauri Umoja huu uchukuwe jukumu la kuunganisha (Co-ordinate) Wanamtang’ata wote wa Dar es Slaam wakutane pamoja na kuchangia juu ya suala hilo na hatimaye kuunda Umoja halisi wa Mtang’ata wa uongozi wake wa kikweli kweli. 

Hivi karibuni nilizungumza na Ahmad M. Massa ambaye ndiye anayesambaza taarifa za mikutano ya Umoja wa Vijana wa Darigube, aliniambia kuwa siku ya Jumapili Novemba 1, 1998, watakutana nyumbani kwa dada yao Mwanamtang’ata Mwanakondo bint Mohammed Jumbe, ni matumiani yangu pamoja na mambo mengine watalipa uzito wake unaostahiki suala hilo na hatimaye kutoa taarifa ili Wanamtang’ata wote waelewe. 

Na isiwe kwa Wanamtang’ata wa Dar es Salaam tu, bali Wanamtang’ata wote popote pale walipo waunde umoja wao ili iwe rahisi kuwasiliana na wenzao wa sehemu mbalimbali. 

Wanamtang’ata tusirudi nyuma tena bali tushikamane kama twacheza msoma wala tusivutane kama twacheza jugwe. 

Mwanamtang’ata mwenzenu, 
Mohammed Khalid Massa, 
Darigube, Tanga. 


Ahsante AN-NUUR 

Ndugu Mhariri 

SISI wanafunzi wa Madrast - AN-NUUR - Hujatul Islamia Kwegoroto iliyoko mkoani Tanga - wilayaji - Lushoto tarafa ya Mlalo kijiji cha Nyasa. Tunayo furaha kubwa sana huku tuliko mbali kulipata gazeti tukufu lenye jina la madrasa yetu. Tumefurahi mno kulipata gazeti lenye kuueleza ukweli sahihi wa dini yetu tukufu Islamu. 

Tunalipata kila Ijumaa jioni saa 11. kamili. 

Wanafunzi wa na-Ustadh fanyeni juhudi kulipata AN-NUUR muelimike. 

Nanyi wazazi wapelekeni watoto chuoni na muwasaidie waalimu wao. 

Ni sisi Wanamadrasa, 
An-nuur Hijatul Islamia, 
Kwegoroto, 
LUSHOTO. 


Mfano gani huu ? 

Ndugu Mhariri 

SHEIKH wetu anatuchanganya sana sisi waumini wa Masjid Barakat-Tandale. 

Hivi karibuni kaozesha. Lakushangaza ulikuwapo mseto wa kutisha. Wa mdundiko walikuwa wakijimwaga kivyao, matarumbeta utadhani kwa Wagala, Maulid nayo ikaingizwa humo humo. 

Jioni kulishwa keki ukumbini, pombe zimesheheni na disko mtindo mmoja. 

Mfano gani huu Masheikh mnatoa kwa wafuasi wenu ? 

Y.I. Islam, 
Tandale. 



An-nuur chunguzeni makala 

Ndugu Mhariri 

Nikifuatilia kwa makini mijadala inayoendelea katika gazeti hili kuhusu kukanusha au kuthibitisha hoja zinazotolewa na Wakristo dhidi ya Uislamu, nimegundua hoja hizo zinapotosha lengo au dhumuni la kuelimisha umma wa Kiislamu na wale wasiokuwa Waislamu ambao husoma au kutoa hoja kwa ajili ya kutafuta ukweli kuhusu Uislamu. 

Hoja zinazotolewa na baadhi ya Wakristo dhidi ya Uislamu kwa kweli ni upuuzi, uzushi na porojo zisizokuwa na msingi wowote, ukizingatia hoja zinazotolewa zimebeba picha ya hasira dhidi ya Uislamu na hazina rejea. Na pale inapotolewa rejea basi, rejea hiyo hupindishwa na kutolewa maana au tafsiri isiyo sahihi. Allah kwenye Qur-an (23:2-3) anasema: "Ambao katika sala zao ni wanyenyekevu. Na ambao katika upuuzi ni wajiepushao". Hapa Mweneyezi Mungu anatufahamisha upuuzi hauna nafasi kwa wale wamchao au wanaomuabudu. Hivyo basi katika kutoa hoja ni lazima rejea za maandiko zitumike kiufasaha ili kupata ukweli halisi wa hoja. Hebu fikiri pale Wakristo wanapokosa theolojia ya maandiko wanapoamua kutoa hoja ambazo zimeambatana na taswira au picha ya hasira wanaposema Mungu wa Waislamu, fundi cherehani, Mtume Muhammad karuhusu liwati, Yesu si Issa n.k. Ndio maana hoja hizo ni upuuzi pale zinapokosa ushahidi. 

Mimi binafsi napenda kumpongeza Sheikh Bernard P. Nyanga katika AN-NUUR Na.169 katika makala yake, "Msiiparamie ovyo Biblia". Sheikh huyu rejea zake ni nzito, pia amesaidia kuwafahamisha Waislamu jinsi Wakristo wanaotaka kutangaza Ukristo kupitia AN-NUUR. 

Kama kweli Wakristo tayari kukanusha makala za Sheikh Bernard Nyagasa na Mchungaji AT Manoni basi toeni hoja za rejea kukanusha makala hizo. Mimi binafsi nakiri hamuwezi kwani Mchungaji AT Manoni ametoa makala yake ya "Kristojia Linganishi". Muda mrefu umepita na hakuna aliyediriki kujibu. Sasa Makadinari, Wachungaji, Mapasta, Mapadri na Wainjilisti huu ni wakati muafaka kujibu hoja hizo kwa kutumia rejea, ili kuwasaidia Wakristo wanaopandwa na hasira. 

Mwishoni napenda kuwashauri AN-NUUR wachunguze hoja zenye msingi zitolewe gazetini. Vile vile nalipongeza AN-NUUR kwa uvumilivu wa kutoa hoja hizo za upuuzi, uzushi na porojo kwani umetusaidia kuonyesha udhaifu wa Wakristo. 

Ustaadha Zawadi Salim 
Popatlal Sekondari 
P.0. Box 5007 
Tanga 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 

TAHARIRI 
Wakipewa fursa watainusuru nchi

Wasomi watetea haki ya wananchi kumiliki ardhi

Serikali izungumze na wananchi–Mzee Gonga

Akina mama watakiwa kushikamana na dini yao

Maoni
Serikali inaWhite Paper:  Wananchi mna nini?

Dondoo za Saikolojia: Hoja kengeza
Na Abu Halima Sa Changwa

Makala ya mtangazaji
Khatamy sio Gorbacheiv!!!

Makala
Malipo ya fadhila
Na Mohamed Saleh

Tanzania tuna sera gani kuhusu kanda
Na Abu Abdullah, Tanga

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo- 2
Na Nandenga wa Mkomidachi

Teknologia
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (3)
Na Hassan Omar

Makala na habari
'Usiiparamie ovyo Theolojia'
Na Charles Kamuhabwa, DSA Mtwara

Mwinyimkuu kufanya sensa ya waumini Magomeni
Na Jamillah Nassoro

Same tusilimu upya

Wazazi Mwanza wahimizwa kuwashonea watoto wao Hijab
Na Idd Katimba, Mwanza

Tuwaige Wangazija, 'tutafanikiwa'
Mwandishi: Maalim Bassalah

Serikali imeweka rekodi ya kutisha – Sheikh Salim
Na Mwandishi Wetu

Muhadhara waunguruma Geita
Na Hussein Abdallah, Geita

Fuateni Sharia ya Allah - Sheikh
Na Badru Kimwaga

Wanawake wa Kiislamu Mburahati wahimizwa kutafuta elimu

Mafunzo ya Qur'an
Vijana wa pangoni

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na lishe
Chakula ni silaha ya kukabiliana na changamoto ya kansa
Na Mujahid Mwinyimvua

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita