AN-NUUR 
Na.173 Rajab 1419, Oktoba 30 - Novemba 6, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Serikali izungumze na wananchi–Mzee Gonga 

MTAALAMU maarufu wa lugha ya Kiswahili nchini, Mzee Shaaban Gonga amesema kwamba haoni ni kwanini viongozi wa serikali wakwepe kwenda kuongea na wananchi wa Nzasa kabla na baada ya kuchomewa nyumba zao wakati wale ni wananchi. 

Kauli hiyo ya Mzee Gonga imekuja kufuatia kilio cha wananchi wa Nzasa kwamba wangependa kuonana na Mh. Rais ili kumweleza kilio chao na azione hali zao. 

Mzee Shaaban Gonga akiongea na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni alisisitiza kwamba haki hii ya wananchi kusikilizwa ni ya msingi sana kiasi kwamba hata wakati wa ukoloni wenyeji walipewa haki ya kutoa maoni yao na ndio maana walimpeleka Mwalimu Nyerere Umoja wa Mataifa ili kutoa maoni yao. 

Akisisitiza nukta yake hiyo, alinukuu kutoka kitabu alichokuwa amekishikilia ‘TANU katika UNO’ sehemu isemayo kwamba "wenyeji wanayo haki kutoa maoni yao kwa wajumbe hao juu ya jambo lolote na pia wanayo haki kuliandikia Baraza la Udhamini kulieleza shida zao au jambo lolote jingine". (TANU katika UNO Uk. 2 Kf. 3). 

Ni kutokana na ukweli huo, Mzee Gonga alihoji wakati ule wananchi walipata haki kuongea na Baraza huku tunatawaliwa na Mwingereza, vipi leo ishindikane serikali kuongea na wananchi wa Nzasa. 

Kuhusu mgogoro wa Nzasa – Kazimzumbwi kwa ujumla Mzee Shaaban Gonga alisema kwamba kitovu cha yote ni suala la haki ya mwananchi katika ardhi. 

Alisema suala la ardhi sio la mzaha na ndio lililokuwa limetawala hisia za watu katika kudai uhuru. Na vile vile ndio maana TANU katika UNO ilitamka wazi kwamba: " Hatutaki ardhi yoyote ambayo haijakodishwa kwa wageni ikodishwe tena. Na tumefurahi kusikia kuwa Gavana ametamka hadharani kuwa hakuna ardhi tena ya kuwapa wageni mbalimbali", alinukuu mzee Shaaban Gonga katika kitabu cha TANU katika UNO. 

Alisema Mwalimu Nyerere alipotumwa UNO alisisitiza kwamba yawezekana hatuna elimu, lakini tuna ardhi, hivyo anashangaa leo mwananchi anachezewa katika suala nyeti la ardhi. 

Alisema pengine itabidi wazee wazungumze na mzee mwenzao Mwalimu Nyerere kabla hawajafa maana miaka 37 baada ya uhuru bado mwananchi hana haki juu ya ardhi yake alikozaliwa na kuishi. 

Mzee Shaaban Gonga ambaye wakati TANU inaanzishwa ndio walikuwa vijana wakitumwa sehemu mbalimbali katika harakati za kudai uhuru, amesema kwamba mgogoro wa ardhi Nzasa una historia ndefu. 

Wakati wa ukoloni, kuna Giriki alitaka kuchukua ardhi yote yenye rutuba inayojumuisha vijiji vya Kazimzumbwi, Kisanga, Mvuti, Dondwe, Kisimba, Bupu na Maruwi. Hata hivyo akasema Mzee Muhunzi kwa niaba ya wananchi alishitaki serikali ya wilaya na Giriki akazuiwa. Hoja kubwa ilikuwa wananchi waende wapi, alieleza na kuhoji. "leo vipi huyo Mtimkavu kudai haki ya wananchi wa Nzasa iwe nongwa. Hii ni mazingira au yupo Giriki mwingine?" 

Kwamba Nzasa ni wahamiaji au wavamizi, Mzee Gonga alisema kwamba hilo haliwezekani. Akasema kwamba wakati Dar es Salaam Boma lipo Avalon ya leo, Boma la Kisarawe lilikuwa Chang’ombe eneo la Kioo Ltd. Mji ulivyopanuka likahamiashiwa Nzasa kwa vile kulikuwa na watu. 

Hata hivyo, akasema kwamba Boma lilikaa kwa muda hapo likahamia Kilimani Kisarawe lilipo leo. Kuambiwa wananchi wa Nzasa ni wavamizi inashangaza alisema. 

Katika suala zima la haki ya wananchi katika ardhi, Mzee Shaaban Gonga alisema kwamba mwananchi hafukuzwi kwa kuonyeshwa jiwe au hati. Unamwonyesha jiwe upate kumuhamisha aende wapi, alihoji. 

Kama ni hati za miaka thelathini au tisini na tisa hizo stahiki yao wageni. Sio mwananchi. Yeye kwake. Huwezi ukamwondoa katika ardhi, na nchi yake bado akawa mwananchi. 

Alisema makabila yote yalikuwa na utaratibu na mpangilio wa ardhi. Lilikuwepo eneo la kujenga mji, eneo la kilimo na eneo la jamii. Kwamba pale watakwenda kuwinda, kuokota kuni, kutambika, kuchimba dawa n.k. Katika mazingira hayo ya kiasili kila Gavana alipotaka kuingilia wazee walikusanyika na kuhoji tukalime wapi, tukaokote kuni wapi, wake zetu kaniki watapata wapi. Maswali hayo yalipowashinda Giriki alinyimwa eneo, alisema na kuhoji kwa masikitiko, "leo Nzasa inachomwa moto wapo wapi kina Mzee Muhunzi". 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 

TAHARIRI 
Wakipewa fursa watainusuru nchi

Wasomi watetea haki ya wananchi kumiliki ardhi

Serikali izungumze na wananchi–Mzee Gonga

Akina mama watakiwa kushikamana na dini yao

Maoni
Serikali inaWhite Paper:  Wananchi mna nini?

Dondoo za Saikolojia: Hoja kengeza
Na Abu Halima Sa Changwa

Makala ya mtangazaji
Khatamy sio Gorbacheiv!!!

Makala
Malipo ya fadhila
Na Mohamed Saleh

Tanzania tuna sera gani kuhusu kanda
Na Abu Abdullah, Tanga

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo- 2
Na Nandenga wa Mkomidachi

Teknologia
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (3)
Na Hassan Omar

Makala na habari
'Usiiparamie ovyo Theolojia'
Na Charles Kamuhabwa, DSA Mtwara

Mwinyimkuu kufanya sensa ya waumini Magomeni
Na Jamillah Nassoro

Same tusilimu upya

Wazazi Mwanza wahimizwa kuwashonea watoto wao Hijab
Na Idd Katimba, Mwanza

Tuwaige Wangazija, 'tutafanikiwa'
Mwandishi: Maalim Bassalah

Serikali imeweka rekodi ya kutisha – Sheikh Salim
Na Mwandishi Wetu

Muhadhara waunguruma Geita
Na Hussein Abdallah, Geita

Fuateni Sharia ya Allah - Sheikh
Na Badru Kimwaga

Wanawake wa Kiislamu Mburahati wahimizwa kutafuta elimu

Mafunzo ya Qur'an
Vijana wa pangoni

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na lishe
Chakula ni silaha ya kukabiliana na changamoto ya kansa
Na Mujahid Mwinyimvua

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita