AN-NUUR 
Na.173 Rajab 1419, Oktoba 30 - Novemba 6, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Malipo ya fadhila 

Na Mohamed Saleh 

ASUBUHI na mapema saa 12.00 wanaonekana wananchi wakiwa wamepanga foleni kwenye ofisi moja katika kijiji hiki. Leo ni kilele cha yale yaliyokuwa yakisemwa na watu mbalimbali. 

Leo ndio siku ambayo wananchi watatoa nafasi kwa waliotoa ahadi mbalimbali kuanza kuzitekeleza. Mtu wa kwanza kaingia ndani, kisha katoka anatabasamu kumaliza kupiga kura yake, uso wake umejawa na matumaini na wasiwasi, matumaini kwamba yule aliyemchagua atapita. Ama wenzake ambao nao wamejipanga mstari hapo watamsaliti. 

Leo kapiga kura yake, ni mtu wa miaka 55 ameanza kupiga kura mwaka 65 alipokuwa na miaka 25 hadi leo na kachagua wale anaotumaini kuwa watamletea maendeleo, watampunguzia adha alizonazo na kufanya maisha yake yaliyobaki kuwa ya furaha. 

Miaka miwili na zaidi kabla ya kuingia karne ya 21 anastushwa na habari zinazotolewa na vyombo vya habari. "Nyumba zimebomolewa huko Ubungo Kimara ili kuleta maendeleo". 

Picha zaonyesha watu wakiwa nje, watoto, wazee, vilema, wagonjwa hawana pa kuishi. Anajitahidi kutabasamu, lakini tabasamu halitokei, uchungu wa ndani unamjaa, anadhani ni wapinzani. Anataka kuwalaani, lakini ah ! Kumbe polisi ndio wanaosimamia zoezi zima la kubomoa nyumba za wananchi. 

Wale waliolipwa pesa zao mwaka 1972 miaka 25 baada ya kupewa pesa zao ndipo wanaambiwa waondoke na nyumba zinabomolewa. Wengine walishauza nyumba na viwanja. Wengi wa wanaobomolewa leo sio wale waliolipwa mwaka 1972. 

Waheshimiwa wakabaki wakiangalia kwenye Luninga "Oh safi sana". 

Mwaka mmoja na miezi kumi kabla ya kuingia karne ya 21 anazidi kutatanishwa na habari zingine mpya. Siku hiyo kaenda kumtembelea mwanae aliyeko Jijini, kwa bahati mwanae ana Luninga "Black & White", usiku saa mbili na nusu, yanakatishwa matangazo ya mpira, anatokea binti mmoja kisha habari yote inaelezwa mzee anasikia sauti "piga yule", mwongeze huyo". 

Kwanza anafikiri ni Burundi risasi zinalia, mtu mmoja anaruka juu na kutupwa chini, damu zinamiminika. Wengine wameshika mawe wakirusha, kisha akadhani labda ni majambazi yamevamia yanataka kuiba, uhh! Kushangaa, polisi ndio wanaopiga risasi, watoto wa shule ndio wanaokamatwa, waliokwishajisalimisha kukubali kuwa chini ya ulinzi ndio wanaozidi kupigwa. "Mh ! Nilikuwa polisi zamani, lakini hizi sheria mpya zinatisha", anajifikiria. Labda ndio utawala wa sheria tulioahidiwa wakati wa uchaguzi", lakini akastuka kidogo. 

Vyombo vya habari vikatangaza mengi baada ya hapo wanawake wamenyanyaswa (utawala wa sheria), wanawake wamewekwa uchi na kusachiwa na wanaume (utawala wa sheria), waliokamatwa wakawekwa ndani kwa miezi mitano bila kupewa dhamana, kisha kuachiwa huru kwa kutokuwa na kosa (utawala wa sheria). Mtoto Chuki kukaa na pingu hospitali bila kupewa matibabu stahiki hadi kupooza (utawala wa sheria). 

VAT: Kwa maendeleo ya Taifa, VAT mkombozi wako

Mwaka mmoja na miezi mitano kabla ya kuingia karne ya 21. "Tutapata maendeleo tu" fikra. 

"Hii ni awamu ya ukweli na uwazi". 

"Huu ni utawala wa sheria". 

Kabla wananchi hawajajua la kufanya baada ya kutoka majanga ya ajali mbaya kabisa kuwahi kutokea katika nchi yetu, ukame, El-Nino, mishahara midogo, ikaja VAT. 

Bei za vitu zikapanda, bidhaa kadhaa zikaanza kukosekana, mfumuko wa bei ukaongezeka, makusanyo ya kodi serikali yakaongezeka. Pato la mwananchi likaporomoka. Ada za shule nazo zikapanda, walimu shule za serikali na vyuo vya elimu ya juu mishahara ni midogo kiasi kwamba inatisha. Huduma za Afya, maji safi shauri yako mwananchi. 

"Tunajitayarisha kuingia karne ya 21 ya sayansi na teknolojia", "VAT kwa maendeleo ya Taifa", wananchi wakashangazwa. Maendeleo ya taifa ?! Ohoo ! Kumbe maendeleo ndiyo haya ! Hakuna madawa mahospitalini, hakuna maji safi na salama, hapana barabara nzuri kipato cha mwananchi chini, shule za serikali No vifaa. "VAT kwa maendeleo ya taifa". 

Maendeleo ya taifa, wananchi bado wanaishi kwenye vidungu hata vikichomwa moto hakuna hasara, maendeleo ya taifa, mzee anatafakari "oh tusibiri tu". Ikawa usiku ikawa mchana mwezi wa kumi ukafika mwaka 1998!! 

Leo hii mzee kaamka, kaenda kutembelea kaburi la baba yake aliyekufa mwaka 1958, anakutakana na bibi mmoja nae anaenda kulizuru kaburi la babu yake, wanaongozana pamoja hadi karibu na pori, watoto wawili wanapanda miembe ndani ya pori hili. 

"Hapa alikuwepo mzee Mwinyimvua akiwa katika shamba hili", anasema bibi yule. Wanaendelea na safari yao, wanamaliza shughuli zao hapo, wanarejea kijijini. Kufika nyumbani kwake, mzee anamkuta mjukuu wake kaja kutoka jijini. "Babu nimekuta askari wengi wa FFU hapo barabarani wakati nakuja kuna nini ?", anauliza mjukuu wake baada ya kusalimiana. 

"Ah mjukuu wangu usiwe na wasiwasi hiyo ni pesa yetu ya kodi ya maendeleo na VAT inafanya kazi, tunapewa ulinzi wa kutosha sasa maana tunasumbuliwa sana na wale Wazungu wawili, wanaotaka kutunya’ang’anya ardhi yetu, sasa naona serikali imeamua kutulinda vilivyo. Mjukuu wangu mimi nilikuwa askari zamani, FFU ni walinzi wazuri sana". 

"Lakini babu mbona walishindwa kuwazuia wale watu wa Arumeru. Walikuwa wakifanya fujo ? Mbona walishindwa kuwazuia askari wenzao walioua watu wasio na hatia pale Mwembechai ? Mh! Mbona nasikia harufu ya moshi; kuna nini ?". 

Wakatoka nje kuangalia kulikoni, "oh! Kwa mtukuu wa mzee Mwinyimvua kuna moto", alisema mzee yule. Maskini hakujua kuwa ule ndio ulikuwa mwisho wake wa kukaa katika nyumba ile, hakujua kuwa hayo ndio malipo ya fadhila ya kura yake. 

Hakujua kuwa malipo ya fadhila ya kura yake ni kupigwa na baridi chini ya mti, kusubiri vyakula vya misaada kutoka kwa watu wenye mioyo ya huruma, mzee alifikiri ni ndoto, mpaka alipokuta usiku ukimkuta chini ya mti wa mwembe ndipo alipotanabahi. 

"Utawala wa sheria" 

"Awamu ya uwazi na ukweli". 

Miaka 37 baaada ya uhuru, ndani ya nchi huru yenye sera za mahitaji muhimu ya binadamu, chakula, malazi na mavazi. Chakula – mihogo na mazao mengine yamekatwa, malazi nyumba zimechomwa moto na kuteketea. 

Mavazi, nguo na vifaa vingine vimeungua na kuteketea. Mahitaji muhimu ya binadamu !! Lakini ni Nzasa sio binadamu !!! Huu ndio uhuru tuliopigania. Hii ndio sheria ? Hii ndio adhabu stahiki ? Mahakama gani ilitoa hukumu hiyo ? Uhuru, Uhuru, Uhuru !!! Tumepata na ukombozi je !. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 

TAHARIRI 
Wakipewa fursa watainusuru nchi

Wasomi watetea haki ya wananchi kumiliki ardhi

Serikali izungumze na wananchi–Mzee Gonga

Akina mama watakiwa kushikamana na dini yao

Maoni
Serikali inaWhite Paper:  Wananchi mna nini?

Dondoo za Saikolojia: Hoja kengeza
Na Abu Halima Sa Changwa

Makala ya mtangazaji
Khatamy sio Gorbacheiv!!!

Makala
Malipo ya fadhila
Na Mohamed Saleh

Tanzania tuna sera gani kuhusu kanda
Na Abu Abdullah, Tanga

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo- 2
Na Nandenga wa Mkomidachi

Teknologia
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (3)
Na Hassan Omar

Makala na habari
'Usiiparamie ovyo Theolojia'
Na Charles Kamuhabwa, DSA Mtwara

Mwinyimkuu kufanya sensa ya waumini Magomeni
Na Jamillah Nassoro

Same tusilimu upya

Wazazi Mwanza wahimizwa kuwashonea watoto wao Hijab
Na Idd Katimba, Mwanza

Tuwaige Wangazija, 'tutafanikiwa'
Mwandishi: Maalim Bassalah

Serikali imeweka rekodi ya kutisha – Sheikh Salim
Na Mwandishi Wetu

Muhadhara waunguruma Geita
Na Hussein Abdallah, Geita

Fuateni Sharia ya Allah - Sheikh
Na Badru Kimwaga

Wanawake wa Kiislamu Mburahati wahimizwa kutafuta elimu

Mafunzo ya Qur'an
Vijana wa pangoni

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na lishe
Chakula ni silaha ya kukabiliana na changamoto ya kansa
Na Mujahid Mwinyimvua
 
 

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita