|
Na. 050 Jumatano Mei 31 - Juni 5, 2000 |
|
|
|
|
|
Dini na siasa haviwezi kutenganishwa Na Mwinjilisti Kamara Kusupa Katika mada hii nitazungumzia dini na siasa.
Kila mahali nitakapotaja neno dini, nataka ieleweke wazi kwamba naitaja
dini katika uhalisi wake na wala siitaji dini katika mazoea ya kibinaadamu
ambapo mara litamkwapo neno dini mawazo ya watu wengi hurukia kwenye Uislamu
au Ukristo kama taasisi badala ya kutazama katika uhalisi wao. Na pia nitaijadili
siasa katika uhalisi wake maana watu wengi wasikiapo neno siasa hurusha
mawazo yao kwenye vyeo na vyama vya siasa kama vile CCM, CUF n.k. wakati
ukweli ni kwamba CCM siyo siasa, wala CUF siyo siasa kwani siasa ina maana
pana na nzito kuliko wengi wajuavyo.
Je siasa ni nini? SIASA ni mpangilio wa maisha kuhusiana na mambo yote yanayohusu maisha ya watu katika ujumla wao. Na dini ni nini? Neno dini limetokana na neno la Kilatini Religio lenye maana ya mahusiano au uhusiano kati ya Mungu na mtu, au mtu na Mungu. Neno la Kiingereza Religion ndilo lililoipiku religio kutokana na ukweli kwamba Waingereza nao walitawaliwa na Warumi kabla ya kututawala sisi. Kutoka kwenye religion ndipo tukapata neno dini katika tafsiri ya Kiswahili itokanayo na Kiarabu. Kwahiyo kwa kifupi dini ni mahusiano kati ya mtu na Mungu, Mungu na mtu na pia mahusiano kati ya mtu na mtu mwingine. Kulingana na vitabu vya Nabii na Mtume Musa hapo mwanzo Mungu alimuumba mtu ama alimfinyanga mtu kutoka kwenye udongo wa mfinyanzi ambao kwa luigha ya Kiebrania udongo huo huitwa "adama". Baada ya kuifinyanga sanamu hiyo, Mungu aliipulizia pumzi ya uzima puani na sanamu hiyo ikapiga chafya, ikawa hai na Mungu akaiita jina lake Adam. Huyo Adam akawa ndiye baba wa wanadamu wote waishio katika dunia hii. Hivyo basi uhusiano wa mtu na Mungu ni uhusiano wa kindugu sawa na ule wa Baba na mwanawe ama mtu na mzazi wake ambao uhusiano wao ni wa damu isipokuwa kwa Adama na Mungu tofauti ni ndogo nayo ni kwamba badala ya kuunganishwa na damu wao wanaungamanishwa na ile pumzi ya uzima iliyotoka nafsini kwa Mungu na kumwingia Adam kupitia puani. Baada ya Adam kuasi, kuhukumiwa na kufa, kuna matukio kadhaa ambayo yalitokea na kuathiri uhusiano kati ya mwanadamu na Mungu. Hatimaye Mungu alimpata mtu mmoja aliyekuwa na sifa ya utii naye ni Ibrahimu. Mungu alimwita na kufanya naye agano, na pia kumwahidi kwamba kwa njia yake Ibrahimu, mataifa yote ya dunia yatabarikiwa. Hatimaye uzao wa Ibrahimu uliongezeka hadi likapatikana taifa la Waebrania wakawa watumwa katika nchi ya Misri, Mungu akamwinua Nabii Mussa na kumtuma aende Misri kuwatoa nduguze toka utumwani. Hapo ndipo tunapopata muungano wa siasa na dini, kwani tunaona katika awamu hii yaani awamu ya pili toka uumbaji wa Adamu, Mungu anashughulika na taifa. Katika awamu ya kwanza Mungu anashughulika na mtu mmoja mmoja yaani "individuals" kama vile Adamu, Habili, Kaini, Henok, Nuhu, na Ibrahim. Katika awamu ya pili Mungu anashughulika na taifa, na katika awamu ya tatu yaani tangu ujio wa Yesu ulimwenguni, Mungu anashughulika na mataifa yote ya dunia. Kwahiyo kwa kifupi tunaweza kuweka muhtasari wa namna hii:- (i) Hapo mwanzo ulikuwa ni uhusiano kati ya Mungu na mtu (ii) Baadaye ikawa ni uhusiano kati ya Mungu na taifa (iii) Na mwisho ikawa ni uhusiano kati ya Mungu na mataifa. Katika kipindi cha Mussa yaani kipindi cha uhusiano kati ya Mungu na taifa moja, Mungu alifanya nao agano ambalo kulingana na maneno ya Nabii Yeremia 31:31 uhusiano wake Mungu na taifa lile ulikuwa sawa na uhusiano au ndoa ya mume na mke. Hivyo Mungu ni yule yule, na mwanadamu ni yule yule lakini uhusiano hauko kama ule wa Adamu na Mungu pale Eden, au Ibrahimu na Mungu pale katika nchi ya Ukaldayo na hatimaye Kaanani. Wala namna ya Mungu kushughulika na mtu siyo ile ile ya enzi za Adamu, Nuhu na Ibrahimu badala yake dini inakuwa sawa na pande mbili za sarafu, upande wa kwanza ni uhusiano kati ya mtu na Mungu, na upande wa pili ni uhusiano kati ya mtu na mtu mwingine aliyepewa jina la jirani yako. Baada ya Mussa kuwatoa Waisraeli nje ya Misri, Mungu aliwapa sheria. Sheria au torati ulikuwa ni mfumo mpya wa maisha badala ya ule mfumo wa zamani yaani mfumo wa utumwa. Katika mfumo wa sheria mambo yote yanayohusu maisha ya mtu yalianishwa na kuwekwa bayana kuanzia maslahi ya binafsi hadi maslahi ya jamii katika ujumla wao. Hakuna chochote ambacho kiliruhusiwa kujiendesha nje ya sheria kuanzia uchumi, biashara, kilimo, elimu, afya na hifadhi ya jamii. Sheria ya Mussa ndiyo iliyotawala uchumi wao, biashara zao, kilimo chao na mambo yao mengine yote yanayohusu maisha ya siku kwa siku ya mtu. Kwa kifupi sheria ya Mussa ilitawala ama iliongoza mahusiano yao yote katika maisha ya siku kwa siku. Ndani ya sheria ya Mussa kulikuwa na sera za uchumi, sera za biashara, sera za kilimo, sera ya ardhi, sera ya afya, sera ya watoto, sera ya wageni, sera ya mambo ya nje, sera ya fedha, mikopo na riba n.k. Ingawa katika torati ya Mussa mtu hawezi kukutana moja kwa moja na neno sera, lakini sera zimo. Kwa mfano Mussa anapoagiza katika toati yake kwamba utakapoingia katika nchi akupayo Bwana Mungu wako na kujipatia shamba uilime ardhi kwa miaka sita, mwaka wa saba uipumzishe ardhi maana ni sabato ya Bwana. Hii ilikuwa ni sheria lakini katika uhalisi wa mambo ilikuwa ni sera ya ardhi. Ama Mussa anapoagiza kwamba ukimkopesha ndugu yako usimtoze riba bali atarudisha kiasi kile kile alichochukua, hii ilikuwa ni sera ya kuzuia unyonyaji kati ya mtu na mtu ili watu wasifikie hali kama tuliyo nayo sasa ambayo madudu kama IMF na Benki ya dunia yanakopesha kidogo lakini yanadai kikubwa ama yanakopesha vichache lakini yanadai vingi hadi kusababisha tatizo la madeni yasiyolipika. Unapozungumzia sera tayari unazungumzia siasa. Mtu hawezi kusema anatekeleza sera lakini hatekelezi siasa ama hajihusishi na siasa. Mtu wa enzi za Mussa alikuwa tofuati na mtu wa enzi za Ibrahimu, Nuhu na Adamu ingawaje mtu alikuwa ni yule yule Mungu pia alikuwa ni yule yule. Enzi za Adamu, Nuhu au Ibrahimu, mtu angeweza kusema mimi ni mtumishi wa Mungu nitashughulika na Mungu wangu tu wala sitashughulika na mambo mengine akawa sahihi, lakini mtu wa enzi za Musa au enzi za leo hawezi kusema atashughulika na Mungutu maana tayari agano la Mungu, au sheria ya Mungu ama neno la Mungu linamlazimisha kuwajibika kwa jirani yake. Kwa sasa mtu hawezi kumtumikia Mungu kwa kumfulia nguo, kumpikia chakula ama kumhudumia Mwenyezi Mungu kwa jema lolote lile bali mtu atamtumikia Mungu kwa kuwatumikia wanadamu wengine. Aidha, mtu hawezi akawa na uhusiano mzuri na Mungu bila ya kuwa na uhusiano mzuri kwanza na mwanadamu mwenzake. Hii ni kwasababu kila binadamu ni sehemu yajamii na pia amegawanyika katika sehemu tatu roho, nafsi na mwili, vyote hivi vimeungamanishwa kuwa kitu kimoja na kumfanya mtu awe kama anavyoonekana. Kwahiyo, Roho ina kazi ya kuwasiliana na Mungu Muumba wake, nafsi ambayo ndani yake mna akili, fahamu na hisia iko kwa minajili ya kuwasiliana na mambo yasiyoshikika lakini yapo na ni ya muhimu, na mwili kazi yake ni kuwasiliana na vitu vya kushikika vilivyo muhimu katika maisha ya binaadamu. Sasa mtu anayetaka mwanadamu atenganishe dini na siasa sijui anataka mambo hayo mawili yatenganishwe katika eneo lipi la mwanadamu; eneo la Roho, au eneo la nafsi ama eneo la mwili? Ni kipi katika maeneo matatu ya binaadamu yaani Roho, nafsi na mwili ambacho kinaweza kusemwa hakina uhusiano wowote na siasa za nchi? Kutenganisha siasa na dini ni sawa na kuthubutu kutenganisha Roho ya mtu na mwili wake au nafsi yake, na ati kutarajia mtu huyo aendelee kuishi. Kupiga kura Zoezi la kupiga kura kama lilivyo ni siasa. Mtu anapojihusisha aidha na kupigiwa kura ama kupiga kura kuwachagua wengine basi huyo moja kwa moja anajishughulisha na siasa. Lakini enzi za Nabii Mussa zoezi la kupiga na kupigiwa kura lilikuwa ni sehemu ya zoezi la kidini. Kwa lugha nyingine kupiga kura ilikuwa ni suala la kidini, kwani katika kitabu cha Mussa kiitwacho kutoka 18.14.24 inaonesha kwamba Mussa alitaka kuendesha utawala wa kibinafsi sana wa kujihusisha na mambo yote na mambo ya kila mtu lakini mkwewe Yethro akamwonya kwamba hivi unavyofanya si vyema haikosi utakonda (utadhoofu) basi jipatie watu wenye sifa zifuatazo wawe watu waliojaa roho, wenye kumcha Mungu, wenye kuchukia mapato ya udhalimu (yaani watu wenye kuchukia hongo na rushwa), watu wakweli (yaani wasiopenda uwongo), kisha ukaweke wawe wakuu wa hamsini, na wakuu wa mamia, maelfu, na makumi elfu, waamue na itakuwa lile neno gumu ndilo utakaloletewa wewe ulitolee uamuzi. Mussa akaona neno hilo ni jema na akaliingiza katika sheria, zoezi la kuwapata viongozi likafanyika hadi likapatikana baraza la watu sabini ambalo lilidumu hadi nyakati za Yesu Kristo, baraza hilo Wayahudi waliliita Sanhedrin. Kwa leo baraza la namna ile tunaweza kulifananisha na Bunge. Sasa je Bunge ni taasisi ya kidini au taasisi ya kisiasa? Je hilo ni suala la kiroho au la kimwili? Zaidi ya yote ebu tuone jinsi Mussa alivyoweza kulipata baraza lile. Ukweli ni kwamba Mussa hakupita katikati ya watu 3,000,000 na kuanza kuchagua watu sawa na mteja anavyochagua bidhaa sokoni badala yake Mussa aliwashirikisha watu (wananchi wake). Ni watu ndio waliofanya uchaguzi isipokuwa Mussa aliweka vigezo au sifa za yule anayestahili kuchaguliwa. Mussa hakuwachagulia watu viongozi bali watu wenyewe ndio waliochagua wakuu wa mamia, hamsini, maelfu na makumi elfu. Tafsiri halisi ya neno hili ni kwamba hapo ulifanyika uchaguzi mkuu, huu ulikuwa uchaguzi mkuu wa kwanza tangu watu wakombolewe kutoka Misri, uchaguzi ambao ulitoa viongozi na watendaji wa kufanya kazi pamoja na Musa. Ikumbukwe ya kwamba zamani hizo Mungu alikuwa pamoja nao mchana akiwafunika kwa wingu ili wasipigwe na jua na usiku aliwafunika kwa nguzo ya moto ili wasipigwe na baridi kali ya jangwani, lakini pamoja na kuwa nao karibu kwa kiasi hicho bado Mwenyezi Mungu hakuwafanyia mambo ambayo wao wanadamu walipaswa kuyafanya. Mungu hakuwachagulia viongozi, alichokuwa amekifanya ni kumchagua (kumuandaa toka awali)Mussa basi, lakini lilipokuja suala la watendaji wengine, Mungu aliwaachia wanadamu wawachague wao wenyewe. Sasa mtu anayetaka siasa itenganishwe na dini ana maana gani hasa? Au ana tafsiri yake potofu ya dini na pia tafsiri potofu ya siasa? Yawezekana wapiga debe wa propaganda ya kutaka kutenganisha dini na siasa wanaajenda yao ya siri. Kwanza wanajua wazi kwamba mfumo wa kidikteta hauko katika ufalme wa Mungu, kwani tukiyaangalia maisha ya Mussa na torati yake, hatumwoni Mussa kuishi kama mtawala wa kiimla (A Totalitarian ruler) asiyesikia la mtu na ambaye haambiliki, bali tunaona Mussa anapokea ushauri wa wanadamu wengine na kuuingiza katika sheria. Musa hakuchukulia kule kuwa (kwake)karibu na Mungu basi iwe kizingiti na mwiko wa kutokuwasikiliza wengine, wala hatuoni Mungu akilikataa shauri jema ati kwa sababu halikutoka kwake yeye mwenye haki, bali anakubali kila lililo jema. Kwa hiyo wale ambao wamezoea kuwafananisha watawala madiktata na Mungu ni kwa sababu awali ya yote hawamjui Mungu. Mungu siyo dikteta, wala dikteta yeyote wa dunia hii siyo mtu wa Mungu, utawala wowote wa kidikteta ni utawala wa kishetani na uko chini ya Mungu wao aitwaye Ibilisi. Maana wale waliomkataa Mungu wa kweli katika fahamu zao Ibilisi ndiye amekuwa Mungu wao. Torati ya Mussa ulikuwa ni mfumo wa kulinda haki kati ya mtu na mtu. Torati haikutolewa kwa Myahudi ili kumnufaisha Mungu bali Wayahudi wenyewe, na manufaa makubwa ya torati ilikuwa ni kwamba kwa kadri jamii ya Kiyahudi ilivodumu katika torati,haki ilikuwa inatendeka miongoni mwao na mara zote walipotokea wafalme katika Uyahudi wasioifuata torati ya Mussa hapo ndipo nchi ilipopata maafa, aidha watu walipatwa na magumu yasiyomithilika kwa sababu ya kuipiga teke haki ya Mungu iliyokuwa ndani ya torati. Matatizo tunayoyapata sasa na hasa kutoka kwa hao wanaojihami kwamba tusichanganye siasa na dini ni kutokana na ukweli kwamba wanajua fika kwamba hatuna mfumo wowote wa kuhakikisha haki inatendeka katika nchi yetu, na katika maisha yetu ya kijamii, na kwa hiyo wanaiogopa dini isije ikawa nuru ya kumulika maovu yao yakaonwa na wananchi. Inaendelea wiki ijayo.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Zanzibar wadai kuyumbishwa na Bara Serikali yatoa muelekeo wa Bajeti na kutangaza njaa Habari za ndani
SMZ haishughulikii mikarafuu -Maalim Seif Mwalimu Mkuu Msimbazi Mseto atishia kujiuzulu Hizi ni 'arobaini' za mapandikizi Waislamu Mbeya wamsusa Sheikh Mkuu wa BAKWATA Masheikh wa BAKWATA waongoza sherehe za kuwasimika makamanda wa vijana wa CCM MAKALA
Makala
MPASHO NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Habari za Kimataifaza Kimataifa Lishe
RIWAYA
Ambari, Mwakipesile wajitosa kugombea DRFA |
|
|
|
|