NASAHA
Na. 042 Jumatano Aprili 5 - 11, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Kuelekea uchaguzi mkuu 2000: 
CUF yaiteka Dar
  • Wazee waifananisha na TANU wakati wa uhuru
Na Mwandishi Wetu

IMEELEZWA kuwa Chama Cha Wananchi(CUF) kimeacha taathira kubwa miongoni mwa wakazi wa Jijini kufuatia mkutano wake mkubwa wa kihistoria uliofanyika katika Viwanja vya Jangwani Machi26, na kufuatiwa na mikutano mingine miwili ya huko Kijitonyama na Kurasini, ambapo maelfu ya wakazi wa jiji walihudhuria.

Wakazi wa jiji walioongea na NASAHA wameeleza kuwa hotuba ya Mwenyekiti wa chama hicho Profesa Ibrahimu Lipumba aliyoitoa katika mkutano wa Jangwani ambayo ilijaa uchambuzi wa kina wa matatizo ya kisiasa na kiuchumi yanayoikabili Tanzania kwa sasa na namna ya kuyatatua, imerejesha ari, imani na matumaini mapya kwa wananchi kwamba wanaweza kuuondoa utawala mbovu madarakani na hatimaye kuondokana na umasikini wa kutisha unaolikabili Taifa hili lenye maliasili lukuki. 

Wakiongea na gazeti hili kwa nyakati tofauti katika Viwanja vya Ugimbi Kaurasini mara baada ya mkutano uliohutubiwa na Mwenyekiti wa chama hicho Wilayani Temeke Mhe. Riachard Tambwe Hiza, wananchi hao wamesema kuwa umahiri wa Profesa Lipumba katika kuchambua matatizo ya kiuchumi, kuanisha sababu za matatizo hayo na hatimaye kuonesha namna ya kuyatatua ni faraja kwao, na kwamba sasa wamepata mwelekeo wa nani anastahili kupewa kura zao mwezi Oktoba wakati wa uchaguzi mkuu. 

"Lipumba ameturudishia matumaini, kwa kweli wengi wetu tulishakata tamaa, maana wale tuliokuwa tumewategemea kumbe bure kabisa. Sasa tumepata mweleko wa kupiga kura uchaguzi ujao", alisema Bw. Mussa Zakaria mkazi wa Kurasini. 

Bi Leokadia Mushi, mkazi wa Kurasini kijiji cha wavuvi alizungumzia mwitiko wa maelfu ya wananchi katika mikutano hiyo, hasa ule wa Jangwani kwa kusema, "Inatia matumaini kuona hatimaye sasa Watanzania wameacha ushabiki na jazba, na badala yake wanaangalia uwezo wa mtu na chama chake. CUF sasa imekubalika kwa wananchi." 

Mzee Hamad Pazi mkazi wa Mbagala Kiburugwa akizungumzia uzoefu wake alisema, "hali ilikuwa hivihivi wakati wa TANU. Sisi wakati huo tukiwa ni vijana tulikuwa tumehamasika kutaka uhuru namna hii hii. Haikupita muda Mwingereza akaondoka." 

Katika uchambuzi wake wa masuala ya kisiasa Profesa Lipumba akihutubia mkutano wa Jangwani, Jumapili Machi 26, alisema hali ya kisiasa Afrika inabadilika kwa kasi na kwamba tayari CCM imeingiwa na woga. 

"... hali ya kisiasa barani Afrika inabadilika, wenzetu wa Senegal wametuonesha mfano... hapa nyumbani CCM wamepata 'presha'", alisema Profesa Lipumba katika mkutano huo ambao wakazi wa jiji sasa wanauita ni wa Kihistoria.

Alitoa kielelezo cha kuwepo hofu ndani ya chama tawala cha CCM, Profesa Lipumba, alisema mabadiliko ya 13 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano yamepitishwa katika jitihada za kumknusuru mgombea urais wa chama hicho. 

"Mabadiliko ya 13 ya katiba ni kielelezo kuwa mgombea wao hakubaliki.... Hawezi kupata asilimia hamsini ya kura zote zilizopigwa", alisema Mwenyekiti huyo wa CUF na kuongeza kuwa wabunge wa CCM walitishwa na kulazimishwa kuyaunga mkono mabadiliko hayo. 

Katika yale aliyaongea kwa upande wa uchumi Profesa Lipumba ambaye ni bingwa wa uchumi aligusia pia suala la Serikali ya CCM kuyasemehe kodi makampuni makubwa yaliyowekeza hapa nchini na hivyo kupoteza mabilioni ya fedha za Kitanzania ambazo zingeweza kutumika kuinua hali ya maisha ya wamnanchi. 

Akitoa mfano alieleza kuwa kampuni ya Ashanti Gold Mines iliyouziwa machimbo ya dhahabu ya Bulyamkulu Geita, inailipa serikali ya Tanzania dola tatu za Kimarekani kwa kila mauzo ya dhahabu yenye thamani ya dola mia moja za Kimarekani, huku ikiwa imepewa msamahawa kodi. 

"...mashrika ya kimataifa yanatushangaa jinsi tunavyotoa misamaha ya kodi kwa makampuni makubwa", alieleza mtaalamu huyo wa uchimi na kuongeza, "ajabu zaidi ni kwamba TRA inawabana wafanyabiashara wa hapa nchini na hali hii inasababisha biashara zao zishindwe kukua, na hivyo inapunguza ajira kwa Watanzania mwaka hata mwaka", alieleza. 

Katika mkutano wa Kurasini Mhe Richard Tambwe Hiza, pamoja na mambo mengine alisema kuwa kusimamia vizuri huduma za kijamii kama vile afya na elimu na kuongeza nafasi za ajira kwa wananchi ndio vigezo vikubwa muhimu vinavyotumiwa na nchi za Ulaya wakati wa kupiga kura, katika kukiingiza au kukitoa chama chochote cha siasa, kinachoshiriki uchaguzi. 

"Hapa kwetu ajira hakuna, watu wanapunguzwa kazi kila siku, lakini bado uchaguzi ukifika wanairudisha CCM madarakani", alisema na kuongeza kuwa upande wa huduma za afya serikali ya CCM hasa ya Awamu ya Tatu imeua kabisa huduma hizo hususan afya na elimu. 

Akikariri takwimu zilizotolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Profesa Ibrahimu Lipumba kuwa wakati wa mwisho wa utawala wa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi zilitengwa shilingi bilioni 27.8 kwa ajili ya ununuzi wa dawa katika hospitali za serikali nchini, lakini utawala wa Rais Makapa ukashusha kiwango hicho mpaka shilingi bilioni 4.2 tu katika bajeti ya mwaka 1996/97 huku Ikulu ikikarabatiwa kwa shilingi bilioni 3.2, Mhe. Hiza alisema kuwa hiyo ni hoja tosha kuwa CCM imeamua kuua kwa makusudi huduma za kijamii nchini. 

Aidha katika mkutano huo kadi kadhaa za chama tawala cha CCM, moja ya NCCR-Mageuzi na moja ya TLP zilirejeshswa, na hatimaye wanachma hao wapya kukabidhiwa kadi mpya za CUF na Mwenyekiti huyo wa CUF Wilaya ya Temeke. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Mnaodhulumiwa lindeni kura zenu

Mbukuzi anguruma Chuo Kikuu:
Wasomi mnatakiwa kukomesha dhuluma

Kuelekea uchaguzi mkuu 2000:
CUF yaiteka Dar

Maalim Seif afunguliwa mashitaka

‘Tume ya Keenja’ haikufanya ilichoagizwa - Wananchi

MPASHO NASAHA
WE THIO LAFKIYANGU TEENA!

Ushauri Nasaha
Namna ya kumfanya mtoto wako aweze kuzungumza

MAKALA
Kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani

WAZO  LA  WIKI
Ajenda mpachiko

MAKALA
Kuporomoka kwa maadili  katika jamii yetu; Sababu na utatuzi wake

Kalamu ya Mwandishi
Ulaya yaiambia Afrika iboreshe demokrasia kabla ya kufutiwa madeni yake

Makala
Wasifu wa marehemu Sheikh Said Sabiq

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (5):
Wananchi mjiandae kulinda kura

HABARI ZA KIMATAIFA

Riwaya
Kisasi cha mauti -2

Lishe
Ni kwa jinsi gani wanawake wanapata utapiamlo

MASHAIRI

MICHEZO

  • Kajumulo atishia kuwanyang’anya Kibadeni Simba
  • Kipukuswa kufuata nyayo za ‘Mgosi’ Hazali
  • Hazali sio Yanga ni Simba ‘kindakindaki’

  • Madadi azionya timu za Ligi Kuu


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita