|
MASHAIRI
Madhalimu wahiliki
Mtukufu ya Jalali, tuwezesha kudiriki,
Tuauni kila hali, tuishinde hii mikiki,
Madhalimu wahiliki, dua yetu ikubali,
Twaomba utukubali, watu hao wahiliki,
Wajalie nyonge hali, tuvichimbue visiki,
Ima wafutie mbali, kwani haki hawataki,
Madhalimu wahiliki, dua yetu ikubali.
Tumetamka kauli, madai hayasikiki,
Tukasema tafadhali, msitupige mikuki,
Ni viziwi hawajaali, wameikalia haki,
Madhalimu wahaliki, dua yetu ikubali.
Njia yetu ni halali, iweje haiendeki!
Tunakwamia mahali, hadithi hairefuki,
Wanatema sumu kali, imenata haitoki,
Madhalimu wahiliki, dua yetu ikubali.
Twakita kwa tahlili, utike ya Maliki,
Tuvukishe bonde hili, wao nyuma uwapaki,
Tuwezeshe kuhimili, wapishe kipito hiki,
Madhalimu wahiliki, dua yetu ikubali.
Tuthibitishe kauli, tutende yalo laiki,
Radhi zako ndo ajili, mwinginewe hatuteki,
Madhalimu wahiliki, dua yetu ikubali.
Witiri utupe hali, Mola mzima mikiki,
Wewe ndiye wa awali, na milele utabaki,
Utufanyie sahali, tuutweze uzandiki,
Madhalimu wahiliki, dua yetu ikubali.
Jihad R. Rashid,
Box 347,
Shinyanga.
Madhalimu wahilikiAdhabu haina tiba
Ndwele hufanyiwa dawa, ndivyo dini ifunzavyo,
Za kufunga na kunywewa, na zile uchanjiwazo,
Za bei na za kupewa, maradhi ziponyeshazo,
Bali adhabu kipewa, dawa hukosa uwezo.
Matendo yanayotendwa, sivyo utu usemavyo,
Njia njema inaepwa, kupupia makatazo,
Ndiyo kisa tunalipwa, adhabu ziumizazo,
Na adhabu tukipewa, dawa hukosa uwezo.
Husemwa ni nzuri dawa, kwa homa tuzipatazo,
Za kunywa na za kudungwa, na vidonge tupewavyo,
La adhabu kutibiwa! Sivyo kanuni ilivyo,
Bali adhabu ikiwa, dawa hukosa uwezo.
Ni jambo hukadiriwa, kwa kuishi tuishivyo,
Kwani Mola kusikiwa, huonwa ya kuwa sivyo,
Watu viziwi wakawa, wasijali wafanyavyo,
Ukimwi ikishakuwa, dawa hukosa uwezo.
Lengo Allah kurudiwa, adhabu tuletewazo,
Tupate watii kuwa, tuepuke makatazo,
Shari itaondolewa, dawa zipate uwezo,
Na maisha kuridhiwa, ili kheri tuwe nazo.
Jihad R. Rashid,
Box 347,
Shinyanga.
Maulid siku njema, kuzaliwa kwa Mtume (saw)
Kutunga imenibidi, kumsifu Muadhama,
Sayidina Muhammad, kazaliwa hizo zama,
Furaha ya Maulid, yahusu Dunia nzima,
Maulidi siku njema, kuzaliwa kwa Mtume.
Nuru imepatikana, kwa kuzaliwa hashama,
Kuzaa Mama Amina, Mtume kizazi chema,
Ndie Bwana wa Mabwana, m-bora wa taadhima,
Maulidi siku njema, kuzaliwa kwa Mtume.
Babae Abdilahi, alifariki mapema,
Kumlea hakuwahi, amekuwa kiyatima,
Kwa uwezo Waillahi, Mtume kakua vyema,
Maulidi siku njema, kuzaliwa kwa Mtume.
Malaika wa mbinguni, Jibrilu kenda hima,
Kamfuata pangoni, kamwambia hebu soma,
Akajibu asilani, mimi sijui kusoma,
Maulidi siku njema, kuzaliwa kwa Mtume.
Jibrilu kaongeza,soma leo hebu soma,
Ikraa katangaza, Muhammad akasoma,
Jina la Mola muweza, Muumba wetu Rahima,
Maulidi siku njema, kuzaliwa kwa Mtume.
Hii ndiyo Qur'an, ilo amrisha mema,
Tumeumbwa Duniani, tuje kumcha Karima,
Sote natuwe makini, Ibada kwetu lazima,
Maulidi siku njema, kuzaliwa kwa Mtume.
Rajabu A. Kirobo,
S.L.P. 100146,
Tandika – Azimio,
Dar es Salaam.
Moyo hunijaa hofu
Nikifikiri mauti, moyo hunijaa hofu,
Ufikiapo wakati, binadamu kuwa mfu,
Haraka hupiga goti, kumshukuru Raufu,
Moyo hunijaa hofu, nikifiri mauti.
Hofu isiyo sauti, rohoni hunisanifu,
Nikilala nikiketi, huikumbuka Masafu,
Nkama nitavuka geti, kwenda njia ilo nyofu,
Ndipo inakuja hofu, nikifikiri mauti.
Kama nitapewa kiti, mbele yake Latifu,
Kupata hiyo bahati, najiona mpungufu,
Pande zote kudhibiti, hawaingii wachafu,
Siku zote ninahofu, nikifiriki mauti.
Hofu ya mauti nyeti, naogopa usumbufu,
Katika wake umati, Muhamadi muongofu,
Siku ya kuwa mauti, nawazia mara dufu,
Moyo hunijaa hofu, nikifikiri mauti.
Japo naswali swalati na swadaka kutiifu,
Zaka na funga za dhati, natenda kwa muda mrefu,
Mauti nikusukuti, sipati ulinganifu,
Nabaki kuwa na hofu, nikifikiri mauti.
Hofu ya kupokelewa, peponi patakatifu,
Au nikakataliwa, kuingia patukufu,
Hapo ndipo nazidiwa, hadi kucheza mapafu,
Na moyo hujaa hofu, nikifikiri mauti.
Hofu yakusumiwa, kuwafata waarifu,
Nawaza na kuwazua, hakuna cha mzoefu,
Nabaki kuomba duwa, kwa hii safar ndefu,
Moyo umejaa hofu, kwa fikira za mauti.
Adidi S. Regemalira,
S.L.P. 15771,
Dar es Salaam.
Wakuu fafanuweni
Mhariri Mhisani, naomba kunipokeya,
Naja kwako gazetini, nina haja uliziya,
Nipange japo pembeni, roho ipate tuliya,
Katika majina haya, wakuu fafanueni.
Wakuu fafanueni, katika majina haya,
Kilo nisibu moyoni, hadi niulize haya,
Kwa hili neno Amani, naona yenda vibaya,
Katika majina haya, wakuu fafanueni.
Kwani tofauti gani, kati ya majina haya,
Nala kwanza neno dini, pili ibada sikiya,
Tatu Kristo ninini, nne, dini Silamiya,
Katika majina haya, wakuu fafanueni.
Vipindi via redioni, vingi nimevisikiya,
Na habari gazetini, sikuacha jisomeya,
Imenishia imani, hadi shindwa jizuwia,
Katika majina haya, wakuu fafanueni.
Mapadri Kanisani, naomba nifasiliya,
Mashee Msikitini, ebu chambueni aya,
Sikumi wala ishirini, majina manne haya,
Katika maana haya, wakuu fafanueni.
Bun Ally Kibaoni, ni mwana wa Mnyongea,
Sikuzaliwa Andeni, Waikwiriri sikiya,
Mtaa uwe kusini, Rufiji yangu wilaya,
Katika majina haya, Masikofu fasilini.
Kaditama-No-Ageni, hapa mwisho nakomeya,
Wabara na Visiwani, majibu na subiriya,
Dk. Mengi sineni, zidi nilouziya,
Katika majina haya, wakuu fafanueni.
Dk. Shamte Ally Mpita (Mnyongeya),
C/o Lamba Lamba Kibaoni Wazo Hill,
Dar es Salaam.
Kulikoni Bungeni -2
1. Illah Mola Manani, wakati umewadia,
Naishika tena peni, ni pate sisitizia,
Siasa iwe pembeni, ukweli twatarajia,
Waliokuwa Bungeni, nini watatuambia?
2. Wizara mambo ya ndani; pesa wameipatia,
Raia tu mshakani, nani atafuatia,
Tukiwa misikitini, wasiwasi hutujia,
Waliokuwa Bungeni, nini watatuambia?
3. Tumewaona Jijini, walikuja tuvamia,
Marungu Msikitini, mabomu walilipua,
Walikufa watu thani, wengine waliumia,
Waliokuwa Bungeni, nini watatuambia?
4. Wengi waliswekwa ndani, makosa wasingizia,
Lengo lilikuwa nini, raia waso hatia,
Kuwatia mashakani, zife zao familia?
Waliokuwa Bungeni, nini watatuambia.
5. Aliyeitwa Hassani, dhamana mkatalia,
Ikiwa ni ndugu Joni, nyumba walimtolea,
Na haikuwa jioni, dhahiri imejionea,
Waliokuwa Bungeni, nini watatuambia?
6. Ikatangazwa Bungeni, sote tuliyasikia,
Adhabu kali jamani, amani walotishia,
Je kule Umasaini, ni nani aligusia?
Waliokuwa Bungeni, nini watatuambia?
7. Sime kubwa mikononi, na moto walitumia,
Wakachoma hadharani, na sababu wakatoa,
Wameijenga amani, msemayo Tanzania?
Waliokuwa Bungeni, nini watatuambia?
8. Wamekataa imani, inayowaharibia,
Ya kwao tangu zamani, Ubabe wametumia,
Makanisa taabani, moto yameteketea,
Waliokuwa Bungeni, haja hamkusikia.
9.Kwa vile siyo Shabani, mabomu yalisinzia,
Wakenda kwa fulani, hilo kushughulikia,
Na kodi Umasaini, vizuri yaendelea,
Waliokuwa bungeni, nini watatuambaia?
10. Machungu mengi moyoni, nashindwa kuvumilia,
Bora wachie peni, machozi yamezidia,
Nashitaki kwa manani, Illah tuhukumia,
Sizitaki kampeni, Wabunge mmetuboa!!!
Wabillah Taufiiq
K.S. Luanda (NOLO),
Dar es Salaam.

|
YALIYOMO
TAHARIRI:
Dawa ya ugaidi si kufanya ugaidi ndani
ya ugaidi
Bakwata yalaani ubabe wa Marekani
Na Mwandishi Wetu
Wanakijiji wawapiga Polisi
Olesiva
Na Mwandishi wetu, Arusha
Waislamu washinda kesi Same
Na Mwandishi Wetu, Same
Wasafiri ATC wadai ndege ya Jeddah
inahujumiwa
Na Mwandishi Wetu
KOSOVA: Bosnia nyingine
Mahojiano kati ya CNN na Bwana Usama
bin Ladin
Historia ya damu za mashujaa Afghanistan
Msikiti wa Wagoma Kigoma wapata
viongozi wapya
Na Suleiman Simba, Kigoma
Muhadhara wanguruma Masjid
Hijaz
Na Said Shariff
Waislamu waitumie Misikiti
ipasavyo
Na Ashraf Yusuph, Moshi
Mpango wa kudhibiti uzazi utawaangamiza
wengi
Na Mwandishi Wetu
Hoja za kutofautisha Yesu na Issa
ni udhaifu, ni uzushi mtupu! - 3
Na Muhibu Said
Wanawake wa Kiislamu washiriki
maonyesho ya kilimo
Na Habiba Swedi
Wanawake wa Kiislamu washauriwa
kupigania haki zao
Na Habiba Swedi, Arusha
Africa Muslims Agency: Inavyohudumia
jamii
Na Mwandishi Wetu
Kitengo cha Zakkah chasafirisha wanafunzi
Na Mwandishi Wetu
Kupinga kifo cha Yesu ni kumpinga
Mungu?
Mahfudhi M. Mahfudhi
MAONI: Porojo za Ngatara -2
Zanzibar na biashara ya utumwa
Na J. Hussein
Marekani ishitakiwe
Na Abubakar Msham
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO
LA TANZANIA - 3
Mafundisho ya Quran
Barua za wasomaji
Mashairi
Masomo ya dini ya Kiislam
Chakula na Lishe
|