AN-NUUR
Na.164 Jamada Awal 1419, Agosti 28 - Septemba 3, 1998
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
Bakwata yalaani ubabe wa Marekani 

- Yasema sheria haziruhusu 
- Serikali yapiga kimya
- UN yakiri ni kosa lakini yagwaya

Na Mwandishi Wetu

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoani Mwanza limesema kwamba linalaani kitendo cha Marekani kuzipiga mabomu nchi za Sudan na Afghanistan. 

Viongozi wa ngazi za juu wa Baraza hilo wamesema kwamba wanashutumu vikali ugaidi uliofanywa katika balozi za Marekani Nairobi na Dar es Salaam lakini pia wamepinga upigwaji mabomu nchi za Sudan na Afghanistan japokuwa imedaiwa kwamba ni kulipiza kisasi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Agosti 22, katika Baraza la Maulid huko Sengerema; Sheikh wa Mkoa Sheikh Salum Hassan Ferej na Makamu Mwenyekiti wa Bakwata Sheikh Idrisa Omar, wamelaani vitendo vya mauaji yanayofanywa kwa sababu yoyote ile iwayo kinyume na sheria.

Sheikh Idrisa Omar amesema kuwa ule wa Dar es Salaam na Nairobi ni ugaidi hata ule wa nchi kuipiga mabomu nchi nyingine ni ugaidi vilevile. Hivyo wote ni wa kupingwa.

Amesema ilichofanya Marekani ni ugaidi kwani hata kama ni kulipiza kisasi, ilitakiwa ifuate sheria na taratibu za kimataifa.

Bakwata Mkoani Mwanza ilifanya Maulid Wilayani Sengerema usiku wa kuamkia Agosti 22, ambayo ilifuatiwa na Baraza la Maulid ambapo mgeni rasmi alikuwa Bw. Jarufu Hamudi Kulindwa Diwani kata ya Pamba akimwakilisha Meya wa Mwanza.

Kauli hii ya Bakwata Mkoani Mwanza inaungana na wapenda amani, watetezi wa haki na utawala wa sheria kote duniani.

Watu mbali mbali waliohojiwa na Shirika la Habari la B.B.C. wameonyesha kusikitishwa kwao na hatua iliyochukuliwa na Marekani kuzishambulia Sudan na Afghanistan wakati hata huo uchunguzi wenyewe haujakamilika.

Aidha wameonyesha kusikitishwa na tabia ya Marekani ya kujichukulia sheria mkononi bila hata ya kufuata taratibu zilizowekwa na Umoja wa Mataifa.

Walisema ni kitu cha ajabu kwamba Marekani imejipa uhakimu, ujaji, muendesha kesi, shahidi na mnyongaji. Katika hali hiyo wamesema hata huo uchunguzi wenyewe sasa hauna maana.

Wakati serikali za Uingereza na Israel ziliunga mkono Marekani, Cuba ilisema kwamba Rais Clinton alipuuza na kutokujali mamlaka ya Sudan na Afghanistan ili kufunika aibu yake na Monica.

Kiongozi wa Taliban Mullah Mohamed Omar amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba mashambulizi ya Marekani ni kielelezo cha chuki ya Marekani dhidi ya wananchi wa Afghanistan. Akaongeza kusema kwamba Osama bin Laden hana kambi Afghanistan.

Nchi mbali mbali duniani ikiwemo Tanzania zilijitokeza kwa vinywa vipana kulaani vigendo vya kigaidi vilivyofanywa dhidi ya balozi za Marekani.

Hata hivyo takriban nchi zote hizo zimekosa kauli juu ya tendo la Marekani kuzishambulia Afghanistan na Sudan. Nyingi zimekaa kimya kama ilivyofanya Tanzania.

OAU kupitia kwa Katibu Mkuu wake Bw. Salim Ahmed Salim ilitoa maneno omakali sana kulaani ugaidi dhidi ya balozi za Marekani. Hata hivyo kufuatia shambulio la Marekani alichoweza kufanya katibu huyo wa OAU ni kusema; "I am deeply concerned" 

Vyovyote tafsiri ya kauli hiyo inavyoweza kuwa lakini si kulaani kama alivyofanya hapo awali. Hali ni hivyo hivyo kwa Baraza la Umoja wa Mataifa.Katibu Mkuu wake Bw. Koffi Anan naye aliishia kusema kwamba ameguswa sana.

Marekani imedai kwamba imekishambulia kiwanda cha Sudan ambacho inadai kinatengeza silaha za sumu. Imedai kwamba inaushahidi wa kutosha unaoonyesha kwamba kiwanda hicho kinatengeneza gesi ilitwaya ‘VX nerve gas’ inayotumika kutengenezea silaha za sumu. Marekani ilikishambulia kiwanda hicho kwa Makombora yaitwayo, "Tomahawk Cruise Missile’ yenye urefu wa meta 5.5 na uzito wa Kgs.1,193 yakiwa na mwendo (speed) wa kilometa 880 kwa saa na uwezo wa kupiga umbali wa masafa ya kilometa 1600.

Hata hivyo watu mbali mbali akiwemo Mhandisi Tom Kanaffin aliyesaidia ujenzi wa kiwanda hicho mwaka 1990 ameyatilia mashaka madai ya Marekani na kusisitiza kwamba kiwanda hicho hakihusiki na utengenezaji wa silaha za kemikali.

Nayo Serikali ya Sudan imeyakanusha madai ya Marekani na kudai ni ‘Mzaha mkubwa’.

Serikali ya Sudan imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulani tendo la Marekani na kupeleka tume ya uchunguzi kuangalia ukweli wa madai ya Marekani.

Hata hivyo Baraza hilo limekutana, lakini likashindwa kutoa uamuzi wowote; baada ya kuambiwa na Marekani kwamba hakuna haja ya kufanya uchunguzi.

Baraza hilo la Usalama limeishia kusema kwamba linahitaji muda zaidi kutafakari.

Akihojiwa na Shirika la Habari la B.B.C. hivi karibuni mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo Bibi Roze Adera kutoka Kenya alikiri kwamba tendo la nchi kuipiga nchi nyingine ni kosa; lakini akasema wanahitaji muda zaidi kupata mawazo ya nchi nyingine zaidi ya Sudan ndipo waamue kulaani au kutokulani na ama iundwe tume ya uchunguzi au la.

Ni kutokana na hali hiyo ya Umoja wa Mataifa kushindwa japo kutoa kauli dhidi ya tendo hili la Marekani, kiongozi wa kidini wa Iran Ayatollah Khamenei amesema kwamba huo ni ushahidi kwamba Umoja wa Mataifa upo kwa maslahi ya Marekani.

Kwa upande wake Talaban imekataa kufanya mazungumzo na Marekani mpaka iombe msamaha kwa tendo lake la ugaidi iliyoifanyia Afghanistan na Sudan na pia ilipe fidia kutokana na hasara iliyosababishwa na shambulio lake.

Maelezo hayo ya Taliban yanafuatia kauli la Marekani kwamba inataka kufanya mazungumzo na Taliban.
 

Juu

YALIYOMO

TAHARIRI: Dawa ya ugaidi si kufanya ugaidi ndani ya ugaidi

Bakwata yalaani ubabe wa Marekani
Na Mwandishi Wetu

Wanakijiji wawapiga Polisi Olesiva
Na Mwandishi wetu, Arusha

Waislamu washinda kesi Same
Na Mwandishi Wetu, Same

Wasafiri ATC wadai ndege ya Jeddah inahujumiwa 
Na Mwandishi Wetu

KOSOVA: Bosnia nyingine

Mahojiano kati ya CNN na Bwana Usama bin Ladin

Historia ya damu za mashujaa Afghanistan

Msikiti wa Wagoma Kigoma wapata viongozi wapya
Na Suleiman Simba, Kigoma

Muhadhara wanguruma Masjid Hijaz
Na Said Shariff

Waislamu waitumie Misikiti ipasavyo
Na Ashraf Yusuph, Moshi

Mpango wa kudhibiti uzazi utawaangamiza wengi
Na Mwandishi Wetu

Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu,  ni uzushi mtupu! - 3
Na Muhibu Said

Wanawake wa Kiislamu washiriki maonyesho ya kilimo
Na Habiba Swedi

Wanawake wa Kiislamu washauriwa kupigania haki zao
Na Habiba Swedi, Arusha

Africa Muslims Agency: Inavyohudumia jamii
Na Mwandishi Wetu

Kitengo cha Zakkah chasafirisha wanafunzi
Na Mwandishi Wetu

Kupinga kifo cha Yesu ni kumpinga Mungu?
Mahfudhi M. Mahfudhi

MAONI: Porojo za Ngatara -2

Zanzibar na  biashara ya utumwa
Na J. Hussein

Marekani ishitakiwe
Na Abubakar Msham

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 3

Mafundisho ya Quran

Barua za wasomaji

Mashairi

Masomo ya dini ya Kiislam

Chakula na Lishe
 
 
 

 

 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita