|
MASHAIRI
Utenzi wa tamasha la Maonyesho ya mavazi Songea
1. Salaam Aleykum,
Umati wa Islamu,
Na Rehema za Karim,
Nawatolea Awali.
2.Awali Niianzishe,
Ndugu Niwakaribishe,
Ahadi Niwafikishe,
Katika Tamasha hili.
3. Lau Ngepata Wakati,
Miaka ya nyuma na kati,
Zingetosha hizi beti,
Kufungulia Kufuli.
4. Zingeghaniwa kwa Wimbo,
Mzuri wenye Marembo,
Walie wivu wa ng’ambo,
Marekani na Itali.
5. Zingeimbwa kwa Maghani,
Wakashangaa majini,
Kwa Nui za Al-wani,
Za kumsifu Jalali.
6. Lakini tunaongea,
Na jua Limetuchea,
Mengi Yametupotea,
Yamebakia Kalili.
7. Umri una Kijicho,
Hukioni Utungacho,
Pindu Ukodoe Macho,
Waambulia Vivuli.
8.Kuwa juani Huoni,
Sikuambii Kivulini,
Zabadilishwa Mewani,
Zote zina Idhilali.
9. Hizi Nyanja za Uzee,
Zianzapo Mvi Chwee,
Vinatoweka vya chee,
Vipawa vingi vya mwili.
10. Pakiongeza Mabwana,
Wakufanyie Hiyana,
Mawazo yako Mapana,
Yarudi kuwa Dhalili.
11. Pamoja Haya Matata,
Bali nitashika Mata,
Na popote Nikisita,
Ni tampa Mwanamwali.
12. Amalizie Kichembe,
Cha kupokea Wajumbe,
Walotoka kila pembe,
Kwa Amri ya Jalali.
13. Wapendwa Wageni wote,
Twaomba Mpige Kite,
Mmevumilia yote,
Vumilieni na Hili.
14. Sasa kwa hii Dibaji,
Tushukuru Muumbaji,
Kujalia kama Haji,
“HIJA” ya Tamasha Hili.
.......inaen delea toleo lijalo
Mwaka mpya wa Kiislamu 1419
1. Moja nne moja tisa, mwaka mpya umefika,
Islam hivi sasa, kote tunafurahika,
Mwaka wa suna ya tasa,tupambe uje pambika,
Wakati wa kuzinduka, ni huu Waislamu.
2. Po pote Waislamu, tuacheni kubweteka,
Mwaka mpya umetimu, ni kheri tukizinduka,
Ni kote kila sehemu, tusichague mipaka,
Wakati wa kuzinduka, ni huu Waislamu.
3. Nasisitiza Elimu, kwetu ilolazimika,
Ni faradhi kwa kaumu, lazima kuelimika,
Tusome tushike zamu, zitupasazo kushika,
Wakati wa kuzinduka, ni huu Waislamu.
4. Elimu ni Mhimili, kidini yafahamika,
Katuusia Rasuli, kabla hajaondoka,
Twende hata kama mbali, Elimu kwenda isaka,
Wakati wa kuzinduka, ni huu Waislamu.
5. Tushikane kwenye dini, dini isiyo na shaka,
Hainayo walakini, kwa Mola yatambulika,
Duniani na Mbinguni, Islamu yatumika,
Wakati wa kuzinduka, ni huu Waislamu.
6. Tushikamane kwa kamba, ngumu isiyokatika,
Si katani si mgomba, Quraani ya Rabuka,
Tushike bila kuyumba, ndipo tutanusurika,
Wakati wa kuzinduka, ni huu Waislamu.
7. Na tusiwe wadhaifu, kusikiza vibaraka,
Tutapata unyongefu, waso sisi kuwashika,
Tujue uharibifu, wa kwao utatufika,
Wakati wa kuzinduka, ni huu Waislamu.
8. Shime kwa Maulamaa, si wakati muafaka,
Msizishike hadaa, dini yetu kuuzika,
Bali huu ni wasaa, yetu kurekebishika,
Wakati wa kuzinduka, ni huu Waislamu.
9. Wajuzeni maamuma, yote yanayopasika,
Elimu kuwapa hima, ujinga kuwaepuka,
Bila ujuzi daima, kwenda mbele ni mashaka,
Wakati wa kuzinduka, ni huu Waislamu.
10. Sote tukubaliane, tuondoe mifaraka,
Si halali tushindane, Waumini kugawika,
Waumini tuungane, aturidhie Rabuka,
Wakati wa kuzinduka, ni huu Waislamu.
11. Tama niliyoyasema, sikusema kwa dhihaka,
Yatakiwa kuyapima, tupavuke pa kuvuka,
Sivyo tutarudi nyuma, kila siku kila mwaka,
Wakati wa kuzinduka, ni huu Waislamu.
Mshauri Mkuu,
Kassim Miraji Haumotile,
S.L.Posta 25578, Dar es Salaam.
Mashujaa Tewa na Dossa
1.Sisi sote wa Karima, na kwake tutarejea,
Kufa jambo la lazima, sote tunaelekea,
Wamepita maasuma, na dini walotgetea,
Tewa umetangulia, akughofiri Karima.
2. Sote tunayo khatima, hayuko wa kubakia,
Na dunia itakoma, uhai kuangamia,
Kisha walofanya wema, peponi wataingia,
Tewa umetangulia, akughofiri Karima,
3. Akughofiri Karima, Tewa umetangulia,
Ulitenda jambo jema, uhuru kupigania,
Wala hukubaki nyuma, heshima kusimamia,
Tewa umetangulia, akughofiri Karima.
4. Ulijua taadhima, ya mtu kuwa huria,
Ndipo uliposimama, na wenzio wenye nia,
Hukujali darahima, ajira ukaachia,
Tewa umetangulia, akughofiri Karima.
5. Harakati zikav uma, nchi ikaitikia,
Huku wewe uko wima, na wala hukutulia,
Lengo tupate heshima, wana nchi Tanzania,
Tewa umetangulia, akughofiri Karima.
6. Mlikuwa kwenye chama, TAA kilotangulia,
Na TANU ikaja nyuma, wito kuuitikia,
Mwalimu wa Butiama, kiti mkamuachia,
Tewa umetangulia, akughofiri Karima.
7. Kisha ikawa salama, huru wakatuachia,
Wakoloni wakahama, kwao wakajirudia,
Ikatwondoka zahama, ikawa twafurahia,
Tewa umetangulia, akughofiri Karima.
8. Ukafanya himahima, Isilamu kutetea,
Nao wayaonje mema, waliyoyapigania,
Nyerere likamuuma, mara akakununia,
Tewa umetangulia, akughofiri Karima.
9. Kisha kufanyiwa njama, kuwa “dini” unatia,
Kwenye siasa ya chama, mambo unayatibua,
Ikafuata dhuluma, uwaziri kukuvua,
Tewa umetangulia, akughofiri Karima.
10. Hukulipakata tama, jingine ukanuia,
Ukasimamia chama, “muslimu welfea”,
Nako akakusakama, mwisho akakifungia,
Tewa umetangulia, akughofiri Karima.
11. Mola akupe rehema, na jaza ilotimia,
Ulifanya mengi mema, sisi tunakumbukia,
Tutayataja daima, na wana kusimulia,
Tewa umetangulia, akughofiri Karima.
12. Umetangulia Tewa, na mwenzio kafatia,
Mashujaa mlokuwa, “waume” wa Tanzania,
Na mwanzo mloelewa, tamu ya kuwa huria,
Na Dossa amerejea, twaomba kughufiriwa.
13. Ni msiba umekuwa, naye kutuondokea,
Wa mwanzo haujapowa, na yeye akarejea,
Twaomba kwa Mola quwwa, na subira kutwekea,
Na Dossa amerejea, twaomba kughofiriwa.
14. Mlijua twaonewa, Wazungu kutawalia,
Nchi inatobolewa, mali wanajitwalia,
Hamasa mkaingiwa, uhuru kupigania,
Na Dossa amerejea, twaomba kughufiriwa.
15. Motakaa alitowa, ipate kuhudumia,
Ikazifanya khatuwa, nchi kuizungukia,
Harakati zikakuwa, watu wakaitikia,
Na Dossa amerejea, twaomba kughufiriwa.
16. Na “Rupia” akatowa, Nyerere kumgawia,
Mithili muajiriwa, akawa atumikia,
Wala bakhili hakuwa, akatoa kutumia,
Na Dossa amerejea, twaomba kughufiriwa.
17. Wamoja nyote mkawa, heshima kupigania,
Hadi huria tukawa, Wazungu wakatwachia,
Yakatwondoka makiwa, na ndoto zikatimia,
Na Dossa amerejea, twaomba kughufiriwa.
18. Malipwa mliyopewa, ni ninyi kuwaondoa,
Wakashika wasokuwa, sifa wakajipatia,
Waasisi wa VIWAWA, Nyerere ‘kitangulia,
Na Dossa amerejea, twaomba kughufiriwa.
19. Nakoma nilojaliwa, witiri zimetimia,
Kwa Mola mtenda pewa, sehemu mlochangia,
Dhuluma mlofanyiwa, Allah atawalipia,
Na Dossa amerejea, twaomba kughofiriwa.
Jihad R; Saballa,
S.L.Posta 347, Shinyanga.
Damu ya Waislamu
1. Ya Rabi Mola Karimu; Muumba hii dunia,
Na ndiye wewe hakimu, siku itapowadia,
Ninaishika kalamu, Rabi kukushitakia,
Damu ya Waislamu, memwagika Tanzania.
2. Tumerushiwa mabomu, risasi kumiminia,
Mekufa Waislamu, wengine wameumia,
Wale walioshutumu, wakaswekwa Segerea,
Damu ya Waislamu, memwagika Tanzania.
3. Kikawa kwetu kisgumu, kipindi kiloingia,
Wakaifukia damu, huku wakishangilia,
Mazishi yalipotimu,wakaja tusimamia,
Damu ya Waislamu, memwagika Tanzania.
4. Ulituona Rahimu, tulivyokiinamia,
Machozi tele na damu, yupi wa kututetea,
Garezani tukadumu, dhamana tukatalia;
Damu ya Waislamu, memwagika Tanzania.
5. Yatima Muislamu, ndo afiye Segerea;
Walipanga tudhulumu, haki ya kuishi pia,
Damu yetu yao hamu, kwa mchanga ifukia,
Damu ya Muislamu, memwagika Tanzania.
6. Amekuwa Mwislamu, shabaha kujifunzia,
Aliyetutoa damu, wakubwa mshangilia,
Bungeni yalipotimu, Makofi walifagia,
Damu ya Waislamu, memwagika Tanzania.
7. Tunakuomba Karimu, Upate tuhukumia,
Waliorusha mabomu, na waliofurahia,
Waliojifanya Walimu, kashfa kututufia,
Pitisha yako hukumu, waondoke Tanzania.
8. Hawa wote madhalimu, Rabi macho wapofua,
Wape adhabu adhimu, washindwe kuangukia,
Wafe kwa magurudumu, maji na risasi pia,
Damu ya Waislamu, memwagika Tanzania.
9.Mola wameuhujumu, Umma ulouridhia,
Hawa siyo wanadamu, uliowatarajia,
Usifuge madhalimu, wakavuruga dunia,
Waliomwaga yetu damu, waondoshwe Tanzania.
10. Mediriki wadhalimu, aya zako kupindua,
Kupotosha kaumu, ione wako sawia,
Wawahishie hukumu, komesha ujahilia,
Wamemwaga yetu damu, Mola twakushitakia.
11.Hakimu wa mahakimu, wewe twakutegemea,
Sicheleweshe hukumu, twaomba kujionea,
Wape wakati mgumu, wazidi kujifutia,
Si halali yetu damu, kwa mchanga ifukia,
12. Tamati Rabi Karimu, ndugu zetu wapokea,
Wape Jannatu Naimu, furaha waongezea,
Na utupe Uislamu; ushindi ulotimia,
Kwa ilomwagika damu, Mola wetu tulijua.
K.S. Luanda (NOLO),
Dar es Salaam.
Chuki twakupa pole
1.Chuki wamekudhulumu, na Chuki kukuchukia,
Chuki uko mahamumu, na wao wafurahia,
Chuki wamekunywa damu, kisha wakajisifia,
Chuki hao wafahamu, kwa dini watuchukia.
2.Chuki inua viganja, nasi tunaitikia,
Chuki Mola ni mmoja, muombe anasikia,
Chuki waliokufuja, Mola atakulipia,
Chuki hao wafahamu, kwa dini watuchukia.
3. Chuki hukuwakosea, wewe ni mwema raia,
Chuki wamekuonea, kwa kuwa Islamia,
Chuki tunakuombea, Mungu akupe afia,
Chuki hao wafahamu, kwa dini watuchukia.
4. Chuki hao mumiani, tumbo wenye kuchumia,
Chuki wewe una nini, hadi wanakuohofia,
Chuki pingu kitandani, haini wakudhania!
Chuki hao wafahamu, kwa dini watuchukia.
5. Chuki wenye chuki nawe, wote tumewatambua,
Chuki Allah yu na wewe, na sisi twakuombea,
Chuki tuungane tuwe, pamoja tuombe due,
Chuki hao wafahamu, kwa dini watuchukia.
Jihad R; Saballa,
S.L.P. Posta 347,
SHINYANGA
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Waislamu hawatokubali kusingiziwa
mambo
Na Mwandishi wetu
Serikali ya Sudan yadhamiria kuleta
amani ya kudumu
Na Mwandishi Wetu
Mwalimu alaumiwa kuwashawishi watoto
waingie ulokole
Na Badru Kimwaga
Wanawake Arusha watakiwa
kutafuta elimu
Na Habiba Swedi, Arusha
Tamsa Tanga yapata viongozi
wapya
Na Masoud Mohamed
Mjue Dr. Abuu Ameena Philips:
Mwanaharakati aliyewasilimisha askari 3000 wa Amerika
Duniani kwa ufupi
Barua ya Ofisa Elimu ina agenda nyuma
yake
Na Mussa Ally Morogoro
Nabii Isa Mwana wa Maryamu ni Yesu
huyo huyo!!
Kuanzishwa ‘Islamic Club’ ni ajenda
ya siri inayoweza kuhatarisha amani Tanzania
Agenda ya siri
Na. Hassan Kimangale
Hatua ya Rais kutengua uteuzi wa
Parole ni ya kizalendo
Na J. R. Msuya
Serikali iwahurumie raia wake
Na BADRU KIMWAGA
Wanawake Waislamu Wilayani
Masasi waanzisha Jumuiya
Na Yousouf S. Kayungilo, Masasi
Kuhifadhika kwa mwanamke ni kuhifadhika
kwa jamii
Na Zuhra Tajiri
Waislamu wekezeni kwenye
kheri -Mwinyi
Na Mwandishi Wetu, Tanga
Biashara ya ufuska yavamia
Z’bar Polisi uchwara’ wanufaika
Na Rajab Rajab
Asimamishwa uongozi kwa kutoa
fat’wa ya Hitma
Na Nadhiru Ishengoma Wetu , Kahama
Aqswa waazimia kufuata Qur’an
na Sunna
Na Mwandishi Wetu
Mafunzo ya Quran
Barua za wasomaji
Mashairi - uzawa wa Mtume (S.A.W)
Masomo
Chakula na Lishe
|