AN-NUUR
Na.161 Rabiul Thani 1419, Agosti 7-13, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
TAHARIRI
Tujali maslahi ya nchi

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Yusuf Rajab Makamba amekuwa akifanya ziara kutembelea wananchi katika sehemu mbalimbali mkoani kwake. Pamoja na mengi anayoripotiwa na vyombo vya habari kuyagusa katika mikutano yake ya hadhara ni suala la Mwembechai. 

Kama vyombo vya habari vimeripoti sawasawa; inaarifiwa kwamba Mhe. Mkuu wa Mkoa anajigamba kwamba ‘Itqaaf’ zinazofanywa na waathirika wa tukio la Mwembechai haziwezi kumdhuru. 

Si jukumu letu kujadili hapa kuwepo au kutokuwepo ‘Itiqaaf’ zinazofanywa kwa kuelekeza maombi dhidi ya Mhe. Makamba. 

Linalosikitisha ni jinsi suala zito kama hili linavyofanywa jepesi; jambo la masikhara na la watu binafsi. Hili si suala la Mhe. Yusuf Makamba na wakaa Itqaaf. Hoja au suala la kuzungumzwa hapa si Mhe. Makamba "kusomewa Itqaaf’ na matokea yake. 

Suala hapa ni uonevu na udhalimu wanaofanyiwa baadhi ya wananchi! Suala hapa ni kutizama masilahi ya kudumu ya Taifa na nchi hii na wala si kunawiri mtu binafsi kama alivyowahi kusema Mhe. Augustino Mrema kwamba Itqaaf zinamfanya anenepe! 

Suala hapa ni kwamba watu wameuliwa pale Mwembechai. Wananchi na Wabunge wao wanahoji nani katoa amri ile ya kuua. Ni sheria gani ya nchi; au ya jeshi la polisi iliyohalalisha mauaji yale! 

Polisi wamevunja msikiti; wamewadhalilisha wanawake; wamewatesa wazee wasio na hatia kinyume cha katiba; sheria za nchi na kinyume cha matamko mbalimbali ya jumuiya ya kimataifa juu ya haki za binaadamu. Haya ndiyo masuala ya kutolea ufafanuzi kwamba serikali imeyafanya kwa misingi ipi na kwa kufuata kanuni zipi! 

Leo mtu anaweza akawa ni Mkuu wa Mkoa na kesho asiwepo. Aidha mtu aweza leo kuwa mzima na kesho hali ikawa nyingine kabisa. Na hii haitegemei itqaaf. Vilevile kutokea kwa yote haya kwa mtu binafsi kwaweza kusiathiri chochote maslahi ya Taifa na nchi kwa ujumla. 

Lakini suala la amani na utengamano wa nchi haliwezi kuwa suala binafsi. Linamgusa na kumuathiri kila mwananchi. 

Dhulma na uonevu hauwezi kudumisha amani. Dhulma na uonevu hauwezi kuleta utengamano. Ndio maana kila mwananchi mwenye busara atafanya kila awezalo kupiga vita dhulma na uonevu ili kujenga mazingira madhubuti ya kudumisha amani. 

Waliouliwa pale Mwembechai ni wananchi wa nchi hii. Wana haki ya kuishi kwa haki yao ya asili toka kwa Mola wao na kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi hii. Kuwaua ni kukiuka haki na sheria hizi. 

Wapo askari waliovunja msikiti na kuwadhalilisha wanawake. Hii ni kinyume cha sheria, maadili na kanuni zote za kimataifa. 

Wapo wazee waliokamatwa na kuteswa bila ya hatia na kisha baadae kuachiwa kwa maelezo kwamba hawana kosa. 

Yote haya ni udhalimu, uonevu, unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binaadamu uliopevuka. 

Waislamu kwa haki yao ya uananchi, wanawajibu wa kukataa kufanyiwa dhulma. Wajibu huo ni agenda muhimu kwao kwani ndio njia pekee ya kuinusuru nchi yetu huko mbele ya safari. 

Tunataraji kila kiongozi na kila mwananchi aione dhulma hii na afanye kila awezalo kuindosha. 
Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI  

Waislamu hawatokubali kusingiziwa mambo 
Na Mwandishi wetu 

Serikali ya Sudan yadhamiria kuleta amani ya kudumu 
Na Mwandishi Wetu 

Mwalimu alaumiwa kuwashawishi watoto waingie ulokole 
Na Badru Kimwaga 

Wanawake Arusha watakiwa kutafuta elimu 
Na Habiba Swedi, Arusha 

Tamsa Tanga yapata viongozi wapya 
Na Masoud Mohamed 

Mjue Dr. Abuu Ameena Philips: Mwanaharakati aliyewasilimisha askari 3000 wa Amerika 

Duniani kwa ufupi 

Barua ya Ofisa Elimu ina agenda nyuma yake 
Na Mussa Ally Morogoro 

Nabii Isa Mwana wa Maryamu ni Yesu huyo huyo!! 

Kuanzishwa ‘Islamic Club’ ni ajenda ya siri inayoweza kuhatarisha amani Tanzania 

Agenda ya siri 
Na. Hassan Kimangale 

Hatua ya Rais kutengua uteuzi wa Parole ni ya kizalendo 
Na J. R. Msuya 

Serikali iwahurumie raia wake 
Na BADRU KIMWAGA  

Wanawake  Waislamu  Wilayani Masasi waanzisha Jumuiya 
Na Yousouf  S. Kayungilo, Masasi 

Kuhifadhika kwa mwanamke ni kuhifadhika kwa jamii 
Na Zuhra Tajiri 

Waislamu  wekezeni kwenye kheri -Mwinyi 
Na Mwandishi Wetu, Tanga 

Biashara ya ufuska yavamia Z’bar Polisi uchwara’ wanufaika 
Na Rajab Rajab 

Asimamishwa uongozi kwa kutoa fat’wa ya Hitma 
Na Nadhiru Ishengoma Wetu , Kahama 

Aqswa waazimia kufuata Qur’an na Sunna 
Na Mwandishi Wetu 

Mafunzo ya Quran  

Barua za wasomaji  

Mashairi - uzawa wa Mtume (S.A.W)  

Masomo  

Chakula na Lishe  
 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita