AN-NUUR
Na.159 Rabi' Awal 1419, Julai 24 - 30, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
MADRASA
Ijue Madrasa Najah 

Hii ni miongoni mwa madrasa kongwe kabisa za mjini Iringa. Ipo katikati ya mji jirani na msikiti mkuu wa Ijumaa. Hivi sasa ina wanafunzi wapatao 310 wakiwa wamegawanywa katika madrasa manne yaani la kwanza hadi la nne. 

Pamoja na masomo ya kawaida ya Maarifa ya Uislamu masomo ya shule kama kusoma na kuandika pamoja na hesabu kwa watoto wadogo hufundishwa. 

Kwa wanafunzi wa darasa la saba na wale wa sekondari hupewa pia masomo ya ziada maarufu kwa jina la tuition. 

Wanafunzi wa madrasa hii hawalipi ada halikadhalika madrasa hujitahidi kuwapatia vitabu. Waalimu wanaoendesha madrasa hii ni Ustadh Dhulkifl Omar, Haruna Mamba, Mohamed Mahmoud na Mohamed Ali. Wengine ni Mansour Ali, Ahmada Madijimbay, Swaleh Abdullatif na Ustadhat Fatihia Ahmad. 

Miongoni mwa matatizo makubwa wanayoikabili madrasa hii ni pamoja na kukosa miradi ya kuingiza fedha au wafadhili wa kulipia posho za waalimu pamoja na vifaa. 

Sehemu ya kusomea pia ni finyu ,jambo linalohitajia kuwepo kwa juhudi za kujenga jengo jipya la madrasa 

Pamoja na masomo madrasa, Najah ina timu yake ya michezo na mazoezi kwa watoto husisitizwa. 
 
 

Ijue Madrasat Dhynurayn 

Hii ni madrasa iliyopo mjini Iringa ambayo ilianzishwa mwaka 1986 na Taasisi iitwayo Dhynurain. Madrasa hiyo hivi sasa ina wanafunzi wapatao 300 wakiwa katika madarasa sita tofauti. 

Kiwango cha elimu kitolewacho ni kile cha Ibtidaiya kikijumlisha masomo ya Tawheed, Fiqh, Qur-an, Sirah na Lugha ya Kiarabu. 

Kuongeza idadi ya wanafunzi na kutoa viwango vya juu zaidi vya elimu ikiwa ni pamoja na sekondari, vyumba zaidi vya madarasa vinaongezwa na sasa hivi tayari vyumba vinane vipo katika hatua za mwisho za kukamilika. 

Wanafunzi wanaosoma katika madrasa hiyo wamewajibika kujinunulia vitabu na madaftari lakini hawalipi ada, wengi wa waalimu wanaosomesha ni wenye elimu ya kiwango cha Chuo Kikuu kutoka vyuo vikuu vya Kiislamu mashuhuri kama Al-Azhar na wachache ni wa kiwango cha sekondari. 

Pamoja na madrasa hiyo ya watoto Dhynurain inaendesha Chuo katika eneo la Ipogolo ambacho huelimisha vijana toka vijijini ili wakirejea wakafanye kazi ya Da’wah katika maeneo yao. 

Chuo hicho kilianza mwaka 1995 na wanafunzi 20; na hivi sasa wapo wanafunzi 60 kutoka vijiji mbalimbali vya mkoa Iringa, Mbeya na Ruvuma. 

Pamoja na kupewa elimu bure wanafunzi hao hupewa malazi, chakula na fedha kidogo za kununulia sabuni. Baadhi ya wanafunzi ambao walimaliza chuoni hapo mwaka 1997 walipatiwa nafasi ya masomo ya juu zaidi katika Chuo cha Imam Shafii, Tanga. 
 

Ijue Markaz Arusha al Islamiy 

Na Shaaban Rajab 

ARUSHA Islamic Centre (Markaz Arusha Al- Islamiy) ipo katika eneo la Majengo Urundini mkoani Arusha, umbali wa kilometa 2.30 kutoka Arusha mjini. 

Chuo kilianzishwa mnamo mwaka 1990 kikiwa kinaongozwa na Mwalimu mmoja Ustaadh Yahya Samli kwenye nyumba ya mtu binafsi ya Mzee Farjallah Hussein katika mtaa wa Sakina Arusha ambaye alijitolea muhanga ili kufanikisha kuanzishwa kwa chuo hiki. 

Miaka miwili baadaye, Mzee Issa Saleh mkazi wa Makao Mapya alitoa nyumba yake yenye vyumba vinane iliyopo mtaa wa Levolosi kwa ajili ya kufanywa madrasa. 

Baada ya kupatikana kwa nyumba hiyo, chuo kilihamishwa kutoka Sakina kwenda Levolosi. 

Kutokana na jitihada za Waislamu, chuo kilipata waalimu wengine na kufikia idadi ya walimu saba, wanne kati yao kutoka katika vyuo vya Kiislamu vya Saudi Arabia na Pakistani na watatu walikuwa wa hapa nchini na nchi jirani ya Kenya. 

Baada ya miaka miwili kupita, chuo kilipata kiwanja chenye ukubwa wa ekari mbili katika eneo la Urundini Majengo ambapo ujenzi wa majengo rasmi ya chuo ulianza pamoja na miradi mingine ya chuo. 

Hadi hivi sasa chuo kina vyumba vitano vya madrasa na ofisi mbili za mwalimu mkuu na ya walimu wote (staff), msikiti pamoja na vyoo. 

Chuo kimegawanyika katika mikondo miwili ambayo ni Ibtidai yaani elimu ya msingi ambapo katika mkondo huu, mwanafunzi anapokelewa baada ya kumaliza masomo ya miaka mitatu kutoka katika matawi ya chuo ya Levolosi na Nduruma. Hadi hivi sasa mkondo huu una wanafunzi 120. 

Mkondo wa pili ni Mutawasit yaani mkondo wa kati ambao wanafunzi husoma kwa muda wa miaka mitatu na hapo tayari atakuwa na uwezo mkubwa wa elimu ya dini na kusoma, kuandika na kuzungumza lugha ya Kiarabu. 

Mkondo huu una wanafunzi 95 na jumla ya wanafunzi wote ni 215. 

Masomo yanayofundishwa ni Tafsiri, Hadithi, Kuhifadhi Qur’an, Mustwalahal-Hadith (uchambuzi wa Hadith), Tauheed, Nahau Swarfa, Tajwidi, na Historia ya Kiislamu. 

Mwanafunzi anapohitimu anapewa cheti (Certificate) na kuombewa katika vyuo vya nje ya nchi hususan katika nchi za Saudia Arabia (Madina), Khartoum Sudan na Mombasa Kenya kuendelea na elimu ya juu zaidi. 

Mpaka sasa kuna wanafunzi wengi waliohitimu katika chuo hiki na wanaendelea kusoma kwenye vyuo vya nje. 

Markaz Arusha Al Islamiy ina wanafunzi kutoka katika mikoa mbalimbali nchini kama vile Dodoma, Singida, Mtwara, Kilimanjaro, Dar es Salaam na Arusha. 

Chuo kina mpango wa kuongeza miradi zaidi ili kiweze kujitosheleza na kujiendesha. Baadhi ya miradi hiyo ni kuanzisha kitengo cha ufundi ili wanafunzi wawe na uwezo wa kujiajiri wanapohitimu, kujenga zanahati, kuongeza matawi katika maeneo mengine na kufungua Thanawil (High School). 

Hata hivyo, bado chuo kinakabiliwa na matatizo mbalimbali ambayo kwa njia moja au nyingine yanakwamisha juhudi za kutoa elimu chuoni hapo. 

Matatizo hayo ni ukosefu wa nyumba za walimu, vyumba vya kulala wanafunzi kutoka mikoani, uzio wa kuzunguka chuo, matatizo ya kifedha na madarasa. 

Kutokana na matatizo hayo, mkuu wa chuo Ustaadh Ally Othman anawaomba Waislamu pamoja na taasisi mbalimbali kutoa mchango wao ili kukinusuru chuo na elimu ya Kiislamu kwa ujumla. 

Chuo kinaongozwa na Ustadh Ally Othman na msaidizi wake Ustaadh Yahya Samli. 
 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI 

Maoni yetu: Umakini wa Wabunge unatia wasiwasi 

AGIZO LA MANISPAA KUPEWA MAJINA YA WANAFUNZI WA KIKATOLIKI 
Na Mwandishi wetu, Morogoro 

Madai ya Ali Ameir kuhusu Chuki yakanushwa 
Na Mwandishi wetu 

AN-NUUR  kwenye Internet 

Mwanamuziki Nyota CAT STEVENS asimulia alivyosilimu 

Watakiwa kuacha kuwatuma watoto mitaani 
Na. Kassim Juma 

Kijana wa Kibarbaig aliyejitolea kupigania dini yake 
Na. Ali Njuki 
 
MAKALA: Zanzibar na tamasha la filamu
Na Said Mzee

'Waislamu wenye sisa kali'
Na. Ustaadh A. S. Fundi 

MAKALA: Maisha ya ndoa kwa Muislamu - 2
Ustaadh Khamis Suleyman Nassoro, Usangi, Mwanga - Kilimanjaro

Pongezi hizi za nini?

Mjibuni Mwinjilisti Kusupa msitukane 
Na Paskal Msemakweli

BARUA YA WAZI KWA WABUNGE

Vigogo wahusishwa na madawa ya kulevya Z'bar
Na Mwandishi Wetu

Da’awa Handeni yashika kasi
Na Ibn Muhammad

Kongamano la vijana wa Kiislamu Masjid Nuur Dar
Na Mwandishi Wetu

Mafunzo ya Quran 

Barua za wasomaji 

Mashairi - uzawa wa Mtume (S.A.W)

Habari za Madrasa 

Masomo 

Chakula na Lishe 
 
 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita