AN-NUUR
Na.159 Rabi' Awal 1419, Julai 24 - 30, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Pongezi hizi za nini 

Wanasheria wana msemo wao mashuhuri unaosema, "Justice delyaed is Justice denied’ yaani haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa. Mtoto Chuki Athumani, mwanafunzi wa shule ya Sekondari, kijana mdogo yatima, amepigwa risasi na polisi kwa makusudi. Akiwa na hali mbaya ya kuuguza jeraha la risasi alifungwa pingu miguuni na baadaye pigu zikahamishiwa mikononi. Mtoto huyu amekuwa katika hali hiyo kwa muda wa miezi minne na siku nne. Ni mgonjwa wa jeraha la risasi, ana pingu hawezi hata kujigeuza vizuri.

Kana kwamba hilo halitoshi kwa muda wote huo hapati matibabu na yuko chini ya ulinzi mkali wa askari kiasi ambacho hata watu wa kawaida wanaogopa kwenda kumwangalia. Mtoto Chuki hospitali ya Rufaa ya Muhimbili iligeuzwa kuwa ndilo gereza lake. 

Hata wale waliopelekwa Segerea hawakufungwa pingu ingawa wote walikosa matibabu. Yeye amefanywa yatima mara mbili, hana baba na kumuhudumia na hana wauguzi wa kumpa dawa na hali yuko hospitali anawaona tu wenzake wanapopewa dawa.

Maelezo ya Waziri Mkuu yalikuwa wakithibitika kuwa wana hatia wataadhibiwa vikali, Polisi waliompiga risasi mtoto chuki walikwisha mhukumu kuwa ana hatia na kwa hiyo kupewa adhabu kali hata bila kufikishwa mahakamani. Amekaa kifungoni "jela’Muhimbili kwa muda wa miezi minne na siku nne. 

Hapa polisi au Wizara ya Mambo ya Ndani ilijichukulia mamlaka ya Wizara ya Sheria ikapitisha hukumu na kumwadhibu mtoto Chuki. Huu ni ukiukwaji wa katiba ya nchi, ukiukwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa sheria pia. Wahusika wa yote haya wameachwa shwari bali wamepongezwa.

Mheshimiwa Kingunge ni Waziri anayeshughulikia habari na siasa katika ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa kuwa ni mtu wa habari na ni hodari wa kazi yake alikuwa anayajua yote yaliyokuwa yanampata mtoto Chuki kwa muda wote. Hatujui kama kumshauri Waziri Mkuu chochote kuhusiana na mtoto Chuki. 

Hapa tunapata hisia mbili. Moja ni kwamba pengine Mheshimiwa Kingunge kwa utu uzima wake, busara zake na uzoefu wake mkubwa wa kazi alimshauri Waziri Mkuu lakini hakusikilizwa. Hili linawezekana hasa tukizingatia namna Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyolishupalia suala la Mwembechai kwa matamko yake makali na mazito ya kutisha. 

Huko Arumeru amekubaliana na madai ya wananchi wa huko akawatekelezea matakwa yao ikiwa ni pamoja na kupunguza kiwango cha kodi kutoka 5,000/- na kuwa 4,000/-.

Ifahamike kuwa wananchi wa Arumeru walijichukulia sheria mkononi. Tatizo la pili ni la Wamasai waliowatishia hata askari wa kutuliza ghasia. Hawa nao walijichulia sheria mkononi. Serikali imewaacha shwari. 

Waislamu wa Mwembechai wamefuatwa na askari ndani ya msikiti na mabuti yao tena usiku wa manane. Waislamu hawa hawajajichukulia sheria mkononi bali polisi wamekwenda kuwachokoza kwenye nyumba yao ya ibada. Walivyoona haikutosha siku ya pili wamekwenda na bundiki na risasi za moto. Huku ni kuazimia kwa makusudi kuua na wakaua.

Hisia ya pili, kama kwa muda huo wote Mheshimiwa Kingunge hakumshauri chochote Mhe. Waziri Mkuu ambaye ni bosi, ni dhahiri kwamba alichokifanya cha kutoka Dodoma moja kwa moja mpaka Muhimili na kuanza kutoa maneno ya faraja kwa mzazi wa mtoto Chuki na kuagiza atibiwe baada ya kuwa amekwishapooza ni kutendo cha kejeli na kutucheza shere Waislamu. Kwa vyovyote huu waweza kuwa ni mchezo wa kuigiza. Baada ya mtoto Chuki kukosa matibabu kwa muda wa miezi minne na siku nne, kuwa kwenye pingu kwa muda huo wote, na kwa kuwa kiwango cha kuumia kwake kulikwisha fahamika na madaktari bila shaka na matokeo yake ya baadaye yalifahamika. Sasa wanatutoa kimasomaso, danganywa-toto kwa maneno mazuri ya faraja na kumtibu mtoto. Tunachotaka si pongezi ni kumuona anatembea.

Haya, Mwenyezi Mungu ajaalie apone atembee ndio basi Waislamu tumeridhika tayari kuwa serikali yetu inatupenda, Rais wetu anatupenda?

Je, Serikali hii inayotupenda imejibu nini hoja za Mheshimiwa K.K. alipotaka maelezo? Mheshimiwa Waziri Mkuu na Ali Ameir wamepiga chenga na kusema wamempeleka hospitali ya MOI na wanamlipIa shs.40,000 kwa siku. Basi ndio hoja zote za KK na Waislamu zimejibwa?

Haya, Mhe. Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na serikali kwa ujumla wake inasema nini juu ya wale waliouliwa kwa risasi na pia marehemu Mohamed Omari aliyefia mahabusu na kuzikwa haraka haraka?

Serikali inasema nini juu ya wale waliouawa kwa risasi pale Mwembechai? Je, hawa uchunguzi wa polisi umekwisha thibitisha kuwa walikuwa na hatia! Kama walikuwa na hatia adhabu yao ilistahili kifo? Je, kama hawakuwa na hatia wale walioua hawastahili adhabu yoyote? Kama walikuwa na hatia je, adhabu ya kifo ndiyo stahilii yao? Hawa waliotoa adhabu hii isiyowastahili basi wao wako huru hivi hivi tu?

Je, Serikali inasema nini juu ya Waislamu walionyimwa dhamana kwa zaidi ya miezi 4 na hali akina Simbaulanga walipewa dhamana haraka haraka? Mhe. Rais anayetupenda" ametamka nini kwa ndugu wa wafiwa wale wa Membechai? Na ametamka nini dhidi ya kitendo cha askari wa kiume kuwavuao nguo wanawake wa Kiislamu hadharani na hali askari wanawake wapo?

Madhila haya yote yamenyamaziwa kimya. 

Huu ni wakati wa muafaka kwetu Waislamu kutumia busara zetu. Haya maneno mazuri ya faraja lazima tuyatafakari kama yana ukweli wowote na sio kejeli na kutupuuza tu.

Ukichunguza matukio tunayofanyiwa Waislamu na jinsi Serikali inavyozima kwa hasira au kwa vitisho kama alivyofanya Mhe. Sumaye safari hii au kwa kunyamaza kimya au kwa kuituma BAKWATA izime kelele za Waislamu.

Kwenye miaka ya 80 huko Mwanza Mwislamu alichomewa vitabu vyake vya dini na kupigwa viboko na sungu-sungu BAKWATA ilisimama na kusema iliyochomwa sio Qur’an. Huko Visiwani Waislamu walipoandamana kupinga kauli ya Sophia ya kutaka kuibadili Qur’an watu waliuawa. Serikali ilichofanya ni kwenda kuwasimanga masheikh kuwa wamechochea fujo na vurugu badala ya kumsimanga yale ambaye hasa ndiye aliyechochea fujo na vurugu lile.

Wakati suala la mabucha ya nguruwe linaunguruma mjini Dar es Salaam huko Arumeru kulitokea mauaji yaliyosabishwa na tofauti za kidini (Ukristo). Namna Serikali ilivyolivalia njuga suala la mabucha ya nguruwe dhidi ya Waislamu ni tofauti kabisa na walivyolishughulikia suala la Arumeru ambako kulitokea mauaji. Baya zaidi suala la mabucha ya nguruwe lilisababishwa na DC wa Kinondoni aliyemtukama Uislamu na Waislamu na pia lilisabishwa na serikali yenyewe kwa kuruhusu kinyume cha sheria mabucha hayo katika maeneo wanamoishi Waislamu kwa wingi. Bado waliodhalilishwa ni Waislamu. Suala la Mwembechai nalo limetokea sambamba na yale ya Wamasai na wananchi wa huko huko Arumeru. Matokeo yake Waislamu wauawa kwa kauli ya serikali na Waziri Mkuu anakwenda kuwabembeleza wananchi wa Arumeru!

Serikali ya awamu ya tatu imejinaki kuwa ni ya Uwazi na Ukweli na kwamba utawala wake ni wa Haki na Sheria. Waislamu tunasubiri kuyaona hayo kuhusiana na suala la Mwembechai. Tunataka wauaji wakamatwe. Waliowadhalilishwa wanawake na kuwatesa Wazee, wafikishwe mahakamani 'inquest' ifanyike na Tume ya uchunguzi iundwe.
 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI 

Maoni yetu: Umakini wa Wabunge unatia wasiwasi 

AGIZO LA MANISPAA KUPEWA MAJINA YA WANAFUNZI WA KIKATOLIKI 
Na Mwandishi wetu, Morogoro 

Madai ya Ali Ameir kuhusu Chuki yakanushwa 
Na Mwandishi wetu 

AN-NUUR  kwenye Internet 

Mwanamuziki Nyota CAT STEVENS asimulia alivyosilimu 

Watakiwa kuacha kuwatuma watoto mitaani 
Na. Kassim Juma 

Kijana wa Kibarbaig aliyejitolea kupigania dini yake 
Na. Ali Njuki 
 
MAKALA: Zanzibar na tamasha la filamu
Na Said Mzee

'Waislamu wenye sisa kali'
Na. Ustaadh A. S. Fundi 

MAKALA: Maisha ya ndoa kwa Muislamu - 2
Ustaadh Khamis Suleyman Nassoro, Usangi, Mwanga - Kilimanjaro

Pongezi hizi za nini?

Mjibuni Mwinjilisti Kusupa msitukane 
Na Paskal Msemakweli

BARUA YA WAZI KWA WABUNGE

Vigogo wahusishwa na madawa ya kulevya Z'bar
Na Mwandishi Wetu

Da’awa Handeni yashika kasi
Na Ibn Muhammad

Kongamano la vijana wa Kiislamu Masjid Nuur Dar
Na Mwandishi Wetu

Mafunzo ya Quran 

Barua za wasomaji 

Mashairi - uzawa wa Mtume (S.A.W)

Habari za Madrasa 

Masomo 

Chakula na Lishe 
 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita