|
|
|
Ustaadh Khamis Suleyman Nassoro, Usangi, Mwanga - Kilimanjaro "Mambo ya nyumba kunga, Aibu kuyaeleza". Wanaambiwa hapo hao waamuzi kama ikiwa kweli nia yao ni kupatanisha basi Allah s.w.t. atawasaidia mpaka yapatikane hayo mapatano ya kheri waliyoya kusudia na Allah anajua nia ya kila mtu; huwezi kumficha. Basi wanahimizwa hapa watu wawe na nia nzuri, na mapendeleo ya kheri juu ya wenzi wao. Isiwe kama baadhi ya viongozi wa dini wanavyoweka mbele maslahi binafsi, kutaka wapate ufadhili fulani ama na mume au na mke ndipo ampe upendeleo katika suluhu hiyo, badala ya nia ya kupata thawabu za kuwafanyia watu suluhu. Na vile vile huyo mke na mume (wasuluhishwaji) wanaambiwa wawe na nia nzuri ya kupatana kwani ‘‘upatana ndio kheri.’ Asiwe kila mmoja kashadidia aliposhadidia – hataki ila hilo alilokuwa akilitaka tu. Isiwe hivyo. Bali wasikilize maneno ya hao waamuzi ili wapate kupatana. Sharti kila mmoja aridhie kusamehe baadhi ya haki zake, sio kushikilia – ndindindi; habanduki alipo. Isiwe hivyo. 36 – "Mwabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni ihsani wazazi wawili, na jamaa na mayatima na masikini na jirani walio karibu na jirani walio mbali, na rafiki walio ubavuni (mwenu) na msafiri aliyeharibikiwa, na wale iliyowamiliki mikono yenu ya kulia (kuume). Bila shaka Allah hawapendi wenye kiburi wajivunao." (4:36). 36 – Wanaamrishwa watu hapa kumwabudu Mwenyezi Mungu tu peke yake, na wamwombe Yeye tu peke yake – Mwombwa Yeye tu Rabbana. Iyyaka naabudu waiyyaka nastainu. (Wewe tu peke yako ndiye tunayekuabudu na Wewe tu peke yako ndiye tunayekuomba msaada). Sura ya 1 Aya ya 5 – Sura ya kufungua kila maombi ya kheri, na ndiyo inatumika katika sala zote- (Tunarudi kwenye yale ya Aya 36). Na waamrishwa wawafanyie ihasani wazee na wengine hao waliotajwa hapo; hata wakiwa hawawakhusu "Ndewe wala sikio; na hata wakiwa si Waislamu. Hata Waislamu wasiosoma wanajua hayo. Utawasikia wanasema ‘Allah Allah Jirani – Walau kaana Baniyani!’ Basi ndiyo hivi Uislamu unavyosema. Na huyo rafiki wa ubavuni, ni yule unayekuwa naye sana, kama Mke (na jamaa zake), Mume (na jamaa zake), Rafiki, unayefanya kazi naye pamoja , na kama hawa. Na ndio huwa mara nyingi mtu kuwasahau. Huenda kuwatafuta walio mbali akawasaidia akawasahau hawa walio ubavuni mwake. Ndio maana ikazidi kuhimizwa hapa. Wakamilishiwe hawa kwanza ndipo utoke nje! ‘Mambo kwa daraja’. Inasemwa kwamba: "Kuweka kitu pasipokuwa mahala pake, ni kama kudhulumu." Basi kuwasaidia walio mbali ukawatupa walio karibu hakukupi thawabu; kutakupa dhambi, kwani ni kudhulumu. (Na Mtume s.a.w. amesema: "Kanihusia mno Jibrilu juu ya wema kwa jirani hata nikadhani atampa haki ya kurithi mali ya jirani wake). Na mwisho wa Aya hii ya 36 mpaka mwisho wa Aya ya 38, wanatajwa watu wabaya asiowapenda Mwenyezi Mungu. Tafauti ya kibri na fakhri ni kuwa: Kibri huwa katika moyo –ukajiona nani kama wewe. Na yakijaa hayo katika moyo, hudhihiri katika maneno kwa kujisifu mwenyewe, kutukana wengine, na kama haya. Kisha hudhihiri katika vitendo – kwa kuwatazama watu kwa jicho la kejeli, kutowajali wanapompitia wakamtolea salamu, kutowaendea katika shughuli zao – na kama haya. Basi kibri kikifika daraja hii huitwa fakhri vile vile. (Ikitokea kuwepo kwa tabia hiyo ya kibri katika nyumba – kama ni mwanamke ni kheri mume amtaliki, au ni mume, basi mke ni bora amuombe kumuacha – ingawa talaka ni halali anayoichukia Mwenyezi Mungu) 37 –"Ambao hufanya ubakhili (wao) na kuwaamuru watu (wengine) kufanya ubakhili (pia kama wanavyofanya wao),na wanayaficha aliyowapa Allah kwa fadhila zake. Na tumewaandalia makafiri adhabu ifedheheshayo." (4:37). Kuficha aliyowapa Mwenyezi Mungu kama vile mtu kuwa na ilimu asiwafundishe watu – akafa nayo. Kama watu wengi walivyokuwa wakifanya zamani. Na wako wanaofanya mpaka sasa pia. Hawakubali kumfundisha mtu, au watamfundisha mtu mmoja tu hivi au wawili watatu waliomkhusu kweli kweli, kwa kuona kuwa riziki yake itakatika, itachukuliwa na hao anaowafundisha. Wala sivyo, kwani kila mtu ana riziki yake, haizidi haipungui. Hata tukisema hataaniwa yeye tu sasa peke yake – wataendewa na hao wengine pia – basi iko nini? Si anajipatia thawaba kabisa za tangu uhai wake mapaka kufa kwake, maadamu ilimu yake ile inaendelea kutumiwa? Kuna riziki kubwa kuliko hii itakayomfaa Akhera wala haitamdhuru duniani? Lakini watu hawataki Akhera. Maangalizi yao ni kutazama tu dunia, kama alivyosema Allah s.w.t. kuwa: "Bali nyinyi mnafadhilisha (starehe za) uhai wa dunia, na hali ya kuwa Akhera ndiyo bora na ndiyo ya kusalia milele." (87:16-17). (Na ukishinda mtihani wa ubakhili katika kuitoa neema ya ilimu kwa wengine wanaoihitaji, basi katika neema nyinginezo utashinda sana – maana hakuna neema bora zaidi kuliko ilimu inayokufikisha mpaka Akhera pa milele, wakati nyingine zote manufaa yake huishia duniani tu). 38 – "Ambao wanatoa mali zao kwa kuonyesha watu wala hawaamini (aliyoyasema) Mwenyezi Mungu wala siku ya mwisho. Na yule ambaye amekuwa shetani ndiye rafiki yake, basi ana rafiki mbaya kabisa." 4:38 – Anayetaka alipwe hiyo Pepo na Mwenyezi Mungu, basi sharti awe anafanya hayo mema yake kwa ajili ya Allah s.w.t., siyo kwa ajili ya kuwa watu wamwone wamsifu. Atakayefanya kwa nia hiyo hatakuwa na malipo yoyote Akhera; kwani kataka aonekane duniani, na keshakuonekana (basi Akhera ataruka patupu), Na huo ni mwisho wa kumnukuu Sheikh Al-Farsy – kwenye tafsiri yake kwa Aya hizo – 34-38, Maelezo yake, pamoja na nyongeza katika mibano kutoka kwetu. Humo tutafaidika na mengi ambayo yamechangia sana kwenye makala yetu. Hii ni njia nyingine ya kujiongezea ilimu bila ya kwenda chuoni ikiwa utayahifadhi. Mtume S.A.W. ametaja pia na sababu za kutoziweka mbele sifa za mali na uzuri katika kuchagua mchumba pale aliposema: "Msioe wanawake kwa kuchagua uzuri wao, ‘asaa uzuri wao ukawa maangamizo kwao; wala msiwaoe kwa kuchagua utajiri wao, ‘assa mali zao zikawapelekea kuhalifu. Lakini waoeni kwa kuangalia imani yao ya dini, hakika kijakazi sura mbaya na rangi nyeusi, mwenye imani ya dini ndiye mbora kabisa." Na hii ni kwa sababu mke ndiye msaidizi na mshauri wa mumewe katika maisha. Na mwenye dini atashauri katika yenye lengo sahihi la kuumbwa – yaani kumuabudu Muumba – Allah (S.W.T.), atashauri kutosahau sala, zaka, saumu na kuishi kwa maadili mema katika jamii – uvumilivu, kutosheka, bila kuwa na tamaa mbaya. Na maisha ya namna hii kuleta baraka na rehema katika nyumba na kujenga kizazi chema. Siku moja Mtume (s.a.w.) aliongea na Sayyidna Omar Al-Khattab R,A, akamwambia: "Ee Omar! Nikuwelekeze kwenye hazina isiyoisha?" Omar akasema: "Bila shaka!" Mtume s.a.w. akamwambia: "(Hazina hiyo) ni mke mwema – ambaye ukimtazama unafurahi, ukimwamuru jambo anakutii, na unapotoka nyumbani anakulindia mali yako na nafsi yake)". Hii ni kama alivyosema katika Hadithi nyingine kuwa: "Dunia ni muhula wa starehefupi tu, na starehe yake iliyo bora, ni mke mwema nyumbani." (siyo magari barabarani, na nyumbani….! (imepokewana Imamu Muslim). Ni busara basi – kwa hiyo, vijana Waislamu wakabadilika katika kuandaa ndoa zao, na badala ya kumgharimia ili asomee kazi ya heshima mchumba anayekusudiwa, bora kumsomesha dini na mengine yote yatajileta yenyewe bila ya taabu. Kuelimishwa Waislamu wanaume na wanawake katika imani ya dini, jukumu ambalo ni la viongozi wa dini badala ya kuonesha umaarufu wao tu juu ya majukwaa ndio ingekuwa suluhu ya matatizo mengi ya Waumini wa dini. Hata katika upande wa kero zinazowapata wanawake ndani ya ndoa za uke wenza, kama zile za Bi Zahra n.k. Mfano mzuri ni ule ambao tunaupata katika Hadithi ya Mtume S.A.W., katika kisa ambapo bwana mmoja alikwenda kumlilia Mtume shida ya maisha akiwa na mke mmoja. Mtume S.A.W.akamshauri aoe mke wa pili. Sahaba huyo alipokea na kutekeleza ushauri huo kwa shingo upande, kwa kuona kama ameongezewa mzigo juu ya mzigo. Na hali ya maisha yake ya dhiki wala haikubadilika. Hakuchoka kurejea tena kwa Mtume, ambaye alimpa ushauri ule ule kuwa aoe mke wa tatu. Japo bila shaka akili zake zilimduru, bwana yule kwa imani yake thabiti kwa Mtume, hakusita kuipokea amri hiyo ya Mtume s.a.w.. Akaoa mke wa tatu juu ya hao wengine wawili aliokuwa anaishi nao kwa maisha ya dhiki. Na ndipo ilipobainika kwake na wengine wa wakati huo na wa baadaye kuwa ushauri unaotokana na Mtukufu Mtume una hikima na miujiza isiyokadirika kwa watu wa kawaida. Kwani, alijikuta akiwa katika hali ya baraka na neema ya neema ya kiwango cha kushangaza kabisa. Mke huyo wa tatu alipewa na wazazi wake mali nyingi
ambayo aliikabidhi kwa mume wao, na kumwambia aifanyie kazi na kinachopatikana
akitumie kwa mahitaji yake na wake zake wote watatu walio katika ulinzi
wake kwa mujibu wa sharia ya dini.
2 Kuchunguza mchumba: Hatua hii imegawanyika katika mifumo ya aina mbili tofauti baina ya watu nayo ni:- Mwelekeo wa Mashariki – ambao ni muafaka na maadili ya Uislamu; (ii) Mwelekeo wa Kimagharibi – Uchunguzi huu ni kwa madhumuni ya kuwapa nafasi msichana na mvulana kwa kila mmoja wao kuweza kumfahamu mwenzake – kwa sura, umbile la urefu au ufupi, unene au mwembamba; na pia kauli na fikra katika mazungumzo ya ana kwa ana kabla ya ndoa. Na zoezi hili kwa upande wa mweleko wa kwanza wa watu wa Mashariki, kama ilivyo sharia za Uislamu, ambapo hairuhusiwi kukutana mwanamume na mwanamke katika faragha-sharti lifanyike kwa njia ya kuuliza ndugu wa karibu na mmoja wao au majirani zake. Na kama kuna lazima ya kuonana na kuangalia hali zile za kimaumbile, basi sharti iwe na jamaa wa msichana wako. Na kwa njia zote hizi, tunapata ushahidi wa Mtume s.a.w. nao unatuambia: "Hawakutani faraghani wawili – mwanamueme na mwanamke, ila shetani anakuwa watatu wao." Ama kwa watu wa mwelekeo wa desturi za Kimagharibi,
wao huchunguza hayo ya kuonana, kuongea, na kupimana fikra zao, na hawatosheki
na hayo tu bali wanafika hatua ya kuchunguza na mwendo wa kila mmoja hasa
akiwa ndani ya mikusanyiko ya watu. Na hayo ni kinyume na Sharia ya Uislamu.
3. Ridhaa: Maadamu mtu amepewa akili timamu, basi anapaswa aitumie kwa busara akili hiyo katikakujiamulia mambo yanayomkhusu katika maisha hadi kufikia khatima njema. Tumpe nafasi hapa Ustaadh Muhammad Rajai wa ‘Raabita’, atusimulie kukhusu tukio la Bi-Khansai binti Khizami alivyoongea na Mtume s.a.w. juu ya uamuzi wa baba yake kumuandalia ndoa na mume asiyeridhika naye. Anasema Bi-Khansai kumwambia Mtume: "Hakika baba yangu amenipa ndoa na mtoto wa ndugu yake, na mimi nimekasirika na jambo hilo:; Mtume akamwambia "Ridhika na hilo alilofanya babako" – (Bi-Khansai) Akasema: "Sina hamu kabisa na hilo alilofanya baba yangu." Mtume s.a.w. akamwambia: "Nenda zako, hana haki baba – olewa na umpendaye". Kisha akasema (Khansai),: "Nimeridhia na hayo ya baba yangu; lakini tu nilitaka watu kwa jumla waelewe kuwa wazazi hawana amri zote juu ya mambo ya mabinti zao." Na wala Mtume hakuikanusha kauli hiyo. Pamoja na hayo lakini – vijana wanaonywa vikali
juu ya tabia ya baadhi wanaoamua kuolewa pasi na ridhaa na idhini ya wazazi
– baba na mama. Au kama wengine wao, wanaofanya mipango ya siri na mama
zao tu bila ya baba ambaye ndiye mlinzi na muamuzi wa mambo yote ya ndani
ya nyumba. Na mara nyingi hawa wamepata mikasa mingi katika maisha bila
ya wao kutambua. Basi nawajihadhari sana vijana!
4 – Fani: Furaha na faraja ya maisha katika jamii ya nyumba, huletwa na wawiliwaliooana – kabla ya hata kuwa na watoto. Kwa hali hiyo, Uislamu umeweka uzito juu ya kila upande unaohusika na azma ya ndoa, upate haki kuchagua mwenzake anayefanana na hadhi yake kulingana na mazingira ya sehemu anamoishi; na pia kulingana na hadhi aliyonayo katika jamii ya watu. Hii pia inaepusha mbali vishawishi vya tofauti zinazoweza kuzuka ndani ya nyumba kutokana na dharau, endapo mke atakuwa ameolewa au mume ameoa mke asiyekuwa fani yake. Mengineyo yanayoambatana na azma ya ndoa, ni agizo la kumpa mke mahari yake atakayodai kwa mume huyo anayemuoa. Sharia ya Uislamu haikuweka kima maalumu – cha chini wala cha juu. Kilichohimizwa ni kile cha kutofanya mahari kama biashara. Na ulamaa wa Kiislamu wote wa mwanzo, wameafikiana juu ya suala la mahari kuwa ni kitu chochote chenye thamani ya mali, na ambacho ataridhika nacho binti anayeolewa. Na hakuna sharia ya kuolewa bila mahari. Hatimaye tunakamilisha zoezi hili kukhusu maisha
ya ndoa, kwa kudokeza kidogo kuhusu hatua ambayo japo iko nje ya utabiri
wa mwanaadamu, ila katika harakati za maisha nalo limekhusishwa!
Talaka: Uislamu katika sharia zake halali, na talaka nayo imo. Ni sheria pale inapobidi, kutengana wawili walioana. Lakini inatakikana kuwe na tahadhari kali inapofikia hali hiyo. Kwanza ni lazima iwe baada ya kuchukua zile hatua zote za kurekebisha tabia ambazo tumetangulia kuzitaja hapa nyuma kwenye Aya ya 34; mpaka hata na hatua za kupeleka wasuluhishi kutoka pande zote zinazokhusika. Vile vile kutengana kwao iwe ni kwa nia ya kusalimisha imani zao. Maana kuishi nyumbani katika hali ya bughdha mume na mke, kunaleta kukosekana baraka na rehma za Allah. Na kuachana bure bure kunaathiri hata wasiokuwa na hatia kama vile watoto. Ndio maana Hadithi ya Mtume s.a.w. akatoa tahadhari kuwa: "Sheria halali ambayo Allah anaichukia, ni talaka." Basi analolichukia Allah, si busara kwa mtu kulifanyia pupa! Tunamuomba Mola atupe ilimu. Atujaze imani, hikima
na fahamu.
|
Maoni yetu: Umakini wa Wabunge unatia wasiwasi AGIZO LA MANISPAA KUPEWA MAJINA YA
WANAFUNZI WA KIKATOLIKI
Madai ya Ali Ameir kuhusu Chuki yakanushwa
Mwanamuziki Nyota CAT STEVENS asimulia alivyosilimu Watakiwa kuacha kuwatuma watoto mitaani
Kijana wa Kibarbaig aliyejitolea kupigania
dini yake
'Waislamu wenye sisa kali'
MAKALA: Maisha ya ndoa kwa Muislamu
- 2
Mjibuni Mwinjilisti Kusupa msitukane
Vigogo wahusishwa na madawa ya kulevya
Z'bar
Da’awa Handeni yashika kasi
Kongamano la vijana wa
Kiislamu Masjid Nuur Dar
Mashairi - uzawa wa Mtume (S.A.W)
|