|
Na. 053 Jumatano Juni 21 - 27, 2000 |
|
|
|
|
|
Sharia kuanza kutumika Kano
KANO, Nigeria JIMBO jingine nchini Nigeria, KANO litaanza kutumia sharia ya Kiislamu rasmi kuanzia leo. Msemaji wa serikali ya Nigeria amesema, polisi wa kulinda usalama na wale wa kuzuia ghasia wamepelekwa kwa wingi jimboni humo. Kano ni jimbo liliopo Kaskazini mwa Nigeria likiwa linafuata nyayo za majimbo ya Zamfara, Sokoto katika kutekeleza mafundisho ya Uislamu. Wakazi wengi wa jimbo hilo ni Waislamu ambao wameafiki mpango wa matumizi ya sharia jimboni, huku wakieleza kuwa kusimamisha sharia ndio lengo la kuwepo hapa ulimwenguni kwa mujibu wa kitabu kikuu cha Waislamu. Kitabu kikuu cha Waislamu ambacho ndio katiba ni Qur'an ambayo imefafanuliwa kwa vitendo na Mtume Muhammad (s.a.w.) ambayo kisheria hujulikana kama Sunnah. Akielezea matumizi ya sharia jimboni humo, Afisa Mwandamizi wa serikali ameongeza kuwa sheria itatumika sehemu zote jimboni humo. Imeelezwa kuwa lengo la serikali kupeleka askari polisi wa usalama na wa kuzuia ghasia ni kuzuia mapigano yanayoweza kusababishwa na Wakristo kwa kule kupinga kwao utekelezaji wa sheria. Mapema mwaka huu katika jimbo la Kaduna kulitokea mapigano kati ya Waislamu na Wakristo, hali ambayo ilisababisha vifo vya Waislamu wengi. Madai ya Wakristo dhidi ya kusimamisha sharia ya Kiislamu ni kuwa na khofu ya kutotendewa haki au kulazimishwa kufuata sharia. Akijibu hoja hiyo, mmoja wa viongozi wa majimbo ya awali kutekeleza sharia alisema, sharia ya Kiislamu haitawalazimisha watu wa dini nyingine,, "Hii ni sharia ya Kiislamu ni kwa ajili ya Uislamu". Rais Obasanjo wa Nigeria amesema jana kuwa haamini kuwa kuanzishwa kwa utekelezaji wa sharia ya Kiislamu nchini humo kutavuruga amani na mshikamano wa Taifa. Baadhi ya serikali katika baadhi ya nchi za Kiafrika zimekuwa zikizuia utekelezaji wa sheria ya Kiislamu kwa madai kuwa amani na mshiakamano vitavurugika, na pia nchi zao si za kidini ijapokuwa wananchi wake wana dini. Katiba ya Nigeria inaruhusu majimbo ya nchini
humo kuunda mfumo wa maisha unaofaa kwawananchi wake.
Kofi Annan akutana na Hizbullah BEIRUT, Lebanon KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Kofi Annan wiki hii alikutana na wapiganaji wa Kiislamu wa Kikundi cha Hizbullah kwa ajili ya suala la amani mpakani mwa Lebanon na Israel. Katika mazungumzo baina yake na kiongozi wa Hizbullah Bw. Hassan Nasrallah, Annan alitilia mkazo suala la askari wa Umoja wa Mataifa kwenda kulinda amani eneo la mpakani kati ya Lebanon na Israel. Kiongozi wa Hizbullah amemueleza Bwana Annan kuwa mapambano na Israel yataendelea hadi maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu na Israel yatakaporudishwa. Alisema, hakuna haja ya askari wa Umoja wa Mataifa kwenda kulinda amani huko kwani wao hawakuwahi kutegemea msaada wowote kutoka Umoja huo. "Tulichukua hatua za kujisaidia wenyewe hatimaye tumerudisha sehemu ya ardhi hivi karibuni", amesema Bwana Nasrallah. Hivi karibuni vikosi hivyo vya Kiislamu viliwasambaratisha Waisrael huko kusini mwa Lebanon katika ardhi ambayo Israel iliikalia kwa mabavu. Tokea kukimbia kwa Israel huko Lebanon kila upande umekuwa ukidai kuwa endapo utashambuliwa hautakuwa na simile. Bwana Annan alifahamishwa na Hizbullah kuwa kuondoka kwa Israel bado hakujakamilika kwani wamekwishavunja baadhi ya makubaliano ikiwa ni pamoja na kutovuka katika mstari wa mpaka katika eneo mojwapo. Katibu Mkuu atawaeleza viongozi wa Israel juu ya suala hilo mara atakapokutana nao katika ziara inayotarajiwa kuifanya siku chache za usoni huko Israel. Israel imekuwa ikiyakalia kwa mabavu maeneo ya ardhi za Lebanon na Syria tangu mwaka 1967. Hata hivyo, juhudi za kidiplomasia zimekuwa zikifanyika ili kuhakikisha kuwa Israel inayarudisha maeneo hayo. Licha ya diplomasia kutumika, mapambano ya kijeshi
imeonesha kuwa ni suluhisho la pekee kuwang'oa Waisrael.
Uislamu washamiri Ujerumani IMERIPOTIWA na mwandishi Suzanne Sternk katika jarida la Echo of Islam kuwa dini ya Kiislamu hivi sasa inashika nafasi ya tatu kwa wingi wa waumini. Idadi ya Waislamu nchini humo ni milioni 2.7 ambao ni asilimia tatu ya Wajerumani wote. Katika jiji la Cologne pekee kuna Waislamu wapatao 70,000. Katika Ujerumani yote kuna idadi ya misikiti elfu mbili na taasisi sza Kiislamu 2500. Historia ya Uislamu katika Ujerumani imeanza katika karne ya 18 wakati Mfalme Friedrich Wilhelm kwa kwanza alipoamuru apewe askari 20 wa Kiislamu kama zawadi ili kuanzisha jumuiya yao na kufanya ibada katika jumba kubwa badala ya msikiti. Baada ya hapo, Waislamu walichukua uraia wa Ujerumani ingawa ilichukua miaka 200 wao kukubalika kama jamii rasmi nchini humo. Mnamo mwaka 1960 wakati Ujerumani ilipohitaji wafanyakazi, iliomba kutoka majirani wa nchi za kikomunisti Waturuki ni jamii iliyoitikiakwa wingi mwaliko huo. Kutokana na imani kwamba wageni watarudi kwao baada ya muda, suala ambalo lilikuwa kinyume, Ujerumani ikawa kivutio kikubwa cha wageni hao kuendelea kuishi miongo kwa miongo. Serikali yaUjerumani ilito marupurupu ili kuwashawishi wageni hao warudi katika nchi zao lakini haikusaidia kuwafanya waondoke nchini humo. Mnamo miaka ya sabini katikati, Ujerumani haikuhitaji tena wafanyakazi wa kigeni, ilitungwa sheria ya kuruhusu wageni kuwa sehemu ya jamii ya Ujerumani. Katika miongo hiyo ya sabini ndipo Uislamu ulipoanza kutambulika rasmi katika Ujerumani. Ingawa kikatiba Ujerumani inaruhusu uhuru wa kuabudu, lakini bado Uislamu hauna fursa ya kusaidiwa na Serikali kama ilivyo kwa dini nyingine za Kikristo na Kiyahudi. Ujerumani ina vyama vya kisiasa vyenye mlengo wa dini ya Kikristu kama vile Christian Democratic Union (CDU). Hata katika vyombo vya habari Uislamu umepewa nafasi finyu, katika Radio Deutchwelle katika idhaa ya Kiswahili kulikuwa na kipindi cha Ulimwengu wa Kiislamu ambacho kimeng'olewa. Kipindi hicho kilikuwa kikitolewa hewani siku ya Ijumaa saa kumi na mbili alfajiri. |
YALIYOMO
Tahariri
Kauli ya Sumaye yawakera wananchi Licha ya Katiba ya nchi kutambua uhuru na haki ya kuabudu: Qur’an kizimbani Wapinzani Waishutumu sheria mpya ya uchaguzi CCM wanatumia pesa za serikali kwa kampeni - Chenyenge USHAURI NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
MAKALA
MAKALA
Lishe
RIWAYA
- |
|
|
|
|