|
Na. 053 Jumatano Juni 21 - 27, 2000 |
|
|
|
|
|
Kweli CUF ni ngangari! Na Maalim Bassaleh KUNA mtu mmoja wa huku Tanzania Bara, hivi karibuni, alikwenda Zanzibar kwa ajili ya shughuli zake za kibinafsi. Akiwa huko visiwani alipata bahati ya kushuhudia mapokezi ya wagombea wote watarajiwa wa nafasi ya Urais kutoka vyama vyote viwili, CCM na CUF. Jumanne, tarehe 13 Juni, 2000 alishuhudia mapokezi aliyoyapata mgombea wa kiti chaUrais wa Zanzibar, kwa tiketi ya CCM, Mheshimiwa Amani Abeid Karume. Mamia kwa mamia ya Wazanzibari walifika bandarini kumlaki mgombea huyo. Yule mgeni alipoona hata wafuasi wa chama cha upinzani cha CUF walijitokeza, kwa wingi, kumfurahikia mgombea huyo wa CCM alisema, "Inaonekana huyu ndiye chaguo la Wazanzibari wote!" Aliendelea, "Hapana shaka huyu ndiye Rais mtarajiwa wa Zanzibar." Kumbe pale alipokuwa ameketi na kutamka maneno hayo ni kijiwe cha wana-CUF. Basi pale pale akajibiwa, "wewe poa tu, huijui Zanzibar. Hujaona kitu bado. Ngojea siku ya kupokelewa Maalim Seif ndiyo utajua kuwa CUF, Zanzibar ni ngangari." Yule mgeni kutoka bara alisema, hakuamini yale aliyoambiwa. Alidhani wale wana-CUF walikuwa wakimdanganya tu. Alihisi yale waliyokuwa wakimweleza ni ushabiki wa kisiasa tu. Amesema, hakuweza kubishana nao kwa sababu wao wote walikuwa ni CUF na yeye peke yake ndiye aliyekuwa mfuasi wa TLP. Ilimbidi anyamaze hata kama hakuwa akikubaliana nao. Amesema, aliwaza moyoni kuwa atangojea siku hiyo ya kumpokea huyo Maalim Seif wao,aone huo umati utakaojitokeza kumpokea. Naam, siku aliyokuwa akiingojea kwa hamu ikafika. Ilikuwa ni siku ya Jumapili, Juni 18, 2000. Kwa maneno yake mwenyewe alisema, "Na bahati yangu kuwa nilikuwa nikipinga moyoni mwangu. Laiti ningalibishana na mwingine ye yote kwa kuwekeana dau leo ningalikuwa nimefutwa dau langu hilo. Ameeleza kama pale mwanzo alikuwa akiona taabu kuamini yale aliyokuwa akiambiwa na wale wana-CUF basi siku hiyo ya Jumapili, kwa ule umma alioona uliojitokeza kuwapokea wagombea wawili wa chama cha CUF, ProfesaIbrahimHaroona Lipumba, anayegombea kiti chaUrais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naMaalim Seif Shariff Hamadi, anayegombea kiti cha urais wa Zanzibar, alikaribia kutoyaamini macho yake. Kama wale waliokwenda kumpokea Mheshimiwa Amani Karume walikuwa kwa mamia, basi hawa waliojitokeza kuwalaki Profesa Lipumba na Maalim Seif ni kwa maelfu! Kulichomstaajabisha zaidi yule mgeni kutoka bara, siyo ule wingi wa watu tu, bali jinsi watu hao walivyoonekana kutojali mvua kubwa iliyokuwa ikiendelea kunyesha tokea alfajiri. Watu hao walikuwa wameroa chepe chepe, lakini walisema, potelea mbali, bora wawashuhidie kwa macho yao wagombea wao, kwa tiketi ya chama chao cha CUF. Yasemekana umma mkubwa ulifika uwanja wa ndege, lakini Polisi waliwazuia wasilikaribie jengo linalotumika kuwapokelea wageni. Watu wengine walijipanga barabarani kuwashangilia wagombea hao walipokuwa wakipita. Aidha, maandamano makubwa ya wana-CUF yalianzia eneo la Kariakoo, ambalo ni jirani kabisa na jimbo la Rahaleo la mwakilishi wa CCM, Mheshimiwa Karume, mpaka kwenye viwanja vya Malindi. Huo uwanja wa Malindi uliotumika kufanyiwa mkutano wa hadhara wa kuwatambulisha wagombea hao wa CUF ulikuwa umejaa maji utadhani bahari au ziwa kubwa. Lakini watu hawakujali, maji hayo na walikaa ndani ya maji hayo utasema walikuwa wakingojea kubatizwa kwa maji mengi! Kuuona umati huo uliokaidi hata mvua iliyokuwa ikiwamiminikia, kwa kasi, tokea alfajiri, yule mgeni alikuwa hana jingine ila kukiri kuwa kweli mapokezi ya Maalim Seif yalikuwa kamambe. Alisema kwa hali aliyoishuhudia, kwa macho yake mwenyewe, na kuamini kuwa Maalim Seif kweli ni ngangari Unguja. Alipoambiwa hiyo aliyoiona ni CUF ya Unguja, jee, anafikiriaje CUF ya Pemba, kisiwa ambacho CCM haikuambulia hata kiti kimoja? Alijibu kuwa kabla ya kufika Zanzibar na kuiona hali halisi ilivyo alikuwa akiwasikia Wana-CUF wakilalamika kuwa katika uchaguzi uliopita wa mwaka 1995, ushindi ulikuwa ni wao lakini walipokonywa;alikuwa akiwaona ni waongo; lakini sasa amesema ana kila sababu ya kuyaamini madai ya chama cha CUF. Amesema katika uchaguzi ujao wa Oktoba 2000, ni wazi kuwa Maalim Seif ataibuka mshindi! Lakini kulikuwa na jambo moja kubwa lililokuwa likiendelea kusumbua kichwa cha yule mgeni wetu. Hakufahamu kwa nini wana-CUF walishiriki kikamilifu katika mapokezi ya Karume ambaye ni mgombea wa CCM na kumbe mapenzi yao bado yapo pale pale kwa Maalim Seif, na bila ya shaka yo yote kura zao watampa huyo huyo mgombea wa chama chao. Alijibiwa kuwa wana-CUF wanakichukulia kitendo cha kuchaguliwa Mheshimiwa Amani Karume na Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM kule Dodoma, kama ni mgombea wa kiti cha Urais wa Zanzibar, kwa tiketi ya chama hicho ni pigo kwa wale waliomfanyia mizengwe mgombea huyo na kutaka kumsimika mgombea wao atakayelinda maslahi yao, baada ya kuondoka Rais wa sasa Dkt. Salmin Amour. Pili, kauli alizokuwa akizitoa Amani Karume tokea alipochukua fomu mpaka alipochaguliwa kuwa ndiye mgombea kwa tiketi ya CCM ni zile zenye kuashiria kutaka kuleta amani na kuendeleza demokrasia Zanzibar. Ni wazi basi kuwa Amani Karume, kama ni Mzanzibari anaonekana kuchoshwa na siasa za uhasama na anataka kuiondoa hali ya wasiwasi iliyotanda katika visiwa hivyo. Rais mstaafu wa awamu ya pili, Al-Hajj Ali HassanMwinyi alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara wa kuwapongeza Mheshimiwa Mkapa kuchaguliwa kuwa mgombea wa kiti cha Urais waJamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mheshimiwa Karume kuwa mgombea wa kiti cha Urais wa Zanzibar, kwa tiketi ya CCM, alisema kwa sasa Wazanzibari wamegawanyika hawana umoja. Aliendelea kusema, "wapo wale wanaosema, 'sisi tunatoka Pemba,' na wap owanaosema, "Sisi tunatoka Unguja". Alieleza siasa hizo za kubaguana zimeifanya Zanzibar iwe na mgawanyiko wa Wapemba na Waunguja, Wakaskazini naWakusini, Wamashariki na Wamagharibi. Naye Amani Karume akijibu hotuba hiyo ya Al-Haj Mwinyi alisema "Ahadi yangu kwenu ni kwamba nitayatekeleza maneno ya Mzee Mwinyi iwapo Mungu atatujaalia."Aliendelea kuahidi kuwa atahakikisha kuwa amani, utulivu, na umoja wa kitaifa vinalindwa. Bila ya shaka yo yote kauli ya Mzee Mwinyi imethibitisha hali ya kubaguana iliyopo Visiwani humo kwa hivi sasa. Na ni wazi kuwa Karume amekusudia kuiondoa hali hiyo. Kwa kweli hakuna anayeumwa zaidi na siasa za ubaguzi nauhasama kama yeye Karume. Ameona vipi wakati akiwa mbele ya Mkutano Mkuu Maalumu wa chama chake cha CCM Zanzibar ulipokuwa ukichuja majina ya wagombea ulivyombagua kwa kumwambia, uso kwa uso, kuwa yeye si Mzanzibari kwa sababu babake hakuzaliwa Zanzibar, ametoka Malawi. Na kwa ajili ya siasa za chuki na uhasama, walipoona hilo halitoathiri cho chote, wakavumbua hila nyingine wakamwambia hafai eti hana elimu ya chuo kikkuu! Basi mtu kama yeye aliyeonja uchungu wa kubaguliwa na chama chake mwenyewe haidhaniwi kuwa atakuwa tayari kutaka kuwabagua wafuasi wa vyama vingine. Ndiyo maana akachukia siasa za ubaguzi na uhasama. Lakini swali la kujiuliza jee atakapochaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ataweza kutimiliza ahadi zake hizo? Hakuna anayemtilia mashaka mgombea huyo. Takriban Wazanzibari wote wanamwamini na wanaelewa kuwa anayo nia hiyo. Lakini Maalim Seif Shariff Hamadi alipokuwa akihutubia ule mkutano wa hadhara uliofanyika Jumapili, katika viwanja vya Malindi alisema, "Hata kama mtu ana nia nzuri kama amani. Bwana Amani anayo nia nzuri. Jee, mfumo ambao atakaoutumikia unataka hayo? Maalim Seif alisema kwa mfano wakati Amani alipokuwa akichukua fomu za kugombania nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama chake cha CCM alisema akifaulu kuingia madarakani atashirikiana na vyama vyote kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Lakini baada ya kupitishwa anasema mambo hayo, ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, yasubiri mpaka uchaguzi umalizike! Maalim Seif akaongeza kusema watu wamtazame yeye. Alipochukua fomu kugombania kiti cha urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha CUF, aliahidi akishinda uchaguzi na kuingia madarakani ataunda serikali ya umoja wa Kitaifa. Baada ya kupitishwa na Mkutano Maalumu wa CUF kule Mwanza alirudia kauli yake hiyo hiyo. Na katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kidongo Chekundu, Dar es Salaam, wa kuwapongeza wagombea wa CUF,alikariri kwa mara nyingine kauli yake hiyo. Akasisitiza, "Na leo hapa katika viwanja hivi vya Malindi narudia kauli yangu nikishinda nitaunda serikali ya mseto." Amesema msimamo wake ni kutaka kuuondoa mfumo mzima wa CCM, huko Zanzibar. Bila ya hivyo, hata akichaguliwa nani, madamu atatumikia mfumo ule ule wa CCM, hataweza kubadilisha hali hiyo iliyopo katika Visiwa hivyo. Kuhusu amani, Maalim Seif alisema kuwa amani katika Visiwa vya Zanzibar imeletwa na chama cha CUF. Ilikuwa ni yeye akishirikiana na viongozi wenzake wa chama hicho, pale walipowatuliza wanachama wao waache hasira, baada ya kuporwa ushindi wao, na kuwaambia watatumia njia za kidiplomasia kudai haki zao. Aliuliza kama wangeliwaachia wanachama wao wachukue sheria mikononi mwao mambo yangelikuwaje? |
YALIYOMO
Tahariri
Kauli ya Sumaye yawakera wananchi Licha ya Katiba ya nchi kutambua uhuru na haki ya kuabudu: Qur’an kizimbani Wapinzani Waishutumu sheria mpya ya uchaguzi CCM wanatumia pesa za serikali kwa kampeni - Chenyenge USHAURI NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
MAKALA
MAKALA
Lishe
RIWAYA
- |
|
|
|
|