NASAHA
Na. 053 Jumatano Juni 21 - 27, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Kauli ya Sumaye yawakera wananchi 
  • Wasema CCM haiwajali 


Na Mwandishi Wetu 

KAULI ya Waziri Mkuu Mhe Fredrick Sumaye aliyoitoa mwishoni mwa wiki kuwataka Watanzania wasio na uwezo wa kulipa shilingi 2,000/- kama ada ya shule za msingi (UPE) wasioe imedaiwa kwamba ni kielelezo kuwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) haimjali mwananchi wa kawaida.

Waziri Mkuu ambaye pia ni mbunge wa Hanang kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliripotiwa na vyombo vya habari vya hapa nchini kusema kuwa mwanaume ambaye hawezi kumlipia mwanae mchango wa elimu kwa wote (UPE) wa sh. 2,000/- kwa mwaka hana sababu ya kuoa wala kuzaa. 

Kwa mujibu wa gazeti moja litolewalo kila Jumapili kwa lugha ya Kiswahili, Bw. Sumaye aliyasema hayo mjini Dodoma katika semina ya wabunge kuhusu 'Watoto wa Tanzania' iliyofanyika katika ukumbi wa Bunge.Gazeti hilo lilimkariri Waziri Mkuu akisema: "kama mwanaume mzima umemfuata mwananke kwao na kuoa, unashindwa kutoa sh. 2,000/- kwa ajili ya mwanao usingepaswa kuoa kabisa". 

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wananchi waliotoa maoni yao wamesema ni jambo la 'kuwasimanga' kuwataka watu wasioe na kuzaa, kwa vile ni serikali ndiyo iliyoshindwa kuwapa wananchi wake uwezo wa kumudu hizo ada. 

"Kabla ya (Mhe.) Sumaye kutushambulia sisi tusio na uwezo angeliangalia suala hili kwa upana angegundua kuwa jambo hili ni aibu kwa serikali yenyewe...", alidai mmoja wa wananchi hao. 

"...itakuwaje mwananchi aliye huru katika nchi yake ashindwe kulipa sh 2,000/- tu kwa mwaka mpaka alazimike kufunga uzazi...kwani hizi kodi wanazochukua wanazipeleka wapi?" alishangaa mwananchi huyo ambaye alijitaja kwa jina moja tu la Baba Moshi. 

Mzee Rajab Masori, mkazi wa Kariakoo, alisema kwamba kauli hiyo ya Waziri Mkuu si jambo geni kwa sababu, CCM ilikwisha sema kuwa ipo mbali na wananchi na hivyo CCM haijui hali halisi ya mwananchi. 

"Alichofanya Sumaye ni kuthibitisha maneno ya Kinguge..., Kingunge aliwaambia wenzake, CCM imekaa mbali na wananchi", alisema Mzee Rajab. 

Bw. Kingunge Ngombale Mwiru, ambaye amewahi kushika nyadhifa muhimu katika Chama Cha Mapinduzi ikiwemo masuala ya Propaganda na Ushirikishwaji Umma, akiongea katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika mwanzoni mwa mwezi huu aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa CCM imekuwa mbali na wananchi jambo ambalo litaiweka pabaya siku wananchi wakianza kuhoji hali hiyo. 

Mzee huyo alisema matatizo ya wananchi sio kuoa au kutokuoa, bali ni umasikini unaoelekea kukithiri. 

"Leo hii wananchi tuna hali ngumu sana, enzi zetu wakati wa TANU mambo hayakuwa hivi, watoto wetu walisoma vizuri, na hata ile CCM ya zamani mambo hayakuwa mabaya lakini hii CCM ya leo watu tunalia..., tunaumia utadhani ni chama cha kukodiwa", alisema Mzee Rajab ambaye alidai alikuwa ni mwanachama wa TANU na baadaye CCM. 

Mwananchi mwingine, Bw. Aidan Temba, alilalamika kwamba CCM imekuwa ikiwajia juu wananchi wanaokituhumu chama hicho kwamba kimeshindwa kuongoza nchi ambapo inawatisha na kuwasingizia kwamba wamekitukana chama ingawa "huo ndio ukweli wa mambo". 

"...kama kodi tunazolipa hazitoshi wao wanapata wapi mishahara mikubwa na wanaweza kuwasomesha watoto Ulaya?", alihoji Bw. Temba. 

"ingekuwa wanatujali wangekubali tukagawana hicho kidogo kinachoingia serikalini, lakini hawa CCM hawana imani na sisi hata kidogo, ...shule za watoto wetu hazina hata madawati, halafu leo wanakimbilia kutuambia tusioe", aliongeza kusema Bw. Temba ambaye hakukubali kutaja anashughulika na nini bali mara zote alikuwa akisema yeye ni mhangaikaji kama alivyo Mtanzania wa kawaida. 

CCM wenyewe wanajua na wamesema kwamba mtu wa chini kama mimi (Mtanzania wa kawaida) kipato changu ni shilingi 400/- tu, inakuwaje Bw. Sumaye anishangae nikishindwa kulipa sh. 2000/- kwa ajili ya mtoto wangu...mimi ninaona Bwana Mheshimiwa anafahamu kila kitu, lakini ameamua tu kutusimanga", alisema mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Bahati Kato. 

Hivi karibuni katika kikao cha Bunge serikali ilitoa taarifa kuwa kipato cha wastani kwa Mtanzania wa kawaida ni nusu dola kimarekani (sawa sh 400/-) kwa kutwa taarifa ambayo iliwaacha wananchi wengi wakiishangaa serikali ni vipi inafikiri wananchi wake wanakifanya ili kuweza kuishi. 

"Mimi ninashangaa sana mambo haya, wao waliosoma na wakapata madaraka wanajifanya wazungu wanazaa mtoto mmoja au wawili, hivi wao wanahani kama tukiwaachia wao tu kazi ya kuzaa wanafikiri nchi hii itakuwa na watu?!" alishangaa na kuongeza kuwa ikiwa mambo ndiyo hivyo basi Tanzania itajaa wageni watupu na "wenye nchi watakuwa wakuhesabu". 

Mwananchi mwingine ambaye alikataa kutaja jina lake alisema anawashangaa viongozi wanaowadhihaki wale waliooa na kuza ndani ya ndoa zao huku ikiwaacha wale wenye kuzaa hovyo nje ya ndoa kana kwamba wao si tatizo. 

"CCM imetujia juu sisi tunaooa na kuzaa ndani ya ndoa mbona haiwaambii kitu wale wanaozaa nje ya ndoa, kwani wao ndio wanazipata hizo hela za UPE (ada ya sh. 2,000/- kwa mwaka kwa shule za msingi)". 

Mwananchi mwingine alisema kuwa kwa mila za kwao usukumani kuoa ni jambo la heshima sana na kwamba utu wa mwanaume hukamilika akioa. 

"Kwetu kama hukuoa basi ujue huna thamani mbele ya watu na unaonekana huna busara", alisema mwananchi huyo na kungeza kuwa mtazamo huo katika kabila lao hutokana na imani kwamba aliyeoa hulazimika kutuliza akili yake kwa vile tayari anayo majukumu. 

Semina hiyo ya 'Watoto wa Tanzania' iliandaliwa kupokea taarifa ya utekelezaji wa mazimio ya mkutano wa taifa kuhusu Uhai, Ulinzi na Maendeleo ya watoto ya Juni, 1991. 

Katika semina hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto, Bi. Mwantumu Malale, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio hayo ambapo alisema uandikishaji wa watoto shule za msingi walio na umri kati ya miaka 7-13 ni asilimia 57 tu. 


Licha ya Katiba ya nchi kutambua uhuru na haki ya kuabudu:
Qur'an kizimbani 
  • Waislam waendelea kuwekwa mahabusu 
  • Morogoro Mahakama ilitakiwa imuite 'aliyeiandika'Qur'an 
  • Musoma aya isemayo Uislam ni dini ya kweli yaitwa kizimbani 
  • Waislamu Musoma waomba msaada kwa wenzao 
Na Mwandishi Wetu 

HABARI kutoka Musoma zinaeleza kuwa Waislam wawili mtu na mkewe ambaye ni mjamzito waliwekwa mahabusu kwa tuhuma za kusikiliza na kuuza kanda zinazodaiwa zenye maneno ya kashfa. Miongoni mwa maneno hayo ni yale yasemayo Uislamu ni dini ya kweli ambayo yanatokana na aya ya Qur'an.

Kwa mujibu wa habari hizo, mtuhumiwa wa 'makosa' hayo ni Bw.Hussein ambaye ni muuza kanda za dini ya Kiislam nje ya Msikiti wa Ijumaa mjini Musoma katika eneo la Mwigobero. 

Habari hizo zinaeleza kwamba Bw. Hussein alikamatwa kwa mara ya kwanza mnamo mwezi Machi, mwaka huu ambapo alichukuliwa yeye na mkewe hadi kituo cha polisi ambako walifunguliwa mashtaka matano. 

Bw. Hussein amedai kuwa mara baada ya kufikishwa polisi walihojiwa na kuwekwa mahabusu kwa siku sita kabla ya kupelekwa mahakamani bila kupewa dhamana ingawa watu wa kuwadhamini walikuwepo. Hata hivyo alisema kuwa mkewe alipewa dhamana mapema baada ya polisi kubembelezwa sana kumpa dhamana mjamzito ambaye hali yake kiafya haikuwa nzuri na ingeathirika zaidi kwa kukaa mahabusu. 

Bw. Hussein amedai kwamba hatimaye walifikishwa mahakamani yeye na mkewe (mshitakiwa No. 2) na kufunguliwa mashtaka yafuatayo:- 

1. Kukutwa wakisikiliza kanda yenye maneno yasemayo Yesu ni Muislamu. 

2. Kusikiliza kanda isemayo Yesu si Mungu. 

3. Kusiliza kanda isemayo Yesu hakuzaliwa tarehe 25 Desemba. 

4. Kusikiliza kanda yenye maneno yasemayo Uislam ndio dini ya kweli. 

5. Kusikiliza kanda isemayo Yesu hakufa msalabani. 

Bwana Hussein amedai kwamba miongoni mwa vielelezo vinavyoshikiliwa na polisi ni redio yake yenye thamani ya zaidi ya laki moja na kanda za Qur'an Tukufu na kasida zipatazo 85 na nyingine 40 zenye mawaidha ya kueneza dini ya Kiislamu, kwa hoja na majadiliano ya hadhara za wahadhiri maarufu wakiwemo Ustadh Mazinge, Rico na wengineo. Kesi hiyo inaendelea katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Mara, watuhumiwa wapo nje kwa dhamana. 

Awali gazeti moja litolewalo mara mbili kwa wiki liliripoti kuwa hakimu mmoja mkoani Morogoro aliamuru watunzi, waandishi na wasambazaji wa Qur'an wakamatwe ili washitakiwe kwa makosa ya uchochezi. 

Waislam nchini wamekuwa wakilalamikia kunyimwa uhuru wa kuabudu kama unavyotambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Ibara ya 19 (2) ambayo inasema: Bila ya kuathiri sheria zinazohusika za Jamhuri ya Muungano, kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari ya mtu binafsi; na shughuli za uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi. 

Pamoja na madai hayo ya kunyimwa uhuru wa kuabudu Waislamu pia wamekuwa wakilalamikia mwelekeo wa kidini wa baadhi ya vyombo vya dola hapa nchini wametoa mfano wa vitendo vinavyoendelea vya kuwakamata Waislam na kuwafungulia kesi zisizostahiki na kuambiwa kuwa kesi hizo zinahusiana na imani za kidini. 

Waislam pia wamekuwa wakilalamikia tuhuma zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa serikali za kuwataka Waislam wasitumie kitabu cha Biblia katika mahubiri yao kwa kuwa Biblia si kitabu cha Waislam na kitendo hicho kimehatarisha kuvurugika kwa amani. Wao (Waislam) wanasisitiza kuwa wanayo haki ya kuhoji na kuitumia Biblia katika majadiliano na wasiokuwa Waislamu pamoja na watu wanaotembea wakigawa Biblia kwa Waislamu. Waislamu wanahoji kuwa iweje tuhuma hizo zitolewe na viongozi wa serikali wakati Wakristo wenyewe hawajalalamika. 

Hata hivyo wakati serikali imekuwa ikiwalaumu Waislam kwa kutumia Biblia, hivi karibuni wakuu wa shule za msingi ambao ni watumishi wa serikali walisimamia zoezi la Makanisa kugawa Biblia kwenye shule zao kwa watoto bila kujali umri wala imani zao za kidini. 

Zoezi hilo la kugawa Biblia limezua mjadala miongoni mwa Waislam. Wamesema kuwa kitendo cha Biblia hizo kugawiwa chini ya uangalizi wa walimu wa shule za serikali kinaashiria kuwa Ukristo ni dini inayotambuliwa na serikali. Dai la serikali kuwa haina dini liko wapi, wamehoji. 

Aidha Waislam wengine wameliona zoezi hilo kama ni hatua ya serikali kushirikiana na makanisa kutaka kuwabatiza watoto wa Kiislam. Wamehoji kuwa iwaje zoezi hilo lifanyike bila ridhaa ya wazazi. 

Waendesha mihadhara ya Kiislam wao wamewataka wale wote wanaopewa Biblia hizo wazipokee ili wazisome na kuzitumia katika majadiliano na Wakristo. "Iwapo tumepewa Biblia hizo tutakopazisoma na kuzijadili, Serikali isitulaumu tena." Mhadhiri mmoja wa kiislam alisema alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habazi hizi. 

Wakati huo huo tukio hilo la kushitakiwa muuza kanda za dini mjini Musoma limeamsha hisia za Waislam wengi nchini. Na taarifa zimeshasambazwa karibu mikoa yote ili kuwafahamisha Waislam juu ya tukio hilo ambapo taarifa hizo zimeamsha ari za Waislam wengi isipokuwa Waislam wachache ambao wamesadikiwa kuwa wanaunga mkono BAKWATA. 

Huko Musoma Waislam wametoa maombi kwa Waislam wenzao nchini kuwaunga mkono na kutoa mshikamano kwa dua, tahajudi, itikafu na michango ambayo itawasaidia kuweka wakili wa kuwatetea. 


CCM yapata kiwewe 

Na Mwandishi Wetu 

MAPOKEZI makubwa na ya aina yake yaliyofanywa na maelfu ya wananchi jijini Dar es Salaam kuwapokea Prof. Ibrahim Lipumba anayegombea urais wa Jamhuri ya Muungano na Bw. Seif Shariff Hamad anayegombea urais wa Zanzibar, wote wawili kwa tiketi za Chama cha Wananchi (CUF), tayari yamejenga hofu katika kambi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho chama tawala, uchunguzi wa gazeti hili umebaini.

Prof. Lipumba Jumamosi iliyopita alipokewa katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam wakati akitokea Mwanza na Bw. Hamad alikuwepo uwanjani hapo baada ya safari yake ya Mbeya ambako, taarifa kutoka ofisi za chama hicho zilizopo Buguruni jijini zimeeleza kwamba pamoja na mambo mengine, wawili hao walikwenda kuimarisha chama. 

Katika ziara zao hizo za mikoani wagombea hao wamekuwa wakionesha azma na matumaini makubwa ya kukiangusha chama tawala (CCM) katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. CUF imekuwa ikiishutumu CCM kwa kushindwa kuboresha hali za wananchi katika kipindi cha miaka arobaini sasa tangu kiwe madarakani. 

Kujitokeza kwa wingi kwa wananchi kumeelezwa na wananchi hao kuwa ni alama ya ushirikiano mkubwa uliomo ndani ya chama cha CUF. 

"Wenzetu wana umoja na ushirikiano..." alisema Bw. Hanzuruni aliyedai kuwa ni mwanachama wa CCM. 

Umati huo uliomiminika kuwalaki Prof. Lipumba na Maalim Seif uliwajumuisha pia wafuasi wa CUF na wananchi wengine kutoka nje ya Dar es Salaam. 

Mwananchi mmoja, Bw. Martin aliyejitambulisha kuwa mkazi wa Kibaha, akionesha jinsi alivyovutwa na hamasa aliyoiona katika mapokezi hayo alisema, "watu tuliofika Dar es Salaam tumeshuhudia kazi ya uhamasishaji inavyozaa matunda..., CUF wanaiweza na wametuthibitishia hivyo". 

Shamrashamra zile ambazo kilele chake kilikuwa katika viwanja vya Kidongo Chekundu ziliwavutia hata wafuasi wa CCM. 

"Watu wa CUF wana msukumo wao binafsi,...wanakodisha magari kwa gharama zao, kwa kweli wameiva", alisema mwananchi mmoja ambaye anafanya biashara kando ya shina moja la wakereketwa wa CCM lililopo Kariakoo. 

Mwananchi huyo aliyejitaja kwa jina la Maulidi pia ameeleza hofu yake kuwa mgombea wa Urais wa Jamhuri kwa tiketi ya CCM, Rais Benjamin Mkapa, atakabiliwa na kazi ngumu kumshinda mgombea huyo wa Chama cha Wananchi. 

"safari iliyopita (uchaguzi wa mwaka 1995) hatukupata tabu kuwashinda (wapinzani) lakini safari hii ... viongozi wetu lazima wafanye kazi ya ziada la sivyo tutaaibika", alisema Bw. Maulidi. 

Mkereketwa mwingine ambaye hakukubali jina lake liandikwe gazetini alikumbushia kauli ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Mkapa, kwamba wana-CCM wasiidharau nguvu ya upinzani kwa vile wapinzani wamedhamiria kuing'oa CCM madarakani. 

"inaelekea (viongozi wa) CUF wamekaa karibu sana na wananchi, na kauli zao zimewateka watu...sasa wanakuja juu na makundi ya watu", alisema mkereketwa huyo. 

Aliongeza kusema kuwa mambo yatazidi kuwa magumu siku viongozi wa CUF wakiruhusiwa kutumia redio na kuweza kusikika kwa watu wengi. 
 

Juu
 

YALIYOMO
 
 

Tahariri
Uhuru wa kuabudu utiwe katika matendo bila ya ubaguzi

Kauli ya Sumaye yawakera wananchi

Licha ya Katiba ya nchi kutambua uhuru na haki ya kuabudu: Qur’an kizimbani

CCM yapata kiwewe

Wapinzani Waishutumu sheria mpya ya uchaguzi

Mtoto wa Afrika yutaabani

CCM wanatumia pesa za serikali kwa kampeni - Chenyenge

USHAURI NASAHA
Dhuluma haiondoki bila kubadili mfumo

Habari za Mikoani

Kalamu ya Mwandishi
Kweli CUF ni ngangari!

MAKALA
Manabii wa kale na mageuzi

MAKALA
CCM na sera za maendeleo

MAKALA
Wajibu wa wananchi kwenye uchaguzi mkuu

Habari za Kimataifa

Lishe
Kuhifadhi matunda kwenye jokofu

RIWAYA
Dunia ndivyo ilivyo - 3

MASHAIRI

MICHEZO

  • Uingereza, Ujerumani nje
  • Washabiki wamshangaa Mkapa, wambeza Sumaye
  • BMT waipiga ngwara FAT

  • -

       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita