AN-NUUR 
Na.170 Jamadul Akhir 1419, Oktoba 9 - 15, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Maoni Yetu
Maisha ya Mtanzania 
yanapokosa thamani
 
  • Badala ya risasi za mpira, risasi za moto
  • Badala ya bomoa, choma moto

  •  
ILI kutuliza ghasia askari polisi popote pale duniani hutumia mabomu ya machozi, risasi za mipira, maji, virungu n.k. Kilombero zimetumika risasi za moto, watu wameuliwa. Mwembechai zimetumika risasi za moto watu wameuliwa. Chama Tawala kikapongeza tukio hilo na tukaambiwa baadhi ya askari wakapewa vyeo kwa kazi nzuri waliyoifanya katika tukio hilo! 

Ni kawaida iliyozoeleka nyumba ikiwa imo katika eneo lisiloruhusiwa; hubomolewa, tena wakati mwingine baada ya kutolewa fidia. Haikuwa hivyo kwa nyumba ya Bw. Mohamed Hassan na mkewe Tausi Rashid, yao ilichomwa moto. Haikuwa hivyo kwa Bw. Omar Sadala (67) yake iliteketezwa kwa moto na akiba yake yote ya chakula kuangamizwa. 

Hali ilikuwa tofauti kwa Bw. Juma Mohamed na mkewe Zaina Athumani walichoweza kunusuru ni roho zao na kitanda chao cha kamba, wakiishia kuanza makazi mapya chini ya mti bila chakula baada ya kila chao hata makopa ya akiba kuteketezwa kwa moto! 

Waliovamia fukwe za bahari na viwanja vya michezo na kujenga mahekalu hatunayo majina lakini ni wazi hayawezi kuwakuta yaliyomkuta Mzee Juma Abdallah ambaye aliambulia kuokoa gogo alilokuwa akitumia kama kiti baada ya nyumba yake kuchomwa moto. Wala hawawezi kupatwa na masaibu yaliyomkuta Bibi Khadija Rashid (65) ambaye hata kitanda na kinu alichofanikiwa kuokoa na kuficha porini havikusalimika baada ya pori lenyewe kuchomwa moto! 

Ni wazi vile vile kwamba watoto wao hawatakosa kwenda shule kama ambavyo watoto wa Halima Mkongwa na Habiba Mwalimu wameshindwa kwenda baada ya sare zao za shule kuunguzwa moto. 

Pamoja na amri ya Serikali ya kuwataka wananchi wa kijiji cha Nzasa wahame katika eneo linalodaiwa la hifadhi ya msitu wa Kazimzumbwi, hatukutarajia zoezi la kuwahamisha wananchi hao lichukue sura ya kutojali wala kuthamini uhai na mali za wananchi. 

Wapo watoto; waja wazito, vilema, wagonjwa na vikongwe. Wengine tunaambiwa wanajifungulia kwenye matuta baada ya nyumba za kuchomwa. Angalau vingetembezwa virungu kuwaswaga watu ndani ya karandinga kuwapeleka makazi mapya. Maana hata kiwete ukimburura unamsaidia kufika haraka. Lakini moto! 

Hawa ni wananchi ambao walitekeleza wajibu wao wa kupiga kura kuiweka serikali iliyopo madarakani, michango ya mwenge wanatoa, huhudhuria mikutano ya hadhara huku wakiungua jua bila kudai posho ya kikao; huwapigia makofi viongozi wao hata bila ya kuelewa wanachosema, hujitibu wenyewe na kuwasomesha watoto wao wenyewe wala hawajauliza kodi na michango wanayotoa inafanyia kazi gani na pengine hutoa hata majina ya wala rushwa. Wanapounguziwa moto nyumba zao nia na lengo ni kuwahamisha au kuwaangamiza! 

Hata kama ni jambazi lililoua, achilia mbali kuvamia msitu; basi zipo taratibu za kisheria za kuliadhibu. Si kulichoma moto lenyewe au nyumba yake. Na hata kama ni katika vita, basi haiwi mmeteka kijiji katika nchi adui halafu mnachoma nyumba za watu mliowakuta ambao si askari walioshika silaha; sikwambii raia wapiga kura wako! 

Baadhi ya taarifa zimefahamisha kwamba mgogoro huu ulifika hadi katika vyombo vya sheria, hukumu ikatolewa wasihamishwe. Lakini shinikizo lilipozidi hawa akina Rashid Hemed, Juma Chaubaya, Maryamu Juma wakadai wapewe japo fidia ili wakitoka hapo wajue wanakwenda wapi. Jibu likawa hampati kitu. Sasa Bw. Juma Chaubaya anasema atafia porini maana hana pa kwenda. 

Atapataje pa kwenda wakati hakuwa na raslimali zaidi ya shamba lake la muhogo, kitanda cha kamba, zaidi ni nguo aliyovaa. Hana senti benki wala ghala la mbaazi na muhogo. Muhogo, kibanda na kitanda vimegeuzwa jivu; aende wapi! 

Tatizo hapa si wananchi hao kuhama au kutokuhama, lakini hii hali ya inayoonekana ya kikatili. Vyovyote iwavyo, hawa ni wananchi. Haistahili kufanyiwa unyama wa kiwango hiki. 

Mzazi kumwambia mtoto wake ukiwapeleka mbuzi machungani nitakupa chakula; nguo kukupeleka shule na kukulea kwa ujumla; huwa kichekesho. Nini maana ya kuwa baba kama jukumu la kulea halipo. Mtoto umwambie ukifaulu hesabu nitakununulia baiskeli. Sio ukifaulu fizikia nitakulea. 

Wananchi walijitolea muhanga kuondoa utawala wa kikoloni kwa sababu ulikuwa wa kibabe, kibaguzi na kidhalimu. Walitamani utawala wa haki na sheria, na zaidi wenye kuwajali na kuthamini uhai wao na mali zao. 

Kama ilivyo kichekesho baba kuahidi kumlea mtoto kama zawadi; ilifikia mahali suala la "Utawala wa Haki na Sheria" kufanywa jukwaa la kuombea kura. 

Pamoja na hayo, wananchi walishukuru kwamba huenda yale ya "Kilombero" na "operesheni vijiji" ikawa ndio mwisho, lakini tukio hili linatuweka kwenye utata mkubwa. Ni mfumo gani hasa wa serikali yetu, maana ipo mingi. Nani aliyeagiza kufanywa operesheni hii? Je, aliagizwa na Mh. Rais; au je, Mh. Rais aliombwa ruhusa ? Na kimya hiki je, Mh. Rais hajapata habari? Ameridhika! 
 
Juu 
 

YALIYOMO 
 
 

TAHARIRI 
Tutaendelea kudhalilishwa mpaka lini ? 

Waislamu wasisitiza: Nyumba ya Waziri Mkuu ni ya Waislamu 
Na Mwandishi Wetu 

Kuchomwa nyumba za wananchi 
Na Mwandishi wetu 

Maoni Yetu: 
Maisha ya Mtanzania yanapokosa thamani 

Nguruwe marufuku Kinondoni – Tume 
Na Kassim Juma 

Watanzania waanzisha Baraza la Waislamu Marekani 
Na Mwandishi Wetu 

Wanawake Hai wamtaka Rais azungumzie mauaji ya Mwembechai 
Na Mwandishi Wetu 

‘Serikali haiwezi kuzuia rushwa’ 
Na Kassim Msuya 

Makala ya Kimataifa 
Nani gaidi: Slobodan Milosovic au Usama bin Laden 
Na Mwandishi Wetu 

Afghanistan washindi dhidi ya uvamizi karne zote 
Na Faiza bint Abubaka 

MAKALA: 
Demokrasia ya rushwa ! 
Na Mwapwani Mohamed 

Tujikwamue na janga la utwaghuti 
Na I. Kikong’ona 

MAONI: 
Nini Jihad na nani Mujahidina ? 

MAKALA: 
Marekani ni magaidi wa haki za binadamu 
Na MUSSA ALLY 

Tufuate Uislamu kwa vitendo na siyo kwa maneno -2 
Mwandishi: Maalim Ali Bassaleh 

Tusihalalishe mauaji ya raia kwa kisingizio cha ‘wananchi wenye hasira’ 
Na Mwandishi Wetu 

Historia ya sayansi na tiba 
Na Dk. Amur A.A. 

Msiwageuze watoto ombaomba 
Na H.E. Omar 

MAKALA YA JAMII: 
Profesa Malise Kaisi acha uzushi dhidi ya Mtume Muhammad 

Sensa ya majaribio: Wananchi watofautiana na serikali 
Na Rajab Rajab - Morogoro 

Uislamu ulivyoingia Zanzibar -3 

Mwembechai wageuka Hame, Bado walindwa na polisi 
Na Badru Kimwaga 

Waislamu Moro waendelea kusaidia wagonjwa 
Na Rajab Rajab - Morogoro 

Mjadala wa Katiba ya Shirikisho kuzinduliwa Dar Jumapili 
Na Mohamed Othman 

Walimu wa dini Tanga wapokea Baiskeli 
Na Abu Said 

Mafundisho ya Quran 
Kutoa katika njia ya Allah: Al-Baqarah aya  264 

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 
Vitu vinavyoweza kuwemo katika vyakula 

  

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita