NASAHA
Na. 057 Jumatano  Julai 19 - 25, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Kalamu ya Mwandishi 

Mamluki wa mageuzi 

Na Maalim Bassaleh 

WAHENGA walisema, "Umoja ni Nguvu; na Utengano ni Udhaifu." Lakini baada ya vyama viwili vya upinzani, CUF na CHADEMA,kutangaza azma yao ya kuunda umoja baina yao, ili kusimamisha mgombea mmoja wa kiti cha Urais, baadhi ya wasomi wetu, wanasiasa na hata waandishi wa habari, wamekuwa wakitoa shutuma, hizi na zile, kuuponda umoja huo!

Ni jambo la kustaajabisha na pia, kusikitisha! Kwa sababu hao hao wanaoupinga umoja huo hivi leo, ndio waliokuwa mstari wa mbele kuvishauri vyama vya upinzani kama vinataka kukiondoa chama tawala madarakani, basi viunganishe nguvu zao. Lakini umoja huo ulipoanza kuchomoza badala yakuupigia debe wao wameamua kuuhujumu'. 

Haieleweki kwa nini wafanye hivyo. Tuseme wao wamegundua kuwa "utengano ndiyo nguvu, na umoja ni udhaifu?" Au bado wanaamini kuwa "Umoja ni Nguvu.....", lakini wana ajenda ya siri dhidi ya umoja huo wa CUF na CHADEMA? Inaonekana hili la pili ndilo lililowapelekea kuushambulia umoja huo. 

Ingawa wametoa sababu nyingi kuupinga umoja huo; lakini sababu kubwa, miongoni mwa hizo walizozieleza, ni tatu. Kwanza, wamedai eti kwa vile CHADEMA ni chama kisichofahamika sana kikiungana na CUF kitamezwa. Pili,eti sera za CUF ni za shari,zinachochea vurugu. Na mwisho wamedai eti chama cha CUF kina mwelekeo wa udini! 

Hapa nimekumbuka usemi wa hekima uliomo katika Biblia unaosema, "Mjinga huamini kila neno; bali mwenye busara huangalia sana aendavyo." (Methali 14:15). Kwa hivyo, ili tusiwe wajinga,kabla ya kuzikubali au kuzikataa sababu hizo,zinazotolewa dhidi ya umoja huo, inatubidi kwanza tuzichunguze; tena,kwa makini. 

Tuanze na ile sababu ya kwanza ya kuwa CHADEMA haina umaarufu itamezwa na CUF . Madai hayo yanastaajabisha sana. Kama madai hayo yanakusudiwa kwa Zanzibar, yanaweza kuwa ya kweli, kwa maana katika visiwa hivyo vyama vyote vya siasa vimemezwa, siyo na CUF tu bali hata na CCM pia. Huko hakuna chama cho chote kingine kinachotamba mbele ya CUF na CCM. 

Lakini huku Bara,katika uchaguzi wa 1995, CHADEMA ilipata viti vitatu vya Bunge wakati CUF iliondokea patupu, haikupata hata kiti kimoja! Basi baina ya CUF na CHADEMA ni chama kipi chenye umaarufu zaidi,na kinachoweza kukimeza chama kingine? 

Na kama itasemwa kuwa CUF ni chama kikubwa kuliko CHADEMA, kwa kuwa katika uchaguzi uliopita kilipata viti 24 huko Zanzibar; basi itafaa tujiulize jee na kama vyama vingine vya upinzani vingalikubali kuungana na TLP,chama cha Mheshimiwa Mrema, navyo vyama hivyo visingalimezwa na chama hicho cha Mheshimiwa Mrema, kwa sababu lilipojitokeza wazo la kusimamisha mgombea mmoja kwa kambi ya upinzani, Mrema alisema ni yeye tu ndiye wa kupewa nafasi hiyo kwa vile yeye ana mtaji wa kura milioni 1.8 alizozipata katika uchaguzi mkuu uliopita.Au chama chenye kinywa kikubwa kinachoweza kumeza vyama vingine vidogo ni CUF tu, vingine haviwezi? 

Sababu ya pili inayotolewa kupinga umoja wa CUF na CHADEMA, ni kuwa eti sera ya CUF ya jino kwa jino, ni ya uchochezi! Mheshimiwa John Cheyo, Mwenyekiti wa UDP,amedai, kuwa hawezi kushirikiana na CUF kwa sababu sera za chama hicho ni za uchochezi na kisasi,ambazo zinaashiria katika kuleta vurugu na machafuko nchini. 

Na kiongozi mmoja wa TLP, amekaririwa akisema sera ya CUF ya jino kwa jino ni sera ya Korani kwa hivyo chama chake hakiko tayari kufuata sera kama hiyo. 

Kupinga sera ya jino kwa jino, kwa Mwislamu ni ukafiri, na kwa Mkristo ni unafiki! Kur'ani Tukufu inasema, "Na humo tuliwaandikia ya kwamba roho kwa roho, na jicho kwa jicho, na pua kwa pua, na sikio kwa sikio, na jino kwa jino, na kwa majeraha kisasi. Lakini atakayesamehe basi itakuwa ni kafara kwake. (Al-Maida 5:45). 

Na Biblia nayo inasema, "Na mtu ampigaye mtu hata akafa lazima atauawa; na atakayempiga mnyama hata akafa atalipa; uhai kwa uhai. Na mtu akimtia mwengine kilema, vile vile kama alivyofanya, naye atafanyiwa vivyo; jeraha kwa jeraha, jicho kwa jicho, jino kwa jino vile vile kama alivyomtia mtu kilema, naye atalipwa vivyo. (Walawi 24:17-20). 

Kwa hiyo tutaona kuwa sera ya jino kwa jino, ingawa inatangazwa sana na chama cha CUF, lakini kwa kweli si sera ya chama hicho, ni sera ya Mungu, iliyomo katika Kur'ani Tukufu na pia katika Biblia. Basi kwa namna hiyo ni sera ya watu wote,Waislamu na hata Wakristo. Labda la kujiuliza ni kwa nini Mungu akaweka sera kama hiyo? 

Biblia inajibu kwa kusema "........ndipo mtamfanyia kama alivyodhani kumfanyia nduguye; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako. Na watakaosalia watasikia na kuogopa, wasifanye tena uovu mfano wa huo katikati yako." (Kumbukumbu la Torati 19:19-20). 

Tutaona kuwa kwa mujibu wa maelezo ya Biblia sera hiyo humzuia yule anayetaka kumdhulumu mwenziwe asite kufanya hivyo kwa kuogopa na yeye asije akalipiziwa dhuluma kama ile aliyoitenda yeye. Basi kama kweli mtu, ni mcha Mungu, hana nia ya kutaka kumdhulumu mwingine kwa nini aiogope sera hiyo? Jino kwa jino, haina maana kwamba mtu atoke na kuwang'ata wengine; bali maana yake ni kuwa atakayetoa jino la mwenziwe naye lake litatolewa! 

Katika kusisitiza matumizi ya sera hiyo Biblia inaendelea kusema, "Wala jicho lako lisiwe na huruma; uzima kwa uzima, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu. (Kumbukumbu laTorati19:21). 

Kwa kuwa sera hiyo ya jino kwa jino, jicho kwa jicho, na pua kwa pua, ni hukumu ya Mungu iliyomo ndani ya Kur'ani Tukufu na Biblia, basi Mwislamu atakayejitokeza kuipinga atakuwa ni dhalimu, au fasiki au kafiri hasa (Al-Maida 5:44, 45, 47). 

Na kama kuna Mkristo atakayedai kuwa sera hiyo imo katika Torati, ambacho ni kitabu cha Agano la Kale, si ya kufuatwa; basi tutamjibu kuwa Bwana Yesu aliyeleta Agano Jipya anasema, "Msidhani ya kuwa nalikuja kuitengua torati au manabii; la sikuja kutengua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu, hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha hivyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni." (Mathayo 5:17-19). Basi vipi Mkristo aikatae sera ya jino kwa jino? 

Mbunge wa Rorya kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi,Mheshimiwa Mabere Marando, hivi karibuni, aliuliza katika Bunge,kama sera ya CUF, ya 'jino kwa jino', inahatarisha amani, jee na ile sera ya 'mtu kwa mtu''shavu kwa shavu','kofi kwa makofi mawili,' inayohubiriwa na kiongozi wa ngazi ya juu wa chama tawala nayo haihatarishi amani? Jee! Na huyo kiongozi anayetangaza sera hiyo atachukuliwa hatua gani? 

Mheshimiwa Marando aliuliza hivyo baada ya wabunge wawili wa chama cha CCM, kutoka Zanzibar walipotaka waelezwe kwa nini serikali haifuti usajili wa chama cha CUF, kutokana na sera yake hiyo ya jino kwa jino, inayolenga katika kuleta fujo na vurumai nchini? 

Lakini kama mtu atatafakari juu ya jambo hilo, kisha akaoanisha na hali ya mazingira ya kisiasa yalivyo nchini, hataacha kujiuliza kwa nini CCM isiwe ndiyo ya kwanza kufutiwa usajili wake? 

Kuna sababu tatu zinazopelekea CCM ifutwe. Kwanza, CCM nayo, ina sera ya mtu kwa mtu, shavu kwa shavu', na'kofi moja kwa makofi mawili'. Jee! Sera hiyo haihatarishi amani? Pili, mara kwa mara,viongozi wa chama hicho wamekuwa wakitoa kauli za uchochezi zinazoashiria kuhatarisha amani. Kwa mfano, hivi juzi, waziri mmoja wa SMZ,amekaririwa akisema serikali ya Zanzibar haitaondolewa madarakani kwa karatasi, kwani ilipatikana kwa mapinduzi! Kauli hiyo ya Waziri inamaanisha kuwa hata kama chama cha upinzani kitashinda kwa wingi wa kura, CCM Zanzibar,haitakubali kukabidhi madaraka kwa chama hicho kilichoshinda! Jee! Kauli kama hiyo haihatarishi amani? Kwa nini basi na CCMisifutwe kwa kauli zake hizo zinazokiuka hata katiba ya nchi na misingi ya haki za binadamu? 

Tatu, kama CUF inatangaza sera ya jino kwa jino, mpaka sasa inahubiri sera hiyo kwa maeno matupu; lakini ile sera ya CCM, ya"mtu kwa mtu', na'kofi moja kwa makofi mawili',inaonekana imeanza kufanyiwa mazoezi na wakereketwa wa chama hicho. Katika zoezi la CCM, la kupiga kura za maoni kwa ajili ya kugombania udiwani, wana-CCM wameripotiwa kutukanana, kufanya vurugu na hata wengine kutoana ngeu. 

Wakati zoezi hilo likiendelea magezeti yalikuwa yakiandika juu ya vurugu hizo. Gazeti moja liliandika, "Kura za Maoni za CCM Vurugu Tupu - Mawe, Ngumi zatawala Mara,Matusi yatawala Dar." Gazeti jingine liliandika, "Udanganyifu Mtupu kwenye kura za Madiwani wa CCM -Vurugu Temeke na Longido." Na gazeti moja liliandika, "Kinyang'anyiro cha Udiwani CCM -Polisi waitwa kutuliza Fujo." Kama mambo ndivyo hivyo yalivyo basi baina ya CUF na CCM ni chama kipi chenye sera za vurugu? Mwisho, juzi Jumatatu, Julai 17, 2000 gazeti moja limeandika, "Mgombea wa CCM avunjwa mkono", katika zoezi hilo hilo la kugombania udiwani. Mbona hawasemi na CCM ifutwe kutokana na sera zake hizo za vurugu? 

Ama yale madai ya Mheshimiwa Cheyo kuwa Muungano wa CUF na CHADEMA unanukia udini, eti kwa sababu viongozi au wagombea wake wote ni Waislamu, hayana msingi wowote. Ni madai yenye kudhihirisha udini alio nao huyo msemaji. Ni kwa sababu wagombea watakaosimamishwa na muungano wa vyama hivyo, katika uchaguzi wa Oktoba, 2000 ndio wale wale waliosimamishwa katika uchaguzi uliopita wa 1995. Mbona hatukumsikia Mheshimiwa Cheyo wakati ule akisema chama cha CUF kinanukia udini? Na badala yake alishirikiana na chama hicho kuunda serikali kivuli ndani ya Bunge? 

Inaonekana Mheshimiwa Cheyo alikubali kushirikiana na CUF, kwa sababu mwaka 1995,chama hicho hakikuwa na umaarufu wowote kitaifa kwa hivyo hakikuwa ni tishio; lakini hii CUF ya 2000 imemshitua, ina kila dalili ya kushinda uchaguzi ujao na kuingia madarakani. 

Kwa hivyo hofu ya udini aliyonayo Mheshimiwa Cheyo siyo kwamba CUF ikishinda itaunda serikali ya Kiislamu, kwa sababu anaelewa kuwa kwa mujibu wa katiba ya nchi hii, hilo haliwezekani; lakini inaonekana yeye, kama walivyo wenziwe wengi, wanaogopa CUF isije ikashinda ikaunda serikali itakayoongozwa na Waislamu! 

Kama kweli Mheshimiwa Cheyo anapiga udini mbona ameinyamazia kimya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuteua wasimamizi wa uchaguzi kwa upendeleo, zaidi ya asilimia 90 ni Wakristo? Jee! Hakuna Waislamu wenye sifa za kuwa wasimamizi? Hivyo tafsiri ya udini ni pale viongozi wa nchi, jumuiya, chama au taasisi wanapokuwa wengi wao ni Waslamu? Lakini wengi wao wakiwa Wakristo inakuwa si udini? 

Ndiyo maana Mwenyekiti wa CHADEMA. Ndugu Bob Makani, alipokuwa akihojiwa na shirika la utangazaji la BBC, alisema kama chama cha CUF kinaambiwa kina udini, kwa kuwa viongozi wake ni Waislamu, mbona na chama cha CCM, hakiambiwi ni cha Kikristo kwa sababu Mwenyekiti wake, Rais Benjamin Mkapa, Makamu wake (Bara), Mheshimiwa John Malecela, na Katibu wake Mkuu, Ndugu Phillip Mangula ni Wakristo. Na kwa hoja hiyo hiyo chama cha UDP,cha Mheshimiwa Cheyo, kitabidi kuitwe ni chama cha UKABILA, kwa sababu viti vyake vyote vya Bunge vimeshinda usukumani tu! 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Tume, PCB na vyama vya siasa mmekiona mliochoandaliwa Oktoba?

Cheyo kuendeleza  ‘mfumo Kristo’

Rushwa katika kura za maoni: 'CCM isitafute mchawi'

CUF yakanusha propaganda za waraka

Wanachama wa  CUF kortini  Kilwa

Waumini waapa kulinda Msikiti

KINYANG’ANYIRO CHA UBUNGE: CCM Temeke wamtaka Bazaar

'Wanafunzi Lindi wamshughulikia Mkuu wa Shule aliyewazuia kuswali'

Milioni moja zachangwa kujenga madrasa

Hata na mimi sijala

USHAURI NASAHA
Jinamizi la ukewenza

MAKALA
Kushindwa kujitegemea ni laana

MAKALA
UDP, TLP wathibitisha hisia za Waislamu kuwa Uislamu ni kero Tanzania

MIPASHO NASAHA
Mwanasiasa wa kisasa

Kalamu ya Mwandishi
Mamluki wa mageuzi

MAKALA
Mrema na Cheyo wajihadhari wasije wakatumiwa kuwavuruga wananchi

MAKALA
Viongozi wa vyama vya siasa na udini nchini Tanzania

Mandela ni mfano wa kuigwa

Burudani/Muziki
Cat Stevens: Historia kwa Ufupi

Habari za Kimataifa

LISHE
Yanayoweza kumdhuru mtoto tumboni

MASHAIRI

MICHEZO

  • Jenerali Ulimwengu amgonga nyundo Mkapa
  • Hassan Affif aitabiria Simba Ubingwa

  •  


    Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita