AN-NUUR 
Na.187 Shawwal 1419, Februari 5 - 11 , 1999 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Uislamu na Mazingira katika Umoja wa Mataifa
 
Na Dk. Wahid
 

Umoja wa Mataifa umekuwa ukiipitia taarifa iliyowasilishwa kwake juu ya Mradi wa Havard wa Mchango wa Dini juu ya Hifadhi ya Mazingira. Mradi huo wa miaka mitatu uliwajumuisha wasomi na wanamazingira 1,000 wakitafiti namna ambazo dini kumi miongoni mwa dini kubwa ulimwenguni, ukiwemo Uislamu, zinaweza kusaidia kuuokoa ulimwengu kutokana na hatari za uharibifu wa mazingira. 

Mradi huo umebaini kuwa dini hazina budi kutumia mafundisho yao ya kiroho kukomesha ufujaji wa rasilimali unaofanywa na mwanadamu. Hali hiyo imepelekea kuundwa kwa Baraza la Dini na Uwiano wa Mazingira. 

Bw. Maurice Strong, Mshauri Mwandamizi wa [Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa] Bw. Kofi Annan, alisema, kwa kile kidogo tunachokifahamu, kinachomtofautisha mwanadamu na wanyama wengine ni kwamba sisi tunao utambuzi wa mema na mabaya na pia tuano uwezo wa kufanya mema na kuacha mabaya. Pia amekiri kuwa ulimwengu sasa hivi umetawaliwa na unasukumwa na tamaa kubwa za uchumi wa kichoyo. 

Naye Bw. Tim Wirth, Rais wa baraza hilo la Umoja wa Mataifa na aliyewahi kuwa Waziri Mdogo wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, amesema tangu kufanyika kwa Wkutano wa 1992 wa Wakuu wa Nchi juu ya Mazingira (Rio de Jeneiro) juhudi za ulimwengu kuhifadhi mazingira zimefifia, na badala yake juhudi za kila nchi zimeelekezwa kujipanua kiuchumi. 

Bado hakujawa na juhudi za dhati katika kuutekeleza wajibu wetu kama makhalifa wa Mwenyezi Mungu kwa vimbe vyake. Uharibifu wa mazingira umetokea kwa zaidi ya karne moja, katika kipindi ambacho u-secular (mfumo wa maisha usiofuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu bali matamanio ya mwandamu) ndio umetawala. U-secular unaona kuwa mwongozo toka kwa Mwenyezi Mungu unamfaa mwanadamu katika mambo yake ya bibafsi tu (na wala siyo yale ya kijamii, kitaifa au kimataifa). Hivyo, sera za uchumi zinalenga kupata na kukuza faida ya mali na wala hazizingatii mafundisho ya mitume (radhi za Allah zawe juu yao wote). 

Si jambo jepesi kwa mtu kutambua mara moja athari za uharibifu wa mazingira. Kwa hoja hii dini pekee haziwezi kufanya lolote kuleta ufumbuzi wa kweli. [kwa mujibu wa u-secular] Dini zinaweza kushulikia vizuri maadili na mwenendo wa mtu tu lakini haziwezi kupanga sera za mataifa na viwanda. Hivyo basi iweje leo umoja wa Mataifa, ambao ni chombo cha ki-secular, umeamua kulishughulika suala la mazingira ulimwenguni kupitia katika dini? 

Hatua kama hii si chochote bali inasaidia kuimarisha imani ya ki-secular ambayo ndiyo inayotawala ulimwenguni. Hatua ya kuziweka dini pamoja kuwa zote ni sawa ili zitoe ushauri wa kimaadili kwa taasisi zenye kutunga sera, inazidi kuibana (kuidunisha) nafasi ya dini katika kutatua matatizo ya kijamii. Jambo hili ni hatari pale Uislamu unapochukuliwa kuwa ni sawa na dini zingine. Uislamu ndio dini pekee ambayo ni itikadi halisi na ya kweli. Hivyo Uislamu hauwezi kuchukuliwa kuwa ni sawa na Ubuddha au Ukristo. 

Uislamu unayo namna yake maalum ya kulishughulikia kila jambo, ikwa jambo hilo ni la mtu binafsi au ni la kijamii. Uislamu unaweza kuyashughulikia tena kwa kina masual sera ya mazingira, wakati katika dini zingine sera zenye kuweza kushulikia mambo kwa kina hushia tu kwa mambo ya mtu binafsi. Wakati wa vita Uislamu ulihakikisha kuwa Waislamu (wapiganaji) hwavidhuru viumbe vya Allah (s.w.t). Wakati wa Jihad, Waislamu wanazuiliwa kuharibu mimea au kuua mifugo pasi na kuwepo sababu halali ya kufanya hivyo. Ikiwa huu ndio msimamo wa Uislamu wakati wa vita, basi hali ikoje wakati wa amani? Hivyo, kuuweka Uislamu sawasawa na dini zingine kimaadili katika kushughulikia suala hili, bila shaka na masuala mengineyo, ni jambo lisilo sahihi. 

Khilafah Magazine 
Ramadhan, 1419 
Januari, 1999 


Barua ya wazi kwa Rais Mkapa
 

MHESHIMIWA Rais, barua hii inafuatia hobuta yako kwenye baraza la Idd Januari 19, 1999. Kama mwananchi ninayeitakia mema nchi hii, nimepitia hotuba yako na kuona kuwa kuna umuhimu wa kuyaweka baadhi ya mambo wazi. 

Mh. Rais, umesema kwenye hotuba yako kuwa umoja ule sasa utakuwa ndiyo sauti ya kweli na ya pamoja ya Waislamu nchini. Kauli hii ina kasoro kwa vile serikali haipaswi kudharau hisia na wingi wa wananchi wengine kwa vile hawatambuliwi rasmi na watawala. 

Kasoro hii imesababisha serikali kung’ang’ania Bakwata tu ingawa sio tena mwakilishi wa Waislamu walio wengi. Serikali adilifu inapaswa kutambua kuwa uwakilishi wa fikra na hisia za jamii ya watu ni muhimu; sio mpaka watambuliwe rasmi na watawala bali kwa vile jamii yao ipo na ni sehemu ya wananchi. 

Serikali yako haishangai maelfu ya wananchi walioitikia Baraza la Idd la Mtambani japo polisi walijitahidi kulizuia? Nasema haya nikiamini wewe tayari unafahamu ukweli huu, hasa kwa kuwa unao watendaji wanaofanya kazi ya kuangalia usalama wa Taifa. 

Naamini kazi zao sio tu kumlinda mtawala, lakini pia kumfikishia taarifa za dhulma zinazoweza kuhatarisha usalama wa Taifa. Vipi akina Ponda wawe na wafuasi wengi vile, na malalamiko yao ndio hayo yamesemwa rasmi hadharani mbele yako na bado wana usalama wako wamsake kama mhalifu. Alichodai Ponda si ndio hilo hilo ulilofikishiwa kwamba wauaji Mwembechai wafikishwe mahakamani na tume iundwe? 

Mh. Rais, ni wewe uliyesema Waislamu waorodheshe matatizo yao mwaka 1995 ulipokuwa unagombea wadhifa huo. Ukiondoa tatizo la Mwembechai, mengine yote ni matatizo ya kabla ya 1995. Yale yamefanyiwa kazi kiasi gani? Kitu gani kinachomfanya mtu asidhani ahadi yako ya Baraza la Idd ni gia nyingine ya kupata Urais mwaka 2000? 

Mh. Rais, Waislamu wanapata hisia kuwa serikali inawacheza shere, na kuwafanya hawawezi kuunganisha wala kuhusisha matukio. Malalamiko yao yameelezwa rasmi na viongozi binafsi na taasisi zao tangu mwaka 1963, 1987, 1992, 1994 na 1998. 

Haihitaji mwananchi kufika sekondari kuona kuwa umekuwa unayafahamu manung’uniko ya Waislamu tangu zamani. Au Mh. Rais ulitaka uambiwe na nani zaidi? Mtu atakuelewa vipi unapohutubia Baraza la Idd na kusema: "... Serikali yangu haipendi raia yeyote binafsi au kundi lolote la wananchi yakiwemo makundi ya dini wajihisi wanyonge au raia wa daraja la pili"? Mwisho wa kunukuu. 

Serikali yako haifuati sheria wala Katiba 

Umesema katika hotuba yako kuwa nchi yetu inaongozwa kwa misingi ya katiba na sheria. Kifungu cha 19 cha katiba ulichokinukuu kinatoa uhuru wa kuabudu. Je, unafahamu kuwa Waislamu Tanzania wanaendelea kunyimwa haki yao ya kuabudu? Mfano, Mwenyezi Mungu anawaamrisha wanawake wavae hijabu, lakini watendaji katika serikali yako, wizarani na katika mashirika wanawakataza kuvaa hijabu? Na wengine wamefukuzwa kazi kwa kuvaa hijabu tu! Au vazi la hijabu linavunja sheria gani ya nchi? Hilo moja tu. 

Mh. Rais, mtu yeyote mwenye nia ya kujua, anafahamu kuwa serikali ina undumakuwili. Mambo mengine yanaendeshwa kisheria lakini ya Waislamu sheria huguguna. 

Kwa mujibu wa Criminal Procedure Act ya 1985 kosa la makusudi kusema maneno yanayodhamiria kuumiza hisia za kidini nikosa linalohitaji waranti katika kumkamata mkosaji, na waranti unatakiwa utolewe na Hakimu pahala pa kazi kufuatia malalamiko, kabla mtu hajakamatwa. 

Maana yake ni kuwa kabla mtu yeyote hajakamatwa na kushitakiwa kwa kosa hili, kwanza mlalamikaji lazime apeleke malalamiko yake na ale kiapo kwenye mahakama kabla ya waranti wa kumkamata mlalamikiwa haujatolewa. 

Serikali yako imekuwa ikivunja sheria kwa kutofuata utaratibu huu. Viongozi wa Waislamu wamekuwa wakikamatwa sio tu bila mlalamikaji kuapa mahakamani, lakini pia bila mlalamikaji kuonekana kabisa. 

Kauli ya Paroko Kanisani inatosha kuwasomba Maimamu Misikitini na majumbani usiku wa manane! Mh. Rais, hivi sheria gani inayowaruhusu askari katika serikali yako waingie na viatu na kunajisi Msikiti? Sheria ipi inayowaruhusu askari wanaume kuwapekuwa wanawake sehemu za siri? 

Haya yote yamesemwa hadi Bungeni nawe bado wasema hujui malalamiko ya Waislamu! Mh. Rais inashangaza na ni udhaifu mkubwa kuona kuwa watendaji wako ati hawakufahamishi ukweli juu ya kudhalilishwa kwa wanawake na kudhulumiwa kwa haki za jamii ya Waislamu katika nchi yao, jamii ambayo wewe umekula kiapo kuhakikisha inatendewa haki. 

Mwisho 

Mh. Rais, kwa kuwa jambo hili limekuwa wazi na sugu, wananchi wema bado wanachukulia ahadi yako kuwa ni ya kisiasa tu isiyo na chembe ya dhamira ya kweli ya kuleta dawa ya dhulma hii. 

Hii ni kwa sababu licha ya kuwa umeyafahamu kwa muda mrefu lakini pia katika kushughulikia suala hili, unategemea watendaji wako ambao wengi wao tayari ni wahanga wa chuki za kidini. 

Haya yanashuhudiwa katika baadhi ya maamuzi kama vile uteuzi wa wajumbe wa Parole na upangaji wa mitihani siku ya sikukuu ya Idd. Huu ni ushahidi kuwa mengi yanapitishwa bila kujali madhara kwa Waislamu. 

Kwa hiyo, kama kweli unayo nia ya kuondoa dhulma dhidi ya kundi moja la wananchi wako, usiwategemee washauri wako wa sasa kwani wameshindwa tayari. 

Baraza lako la mawaziri ni lemavu na haliwezi kufanya kazi hii kwa kuwa lina uwiano mbaya kati ya watu wa dini za wananchi; na hivyo huwezi kuondoa hisia za kidini katika ushauri na maamuzi yao na hili wananchi hususan Waislamu wanalishuhudia katika vyombo vya dola (polisi) na mahakama jinsi zinavyoshughulikia mambo au matatizo ya Waislamu. Hata hivyo, dawa ya kudumu ya tatizo hili inabakia kuwa ni uwiano sawa wa uwakilishi katika kila eneo la watendaji wa serikali. Vinginevyo kishindo cha kunyongesha jamii moja huwa ni kikubwa siku zote. 

Maryam Yahya, 
Kiwalani, 
Dar es Salaam. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
  

Tahari 
Mauaji ya Mwembechai; Mh. Rais apewe kanda

Matokeo ya mitihani darasa la saba serikali ieleze: Je, Waislamu ni taahira au kuna agenda ya siri

Hijab ivaliwe shuleni

Wenye siasa za kikaburu wasimyumbishe Rais

Hatuko tayari kuruhusu viwanja viporwe  -   Manyema

Maoni yetu
Kauli ya Waziri Mkuu Bungeni: Tumsikilize nani?

DONDOO ZA KISAIKOLOJIA: PEDOPHILIA

Mjue Usama bin Ladin -3

Uislamu na Mazingira katika Umoja wa Mataifa
Na Dk.  Wahid

Barua ya wazi kwa Rais Mkapa

Barua za Mtume (s.a.w.) za Jihad katika Internet
Na. Zituzzaman Hoque

Kutoka magazeti ya zamzni

Rais Mkapa atekeleze hadi yake kwa hadhari
J.R. Msuya, Moshi

Mashirika ya Dini yaelekeze misaada vijijini
Na KAWELE  SAIDI 

Hotuba ya Mh. Kitwana Kondo (MB) aliyoitoa Bungeni Dodoma

Ni serikali ipi anayoiwakilisha Sumaye
Na Abu Salim

Sehemu ya maelezo ya Waziri Mkuu bw. Frederick Sumaye bungeni

Zanzibar ni nchi au mkoa?.
Na SALUM ALI 

Sheikh Bafadhil aamuru kusimamishwa shughuli za African Muslim Agency Moro

Vijana Arusha njooni mnione - Alhaj Mollel

Waislamu Korelo wazama kwenye ushirikina

Waislamu Hanang’ wajenga Msikiti

Sayansi na Teknolojia 
[Jifunze ‘Kubana’ Majalada] 

Masomo ya Kiislam 

Barua za Wasomaji 

Chakula na Lishe 
[Ni hatari kuwaambia wananchi wasichague chakula] 

Kumbukumbu ya mauaji Mwembechai
 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita