|
|
|
Waislamu wamuasa
asiingilie kazi za Serikali
SHEIKH wa Bakwata Mkoa wa Morogoro Sheikh Omar Bafadhil ametoa amri kwa African Muslim Agency na taasisi ya Muslim Foundation kusimamisha shughuli zake mara moja kuanzia Januari 28, mwaka huu. Akizungumza na mamia ya Waislamu katika Msikiti wa Ijumaa Barabara ya Boma mjini hapa na kunukuliwa na kituo cha televisheni cha Abood cha mjini Morogoro, kiongozi huyo wa Bakwata alisema kuwa amechukua hatua hiyo kutokana na taasisi hizo kuhatarisha amani, usalama na utulivu katika mkoa huo. Katika barua yake rasmi ya Januari 28, mwaka huu aliyomwandikia mwakilishi wa African Muslim Agency (AMA) Sheikh Ariff Nahdi yenye Kumbukumbu namba BKW/MK/MG/495 ambayo ANNUUR inayo nakala yake, Sheikh Bafadhil alisisitiza kwamba anasimamisha shughuli za ujenzi wa Misikiti na madrasa hadi hapo viongozi wa Bakwata watakapokutana na hao wafadhili wanaotoa mamilioni ya fedha za kuendeleza shughuli hizo ili wajue masharti yanayotolewa na mwakilishi huyo katika ujenzi yanatokana na yeye binafsi pamoja na kundi au la. Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umegundua kuwa hakuna taasisi yoyote mjini hapa, mkoani hadi taifa inayoitwa Muslim Foundation kama barua ya Sheikh Bafadhil ilivyonakiri kupiga marufuku taasisi hiyo. Badala yake ipo taasisi inayoitwa Morogoro Islamic Foundation, Mudir wake akiwa ni Sheikh Suleiman "Kiriri" Suleiman na si Arif Nahd kama barua ya Bafadhil inavyosema. Wakati hayo yakijiri, mamia ya Waislamu wa mjini hapa hivi sasa wako katika mjadala mkali juu ya mwenendo unaotia wasiwasi wa kiongozi huyo wa Bakwata mkoa. Wakiongea na gazeti hili kwa nyakati tofauti hivi karibuni, Waislamu kadhaa wa mjini hapa walionyesha kushangazwa na kiongozi wa NGO moja yenye hadhi ya kitaifa kusimamisha shughuli za NGO nyingine yenye hadhi ya kimataifa kwa amri. "Nimesoma kwa makini barua ya Sheikh Bafadhil yenye nakala kwa RPC, RCO, Afisa Usalama wa Taifa, DC na OCD. Kilichonistaajabisha ni kuwa hata bosi wake Sheikh Bafadhil (yaani Mufti wa Bakwata) hajampelekea nakala, wala Wizara inayozisajili taasisi hizo na ndiyo yenye madaraka na mamlaka ya kusimamisha shughuli zake nayo pia hajapeleka nakala", alisema Bw. Othman Hamza mkazi wa mji mpya Morogoro. Muumini mwingine wa Msikiti wa Boma aliyejitambulisha kwa jina la Bibi Khadija Mfaume ambaye ni Daktari wa mifugo kitaaluma, aliliambia gazeti hili kuwa ana wasiwasi kwamba upo mkono wa wenye dhamira mbaya nyuma ya Sheikh Bafadhil wenye nia ya kuhujumu umakinifu wa Waislamu juu ya ahadi za Rais Mkapa kushughulikia matatizo ya Waislamu aliyoitoa katika Baraza la Idd kule Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam mwezi uliopita. Dk. Mfaume alisema kuwa haiyumkini kwa kiongozi wa NGO moja kudiriki
kuingilia kazi za Waziri wa Mambo ya Ndani na kuamuru NGO nyingine isimamishe
shughuli zake.
Vijana Arusha njooni mnione - Alhaj Mollel VIJANA wa Kiislamu mkoani hapa wametakiwa kufika ofisi ya Bakwata ili kubadilishana mawazo na kupanga mikakati ya maendeleo kwa jamii nzima ya Kiislamu. Wito huo umetolewa na Alhaj Mohammed Mollel ofisini kwake alipotembelewa na mwandishi wa habari hizi mwishoni mwa juma lililopita. Akifafanua zaidi, Alhaj Mollel ambaye ni Katibu wa Bakwata Mkoa, amewataka vijana kutojiweka nyuma katika kupigania dini yao na wala wasijishughulishe na malumbano yatokanayo na chuki binafsi kati ya mtu na mtu ama kikundi na kikundi badala yake watumie ujana wao kuirekebisha jamii ya Kiislamu. Alhaj Mollel alikiri kuwapo kwa tofauti za kiitikadi miongoni mwa Waislamu, lakini akasema yeye binafsi yuko tayari kushirikiana na vijana wa madhehebu yote ili mradi lengo ni kuiendeleza dini ya Mwenyezi Mungu. Akizungumzia juhudi zinazofanywa na Bakwata mkoa katika suala zima la kuwalea yatima na wajane ambao wanaongezeka siku hadi siku hapa Arusha, Katibu huyo alisema chombo chake kinakamilisha taratibu za kuanzishwa kituo cha kuwalea yatima na wajane kitakachojengwa Njiro nje kidogo ya Manispaa ya Arusha. Aidha, alifahamisha kuwa kazi ya kukiendesha kituo hicho itashirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu ambao ndio wafadhili wa mradi huo. Alipoulizwa endapo kuna juhudi zozote hivi sasa zinazofanywa na Bakwata mkoa za kuwahudumia yatima na wajane kabla ya kuanza kwa kituo hicho, Alhaj Mollel alikiri kuwepo kwa juhudi hizo ambapo hata hivyo alisema zinawahusu yatima tu. Akifafanua alisema, Bakwata kwa kutumia fungu maalum ambapo pia huchangiwa na Waislamu katika Misikiti mbalimbali imeweza kusomesha yatima wanne elimu ya sekondari katika shule ya Kiislamu Bondeni ilioko mjini hapa, na yatima mmoja katika shule ya Old Moshi ilioko mkoani Kilimanjaro na shule ya sekondari Enaboshu nayo pia ya Arusha. Kadhalika, kuna jumla ya yatima 68 wanaopatiwa huduma ya mavazi na chakula. Hata hivyo, alikubali kuwa hana habari yoyote juu ya yatima walioachwa na marehemu Dossa Salim Dossa aliefariki mwaka jana kwa kupigwa risasi katika eneo la mahakama ya mwanzo Maromboso na askari aliyekuwa akimkimbiza mahabusu aliyekuwa akijaribu kutoroka akiwa chini ya ulinzi na habari hizo kuandikwa kwa kirefu na gazeti hili. Baada ya kufahamishwa hali halisi ya familia ya hayati Dossa, Katibu wa Bakwata Alhaj Mollel aliagiza watoto wa marehemu walio katika umri wa kuanza shule ya msingi waanze mara moja na kwamba Bakwata mkoa itagharamia elimu ya watoto hao. Alhaj Mollel pia alizipongeza juhudi zote zinazofanywa na Waislamu binafsi
za kuwahudumia yatima hapa mjini na akawataka Waislamu hao kuendeleza juhudi
hizo ikiwa ni pamoja na kuzipanua hadi vijijini ili yatima wote wa Kiislamu
wanufaike na kwamba Bakwata iko tayari kushirikian nao.
Waislamu Korelo wazama kwenye ushirikina MAELFU ya Waislamu Morogoro vijijini wakiwemo Masheikh wao wamezama katika ushirikina na baadhi yao kula kiapo kwa Kiruguru "Chihendo nghalekwa" kuwa kamwe hawatoweza kuacha mila zao za jadi zinazokwenda kinyume na mafundisho sahihi ya Uislamu. Uchunguzi uliofanywa na ANNUUR hivi karibuni huko vijijini umegundua kuwa mioyo ya Waislamu wengi wa Uruguruni imeota kutu kiasi cha mila zao za jadi kuheshimika sana kwa kupewa nafasi ya kwanza na Uislamu wao kuupa nafasi ya mwisho. Baadhi ya Waislamu wa Korelo wameliambia gazeti hili kuwa idadi kubwa ya Masheikh wa Uruguru wamezama katika shirki kiasi cha kutumia hata Misikiti kwa kuendesha na kuratibia shughuli hizo ikiwa ni pamoja na kupiga bao (ramli) na kuandalia ibada za kafara kwa mizumu. Shughuli nyingine, Waislamu hao walimueleza Mwandishi wa habari hizi kuwa ni pamoja na kushiriki kikamilifu katika sherehe za kurithisha vyeo vya jadi (cheo cha Mlungu na kile cheo cha maji) ambavyo vyote hutawaliwa na ushirikina, mitungi ya pombe ya majina mbalimbali kama vile Nghangolola (pombe ya Gubiko au Ushingi), Nduga, Lwindi, Nghula, Mlawo, Duga, Mbeta, Nghanyaga (zote ni aina za pombe za ngomani) na kitemakumbi (pombe ya kuwaita ndugu shaurini) n.k. "Masheikh wetu wengi wanategemea sana Changila mbago (ada ya kuingilia porini kuchuma dawa) na Tumbavi (ada ya kumponyesha mgonjwa) kuendesha maisha yao ya kila siku", alisema Mama mmoja mkazi wa Bwakila juu akithibitisha ushirikina unaofanywa na viongozi hao. "Hali ni mbaya huku kwetu kiasi cha kufikia swala ya faradhi kucheleweshwa hata saa nzima, kisa, eti Imamu kalala, asiguswe hadi aamke mwenyewe", aliongeza kusema Bw. Abdulhamid Muhulo mwenyeji wa Mgeta Morogoro vijijini. Baada ya kuishiwa
nguvu, sasa wanaomba msaada
WAISLAMU wa kijiji cha endagaw - Endasak katika wilaya ya Hanang’ mkoani Arusha wanawaomba Waislamu popote walipo kuwapa msaada wa hali na mali ili kumalizia jengo la Msikiti wao. Msikiti huo ambao ulianza kujengwa mwezi Julai mwaka jana, kisha kuwekwa jiwe la msingi na Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Wilaya hiyo Mh. Frederick Tluway Sumaye Agosti 29, 1998 umefikia ngazi ya umaliziaji, hivyo zinahitajika nguvu za ziada. Akizungumza na ANNUUR hivi karibuni mjini Arusha, Sheikh wa wilaya hiyo ambaye pia ni Imam wa Msikiti huo, Sheikh Waziri Omar Mollah alisema hivi sasa wameishiwa nguvu za kumalizia Msikiti huo. "Tulianza kujenga tangu Julai mwaka jana, tumejitahidi, Alhamdulillah, lakini sasa hivi nguvu hatuna tena, tunawaomba ndugu zetu Waislamu wanaojua umuhimu wa nyumba ya Allah (s.w.) watusaidie kumalizia tulipokwamia", alisema Sheikh Omar. Aidha, Sheikh Omar alisema yeyote mwenye vifaa vya ujenzi kama saruji, nondo au vioo awasiliane na mkuu wa wilaya hiyo kwa simu au S.L.P. 10 Katesh. Au atumie Account No. 13130/16 National Microfinance Bank Ltd Katesh - Hanang’. Wakati huo huo, Waislamu wa Masjid Nuru - Endagaw wameitaka Bakwata mkoa wa Arusha kutekeleza ahadi waliyoiweka viongozi wa Bakwata mkoa wa Arusha (Sheikh Kisiwa Ali na Alhaj Mollel) siku ya uwekaji wa jiwe la msingi ya kuchangia shilingi laki moja kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti na badala yake kukaa kimya hadi hivi sasa licha ya kukumbushwa mara kadhaa. Katika barua iliyoandikwa Januari 15, mwaka huu na kusainiwa na Imam wa Msikiti huo ambayo ANNUUR inayo nakala yake imewataka viongozi wawe mfano mzuri wanaposhindwa kutimiza ahadi imedai kuwa ni chukizo kubwa kwa Mwenyezi Mungu. |
YALIYOMO
Tahari
Matokeo ya mitihani darasa la saba serikali ieleze: Je, Waislamu ni taahira au kuna agenda ya siri Wenye siasa za kikaburu wasimyumbishe Rais Hatuko tayari kuruhusu viwanja viporwe - Manyema Maoni yetu
DONDOO ZA KISAIKOLOJIA: PEDOPHILIA Uislamu na Mazingira katika
Umoja wa Mataifa
Barua za Mtume (s.a.w.) za Jihad katika
Internet
Rais Mkapa atekeleze hadi yake
kwa hadhari
Mashirika ya Dini yaelekeze
misaada vijijini
Hotuba ya Mh. Kitwana Kondo (MB) aliyoitoa Bungeni Dodoma Ni serikali ipi anayoiwakilisha
Sumaye
Sehemu ya maelezo ya Waziri Mkuu bw. Frederick Sumaye bungeni Zanzibar ni nchi au mkoa?.
Sheikh Bafadhil aamuru kusimamishwa shughuli za African Muslim Agency Moro Vijana Arusha njooni mnione - Alhaj Mollel Waislamu Korelo wazama kwenye ushirikina Waislamu Hanang’ wajenga Msikiti Sayansi na Teknolojia
Chakula na Lishe
|