|
Na. 034 Jumatano Februari 9 - 15, 2000 |
|
|
|
|
|
Ndoto ya ajabu MTUNZI: Marcussy Mzee Matachi Abdallah ni kijana mrefu, mweupe kiasi na mwili uliojengeka vizuri. Ana elimu ya kutosha, kwani hivi karibuni amemaliza masomo ya kidato cha sita, amefaulu vizuri katika masomo yake yote toka katika sekondari moja ya mjini Morogoro. Kutokana na ajira kuwa za matatizo miaka ya hivi karibuni, Matachi anajikuta naangukia kufanya kazi katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya mkoa Morogoro, kazi hiyo ameamua kuifanya baada ya kupata kishawishi toka kwa rafiki yake aitwae Zakaria, ambaye walisoma wote shule ya msingi miaka kumi na tano iliyopita. Alianza kazi hiyo kwa hofu ya woga, lakini aliizoea siku hadi siku, akaipenda kazi hiyo kutokana na marupurupu mazuri na mshahara mnono aliopata, tayari alishatimiza miaka karibu sita akifanya kazi ndani ya chumba cha maiti. Siku moja usiku wa manane akiwa peke yake ndani ya chumba cha maiti, anasikia mlango unagongwa, Matachi alipofungua mlango akatokea mwanamke mrembo wa kupindukia akaomba apewe maji ya baridi anywe sababu amechoka, tena ana kiu. Kijana Matahci akiwa bado ameduwaa ghafla akasikia kishindo kikubwa, alibaki pale mlangoni akitetemeka kijasho chembamba kinamtoka, alitaka kukimbi lakini akashindwa, aliendelea kusimama pale mlangoni akijiuliza kile kishindo ni cha nini, na yule mwanamke ni nani, mara akasikia sauti kali za watu zikiongea pale ndani hofu ikamzidi moyoni. Baada ya muda yule mwanamke akatoweka pale mlangoni, ndipo Matachi akaona akiendelea kuwa mwoga kiasi kile na yeye ni mwanamume si vizuri, akaufunga ule mlango kwa nguvu akarudi ndani ili kujua ni watu gani waliokuwa wakiongea kwa sauti kali. Hivi nyinyi mnaongea humu ndani ni akina nani? Alijikuta akiuliza kwa sauti kali iliyojaa mtetemo. Lakini hakupata jibu. Ukimya ukatawala, hapakuwa na sauti ya aina yeyote kila kitu kilikuwa sehemu yake kama kawaida. Hakuwa na la kufanya tena, alijiuliza moyoni yule mwanamke wa ajabu ametokea wapi, au ni mzimu, je wale watu waliokuwa wakiongea ni watu wanatokea wapi, wanaweza kuwa maiti wamefufuka? Hata kama wamefufuka wametokea wapi ili hali maiti wote wamefungiwa ndani ya mafriji. Maswali yote haya hakupata jibu. Matachi alikaa chini akaweza na kukumbuka kuwa siku moja aliipasua maiti ya mwanamke mmoja aliyefariki kutokana na ajali ya gari, mwanamke huyo kidoleni alikuwa amevalia pete kubwa ya dhahabu, ambayo Matachi aliichukuwa, lakini pete hiyo ilikuwa ya ajabu, sababu tangu aichukue na huiweka ndani ya mfuko wa suruali yake ile pete haitoki ndani ya ule mfuko isipokuwa anapokuwa ndani ya chumba cha maiti. Akatoka mbio mpaka mwenye droo zinakohifadhiwa maiti akavuta ile droo, akaiona ile maiti ya yule mwanamke imelala ikitabasamu, akaitoa ile pete akairudisha kwenye kidole cha yule maiti, maana hakutaka tena kusubiri yasije kumkuta makubwa zaidi. Baada ya hapo akaona ni bora atoke aende nyumbani usiku ule, lakini alipokwenda mlangoni alipoufungua mlango haukufunguka, likamjia wazo jingine, akaelekea dirishani, ajabu ni kwamba juu ya kutumia nguvu zake zote lakini dirisha nalo halikufunguka wala kutikisika hata kidogo. Akatoka hapo akalifuata dirisha jingine lakini huko nako mambo yalikuwa hivyo hivyo, akachanganyikiwa. Ghafla alisikia sauti ya mwanamke ikisema, "wewe unajifanya mjanja sasa leo utakiona cha moto." Matachi akaangua kilio kwa sauti ya juu huku akipiga kelele akiomba msaada toka nje kwa watu lakini hakuna aliyesikia kelele hizo. Akakata tamaa, akarudi kwenye kiti kukaa akisubiri nini kitatokea. Alipokutanisha macho yake na saa ya ukutani ikamwonyesha kuwa imetimia saa nane na nusu usiku, hakuweza tena kupata usingizi. Mawazo yote yalikuwa juu ya vile vituko vya ajabu. Mara kishindo kingine kikubwa zaidi kikasikika. Matachi akatazama kilipotokea, akaona kitu kikubwa cha duara kimeanguka sakafuni. Akakisogelea na kukiokota. Baada ya kukiangalia akakitambua, akakitupa chini akarudi mbio mpaka pale alipokaaa mwanzo huku akipiga kelele ovyo. Kitu hicho kilikuwa ni kichwa cha binadamu, tena cha mwanamke mrembo aliyetajamali kwa uzuri, alitishika sana. Akakiri kuwa kwa mara ya kwanza katika maisha yake amepatwa na woga kama mtoto wa kike. Lakini hakuwa na la kufanya kwa siku ile, hakuweza kutoka ndani ya chumba, wala hakuna aliyesikia kelele zake za kuomba msaada. Akiwa bado anatapatapa asijue nini la kufanya, akaona kivuli cha mtu kikimnyemelea kimeshika shoka mkononi. Mtu huyo alikuwa ni mrefu sana amevalia joho jekundu. Matachi akageuka kumwangalia mtu huyo ili ikiwezekana ajihami vilivyo. Ile kugeuka tu yule mtu alirusha shoka lililomkosakosa Matachi na kuanguka hatua chache toka pale alipo Matachi. Aliinama na akaliokota lile shoka, akatanabahi kuwa ni shoka la mule chumba cha maiti ambalo yeye mwenyewe ndio hulitumia. Akanyanyua uso kumwangalia yule mtu, lakini hakumuona yeye wala kivuli chake. Akapiga moyo kondo kuanza kumtafuta nyumba mzima lakini hakumuona, hapakuwepo hata dalili tu za kuwepo tena mtu. Akarudi kwenye kitichake pumzi zikimwenda mbio, akaketi chini amechanganyikiwa, akaelewa sasa ni kifo tu alichokuwa akisubiri. Mara akasikia sauti za watu zikinong'ona kwa mbali mle ndani, huku wakinyata kuelekea kule alipokuwa amekaa. Akasimama na kuuliza kwa hasira iliyojaa woga "nyinyi ni akina nani?" "Ni mimi Kisisina na wapambe wangu", ilijibu sauti ya kike kwa kicheko cha dharau. "Majini na binadamu wote tumeumbwa ili tumuabudu Mungu tu, nihurumie na utapata baraka tele kwa Mungu", hiyo ilikuwa ni kauli ya Matachi ikiomba msamaha. "Kama nitapata dhambi kukuua wewe mwizi wa pete ya dhabu, wacha niipate, lakini wewe lazima ufe", ilijibu sauti ya yule mwanamke. "Nisamehe, nisamehe ewe Kisisina, niachie maisha yangu nipo tayari kukupa pesa zangu zote na dhahabu za mke wangu na chochote utakacho nitakupa", alilalama kwa kutetemeka Matachi. "Mimi sitaki pesa, dhahabu wala kitu chako chochote, mimi nataka roho yako, basi", ilisisitiza ile sauti ya kike. "Je wewe ni dini gani, kama ni Muislamu toa shahada kwa mara ya mwisho kwa Mola wako", alimaliza kusema kwa kitisho. Matachi akakata tamaa, akajua maisha yake sasa yamefikia mwisho hapa duniani. Yule mpambe wa Kisisina akachukua kamba na kiti akamfuata Matachi, akamfunga kitanzi shingoni, kisha Matachi akapandishwa juu ya kile kiti. Muda wote huo Matachi alikuwa ametulia hana la kufanya isipokuwa kutii amri tu mithili ya mbwa amwonapo chatu. Kitanzi kikamkaza shingoni, akaanza kuhisi maumivu makali sana, na kupumua kwa taabu, mate yakamkauka na giza likatanda machoni mwake. Akapiga kelele za kuomba msaada, lakini sauti haikutoka. Mpaka hapo Matachi alikuwa hawezi kutazama wala kuzungumza, akatoa shahada ya mwisho, akawa anasikia kwa mbali yule mwanake akisema kila nafsi itaonja mauti, na sifa ya kuonja hapa ni uchungu. Ewe binadamu angalia roho yako inavyotoka kwa taabu, yote hii ni sababu ya madhambi yako hapa duniani, hukutaka kumkumbuka Mola wako na sasa leo kwake unarejea. Ole wako wewe uliyetangulia na waliobakia ulimwenguni, wanayaponda maisha pasipo kukumbuka kwamba ipo siku nao watatakiwa kufa na wafahamu kwamba mambo mema tu ndiyo itakuwa salama yao mbele ya Mungu, ilimaliza ile sauti. Kwa mbali alisikia sakata nyingine ikimwita, "Matachi, Matachi wewe Matachi", ilikuwa ni sauti ya mke wake, mama Asha. Matachi alijitahidi kujitingisha, mara akastuka, kijasho chembamba kilikuwa kinamtoka, akamwangalia mke wake, uso wote umemjaa hofu. Ilikuwa ni ndoto ya kutisha na ya ajabu, iliyompata hofu kubwa katika maisha yake. Matachi akawa Muumini kuanzia siku ile akaachana na ulevi akarudi kwa Mola wake. MWISHO |
YALIYOMO
Tahariri:
Serikali inakwamisha barabara ya Kibiti-Lindi -CUF Waislamu kuadhimisha mauaji ya Mwembechai J’pili Wazanzibar sasa wataka kuuona Mkataba wa Muungano Wanawake wa Kiislamu watakiwa kupinga unyanyasaji wa kijinsia Rufaa za chaguzi za serikali za mitaa na vitongoji MAKALA
MAKALA
Kalamu
ya Mwandishi
Makala
USHAURI
NASAHA
MAKALA
LISHE
Michuano ya soka Mataifa ya Afrika |
|
|
|
|