Zikiwa zimesalia siku 26 kupiga kura:
Wafumwa wakigawa shahada za kuibia kura

JUZI kundi la wana CCM na watendaji wa serikali mjini Mwanza, walivamiwa wakidaiwa kugawa shahada za kuibia kura.

Mkasa huo ulitokea katika eneo la mlango mmoja kata ya Mbugani baada ya vyama vya CUF, NCCR na TLP kuvamia ofisi ya Mtendaji Kata na kuwakuta Mwanasheria wa Manispaa ya Mwanza, Katibu Mtendaji, Mwandishi Msaidizi wa wapiga kura na Mgombea wa CCM Mzee Ngofilo, wakiwa wamekamatia shahada na vitabu vya shahada kadhaa visivyotumika.

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo, mbali ya shahada hizo, "ambush" hiyo ilikuta vitabu vya shahada vilivyojazwa majina hewa kimoja kikiwa na nambari 163/d/31/354 na vingine vikiwa vimejazwa namba bila kuwa na majina.

Watu waliokutwa katika ofisi hiyo akiwemo mgombea wa CCM walitoka nje na kukimbia wakiwaacha ofisini wanachama hao wa vyama vya upinzani.

Waliotimua mbio wametajwa kuwa ni pamoja na Mtendaji wa Kata, mgombea udiwani wa CCM kata ya Mbugani Mzee Masalu Ngofilo na mwandishi wa wapiga kura Bw. Iddi.

Mkasa huo uliodumu kuanzia saa 4:30 asubuhi hadi saa 8 mchana ulimkumba mwanasheria wa Manispaa ambaye anadaiwa kufika katika kikao hicho akiwa na gari la mkurugenzi wa manispaa lenye namba SM 2678.

Katika kuzingira ofisi hiyo, mtu mmoja katika walioitwa kuchua shahada,alikamatwa ambapo alitoa maelezo kuwa walikuwa wamepewa maelekezo waje wapewe shahada za kupigia kura na namna ya kuzitumia.

Mtu huyo aliyejulikana kwa jina la Stansioza Mgoma Robert alidai kuwa yeye na wenziwe walipewa maelekezo na viongozi wa CCM ambao hakuwataja, kwenda kuchukua shahada hizo ofisini hapo.

Imeelezwa mkasa huo ulitokea baada ya baadhi ya watu waliotakiwa kwenda kuchukua shahada hizo ofisini hapo kuripoti kwa vyama vya upinzani.

Watu hao ambao kila mmoja alitakiwa apeleke majina ya watu 20 anaowajua walidai kuwa walipewa taarifa hizo na baadhi ya jamaa zao ambao ni watendaji wa Manispaa, ofisi za kata na wakereketwa wa chama tawala.

Hekaheka ya uvamizi huo uliishia kituo cha Polisi wilaya ambapo mkuu wa kituo alikataa lisifunguliwe jalada na

kutaka suala hilo liahirishwe hadi jana.Aidha taarifa zinaeleza kuwa polisi waliwaachia watuhumiwa waondoke na vitabu vyao.

Hata hivyo jana wahusika wa vyama CUF,TLP na NCCR walipofika kituoni OCD alikataa kuzungumzia suala hilo na kuwataka wawasiliane na kamanda wa polisi mkoa (RPC).Lakini RPC naye alidai kutokujua suala hilo na kutaka apewe muda kulishughulikia.

Katika mkutano wa jana wa kampeni za ubunge kupitia chama cha CUF tukio hilo lilitajwa kama ushahidi wa mbinu za CCM za kuiba kura.

Jijini hapa suala hili limekuwa ni gumzo kubwa ambapo inadaiwa kuwa shahada zinazodaiwa kugawiwa zinaleta wasiwasi kuwa huenda idadi ya wapiga kura iliyotangazwa ikawa na walakini.

"Kama idadi ya wapiga kura ishatangazwa, hawa wanaogawiwa shahada leo wataingizwa kwenye orodha ipi?",amehoji Bw.Yusuf.

Umekuwepo wasiwasi juu ya idadi ya wapiga kura kutokana na jinsi zoezi hilo lilivyokuwa limedorora kiasi cha kuwafanya viongozi wa serikali kujaribu kutoa ushawishi na hata kuwakemea viongozi wa serikali za mitaa.

Hata hivyo Tume ya uchaguzi ikaja kutangaza kuwa idadi ya waliojiandikisha kupiga kura ni kiasi cha milioni tisa na laki sita upande wa bara.

Idadi hiyo ilielezwa ni sawa na asilimi 97 ya makadirio ya awali ya watu waliotarajiwa kujiandikisha katika zoezi hilo.

Tume ilidai kuwa ingawa awali kulikuwa na wasi wasi wa kuweza kufikia kiwango cha wapiga kura waliokadiriwa kutokana na kasi ndogo ya watu kujiandikisha, hata hivyo idadi hiyo iliongezeka siku ya mwisho bada ya watu kujitokeza kwa wingi.

Hata hivyo watu walilitilia mashaka dai hilo kwa madai kuwa siku ya mwisho haikuonekana misururu ya watu ambayo ingeweza kuleta ongezeko la idadi ya zaidi ya robo tatu kulinganisha na waliojiandikisha masiku kadhaa yaliyotangulia.

Katika hatua nyingine wananchi kadhaa Jijini wamemtaka Mwenyekiti wa Tume Jaji Lewis Makame kutoa maelezo juu ya taarifa za kuwepo wapiga kura hewa katika idadi iliyotangazwa na Tume yake.

Akizungumza na Gazeti hili Amir wa Shura ya Mamamu Sheikh Juma Mbukuzi amesema amani ya nchi hivi sasa iko katika mikono ya Tume ya Uchaguzi dosari yoyote ya kiuadilifu itakuwa na gharama kubwa.

"Nawaomba Majaji wayaambate maadili ya Ujaji ya uadilifu na kusimamia haki tupu, wasiwe tayari kuyumbishwa na yeyote hiki ni kipindi kigumu sana", ameasa Sheikh Juma.

Aidha alionya kuwa kuthubutu kukhini uadilifu katika suala la kura ni hatari inayoweza kuliangamiza Taifa.

"Vizazi vitawalaumu wale watakaojasiri kukiuka maadili ya dhamana walizokabidhiwa, amesisitiza Shekh Mbukuzi.

Katika wimbi hilo la nasaha kwa Tume ya Uchaguzi, Askofu Mstaafu wa KKKT Elinaza Sendoro akizungumza juzi aliiasa Tume ya uchaguzi kufanya uadilifu.

Askofu Sendoro alisema kumekuwa kukijitokeza kasoro katika utendaji wa Tume zinazoweza kuathiri uchaguzi na hatimaye kuvuruga amani nchini.


St. Thomas alikofia Nyerere'


WANA CCM mjini Moshi wamedaiwa kuvumisha kuwa Bw. Philemon Ndesamburo ni mgonjwa sana na amelazwa katika hospitali alikofia Mwalimu Nyerere mjini London.

Kufuta uvumi huo, Bw. Ndesamburo jana alihutubia mkutano wa kampeni huku akinyeshewa na mvua.

CCM wamedaiwa kutoa uvumi huo baada ya Ndesamburo kutokuonekana mjini Moshi kwa muda mrefu.

Bw. Ndesamburo alikuwa jijini Dar es Salaam kwa shughuli zake binafsi na zile za chama chake.

Uvumi huo ambao umedaiwa kuanzishwa na hata kuzungumzwa majukwaani na baadhi ya wagombea udiwani wa CCM uliwatia wasiwasi wananchi wengi mjini Moshi na kuzua gumzo kila kona.

Uvumi huo umeelezwa kuwa ni kutapatapa kwa wagombea wa CCM baada ya kuona kuwa wananchi wamewahama.

Katika mkutano wa jana uliofanyika kata ya Bondeni, umati wa watu ulihudhuria bila kujali mvua iliyokuwa ikinyesha.

Bw. Steven Wasira aliyehudhuria mkutano huo alieleza jinsi serikali inavyofuja hazina ya nchi huku ikitelekeza huduma za elimu na afya.

Alizitengua takwimu zilizokuwa zimetolewa na Rais Mkapa akidai sekta ya elimu hupewa mgawo mkubwa katika bajeti.

Akihutubia umati wa watu katika mkutano mwingine wa hadhara wa kampeni katika eneo la Karanga juzi, Ndesamburo alisema CHADEMA na CUF mwanzo waliwaita viongozi wa vyama vyote akiwemo Augustine Mrema, Bwana Cheyo na Mbatia kutaka kuweka mgombea mmoja. Lakini ilipofika mwisho wakajitoa mmoja baada ya mwingine, sijui sababu yake ni nini? Lakini nahisi ni nguvu ya fedha ndiyo ilitumika kusambaratisha umoja wa wapinzani", alisema.

Naye Mwinjilisti Kamara Kusupa ambaye yupo mkoani Kilimanjaro kumpigia debe mgombea wa Urais wa Chama cha CUF na CHADEMA, Prof. Lipumba, alisema Ndesamburo ni shujaa na mtu asiyeogopa. Amesema, yeye alikuwepo tangu mwanzo wa mfumo wa vyama vingi hata wakati ule Waziri wa Mambo ya Ndani Mrema alipozidisha vitimbi kwa upinzani na kupiga mabomu mikutano na maandamano ya wana mageuzi, bado Ndesamburo alikuwa mwanamageuzi.

"Angalieni wafanyabiashara wengine wako CCM si kwa sababu ya kupenda sera za CCM, wala kuridhika na uongozi wa chama hicho bali wako kwa ajili ya kujikinga ili wasibughudhiwe na dola katika biashara zao. Wengine wanaweka bendera na picha za Mkapa ili serikali isiwasakame katika shughuli zao", alisema.

Mwinjilisti Kusupa alisema, Lipumba atakapokuwa Rais atakula kiapo cha kulinda katiba kwa hiyo atatawala kwa kutumia katiba na kuwa Rais wa Watanzania kama walivyokuwa Nyerere, Mwinyi na Mkapa.

Wakati huo huo, Prof. Maghembe ambaye amekuwa akinadiwa na wapambe ambao hutanguliza matusi dhidi ya Waislamu ameendelea na kampeni zake huko Mwanga.

Akiwa Ugweno hivi karibuni aliambulia watu 8 huko Vuchama na Kifula akapata watu 16 wa kumsikiliza akimwaga sera zake kuomba kura.

Hali hiyo ilimpelekea Prof. Maghembe kuhamishia kampeni zake maeneo ya Tambarare ikiwemo Toloha na kwakoa.


Lipumba aingia Tabora kwa kishindo
MGOMBEA Urais kwa tiketi ya CUF na CHADEMA, Profesa Ibrahim Lipumba aliingia mjini Tabora juzi usiku na kupokelewa na maelfu ya wakazi wa mji huo waliokuwa wakimsubiri kwa hamu kuanzia nyakati za mchana.

Profesa Lipumba alikuwa akitokea Wilayani Nzega ambako alifanya mikutano ya hadhara ya kampeni zake.

Wakazi wa mji huu ambao walisitisha shughuli zao ikiwa ni pamoja na kufunga maduka walijipanga maeneo ambayo mgombea huyo angepita kuelekea ofisi za chama cha CUF mkoani hapa.

Hoi hoi na vifijo vilisikika sehemu mbali mbali za mji mnamo saa tatu za usiku baada ya Profesa Lipumba kuwasili katika viunga vya mji huu.

Umma mkubwa uliojitokeza katika mapokezi hayo uliongozana kupitia bara bara mbali mbali hali iliyosababisha magari kushindwa kupita na shughuli nyingine kusimama.

Profesa Lipumba atakuwa mkoani Tabora kwa siku tatu ambapo jana alitembelea Urambo na Sikonge kukamilisha ratiba yake kabla ya kurejea mjini hapa ambapo siku ya jumatano atahutubia mkutano wa hadhara eneo la nje la uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

Anatazamiwa kuondoka Tabora jumatano usiku kuelekea Kigoma mjini.

Wakati huo huo, Wananchi wa Igunga juzi walisimama kidete kusikiliza mkutano wa kampeni wa CUF licha ya kutishwa na polisi waliokuwa wamejazana mkutanoni hapo.

Mkutano huo uliokuwa unahutubiwa na mgombea mwenza wa Prof. Lipumba juzi, ulikuwa na askari wengi wakiwemo FFU tofauti kabisa na mikutano mingine ya kisiasa ambayo imewahi kufanyika.

Pamoja na mazingira hayo ya kutisha, wananchi walifurika wakiwaacha polisi wakirandaranda na silaha zao.

Baada ya kuona vitisho hivyo havikuwazuia wananchi, Mkuu wa kituo cha polisi Igunga aliamuru mkutano huo ufungwe saa kumi na nusu.

Hata hivyo, Bw. Nassor Khamis aliyekuwa akihutubia mkutano huo alimkatalia akimweleza kuwa mwisho wa kampeni ni saa kumi na mbili jioni.

Katika mkutano huo Bw. Nassor aliwaahidi wananchi kuwa iwapo watamchagua Prof. Lipumba, atahakikisha kwamba kodi zilizopo zinarekebishwa ili ziwe sambamba na kipato cha mwananchi na ziweze kulipika na wakati huo huo kutumiwa kwenye sekta muhimu.

Aidha, Bw. Nassor alisema kuwa kodi ambazo ni za manyanyaso hazistahili kuwepo ikiwemo kodi ya maendeleo ambayo alidai kwamba haina kigezo chochote cha kipato.

Katika sera ya haki sawa kwa wote, Bw. Nassor alisema kuwa akiwa kama mwanasheria atahakikisha kuwa anarekebisha hali za mahakama ili kuweka mazingira mazuri ya kutenda haki kwa wananchi. Alisema siku hizi mahakama zimekuwa nyumba za kununulia haki ambapo mwenye haki hapati haki yake.

Aidha, alisema kuwa atahakikisha jeshi la polisi linafanya kazi kama chombo cha serikali na sio kama chombo cha chama tawala kama ilivyo hivi sasa ambapo jeshi hilo alidai limekuwa likitumikia siasa baala ya kulinda usalama wa raia.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook