Hayo ni maneno ya Seif Sharif Hamad alipohutubia umati wa wananchi wa Unguja hivi karibuni.
Maalim Seif anayegombea Urais kupitia CUF alikuwa akichambua jinsi Zanzibar inayoathiriwa na mfumo wa sasa wa Muungano.
Amesema, kwa mfumo wa sasa wa Muungano Zanzibar hairuhusiwi kuwa na Benki Kuu ambapo Waziri wake wa Fedha huwa tu kama karani aliyevikwa kilemba cha ukoka.
Amesema, hicho ni kikwazo kikubwa ambapo Zanzibar inashindwa kupanga mipango yake ya maendeleo.
Akitoa mfano amesema, huko nyuma Zanzibar ilishatumia fedha nyingi sana kubuni miradi mbalimbali lakini Waziri wa Fedha wa Muungano akakataa.
Amesema, hivi sasa serikali ya Zanzibar hairuhusiwi kutumia kodi inayokusanywa Zanzibar. Bali yote hupelekwa Benki Kuu Dar es Salaam.
"Bendera hatuna... hata kuamua mambo ya nje hatuna uwezo. Basi jamani hata hizi fedha ambazo zinakusanywa katika nchi yetu kuzitumia hatuna ruhsa?" anahoji Seif huku umati wa watu ukipigwa na mshangao.
Maalim Seif amesema, mtaji wa Zanzibar katika kuanzishwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilikuwa asilimia 11.4. Na kwamba ilikuwa wapate mgawo wa asilimia hiyo (11.4), lakini akasema kwa miaka 20 hawakupewa hata senti moja, na walipoanza kupewa wanapewa asilimia 4.5.
"Sasa wameamua kutupa, wametupa asilimia 4.5. Na anakuja Dkt. Omar (Makamu wa Rais) anajisifu, Rais Mkapa anawapenda Wazanzibari, anawapa fedha, sijui anawapa nini. Hatupi Bwana. Ile ni haki yetu, tena tunadhulumiwa. Kwa hiyo asizuke mtu akajisifu huyu mtu anaipenda sana Zanzibar. Haipendi hata kidogo". Amesema.
Kuhusu muundo wa muungano amesema, ni Wizara nne tu zilizo katika muungano. Mambo ya Ndani, Ulinzi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Wizara ya Elimu ya Juu.
Akahoji, Wizara nyingine kama Kilimo, Afya na Elimu na nyingine zimepata wapi mamlaka ya kuwa Wizara katika serikali ya Muungano, wakati si Wizara za Muungano.
Utata huo amesema, unaiathiri Zanzibar kwa vile katika mashirika kama UNESCO, WHO na FAO ni Waziri wa Bara anayewakilisha na Zanzibar haimo hivyo hukosa misaada ya mashirika hayo.
Aidha, Maalim Seif amehoji ni kwanini dhahabu na almasi imefanywa si jambo la muungano, kinyume na ilivyofanywa kwenye mafuta.
Katika hotuba hiyo aliyodai ni ya kumtoa paka ndani ya gunia, amesema, Zanzibar ina mafuta mengi sana lakini kwa kufanywa ni suala la muungano, lau yatachimbwa Zanzibar itapewa bilioni 4.5 tu kati ya bilioni 100 zinazotarajiwa kupatikana kwa mwaka.
Amesema, wao wanaporwa mafuta yao wakati dhahabu na almasi itabaki kuwa ya Watanganyika peke yao.
Seif alimalizia hotuba yake kwa kuwaambia Wazanzibari kuwa kipigo wanachopewa sasa ni ili wachoke wakate tamaa wasiiteteee nchi yao.
(Soma hotuba yote... bonyeza
hapa).
UVUMI kuwa mgombea Ubunge jimbo la Mwanza mjini amenunuliwa umeenea kiasi cha kuwatia wasiwasi wana CUF.
Habari kutoka Mwanza zinaeleza kuwa mashabiki wa CUF wamekuwa wanyonge huku CCM wakitamba kuwa washaondosha mwiba uliokuwa umewakalia kooni.
Uvumi huo umepata nguvu baada ya Bw. Omar Mbalamwezi kutokuonekana jukwaani wala mjini Mwanza kwa wiki mbili sasa.
"Ishakuwa upuuzi, hata hiyo kura ya Rais sipigi na shahada lenyewe nalichana", alisema Bwana mmoja kutoka Mwanza akielezea masikitiko yake kwa kutokumwona mgombea wake kwa muda mrefu.
"Hatuna raha mitaani hapa wakereketwa wa CCM wanatamba, "kiko wapi milioni 12 zishamtoa imani", alisema Bwana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Kishepo.
Kufuatia kutokuweko kwa Bw. Mbalamwezi, imeelezwa kuwa vyama vingine vimeanza kupumua, kwani vilikuwa havipati watu alipokuwa anafanya kampeni zake.
Habari kutoka Mwanza zimeeleza kuwa, kila siku toka mwanzoni mwa wiki, watu wamekuwa wakimiminika kituo cha mabasi na stesheni ya Reli kuangalia huenda watamkuta amerudi.
"Wiki yote hii watu wamekuwa wakienda kituo cha basi kuangalia kuwa amerudi, lakini wapi, inatutia wasiwasi sana", alisema Bw. Titus Mbura akiongea na mwandishi wa habari hizi jana.
Amesema, mgombea Ubunge wao alikuwa arudi mwishoni mwa wiki iliyopita kutoka Dar es Salaam alikokwenda kwa shughuli zake maalum.
"Kuchelewa kwake kunatutia wasiwasi kwani kabla hata hajaondoka kulishakuwa na uvumi kuwa CCM wanataka kumnunua. Hata hivyo akasema kuwa maneno hayo hayakuwa rasmi bali yakisemwa na washabiki tu mitaani.
"Japo yalikuwa maneno ya wakereketwa, lakini hatuwezi kuyapuuza", alisema.
Hata hivyo taarifa nyingine zimedai kuwa Bw. Mbalamwezi mwenyewe kasema kuwa, aliwahikufuatwa na baadhi ya vyama wakitaka kumpa fedha ajitoe.
Wasiwasi huo ukiendelea huko Mwanza, gazeti hili lilimsaka na kumpata Bw. Mbalamwezi akiwa jijini hapa.
"Mimi siwezi kuwasaliti wananchi wa Mwanza", amesema Bwana Mbalamwezi akiongea na mwandishi wa habari hizi jana.
Amesema, anawajua wanaoeneza uvumi huo lakini hawataambulia chochote.
Bw. Omar Mbalamwezi amesema, amechelewa kurudi Mwanza kutokana na kutokukamilisha haraka kwa shughuli zake zilizokuwa zimemleta Jijini Dar es Salaam.
Amesema, anatarajia kuondoka Jumamosi au Jumapili keshokutwa kuelekea Mwanza.
Bwana Mbalamwezi amedai kuwa yeye ameazimia kuingia katika kinyang'anyiro hicho na kamwe hayuko tayari kuwasaliti wananchi wa jimbo hilo.
Akiongea na gazeti hili jana Bwana Mbalamwezi ambaye yuko jijini kwa shughuli za kibiashara amesema ni sawa na kujipa laana iwapo atakubali kurubuniwa.
"Ninasikia yuko mgombea wa chama kimoja anayeeneza uvumi kuwa mimi nimenunuliwa yeye angejitahidi kueleza sera za chama badala ya kujisumbua kutamka maneno kama hayo", alidai Bwana Mbalamwezi.
Amewataka wananchi wa Mwanza mjini kutobadili msimamo kutokana na 'upuuzi' unaoenezwa na baadhi ya watu.
"Kukubali kununuliwa na CCM niachie wajibu huu
ni sawa na kuramba matapishi yangu, katu sitafanya hivyo na Mwenyezi Mungu
anashuhudia", alisisitiza Bwana Mbalamwezi.
VIONGOZI wa CCM wilayani Mwanga wameshutumiwa kwa udini na ukabila.
Imedaiwa kuwa viongozi hao ndio wanaowagawa Walutheri wilayani humo na kuleta mifarakano ya watu wa Ugweno na Usangi.
Shutuma hizo zimetolewa na mgombea Ubunge jimboni hapo kupitia Chama cha CUF, Bw. Oliver Msuya.
Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Mwanga juzi Jumatano, Msuya amesema, mgogoro kati ya Walutheri umedumu kwa sababu viongozi wa CCM wenye madaraka wanauchochea kwa kuunga mkono upande mmoja.
Aidha, amedai kuwa viongozi hao wamekuwa na ubaguzi ambao umewachonganisha watu na kuleta fitna kati ya watu kutokana na maeneo wanayotoka.
Bw. Msuya amedai mtafaruku uliotokea hadi watu kukatana mapanga na kufyekeana migomba umechochewa na kupaliliwa na viongozi hao.
Hata hivyo hakufafanua ni fitna gani iliyotolewa na CCM na kuwagawa watu wa wilaya ya Mwanga.
Bw. Cleopa Msuya, kigogo wa CCM amekuwa akizunguka wilayani humo akidai kuwa CUF ni chama cha kidini. "Uzee wao binafsi na uzee wa chama chao unawasumbua. Lazima safari hii tujikomboe", amesema Bw. Mfinanga wa Mruma.
Habari kutoka Mwanga zinaeleza kuwa mkutano huo ulikuwa mkubwa sana na haujawahi kufanyika mkutano wa kisiasa wa aina hiyo wilayani humo.
Mkutano huo umeelewa kama pigo kubwa sana kwa CCM kwani mikutano yake yote iliyowahi kufanya haijawahi kukusanya japo theluthi ya umati wa juzi.
Taarifa zinasema kwamba, mkutano mkubwa zaidi unatarajiwa kufanyika hivi karibuni ambao utawaleta Bw. Ndesamburo na Tambwe Hiza.
Wilaya ya Mwanga na ile ya Same zimekuwa ndio wilaya pekee mkoani Kilimanjaro ambazo bado zilikuwa ngome ya CCM.
Huko Hai, Bw. Freeman Mbowe amewaambia wananchi kuwa suala lililobaki ni ulinzi wa kura na sio kupiga kampeni kuzitafuta.
Katika mtizamo huo huo wananchi wa eneo hilo wamedai kuwa kama ni ngangari basi wao ndio watakuwa ngangari hasa.
"Sisi hatuna wasiwasi na kupata ushindi Bwana Mbowe. Ila tunawaonya CCM, wasithubutu kuleta udanganyifu wowote au kuiba kura. Kama ni ngangari wataikuta kwetu", amesema Bw. Kimaro mmoja wa wanachama wa CHADEMA.
Bw. Mbowe anagombea Ubunge Hai kupitia chama hicho
cha CHADEMA.
WATU wanaosadikiwa kuwa ni wakereketwa
wa CCM juzi walivuruga mikutano ya Prof. Lipumba Tandahimba.
Watu hao wakiwa katika makundi mawili walianza kwa kurusha matusi na kupiga kelele hali iliyofanya kusiwe na masikilizano.
Polisi waliokuwepo hawakuchukuwa hatua yoyote hali iliyofanya watu hao kufanya fujo kadiri walivyotaka.
Hali hiyo ilimwandama pia mgombea mwenza Bw. Nassoro Khamis alipofanya mikutano yake kwenye vijiji vya wilaya hiyo ambapo kundi la wanachama wa CCM liliingilia mikutano hiyo kwa nyakati tofauti na kutawanya watu waliokusanyika mkutanoni na kusababisha kuvunjika kwa mkutano.
Viongozi wa CUF wilayani humo wamedai kwamba vurugu hizo ziliandaliwa na viongozi wa chama tawala pamoja na makada wao ndio maana hata polisi walitizama tu bila kuingilia.
Wamesema baada ya kuona hawana watu, sasa CCM inakodi watu kuvuruga mikutano ya CUF.
Hata hivyo juhudi za Mwandishi kuwapata Viongozi wasemaji wa polisi na Viongozi wa CCM Wilayani Tandahimba kuzungumzia suala hilo hazikuweza kufanikiwa.
Akiwa Newala, mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha CUF na CHADEMA, Prof. Ibrahim Lipumba amedai kwamba atashughulikia tatizo la rushwa nchini kwa kuanza kuwashughulikia sangara wakubwa na kumalizia na dagaa.
Prof. Lipumba alisema hayo wakati alipokuwa akihutubia wananchi wa wilaya ya Newala katika mkutano wa kampeni uliofanyika juzi wilayani humo.
Prof. Lipumba alisema, serikali ya CCM imekuwa ikiwakumbatia vigogo wanaobainika kula rushwa halafu inawafuatilia wala rushwa wadogo. Alisema kuwa pamoja na Rais Mkapa kudai kwamba anapambana na rushwa nchini, bado tatizo la rushwa limekithiri kutokana na kuwalinda vigogo wanaojishughulisha na vitendo vya rushwa.
Aidha, Prof. Lipumba alisema, Tanzania hivi sasa katika orodha ya nchi zinazoongoza kwa rushwa duniani ni ya saba wakati katika bara la Afrika ni nchi ya tatu baada ya Nigeria na Cameroun.
Prof. Lipumba aliahidi kwamba iwapo atachaguliwa elimu ya msingi itakuwa ni haki ya kila mtoto na kwamba mzazi atakaposhindwa kulipa ada serikali itagharamia. Alisema kuwa kila mtoto ataendelea kusoma kwa kadri ya uwezo wa akili yake na sio kusoma kwa kadri ya uwezo wa fedha za wazazi wake.
Aidha aliongeza kwamba serikali yake itatenga robo ya matumizi yote ya serikali kwenda kwenye sekta ya elimu ili kuboresha hali ya elimu nchini.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |