Harakati za kudai uhuru wa Tanganyika

JULIUS Kambarage Nyerere alikuja Dar es Salaam mwaka 1952 akiwa kama mwalimu wa shule ya St. Francis College, Pugu. Nyerere alikuwa na Mwapachu huko Tabora katika mwaka 1945, na Makerere College na baadaye nchini Uingereza wakichukua masomo ya juu. Inawezekana kwamba Nyerere kufuatia harakati za chama cha TAA, alisikia kuhusu Abdulwahid kupitia kwa Mwapachu alipokuwa bado yuko Uingereza. Mwapachu na Nyerere walikuwa wanafunzi katika Makerere College wakati ambapo Kasella Bantu na Nyerere walifundisha katika shule moja, St. Mary's School huko Tabora. Ameandika Mwandishi maarufu wa historia ya Tanganyika, BW. MOHAMED SAID katika kitabu chake The Life and Times of Abdulwahiid Sykes.

KASELLA Bantu mwanachama wa TAA mwenye msimamo mkali sana na mwenye msimamo usiotetereka wa kupinga ukoloni alijiuzulu kufundisha na alikuja Dar es Salaam kujiunga na Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC).

Katika hotuba ya kuaga yenye kuhuzunisha ambayo Nyerere aliitoa tarehe 5 Novemba, 1985 kwa Wazee wa Dar es Salaam, kikundi cha Waislamu pekee wakazi wa mjini waliomuunga mkono tangu kuundwa kwa TANU, Nyerere aliwaambia wasikilizaji wake kwamba ilikuwa Kasella Bantu aliyemtambulisha yeye Nyerere kwa Abdulwahid.

Hii ilikuwa ni moja ya zile nyakati adimu sana ambazo Nyerere alizungumza hadharani kuhusu siku zake za mwanzo na ilikuwa mara ya kwanza kutaja jina la Abdulwahid hadharani akimhusisha na historia yake mwenyewe na ile ya chama.

Nyerere alikuwa mgeni kabisa mjini Dar es Salaam na kama ilivyokuwa mazoea, Kasella Bantu alimchukua Nyerere kwa Abdulwahid kukamilisha kufahamiana na kukutana na watu maarufu wa pale mjini. Mbali na Dossa Aziz aliyekutana na Nyerere kwa muda mfupi katika mkutano mkuu wa TAA April, 1946, Kasella Bantu mwenyewe na Denis Phombeah, hakuna mtu mwingine katika makao makuu ya TAA aliyewahi kusikia habari za Nyerere.

Wakati huo, Abdulwahid na mdogo wake Ally, walikuwa na mawasiliano na International Union of Socialist Youth iliyokuwa Austria na mipango ya kupeleka mjumbe Umoja wa Mataifa, NewYork ilikuwa mbioni. Nyerere na baaadaye Mwapachu walirudi toka Uingereza wakiwa wameshawishika na mawazo ya Fabian Society, kikundi cha wasomi cha mrengo wa kushoto cha Labour Party ya Uingereza.

Abdulwahid, Nyerere, Ally, Dossa Aziz, Mhando, Rupia, Dunstan Omari na wengine walizoea kukutana kila Jumapili kwa ajili ya baraza ama nyumbani kwa Dossa Aziz mtaa wa Congo au nyumbani kwa Abdulwahid mtaa wa Stanley. Sehemu hizi ndizo ambazo wazalendo hawa walikuwa wakikutana kujadili mustakabali wa Tanganyika.

Midahalo ya kisiasa miongoni mwa wazalendo hawa vijana sasa ilihama toka mada za manung'uniko ya ndani ya nchi hadi masuala ya kimataifa ya mrengo wa kushoto yahusuyo serikali na maamuzi binafsi ya Waafrika wenyewe.

Ilivyoonekana Mwalimu Nyerere alimuona Abdulwahid kuwa ni mtu mwenye akili sana, asiye na choyo na mtu wa kupendeka. Kwa upande mwaingine Abdulwahid alimwona Nyerere kuwa ni mtu aliyeelimika sana na mwenye ustadi wa kupendeza wa kujadiliana.

Nyerere alipata nafasi ya kuifahamu dunia vizuri na kutiwa bidii kwa siasa za Fabian Society wakati alipokuwa mwanafunzi nchini Uingereza. Midahalo yenye maana sana ilijitokeza katika yale majadiliano ya siku za Jumapili wakati akili na ujuzi wa kisiasa wa Abdulwahid viliushinda kabisa ustadi usio na hakika wa kujadiliana wa Nyerere.

Nyerere hakuwa na uzoefu wa ujuzi wowote wa kisiasa uliostahiki kutajwa wakati huo wa kulinganisha na ule wa Abdulwahid. Chama cha African Association huko Tabora kiliposhiriki katika ule mgomo wa jumla wa mwaka 1947 Nyerere hakujihusisha na chama hiki cha wafanyakazi ingawa alikuwa katibu wa chama hicho.

Kutokana na sababu hiyo kuheshimiana kulitokea baina ya Abdulwahid na Nyerere. Kila Jumapili Nyerere alikuwa akisafiri toka Pugu hadi Dar es Salaam kuhudhuria mikutano hii isiyokuwa ya kawaida. Baada ya mikutano ama Dossa Aziz au Dunstan Omar alimrudisha Nyerere kwa gari hadi Pugu. Hivi ndivyo Nyerere alivyokuja kuingia ndani ya duru za ndani zaidi za TAA katika makao makuu na hatimaye akajapendekezwa kugombea cheo cha juu kabisa cha uongozi wa chama, April, 1953.

Uongozi wa TAA ulimpendekeza Julius Nyerere ili kukiimarisha chama kwa kuwa ni Mwafrika aliyesoma sana. Ilibakia kwa Nyerere kulikubali au kulikataa shauri hilo; kabla yake Chifu Kidaha Makwaia alishauriwa kuchukua uongozi wa TAA ili kuchukua urais lakini alilikataa shauri hilo. Ilikuwa jambo moja kujadili siasa na jambo jingine kabisa kuongoza chama cha kisiasa kinachokusudia kunyakua madaraka ya serikali ya kikoloni na mtu ilibidi ajitayarishe kwa lolote linaloweza kutokea.

Nyerere alikuwa mwalimu aliyefundishwa na Wakatoliki wa Roma na alipitia mfumo huo ambao huwafanya wale walioupitia wawe watiifu na waaminifu kwa vyote viwili kanisa na serikali.

Vile vile Nyerere alikuwa chini ya ushawishi wa Padri Richard Walsh aliyepanga nafasi yake ya masomo ya juu nchini Scotland. Kanisa na mamlaka za kikoloni zote zilikuwa adui wa siasa za kiafrika. Inasemekana kwamba Padri Walsh alikuwa na"ushawishi wa kutosha juu ya maisha na fikra" za Nyerere. Alimlea Nyerere na alimfanya ajiunge Edinburgh University. Haikuwa sababu kwamba arudi kuipinga serikali. Kanisa lilimtarajia Nyerere abakie kwenye kazi ya Ualimu katika shule yoyote ya misheni nchini Tanganyika.

Nyerere alikuwa ndio kwanza amerudi toka masomoni nchini Uingereza mwaka uliopita na alikuwa anataka kutulia aanze maisha. Wale vijana wa mjini aliowakuta wakicheza katika siasa mjini Dar es Salaam kama Abdulwahid na mdogo wake Ally, na Dossa Aziz walikuwa matajiri wakiishi ndani ya mazingira yao wenyewe.

Nyerere alijua yeye kama kamwe asingeweza kujenga msingi wa kisiasa katika mazingira ya Dar es Salaam ya miaka ya 1950 ambako siasa ilichukua tabia za Waislamu. Mwanzoni Nyerere hakutaka kulikubali shauri hilo.

Uongozi wa chama cha TAA ulielewa na kutambua thamani ya elimu ya Nyerere na uwezo wake kwa uongozi wa baadaye wa chama na nchi yenyewe. Abdulwahid pamoja na watendaji wa TAA waliamini kwamba kuwa na Mwafrika aliyeelimka sana nchini kama rais wa chama kungeimarisha uongozi wake na kutoa sura nzuri machoni pa serikali ya kikoloni.

Nyerere alipata kusema kwamba, ilikuwa dhahiri yake kufundisha kwa muda kisha aingie kwenye siasa. Hatimaye Nyerere alifanywa kuukubali ule uongozi ambao TAA ilimpa.

Shindano baina ya aliyekuwa rais, Abdulwahid na Mwalimu wa shule asiyefahamika, Julius Nyerere, lilifanyika kwenye Arnatouglo Hall tarehe 17 April, 1953. Nje ya duara la uongozi wa TAA ambao ulimpendekeza kugombea, Nyerere alikuwa mgeni kabisa kwa wote waliokuwa na haki ya kupiga kura.

Shughuli za kisiasa za Nyerere zinaanza tangu siku hii. Hapa alikuwepo Nyerere, mgeni na mtu aliyekuwa hana historia ya kuongoza mapambano ya watu dhidi ya serkali ya kikoloni. Familia ya Sykes ilikuwa imehusika na siasa za kienyeji mjini Dar es Salaam kwa takribani robo ya karne wakianzisha na kuongoza vyote viwili vyama vya African Association na Al Jamiatul Islamiyya. Abdulwahid kama mtoto wa Kleist Sykes alikuwa mmoja wa familia iliyojadili hadharani masuala ya kisiasa ya siku zile na kuyaandika wakati mwingine wakiandikiana barua na mamlaka ya kikoloni.

Uchaguzi ulikuwa wa kuinua mikono. Phombeah aliyekuwa mfawidhi wa Arnatouglo Hall alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo. Phombeah aliwaomba wote wawili Abdulwahid na Nyerere kutoka nje ya ukumbi ili uchaguzi uanze. Wiki nzima kabla ya uchaguzi Phombeah alikuwa akizunguuka huku na kule akimfanyia kampeni Nyerere. Lakini hakukuwa na haja ya kufanya hivyo, duara la ndani kabisa la TAA la Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz na Rupia lilikuwa tayari limekwishaamua kumfanya Nyerere awe rais wa chama.

Uchaguzi ilikuwa kutimiza utaratibu tu. Baada ya Abdulwahid na Nyerere kutoka nje upigaji kura ulianza Abdulwahid "alishindwa" uchaguzi - kushindwa kwa mara ya kwanza katika maisha yake yote ya kisiasa. Nyerere alishinda uchaguzi huo dhidi ya Abdulwahid aliyekuwa rais wakati huo kwa kura chache sana. Huu ulikuwa ndio mwanzo na mwisho kwa ushawishi wa familia ya Sykes katika chama cha TAA na mwanzo wa shughuli za kisiasa za Nyerere. Tangu siku ile historia ya kisiasa ya Tanganyika kamwe haikuwa ile ile tena.

Inastaajabisha kitu kama hiki cha masafa ya maisha ya Nyerere hakijaandikwa au kupewa umuhimu na waandishi wa vitabu vya historia ya Tanganyika.

Katika kazi yake yote ya kisiasa Nyerere katu hajapambana na mpinzani mgumu kuliko Abdulwahid. Shindano hili baina ya Abdulwahid na Nyerere limekuwa hekaya. Baadhi ya taarifa zinasema kuwa Abdulwahid alishinda uchaguzi ule, wengine wanasema Nyerere alishinda kwa kura moja; taarifa nyingine inasema kwamba wanachama wa TAA ilibidi wapige kura mara tatu ili kupata mshindi kwa kuwa zilikuwa zikifungana. Dossa Aziz anatoa taarifa kwambaAbdulwahid hakushindwa katika uchaguzi ule na anaendelea kusema kwamba:

"Hakukuwa na namna yoyote Nyerere angeweza kumshinda Abdulwahid katika Dar es Salaam ya miaka ya 1950. Abdulwahid hakushindwa katika uchaguzi ule. Sisi sote tulitaka iwe vile. Uongozi wa TAA tulimtaka Nyerere ."

Hayati Nyerere mwenyewe hakupata kamwe kuzungumza kuhusu uchaguzi huu au namna alivyokuja kukiongoza chama mjini Dar es Salaam. Kiasi cha karibu sana alichofika kumfikiria Abdulwahid kilikuwa katika ile hotuba ya kuwaaga Wazee Dar es Salaam, hata hivyo hakuweza kueleza cheo alichokuwa akishika Abdulwahid wakati yeye Nyerere alipojiunga na chama cha TAA katika mwaka 1952.

Ili kuweka mashaka yaliyowakabili Abdulwahid, Nyerere na uongozi wa TAA, hususani ile duara la ndani zaidi, mtu lazima atambue kwamba Waislamu ndio waliokuwa wengi mjini Dar es Salaam na walikuwa wamedhibiti siasa za mtaani. Waislamu wachache sana walikuwa na imani na wale Wakristo walioelimishwa na Wamishonari. Wakristo walionekana kuwa wako karibu na serikali ya kikoloni kupita kiasi kuweza kushika nafasi za uongozi katika harakati za kugombea uhuru. Na watu waliutumia uchaguzi ule kuonesha pingamizi lao kwa Nyerere.

Nyerere alionekana na baadhi ya wanachama kama si mwenzao na hawakumuunga chamani. Nyerere alikuwa mgeni pale mjini, alikuwa hana msingi wake mwenyewe wa kisiasa na kwa muda mrefu katika wiki alikuwa Pugu, nje kidogo ya Dar es Salaam, akifundisha.

Abdulwahid alikuwa mwenye kuonekana mara kwa mara, kama rais wa TAA aliifanya ofisi yake ipendeze. Alizoea kuwakaribisha watendaji wa TAA nyumbani kwake kwa chakula cha mchana na usiku na hili liliongeza umaarufu wake. Wakati huo wengi walidhani Nyerere asingefaa katika nafasi ile ya Abdulwahid.

Marehemu Tewa Said alipata kueleza kwamba siku ile kabla ya uchaguzi pale Arnatouglo Hall, Abdulwahid alikwenda nyumbani kwake jioni. Wakati huo Tewa akikaa mtaa wa Pemba si mbali sana toka nyumbani kwa Abdulwahid. Abdulwahid alimwambia Tewa haya kuhusu mabadiliko ya uongozi ambayo waliamua yafanyike kwenye chama cha TAA:

"Tewa, kesho tunakwenda kumpa huyu mtu, Nyerere, mamlaka ya kuendesha nchi hii. Kuanzia hapo, mara tu tutakapomchagua kutuongoza hakuna namna ya kumnyang'anya mamlaka hayo. Hatumfahamu vizuri sana lakini natumaini kila kitu kitakwenda vizuri."

Tewa akikumbuka matukio yaliyopelekea Nyerere kuchaguliwa kama rais wa TAA anasema:

"Kitu pekee alichokuwa nacho Nyerere zaidi ya marehemu Abdulwahid kilikuwa ile digrii ya chuo kikuu. Abdulwahid kwa takribani miaka minne tangu akamate ofisi katika mwaka 1950, alikataa kuitisha mkutano wa wajumbe kwa sababu moja au nyingine, mpaka alipokutana na Nyerere. Ninaamini kama Abdulwahid angekwenda Makerere tungeunda chama cha TANU mapema zaidi, labda kabla ya mwaka 1954 na Abdulwahid angekuwa rais, hata kama angeshindana na Nyerere. Lakini nadhani Allah alitaka iwe hivyo."

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook