CCM imefuja amani - Lipumba

CHAMA Cha Mapinduzi, kimeshutumiwa kwa kufuja hali ya amani na utulivu nchini.

Prof. Ibrahim Lipumba amesema, CCM imeshindwa kutumia hali hiyo ya amani kusimamia vizuri mipango ya maendeleo.

Amesema, kwa kufuja hali hiyo Tanzania hivi sasa imekuwa nchi ya 5 kwa umaskini ikiwa juu ya nchi zile ambazo zina vita vya ndani ambazo ni Eritrea, Ethiopia, Siera Leone na Liberia.

Prof. Lipumba ameyasema hayo, alipokuwa akiwahutubia wananchi mjini Muheza hivi karibuni.

Prof. Lipumba aliye Mwenyekiti wa CUF amesema, iwapo wananchi wanataka kuondokana na matatizo, wahakikishe wanatumia kura yao vizuri.

Amesema, hali ya hewa ya Muheza na Tanga kwa ujumla ndio iliyowapa tamaa Wajerumani 1848 ya kutawala ardhi ya Tanganyika.

Prof. Lipumba alisema kwa hali hiyo ya hewa na ardhi nzuri yenye rutuba ndiyo iliyowapelekea wakoloni hao kuanzisha mashamba makubwa ya katani katika mkoa huo, mashamba hayo ya mkonge alisema mtaalamu huyo wa uchumi ndiyo yalikuwa kichocheo cha kujengwa kwa Bandari ya Tanga na kuanzishwa viwanda kadhaa kikiwemo cha mbolea ambapo maelfu ya wananchi kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania walimiminika Tanga kutafuta ajira.

Lakini alisema Profesa Lipumba pamoja na Mwenyezi Mungu kuwajaalia watu wa Muheza neema hizo, hali zao za maisha zimekuwa taabani kutokana na kuanguka kwa zao la katani mwaka hadi mwaka.

Akitoa takwimu kukazia nukta hiyo alisema, mwaka 1964 Tanzania ilizalisha tani 240,000 za katani kati ya hizo tani 140,000 zikiwa zimezalishwa na mkoa wa Tanga pekee. Lakini mwaka jana (1999) nchi nzima ilizalisha tani 24,000 tu ikiwa ni asilimia kumi tu ya misimu ya mwaka 1984.

Aliwaambia wananchi hao wa Muheza kuwa kuporomoka huko kwa uzalishaji wa bidhaa za kilimo licha ya uwepo hali nzuri ya hewa ni matokeo ya sera mbovu za chama tawala cha CCM ambapo kimekuwepo madarakani kwa miongo minne sasa.

Awali akiongea na wananchi hao, mgombea mwenza wa Urais Mhe. Nasor Khamis aliwataka wananchi hao kuondokana na woga dhidi ya vyombo vya dola ambavyo alidai hivi sasa vimejitokeza waziwazi kuhakikisha CCM inarudi madarakani.

Aidha, Mhe. Nasor aliwataka polisi kuelewa kuwa wao ni waajiriwa wa serikali na sio CCM, hivyo wanapaswa kutenda kazi zao kwa mujibu wa kanuni zinazotawala jeshi hilo na sio kuibeba CCM.


CCM yagaragazwa topeni - Sheikh


BAADHI ya wagombea Ubunge wameelezwa kukitia doa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wagombea hao wanaotuhumiwa kutoa rushwa wamejenga taswira ya uovu wa rushwa kukubalika katika chama hicho tofauti na kauli za majukwaani.

Sheikh Ally Bassaleh amesema, kuwepo kwa taarifa za utoaji rushwa kwa baadhi ya wagombea Ubunge kupitia CCM ni aibu kwa chama hicho, kinachojitangaza usafi na kupambana na rushwa.

Sheikh Bassaleh ambaye alikuwa akizungumza na waumini Ijumaa iliyopita, aliwataka wananchi kuwaepuka watoa rushwa na wasiwape kura.

Alisema, rushwa ni adui wa haki na moja ya dhulma inayopigwa vita na vitabu vitakatifu vya Mwenyezi Mungu.

"Uislamu unapinga dhulma yoyote, rushwa ni miongoni mwa dhulma, hivyo hatuna budi kuipinga kwa kuwakatalia watoa rushwa kupata madaraka", alisema Sheikh.

Aliongeza kuwa, ikiwa watu wa namna hiyo watachaguliwa kuna hatari ya kupata viongozi watakaoendelea kuleta dhiki kwa wananchi kwa vile hawatakuwa na uadilifu.

"Kiongozi mwadilifu hapatikani kwa rushwa, bali uwezo wake na sifa zake, hivyo tuwachague kwa vigezo hivyo badala ya milungura, vingozi wa namna hiyo ni hatari kuliko petroli katika moto", alisema.

Aidha, aliwaasa Waislamu kusimama kidete kutetea haki zao bila kujali hali na itikadi zao za kisiasa kwani Uislamu ni mmoja tu na unaongozwa na Qur'an.


Vijana oeni - Imam

IMAM msaidizi wa Msikiti wa Kwa Mtoro, Sheikh Abdallah Mohamed amewataka vijana waumini wa dini ya Kiislamu waoe badala ya kuogopa hali ngumu na kuchangia kuwepo kwa watoto wa mitaani.

Sheikh Abdallah aliyasema hayo wiki iliyopita alipokuwa akiwahutubia waumini kabla ya swala ya Ijumaa Msikitini hapo. Amesema, imekuwa ni desturi kwa vijana kukimbia kufunga ndoa kwa maelezo, hali zao kiuchumi haziwaruhusu.

Akishangaa, Imam huyo alisema, licha ya kuhofu uwezo wa kuwatunza wake zao, vijana hao hao huwaweka vimada tena kwa gharama kubwa na kuuliza uwezo huo wa kutunza haramu huupata wapi?

"Vijana madai ya kutokuwa na uwezo ni kufuru. Iweje uweze kugharamia vimada lakini gharama za kutunza mke halali ndio udai hamna uwezo huo?" Aliulia Sheikh Abdallah.

Aliwaasa vijana na waumini wa Kiislamu kwa ujumla kuachana na kasumba za kimagharibi ambazo ndio zinazochangia kuzaa nje ya ndoa na pia kuambukizwa magonjwa ya zinaa ukiwemo ukimwi.

Sheikh Abdallah alikumbusha pia umuhimu wa waumini kumuogopa Mwenyezi Mungu na kumtii Mtume Muhammad kwa kujiepusha na kila jambo ovu.

Alimalizia kwa kuwakumbusha waumini kuwaamrisha wake na watoto zao kujisitiri miili yao ili kupunguza vishawishi vya maovu na kuwaambia maasi huanza kuzuiwa katika majumba yao na ndipo kufuata kwa majirani na nchi nzima kwa ujumla.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook