Lishe

Aina mbali mbali za uji

KAMA tulivyoona makala iliyopita mjadala kuhusu chai na uji, kila msomaji ameona kuwa uji ndio hasa unaopaswa kupewa nafasi.

Kama hivyo ndivyo ni ninayo furaha kukuletea aina kadhaa za uji ambazo unaweza kujichagulia.

Kabla ya kuzifahamu aina za uji ni vyema tukafahamu kwa utangulizi mahitaji makuu ya uji.

Unga ni hitajio kuu la uji. Lakini kulingana na aina za uji zilizopo, mahitajio mengine ni kama , mchele, ngano, mtama au uwele, ulezi na mahindi.

Vyote vinaweza kutumika bila ya kusagwa, yaani katika mtindo wa chenge chenga au kwa kusagwa(unga).

Watu wengi hupenda kukoboa nafaka kabla ya kusaga. Nafaka zinapokobolewa huondoka kiine na ngozi yake. Vyote hivi viwili huwa na virutubisho muhimu sana kwa afya. Kwa kule kutokujua kwetu ndio maana tunavitoa na kuvitupilia mbali. Mbaya zaidi wengine hukoboa kisha kuloweka siku moja au mbili. Kwa kweli ni hasara kubwa tunayojipa bila kujua tusifanye hivyo kamwe.

Vyakula tulavyo kila siku kama ugali na wali vimekobolewa sana au kulowekwa, basi ni angalau tufidie kutoka kwenye uji usiokobolewa nafaka zake.

Uji wa nafaka zisizokobolewa huwa na ladha tofauti kabisa na ule uliokobolewa. Ni vizuri kuwa na unga tofauti kati ya wa uji na wa ugali.

Baada ya hayo kwa ufupi, tuziangalie aina za uji.

Uji wa Dona

"Donna" ni neno litumikalo kwa unga wa mahindi usiokobolewa. Mahindi makavu huoshwa na kukaushwa bila ya kuloweka na kisha kusagwa. Unga huu waweza kusagwa na karanga mbichi au za kukaanga. Unga huu huwa na rangi kulingana na aina ya mahindi., mengine meupe na mengine mekundu au njano. Hii itategemea na upatikanaji au matakwa binafsi. Uji huu hutumika sana kwa nyakati za njaa kali kwani una nguvu na ladha nzuri hata bila kuwekwa kitu kingine. Waweza kutumika siku zingine zozote bila kujali ni njaa au shibe.

Unaweza ukatengeneza mzito sana au kiasi au mwepesi kiasi. Iwapo una ng'ombe au fedha za kununua maziwa, changanya na maziwa na sukari kidogo sana. Wenyewe ulivyo unavirutubisho vingi na mafuta ndani yake, si lazima kutia mafuta kama utapenda weka kidogo kidogo sana.

Jinsi ya kuupika

Chemsha maji kwenye sufuria ya kiasi kulingana na idadi ya vikombe unavyotaka mpaka yawe moto sana.

Wakati maji yanachemka, chukua unga nusu kikombe kama umeweka maji vikombe vitatu. Koroga bakuli hadi umalize vifundo fundo.

Maji yakisha chemka, mwagia unga uliokoroga kwenye maji huku ukiwa unakoroga ili kuzuia unga kufungana. Ukisha jichanganya vizuri na kuanza kuchemka, acha uchemke kwa takribani nusu saa. Kumbuka donna ina mafuta na pumba ambavyo vinahitaji kuiva vizuri. Iwapo uji ni mwepesi sana, lazima utajaa sufuria na kumwagikia kwa kulowanisha mapovu. Ili kuzuia hii koroga unga mwingine kidogo na umwagie ndani yake koroga na acha uchemke.

Iwapo donna ina karanga mbichi, uji wake uachwe uchemke zaidi. Pia waweza kuweka karanga za kusagwa hali ya kuwa uji unachemka. Kwa wenye "blender" ni rahisi kusaga siku hiyo hiyo, kwa sisi wenye majiwe na vinu, ni vizuri kuandaa karanga nyingi kwa matumizi ya kila siku.

Maziwa ya mgando(mtindi) huwekwa uji unapokuwa umeshaiva na kuipuliwa tayari kwa kunywewa. Weka mtindi wakati uji ungali moto weka sukari kidogo au chumvi na kunywa taratibu.

Kama hutumii karanga au maziwa mtindi, waweza kutumia siagi kama blue band au Tan Bond(magarine). Siagi iweke wakati uji umeshaiva na tayari kwa kunywewa ni vizuri kila mtu akaweka kwa kiasi chake kama itatoka.

Maziwa "fresh" ni vizuri yakawekwa kwenye uji ulio mzito kidogo. Hakikisha maziwa yawe yamechemshwa kwanza ili kuuwa wadudu. Viungo vingine kama tangawizi na pili pili manga ni uamuzi wako binafsi. Lakini hufanya uji uwe unavutia zaidi.

Pamoja na mambo yote hayo, uji wa donna uliochemka sawa sawa ni mtama sana kama ulivyo bila chochote.

Kwa ufupi ni kama hivi:

Unga + maji + chumvi

Unga + maji + sukari kidogo

Unga + maji + maziwa + sukari kidogo

Unga + maji + karanga + sukari kidogo au chumvi

Unga + maji + mtindi + sukari kidogo

Unga + maji + blue band + sukari kidogo

Unga + tui + chumvi kidogo

Unga + tui + sukari kidogo
 

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook