Mbunge wa CCM aishambulia CUF

MBUNGE wa CCM jimbo la Handeni mashariki, mheshimiwa Dk. Abdallah Kigoda amedaiwa kusema sera ya CUF ya jino la jino inahatarisha amani na utulivu nchini.

Dk. Kigoda ambaye pia ni waziri wa Nishati amedai kuwa CUF imeamua kuwa na sera hiyo kwa kuwa imefilisika kisiasa.

Aliyasema hayo alipokuwa akizindua Tawi la wakereketwa wa CCM Kwamngumi mjini Handeni hivi karibuni.

Aidha waziri huyo wa Nishati alimponda mgombea wa kiti cha Urais wa chama cha CUF Profesa Ibrahim Lipumba kuwa chama chake hakina sera ila ni udanganyifu.

Alidai Profesa Lipumba ni mwenzake na kwamba wamesoma wote lakini anamsikitia kwa kule kujiunga na chama ambacho amedai hakina uelekeo.

Alisema chama cha CUF ni cha Wapemba ndio maana huku bara hakipo wala hakina mwakilishi wake kwenye majimbo yote.

Katika hotuba yake hiyo Dk. Kigoda pia ameyashutumu matawi ya CUF ya Kosovo na Chechnya kwa madai kuwa yanatishia umwagaji wa damu nchini.

Hata hivyo hakueleza ni kwa vipi matawi hayo ya chama cha CUF yanaweza kuharibu amani ya nchi.

Katika uzinduzi huo bendi ya muziki ya SOT Jazz Band ilitumbuiza wananchi kwa wimbo maarufu wa Marehemu Salum Abdallah uitwao "wanawake wa Tanzania".

Wakati huo huo, katika kibanda kimoja cha biashara katika soko la wazi mjini Handeni kumetundikwa bango kubwa lenye maandishi yanayosomeka kuwa, "hatutaki mikopo, tunataka haki zetu".

Bango hilo ambalo limewekwa mkabala na mlango wa kuingilia sokoni hapo imedaiwa ni ujumbe kwa wanasiasa wanaowaendea wafanyibiashara hao kuwataka waorodheshe majina yao na kiasi cha mikopo wanachohitaji ili wakopeshwe.

Imedaiwa kuwa kumekuwa na upitishaji wa karatasi inayomtaka kila mfanyibiashara wa soko hilo aorodheshe jina ili apewe mkopo.

Pamoja na karatasi hiyo ya mikopo, zawadi mbali mbali zikiwemo khanga imedaiwa hutolewa kwa akina mama vijijini.

Hata hivyo, taarifa zaidi zinafahamisha kuwa zoezi hilo huenda likasababisha migogoro ya kifamilia kwa kuwa baadhi ya kinababa wamekuwa wakihoji kwanini wake zao wapewe zawadi.


Kufuatia ziara ya Rais Mkapa:
Wakereketwa wa CCM wafadhaika Mwanza


BAADHI ya wakereketwa wa CCM wamedai ziara ya Rais Mkapa imewavunja nguvu mbele ya wapinzani.

Wamesema, walitaraji mapokezi, shamra shamra na hotuba ambapo zingepiku zile za chama cha CUF.

"Japo hakuwa amekuja kichama ametukata makali. Hatuna kauli tena mbele ya hawa ngangari", amesema Bw. Joseph wa mjini Mwanza.

"Hatukuwa na raha muda wote viongozi wa CUF walipokuwa hapa. Tuliona kana kwamba mji wote umekuwa wa wapinzani", amesema Bw. Daudi Mbura wa Mabatini.

Bwana Daud amesema, alifarijika kuwa Rais Mkapa anakuja. Kwamba angezibomoa hoja zote za viongozi wa CUF ambazo amedai zimewachanganya watu wengi.

"Tulitaka tulipize kisasi. Tuwapiku mapokezi yao na shamra shamra zao. Sasa hatuna uso mbele ya wapinzani", amedai.

Kauli hizi za wakereketwa wa CCM zimekuja kufuatia ziara ya Rais Benjamin Mkapa mjini Mwanza Jumatatu wiki hi haikwenda kama ilivyotarajiwa.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana mjini hapa, serikali mkoani humo ilipanga mapokezi makubwa ya Rais kabla ya kuhutubia wanamichezo wa UMISETA na wananchi kwa ujumla.

Gazeti la Msanii Afrika toleo la Jumamosi namba 436, likikariri taarifa ya mkuu wa mkoa huo, liliandika kuwa Rais ilikuwa ajibu hotuba iliyotolewa na Mwenyekiti wa chama cha CUF Prof. Ibrahim Lipumba katika viwanja vya Furahisha mjini hapa.

Gazeti hilo limeandika kuwa katika hotuba yake Profesa Lipumba pamoja na mambo mengine aliyoyangumza aliituhumu serikali kwa matumizi mabaya ya fedha ikiwa ni pamoja na kutumia fedha nyingi kutengeneza Ikulu kila mwaka.

Siku moja kabla ya ziara ya Rais, serikali mkoani humo iliwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kumlaki Rais kwa kujipanga kando kando ya barabara ambazo msafara wake ungepita.

Taarifa hiyo pia iliwataka wananchi wafike kwa wingi uwanja wa Kirumba ambako pamoja na kufungua michezo ya UMISETA, Rais angehutubia wananchi.

Hata hivyo, pamoja na matangazo hayo, wananchi mkoani hapa hawakujitokeza kwa wingi kumpokea Rais wala kwenda kumsikiliza katika uwanja wa Kirumba hali iliyosababisha ahutubie wanafunzi watupu wanaoshiriki michezo hiyo.

Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia wapenzi wa vyama hivyo viwili wakitambiana.

"Mlisema mnatupiku kiko wapi", wamesikika vijana wa CUF wakiwaambia wakereketwa wa CCM eneo la Kirumba.

Katika hotuba yake, Rais aliwataka wanafunzi watumie michezo hiyo kujenga umoja wa kitaifa ili kuenzi na kudumisha amani na mshikamano wa Watanzania.

Aidha, Rais aliwataka wanafunzi hao wajihadhari na ugonjwa hatari wa Ukimwi unaotishia maisha ya Watanzania wengi hasa vijana.

Katika ufunguzi huo, Rais pia alikuwa mgeni rasmi katika pambano la mpira wa miguu la mashindano hayo lililofanyika siku hiyo kati ya kanda ya kaskazini na kanda ya kati ambalo mshindi ilikuwa kanda ya kati kwa mabao 3-2.

Rais akiwa amevalia suti ya michezo siku hiyo aliondoka uwanjani hapo ilipokamilika nusu ya kwanza ya mchezo huo.


Wavamiwa msikitini na kupigwa

WAUMINI wa Masjid Majumui Tegeta magengeni wameeleza kuwa vijana waliokamatwa na polisi hawakufanya fujo Msikitini.

Wakiongea na AN-NUUR kwa nyakati tofauti jana adhuhuri mara baada ya swala msikitini hapo wamesema, kilichotokea ni vijana hao kuvamiwa ndani ya Msikiti na kupigwa.

"Wao walikuwa ndani ya Msikiti na wao ndio waliopigwa na vijana wa kihuni wasiopungua 40 walioshirikiana na wazee wa Msikiti", amesema muumini mmoja.

Waumini hao ambao hawakuwa tayari majina yao kuandikwa gazetini wameeleza kuwa tatizo ni kuwa viongozi waliopo hapo hawajachaguliwa na waumini na kuwapingia wahadhiri cha kuongea watembeleapo.

"Anapokuja mhadhiri lazima ahojiwe nini atazungumza, kama ataongea yatayowahusu basi hapewi ruksa, sasa sisi waumini linatuudhi sana", alisema.

Aidha, walieleza wanapohoji (waumini) wazee hao wanaenda polisi na kutoa ripoti kuna watu wanaleta vurugu msikitini na polisi huja kuwachukua bila kujua tatizo lenyewe.

Wamesema, hakuna uharibifu wowote uliotokea Msikitini hapo kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari mapema wiki hii na hakuna aliyetishia amani.

Wakielezea sababu ya kukamatwa vijana hao, ilikuwa baada ya ibada ya Itiqafu iliyofanyika Juni 17 (Jumamosi) kuamkia Juni 18 (Jumapili), katika polisi kuingilia migogoro ya misikitini bila ya kuangalia ukweli ukoje, na kuwataka polisi kuacha tabia hiyo.

Walieleza kuwa baadhi ya wazee walikwenda kituo cha polisi na kueleza kuwa kuna vijana wanaoongea siasa msikitini.

"Walienda kuripoti polisi, polisi waliwaeleza wao hawana ruhusa ya kuingia msikitini", amesema mmoja wao.

Walisema vijana hao wakiwa ndani ya Msikiti saa nane na nusu Julai 18 lilitokea kundi la vijana wa kihuni kuwavamia msikitini wakiwa na viatu vyao wakidai wametumwa na wazee wawatoe.

"Tulizingirwa ndani ya Msikiti na vijana tusiowajua na wapi wanatoka. Waliingia na viatu na kutupiga sana na mmoja kuzirai", amesema mmoja aliyenusurika kukamatwa.

Waumini hao walieleza kuwa vyombo vya habari pia vinachangia kukashifu Uislamu na kuwazushia mambo yao kwa lengo la kuwagawanya Waislamu.

AN-NUUR ilifika msikitini hapo na hapakuwa na uvunjaji wowote wa mlango kama ilivyoripotiwa.

Mapema wiki hii baadhi ya vyombo vya habari viliripoti "Waislamu kortini kwa fujo msikitini na kupora mlango wa Msikiti".

Vijana hao walipigwa ndani ya Msikiti ni Athumani Hussein (32), Hussein Salum (20), Habibu Shiloo (29), Mselem Athuman (35) pamoja na Mohamed.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook