Waislamu kuandamana Dar kulaani Russia
 

WAISLAMU Jijini Dar es Salaam huenda wakaandamana siku chache zijazo kulaani majeshi ya Russia kuvamia Jamhuri ya Chechnya.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwepo kwa harakati za maandalizi ya maandamano hayo yanayotazamiwa kumalizikia Ubalozi wa Russia jijini.

Wiki iliyopita dua maalum ilifanyika kuwaombea wapiganaji wa Chechnya na kuilaani Russia kwa hatua zake za kinyama dhidi ya Waislamu nchini humo.

Dua hiyo iliyoandaliwa Msikiti wa Mtambani ilihudhuriwa na maelfu ya waumini wa dini ya Kiislamu jijini na mikoa ya jirani.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'an Waislamu wote duniani ni ndugu wanaotakiwa kuoneana huruma na kusaidiana kwa hali na mali.

Majeshi ya Russia hivi sasa yanaelekea kuuteka mji mkuu wa Chechnya Grozny, hata hivyo yamekuwa yakikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wapiganaji wa Kiislamu wa nchi hiyo iliyojitenga miaka mitano iliyopita baada ya kusambaratika kwa iliyokuwa Soviet Union.

Maelfu ya raia wa Chechnya wameripotiwa kuuawa na wengine kuihama nchi hiyo kufuatia mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na majeshi ya Russia.

Majeshi hayo yakitumia mizinga, mamia ya vifaru, mamia ya ndege za kivita na silaha nyingine nzito yamekuwa yakielekeza mashambulizi dhidi ya makazi ya raia.

Majengo katika miji mbalimbali ukiwemo mji mkuu Grozny yameharibiwa vibaya kwa mashambulizi ya ndege na vifaru vya Russia.

Wapiganaji wa Chechnya wameahidi kuendelea na mapambano dhidi ya wavamizi hao wa Kirusi muda mrefu ujao.

Upinzani wa wapiganaji hao umesababisha hasara kubwa kwa wavamizi ambapo hadi sasa taarifa kutoka uwanja wa mapambano zinaonesha kwa muda wa miezi miwili zaidi ya askali 2350 wa Russia wameuawa, ndege za kivita 10, helkopter 12 kudunguliwa na vifaru 85 kuharibiwa.

Aidha, taarifa zinafahamisha zaidi ya wapiganaji 45 na raia wapatao 150,000 wa Chechnya wamekwisha uawa katika mapambano hayo.

Waziri Mkuu wa Russia Bwana Putin, juzi alitangaza rasmi kuanza kwa operesheni kubwa ya kijeshi inayoshirikisha askari zaidi ya 100,000 na vifaa vizito vya kijeshi kuuteka mji wa Grozny kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Wapiganaji wa Chechnya wapatao 7000 waliojichimbia katika milima ya Grozny wamejizatiti kutoa upinzani mkali kwa wavamizi. Mchechen mmoja akikabiliana na wastani wa Warusi 14.

Katika Badri Muislamu mmoja alipambana na makafiri watatu. Katika suratul Anfal Allah amesema kuwa waumini 20 wenye kusubiri waweza kupambana na makafiri 200 (mmoja kwa kumi).

Wachechen ni mmoja kwa 14 huku wakiandamwa na kimbunga cha ndege, vifaru na helkopta.

Baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa juzi viliwaonesha wapiganaji hao wakitungua ndege moja ya kijeshi ya Kirusi huku wakitamka "Allahu Akbar".

Wakati huo huo, baadhi ya waumini jijini mwanzoni mwa wiki hii walifika ofisi za gazeti hili mtaa wa Mahiwa kuulizia uwezekano wa kufika Chechnya.

Mmoja wa watu hao ambaye alijifahamisha kuwa ni askari mstaafu wa jeshi la wananchi wa Tanzania, alimueleza mwandishi kuwa yeye hakuwa na cha kuwasaidia Wachechen ila ujuzi wa kijeshi alionao.

Askari huyo mstaafu ambaye alidai alishiriki vita mbalimbali vya ukombozi Afrika aliomba aelekezwe Ubalozi wa Chechnya hapa nchini, hata hivyo aliambiwa kuwa nchi hiyo haina ubalozi Tanzania. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook