KUTOKA MAGAZETI YA ZAMANI
 
 
Si 'Muungano' bali...
 
AN-NUUR Jamaduthan 1414 A.H, Desemba 1993
 

MJADALA unaendelea nchini kote juu ya kuundwa kwa serikali ya Tanganyika na muundo wa Muungano wa Zanzibar na Tanganyika. Inavyoelekea yapo matatizo, dosari na sababu za msingi zilizopelekea wananchi kuhoji muundo wa sasa wa Muungano na kuleta hoja ya kuundwa kwa serikali ya Tanganyika ni yenye kuundwa kama si leo kesho.

Lakini wapo pia wanaopinga kabisa kuundwa kwa serikali ya Tanganyika.

Aliyejitokeza kwa nguvu na kwa ukali hadharani kupinga hoja hiyo ni Mwalimu Julius Nyerere, katika kupinga hoja hiyo Mwalimu anatoa hoja zifuatazo:

Hoja ya kuundwa kwa serikali ya Tanganyika imeletwa kwa kuwachoka Wazanzibari na Waislamu. Ufupi wa maneno Mwalimu Nyerere anadai hoja ya kuundwa Serikali ya Tanganyika imetokana na chuki za kidini - Wakristo kuwachukia Waislamu.

Hoja haipo katika sera za CCM na taratibu zimekosewa.

Kuundwa kwa serikali ya Tanganyika kutavunja Muungano na kutavunja Tanganyika pia.

Ukizingatia sifa nyingi ambazo Nyerere alijilimbikizia wakati wa utawala wake na sasa si vigumu kuelewa kwa nini anapinga kuundwa kwa serikali ya Tanganyika. Mambo yake yote aliyoyaanzisha kwa vishindo huku akisifiwa kuwa zidumu fikra zake, yamekuwa yakiporomoka moja baada ya jingine huku mwenyewe akiona. Lililosalia ni Muungano; nao ukiporomoka haitaleta picha nzuri katika historia yake katika siasa.

Lakini lililo gumu kueleweka ni hatua ya Mwalimu Nyerere kutumia Turufu ya udini kuwagawa Wabunge; wana-CCM na Wa-Tanzania kwa ujumla katika suala hili. Kauli hiyo ingesemwa na Muislamu ingepewa mtizamo tofauti na labda isingeeleweka hasa miongoni mwa Waislamu. Lakini kusemwa na Mwalimu Nyerere kunaleta mkanganyiko zaidi. Kwanini; (udini ulikuwa umejengeka). Hali hiyo ilipelekea Masheikh kumlalamikia lakini akawanyamazisha kwa kuwashutumu kuwa wanachanganya dini na siasa. Miongoni mwa Masheikh hao wapo waliofukuzwa nchini; waliowekwa kizuizini, waliofukuzwa katika chama na kadhalika.

Sheikh Hassan bin Amir katika waraka wake kwa Waislamu mwaka 1963 aliutaja udini uliokuwa unajengwa Tanzania kwa kutoa mifano ifuatayo:

Kuingizwa nchini Tanganyika mara tu baada ya uhuru vimedali vidogo vidogo vyenye picha ya bendera ya Tanganyika usoni na katikati ya bendera hiyo amesimama Mama Maria na mtoto mchanga na nyuma yake maandiko 'MARIA MTAKATIFU ULINDE UHURU WA TANGANYIKA'.

Gazeti la KIONGOZI la tarehe 1/8/1963 lilimuonyesha Bwana George Kahama akipewa cheo cha dini na Pope kwa kuwakilisha serikali ya Tanganyika katika mkutano wa Makanisa ya Roma.

Mwaka huo huo wa 1963, mnamo tarehe 24 mwezi wa nane, Baraza Kuu la Makanisa ya Kilutheri Tanganyika lilitoa matangazo kuwa Uhuru wa Tanganyika ulikuwa 'Chini ya Msalaba'.

Tarehe 17/5/1963 Makanisa yalifanyia mkutano wao ndani ya Bunge.

Alipokufa Pope Yohana wa 23 bendera ya taifa ilipepea nusu mlingoti nchi nzima!

Kabla ya kifo chake Pope Yohana wa 23 alimletea Mheshimiwa Nyerere barua ya pongezi kwa kuupanua Ukristo- barua ambayo ilitiwa saini na Pope mwenyewe. Barua hiyo imetangazwa kwenye gazeti la Tanganyika Standard.

Gazeti la Reporter la Kenya la tarehe 20/6/1963 lilitangaza katika ukurasa wake wa mbele: "KUIBADILI AFRIKA YA MASHARIKI KUWA KATIKA DINI YA ROMANI CATHOLIC". Ndani ya gazeti hilo ukurasa wa 18 liliwataja waliopewa dhamana ya kufanikisha jambo hilo kuwa ni: Uganda - Kiwanuka, Kenya - Mboya na Tanganyika Mheshimiwa Nyerere.


Mchango wa Chuo Kikuu
 
Gazeti la Mwafrika - Jumapili Machi 16, 1958
 

MCHANGO wa Chuo Kikuu unaendelea vizuri sana na umefikia idadi ya shilingi 7,971.00. Msaidizi wa Waziri wa Ardhi Bw. P.K Makwaia amesaidia shilingi 500. Katika mchango wa kwanza Mhe. Bwana Julius K. Nyerere ametoa sh. 200. Sh. 841 zilichangwa na wajumbe wa Tabora. Wengine waliochanga ni:

Mhe. Salum Athumani Dar es Salaam Sh. 500
Ibrahim Bofu Dar es Salaam Sh. 150
Schnaider Plantan Dar es Salaam Sh. 100
Abdallah Saidi Dar es Salaam Sh. 100
Kondo Salum Dar es Salaam Sh. 100
Abbas Sykes Dar es Salaam Sh. 100
Bibi Panya Majaliwa Dar es Salaam Sh. 500
Mchango bado unaendelea.

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook