Changieni maendeleo ya Uislamu- Sheikh Mbukuzi
 

IMAM Masjidi Mujahiduun Sheikh Juma Mbukuzi ambaye pia ni Amir wa Waislamu mkoa wa Dar es Salaam amewataka Waislamu wachangie maendeleo ya Uislamu kwa hali na mali kwa kutaraji radhi za Allah (s.w.).

Sheikh Mbukuzi amesema Waislamu wanatakiwa watumie fursa waliyonayo/wanayoipata katika kuchangia na kuleta maendeleo katika Uislamu.

"Mtu yeyote anayekwaza maendeleo ya Uislamu huyo ni adui mkubwa wa Uislamu", alisema.

Aidha, Sheikh Mbukuzi amesema Misikiti itumike kikamilifu katika kuuendeleza Uislamu.

"Fanyeni fikra... Misikiti sio mahali pa kuja kusali tu na kuondoka. Tumieni Misikiti kujiendeleza kiuchumi, kielimu, afya na kadhalika mtapata hadhi hapa duniani na mbele ya Allah (s.w.) mtakuwa ni wenye kuridhiwa", amesisitiza Sheikh Mbukuzi.

Aidha Sheikh Mbukuzi ametoa shukrani kwa waumini wa Masjidi Mujahiduun kutokana na michango yao inayotarajiwa kufanikisha ujenzi wa shule ya msingi Msikitini hapo, hivi sasa Msikiti huo una shule ya awali (chekechea).


Malalamiko yafikishwa kwa Mkuu wa Wilaya
 

UMOJA wa Akinamama wa Kiislamu mjini hapa umempelekea malalamiko mkuu wa wilaya juu ya hatua ambazo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro inayochukua kutaka kuwanyang'anya kiwanja chao kilichopo Kitalu U.

Kwa mujibu wa barua ya umoja huo yenye kumb. Na. TRB/1/22 ya Oktoba 25, 1999 ambayo gazeti hili inayo nakala yake inasema kwamba wao kama wamiliki halali wa kiwanja hicho, kwa mujibu wa nyaraka zilizoorodheshwa kwenye barua yao ya Septemba 27, 1999 aliyopelekewa Mkurugenzi wa Manispaa wamedai bado ameshindwa kulitolea uamuzi suala hili.

Ofisi ya Mkurugenzi ilijibu barua ya kina mama hao Septemba 29, 1999 ikiwa na Kumb. Na. R10/MMC/1/140 ambapo sehemu ya barua hiyo inasema "Utaratibu wa kubadilisha matumizi kutoka eneo la wazi kuja kwenye matumizi ya ujenzi haukukamilishwa".

Wakijibu hoja hiyo katika barua yao iliyosainiwa na Katibu wake Mwanaidi Nassibu ilipinga suala hilo na kudai kwamba kama taratibu hizo hazikukamilika wasingepewa "Offer" kibali cha ujenzi pamoja na kupitishwa ramani yake.

Kuhusu hoja iliyotolewa na Manispaa kuwa kiwanja kilitolewa bila kupimwa, barua hiyo imesema jambo hilo siyo kweli kwa sababu kiwanja kinajulikana ukubwa wake na mipaka yake (SQM 4050 Kitalu U).

Barua hiyo ya malalamiko kwa Mkuu wa Wilaya imeendelea kueleza kuhusu suala la kibali cha ujenzi kudaiwa na Manispaa kuwa kilipitwa na wakati kwa misingi kuwa hawakujenga kwa kipindi cha miezi sita. Barua hiyo ilisema:

"Suala hilo siyo kweli kwani tangu Julai 14, 1992 tayari ujenzi ulianza mpaka kufikia hatua ya msingi, kwa hatua tuliyofikia ya ujenzi ndiyo maana hatukupewa maelezo yoyote kutoka Manispaa juu ya kuisha muda wa kibali cha ujenzi tangu kitolewe".

Kuhusu mgogoro unaotajwa kusababishwa na CCM kata ya Mbuyuni kugawa sehemu ya Kiwanja kwa ajili ya vibanda vya biashara, umoja huo umemwambatanishia Mkuu wa wilaya moja ya barua zilizotolewa na CCM kugawa eneo hilo.

Nakala ya barua hiyo ya malalamiko imepelekwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa, Mhandisi wa Manispaa, Mwanasheria wa Jabal Hira Islamic Centre pamoja an Afisa Mtendaji kata ya Mbuyuni.

Katika toleo lake la mwezi Rajab 1420, Ijumaa Oktoba 15-21, 1999 gazeti hili liliandika habari ya CCM Wilaya ya Morogoro kudaiwa kupora kiwanja Kitalu U mtaa wa Sabasaba mjini hapa ambacho ni mali ya umoja wa wanawake wa Kiislamu Morogoro.

Taarifa hizo zilidai kuwa baada ya CCM kupora kiwanja hicho imekuwa ikiviuza vipande vipande eneo hilo kwa shilingi 50,000 ambapo kati ya hizo shilingi 30,000 kwa ajili ya kuimarisha chama hicho na shilingi 20,000 kwa ajili ya ufunguzi wa Tawi. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook