KATIKA hali isiyo ya kawaida Masjid Shadhily juzi katika swala ya Asri kuliswaliwa jamaa tatu kwa wakati mmoja huku waumini wengine wakiukimbia Msikiti kuwahi kuswali katika Misikiti ya jirani.
Waumini mbalimbali walioswali katika Msikiti huo wameeleza kuwa kundi moja likiwa na Imam wake liliswali katika korido nje huku waliokuwa ndani wakimfuata Imam wa kawaida.
Imeelezwa pia kuwa sehemu ya walioswali juu waligawanyika makundi mawili. Kundi moja lilimfuata Imamu wa kawaida wakati kundi lingine liliunda jamaa yake.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na waumini mbalimbali baada ya swala, tofauti na mgawanyiko huo ulitokea baada ya waumini kutokuafikiana juu ya kumuombea Dua Mwalimu Nyerere Msikitini hapo.
Waumini walio wengi hawakukubaliana na tangazo la Imam wa Msikiti huo Sheikh Nurdeen Hussein Shadhly la kufanyika kwa Dua hiyo.
Japo hakuna ubishi juu ya kuwatakia Shifaa wagonjwa wa aina yoyote kwa ujumla, lakini upo utata katika suala la kuandaa dua maalum ndani ya Msikitini alisema Bw. Hussein aliyekuwa miongoni mwa waliomhalifu Imam wa kawaida.
"Na maadhali hili ni suala la kidini ni lazima sheria na fat'wa za kidini ziangaliwe ili hata hiyo Dua yenyewe iwe na manufaa", alisisitiza.
Kutokana na utata huo wa Fat'wa ya kidini juu ya Dua; mamia ya Waislamu walioswali Msikitini hapo walitawanyika na kuwaacha wachache wakishiriki dua. Lakini hata waliosalia wengi wao walibaki kuwa watazamaji wakiwaachia wageni waliokaa mistari ya waheshimiwa wakiendelea na zoezi.
Mgeni rasmi katika dua hiyo alikuwa Makamu wa Rais Mhe. Dk. Omar Ali Juma. Wengine waliohudhuria dua hiyo walikuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni Prof. Juma Athumani Kapuya na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Yussuf Rajab Makamba.
Serikali imekuwa ikitoa wito kwa wananchi wamwombee dua na kumtakia shufaa Mwalimu Nyerere.
Mwalimu ambaye yuko Uingereza akiendelea na matibabu, anasumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya damu.
Habari za hivi karibuni zimeeleza
kuwa anaendelea kupata nafuu japokuwa imeripotiwa kuwa amegundulika kuwa
na ugonjwa wa homa ya manjano (Jaundice).
--
|
|