JUMAMOSI ya Septemba 25 mwaka huu wafuasi wa CCM wa eneo la Magomeni Mzumbe Jijini walivamia ukumbi wa Madrasat Al Azhar Sharif Na. 49 kuanzia saa nne asubuhi na kufanya kikao katika madrasa hiyo.
Wafuasi hao walimuendea Mwalimu mmoja na kumueleza kwamba watakuwa hapo kuanzia saa nne hadi saa tano asubuhi hiyo.
Chanzo chetu kimedokeza kuwa kikao hicho kilikuwa na lengo la kumchagua mgombea wa Uenyekiti wa serikali za Mitaa.
Pamoja na kufahamu fika kuwa madrasa hiyo kuwa inafundisha asubuhi na mchana kuanzia saa nane hadi saa kumbi na mbili, kiongozi mmoja katika kikao hicho alisikika akisema endapo kikao hakitakwisha kwa muda huo wa masaa mawili basi wangeendelea tena saa tisa alasiri.
Kama ilivyo utaratibu wa madrasa hiyo ilipofika saa nane mchana walifika na kuingia kuanza masomo yao ya siku hiyo kama ilivyo katika ratiba yao. Ilipofika saa tisa wana CCM walivamia Madrasa na kuwataka walimu na wanafunzi kutoka nje.
Kikao hicho kiliendelea hadi saa kumi na mbili jioni na kwa wakati wote wanafunzi walikuwa wakizagaa ovyo nje na walimu wao wakiwa hawana la kufanya.
Madrasata Al Azhar Sharif
iliyopo Magomeni Mzumbe Na. 49 ilianzishwa mwaka 1994 ikiwa na wanafunzi
takriban 30 na hivi sasa ina wanafunzi zaidi ya 120 na ina walimu saba
kwa hivi sasa.
WAISLAMU wametakiwa wazielewe haki zao za Kiislamu na wametakiwa kumfanyia ibada Allah (s.w.) bila ya kumshirikisha na chochote kile.
Aidha, wametakiwa kuwa tayari kuhukumiwa na sheria za Allah (s.w.) ili waweze kupata salama duniani na akhera.
Akiwahutubia mamia ya Waislamu kabla ya sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Nunge mjini Dodoma hivi karibuni, Ustadh AbdulRahim Mussa Kondo alisema kuwa Allah (s.w.) amewaahidi kuwaingiza peponi wale wote watakaomtakasia ibada yake pasina kumshirikisha.
Ustadh Musa alisema kuwa iwapo Waislamu watachagua kusali; kufunga; Hijja na ibada nyingine. kisha wasiwe tayari kuhukumiwa na Qur'an watakuwa wamemshirikisha Allah (s.w.) katika dhati yake, hivyo itakuwa muhali kusalimika na adhabu zake, kwani yeye Allah (s.w.) amewaita watu aina hiyo ni makafiri, madhalimu na mafasiki, hivyo watu wa sifa hizo hawawezi kusalimika.
Ustadh Mussa alisema kwa masikitiko kuwa huo ndio Uislamu uliopo na tulionao kwa Waislamu wa leo, Uislamu wa nusu nusu, ambao Allah (s.w.) ameukemea na kuahidi adhabu kubwa (Qur'an 2:85-86).
Aidha, aliwataka Waislamu waepukane na mtazamo potofu wa kujiamini kuwa Allah (s.w.) anaweza akatoa upendeleo kwa umma huu hali ya kuwa Qur'an inafuatwa nusu nusu, hilo halitowezekana kamwe mbele ya Allah (s.w.).
Wakati huo huo Waislamu wametakiwa wazitumie vizuri neema za ujana, uhai, utajiri na elimu, kwani neema hizo zikitumiwa vibaya, Waislamu wasije wakajuta; siku ambayo majuto yao hayatawasaidia kitu mbele ya Allah (s.w.).
Akiwahutubia mamia ya Waislamu
katika hotuba yake yake ya sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Nunge Sheikh
AbdulAziz aliwaambia Waislamu kuwa hakuna mja atakaye nyanyua mguu wake
kuingia peponi au motoni kabla hajatakiwa kujibu jinsi gani alivyozitumia
neema hizo nne, hivyo aliwataka Waislamu kuwa waangalifu juu ya neema hizo
ambazo wengi wamepumbazwa na wamejisahau kuzitumia kwa kuhuisha dini ya
Allah (s.w.).
--
|
|