Adhabu na upeo wake
Na Dkt. Abdallah Saffari
Sheria hutamka aina ya adhabu na ukomo wake ambayo mahakama huweza kutoa mintaarafu ya makosa mbalimbali. Aina kuu za adhabu ni kifungo, faini, wakati mwingine viboko kwa baadhi ya makosa. Adhabu hizo huweza kutolewa moja moja au zote kwa pamoja kama sheria imeruhusu (F. 167(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).
MAHAKAMA yana uhuru mkubwa mno wa kuamua adhabu ya kutoa na viwango vyake kutokana na mazingira ya shauri linalohusika. Shauri lililopo ni kuwa adhabu inayotolewa iwe halali, kwamba inastahili kutolewa na kwamba haikiuki ukomo uliowekwa na sheria. Mathalan kosa la wizi wa kawaida huadhibiwa kwa kifungo cha hadi miaka saba (F. 265, Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Sheria za Tanzania).. Hivyo uhuru wa mahakama hapo ni kutoa adhabu isiyozidi miaka saba.
Kila mahakama yana uwezo wake wa kutoa adhabu. Kwa mfano mahakama ya wilaya na Hakimu Mkazi hayawezi kutoa adhabu ya kifungo zaidi ya miaka kumi (F. 168(3) Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j) kwa kosa lolote lile hata kama sheria inaruhusu kifungo kirefu zaidi ya hapo (f. 286, Kanuni ya Adhabu, i.h.j). Isipokuwa mahakama ya wilaya yanaweza kupitisha adhabu ya kifungo cha uwezo wake kwa masharti kwamba adhabu hiyo inathibitishwa na Mahakama Kuu (F. 168(4) na 171(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Wakati uthibitisho wa Mahakama Kuu unasubiriwa mshitakiwa anaweza kupewa dhamana (F. 172(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai i.h.j).
Aidha kuna baadhi ya makosa ambayo yamewekewa kiwango cha chini cha adhabu kwa mujibu wa sheria ya viwango vya adhabu (Sheria Na. 1. 1972). Kwa mfano kosa la kuibia serikali au chombo cha umma huadhibiwa kwa kifungo sio chini ya miaka mitano. Hapo mahakama hayawezi kutumia uhuru wa kutoa adhabu ya kifungo chini ya miaka mitano kwa sababu hayana uwezo huo. Na kosa la ujambazi huadhibiwa kwa kifungo sio chini ya miaka thelathini. Katika hali hii mahakama lazima yapitishe adhabu hiyo.
Adhabu ya kifo ni lazima itolewe dhidi ya mshitakiwa aliyepatikana na hatia ya mauaji ya kukusudia (F. 197, Kanuni ya Adhabu, i.h.j). Mahakama Kuu yana uwezo wa kutoa adhabu ya juu kabisa ambayo imewekwa na sheria (F. 166, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j. Angalia Gray Mattaka na Wenzake v. R. (1971) E.A. 495).
Ni bora kuziangalia aina kuu za adhabu vizuri zaidi kama ifuatavyo:
(a) Kifo: Adhabu hii ambayo ndiyo kubwa kupitia zote hutolewa kwa makosa ya kuua kwa makusudi na huweza kutolewa kwa makosa ya uhaini. Katika kesi ya kwanza ya uhaini Tanzania ya R.v. Grey Mattaka na Wenzake (1971) E.A. 495). Mahakama Kuu hayakupitisha adhabu ya kifo bali ya vifungo vya miaka mbalimbali hadi maisha.
(b) Kifungo: Makosa mengi ya jinai huadhibiwa kwa kifungo kuanzia miezi michache na hata maisha. Mambo ya muhimu ni kuona iwapo sheria inatoa adhabu hiyo na ukomo wake. Aidha, uwezo wa mahakama yanayopitisha adhabu hiyo muhimu kuangaliwa. Adhabu ya kifungo ambayo haiafikiani na masharti hayo ya sheria sio halali na inafaa kukatiwa rufani au kufanyiwa masahihisho mara moja.
Kwa kawaida mahakama hayatoi adhabu ya kifungo kwa wakosaji wa kwanza hawa wale wa makosa madogo madogo (Halfani v. R. (1969) H.C.D. n.234). Watoto wadogo hawatakiwi wafungwe ndani ya magereza ya kawaida (F. Sheria ya Wahalifu Watoto, Sura ya 13, Sheria za Tanzania).
(c) Faini: Hii ni aina nyingine kuu ya adhabu ambayo mara nyingi sheria huyapa mahakama uwezo wa kuitoa, badala ya kifungo au kuitoa pamoja na kifungo kutegemea uzito na mazingira ya kosa linalohusika. Kutegemeana na ukomo wa faini ambayo sheria imeweka, mahakama ya wilaya yanaweza kutoa faini isiyozidi shilingi 30,000 (F. 168(3)(c), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Yakipitisha amri ya faini zaidi ya hapo lazima yapeleke amri hiyo ithibitishwe na Mahakama Kuu (F. 168(4), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Iwapo hakuna kiwango cha juu cha faini mahakama yatatoza faini ambayo sio kubwa sana (Msingi wa utaratibu huu umetokana na Sheria za Kiingereza yaani 'Common Law').
Uzito wa faini unatakiwa ulingane na uwezo wa mshitakiwa. Kutoza faini ambayo kwa vyovyote haiwezi kulipwa na mshitakiwa kwa vile ni nje ya uwezo wake kimali ni sawa na kumkomoa mshitakiwa huyo. Wakati mwingine baadhi ya mahakimu hutoza faini kubwa mno badala ya kifungo. Matokeo washitakiwa hushindwa kulipia faini hizo na kwenda gerezani kutumikia kifungo. Uteuzi wa kifungo au faini yafaa uwe uteuzi hasa, sio uteuzi tu kwenye mwenendo wa shauri.
(d) Viboko: Adhabu ya viboko huweza kutolewa mintaarafu na makosa machache. Mahakama ya Wilaya na Hakimu Mkazi yana uwezo wa kutoa adhabu hiyo hadi viboko 12 tu (F. 170(2)(b) Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Idadi zaidi ya hiyo itabidi ithibitishwe na Mahakama Kuu (F.168(4) NA 171(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Masharti mengine ya utoaji wa adhabu ya viboko yanaelezwa na Sheria ya Adhabu ya Viboko (Sura ya 17, Sheria za Tanzania).
(e) Kupiga Tanchi: Mahakama yanaweza kupiga tanchi kitu au mali yoyote iliyotumika katika uhalifu au iliyokusudiwa kwa jambo hilo (F. 351, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Adhabu kama hiyo huweza kutolewa mintaarafu ya sheria kama ile ya Hifadhi ya Wanyama Pori (Sheria ya Kuhifadhi Wanyama Pori, Na. 17, 1974) ambapo mahakama yanaweza kupiga tanchi gari au bunduki iliyotumika katika ujangili (K.h.j).
(f) Kulipa fidia: Endapo mahakama yanaona malalamikaji amepata madhara kutokana na kosa ambalo mshitakiwa ametiwa hatiani, yanaweza kuamuru mshitakiwa amlipe fidia mlalamikaji, au mtu yeyote, kama vile shahidi, ambaye amepata madhara (F. 348(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Madhara ni pamoja na maumivu ya mwili au hasara ya mali. Sharti ni kuwa fidia hiyo iwe inaweza kutolewa katika shitaka la madai dhidi ya mshitakiwa anayehusika (K.h.j). Fidia inaweza kuwa badala au nyongeza ya adhabu nyingine kadiri mahakama yanavyoona sawa (K.H.J). Aidha, fidia hiyo inaweza kulipwa kwa mali au fedha taslimu, hata huduma (K.H.J).
Hakuna ukomo wa kiwango cha fidia ambayo mahakama inaweza kuamuru kulipwa ilimuradi iwe sawa na kuridhisha. Kama ni hivyo ina maana mahakama yanaweza kuamuru kiasi chochote cha fidia kulipwa. Katika R. v. Doto Bakari (1967 H.C.D. n.211) mahakama yalisema kwamba fidia hiyo, kwa vyovyote vile isizidi Shs 2,000. Sisi tunaona uamuzi huo unaibana mno sheria ambayo kwa kweli imetoa uhuru mpana kabisa wa kiwango cha fidia. Kuamuru kulipa fidia katika shauri la jinai kutapunguza kufunguliwa kwa mashitaka mapya ya madai katika mahakama hayo hayo kuhusiana na mazingira yale yale. Jambo hili litapunguza msongamano wa mashauri na upotezaji muda wa kazi.
Lakini kwa upande mwingine tunaona kuwa iwapo fidia ambayo mahakama inakusudia kuamuru kulipwa ni kubwa mno basi bora shauri hilo lishughulikiwe rasmi kimadai. Au kiasi fulani cha fidia kiamuliwe kulipwa na mlalamikaji aelezwe juu ya haki yake ya kufungua shauri la madai kupata fidia kubwa ambayo pengine anastahili. Mwenendo wa mashauri ya madai na jinai pamoja na utaratibu wa kuthibitisha madai ni tofauti. Hivyo uamuzi wa kufungua mashauri ya madai utayapa mahakama yanayohusika fursa adhimu ya kuamua kiwago kinachostahili kulipwa. Iwapo mahakama yataamuru fidia ilipwe katika shauri la madai yatatilia maanani fidia ambayo ilikwishaamriwa kulipwa katika shauri la jinai mbele ya mahakama ya awali (F.350(3), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Bali kwa sasa tunaona Shs 2,000 ni kiasi kidogo sana kutolewa kama ukomo wa fidia katika mashauri ya jinai.
Mshitakiwa anaweza kukata rufani dhidi ya amri ya kulipa fidia iliyotolewa na mahakama katika shauri la jinai (F. 348(3), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Mbali ya mlalamikaji, fidia inaweza kutolewa hata kwa mshitakiwa ambaye hakuonekana na hatia iwapo mahakama yanaona mashitaka dhidi yake yalikuwa hayana msingi (F. 347, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Fidia hiyo ni kwa usumbufu na hasara iliyopatikana.
Hata hivyo ni nadra sana
mshitakiwa kulipwa fidia kwa mujibu wa fungu hili la sheria.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |