Serikali yadaiwa kuhatarisha amani


IMEELEZWA kuwa pamoja na serikali ya Tanzania kufahamu kuweko kwa hali inayotishia amani ya nchi kutokana na madai ya Waislamu kwamba wanabaguliwa; imeamua kukaa kimya badala ya kutafuta ufumbuzi.

Hali hiyo imekuwa chachu ya kudidimia amani ya nchi huku hali ikizidi kuwa mbaya kila siku.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyochapishwa na serikali ya Marekani hivi karibuni; Tanzania imeelezwa kutoa uhuru wa dini lakini wakati huo huo imedaiwa kukabiliwa na shutuma kutoka kwa Waislamu kuwa inawabagua na kuwapendelea Wakristo.

Imeelezwa kuwa yamekuwepo madai ya Waislamu kubaguliwa katika fursa za elimu na ajira.

Ripoti hiyo ya Marekani iliyonukuliwa na gazeti la Kanda hii ya Mashariki ya Afrika hivi karibuni imeeleza kuwa hali inazidi kuwa mbaya kwa sababu serikali haitaki kuchukua hatua pamoja na kufahamu kwake kuwepo kwa tatizo.

Kukataa serikali kushiriki katika mdahalo au mazungumzo juu ya mahusiano ya kidini nchini Tanzania yaliyokuwa yameandaliwa na USAID; kumetajwa kama kielelezo kwamba serikali ya Tanzania haipo tayari kulizungumzia suala hili.

Shirika hilo la Kimarekani (US Agency for International Development), mwezi Aprili mwaka huu liliandaa mdahalo ambao uliwajumuisha Waislamu na Wakristo kuzungumzia mahusiano baina yao.

Habari kutoka ndani ya mdahalo huo zilieleza kuwa Wakristo kwa upande wao walidai kuwa chokochoko zote zinaletwa na Waislamu kwa chuki zao na wivu wao kwa kutokuwa na elimu na maendeleo.

Hata hivyo imeelezwa kuwa Waislamu waliohudhuria mdahalo huo walieleza kuwa amani ya nchi hii inavunjwa na Wakristo kwa kuhini na kutumia vibaya amana (Trust) na imani waliyokuwa wamepewa na Waislamu.

Waliwakumbusha kuwa ni wazee wa Kiislamu walioanzisha TAA na TANU na kupigania uhuru wa nchi hii. Aidha, walieleza kuwa lau Waislamu wangekuwa na chuki na Wakristo wasingempokea Mwalimu Nyerere wakampa amana ya uongozi.

Mmoja wa kina mama Waislamu waliokuwa wamehudhuria mdahalo huo ameripotiwa kueleza kuwa amekuwa akibezwa si kwa kuangalia ayafanyao au asemayo lakini kwa kuwa tu kavaa hijab.

Kuhusu kuondoa hatari ya kuvurugika kwa amani ya nchi hii, mdahalo uliambiwa kuwa hilo litawezekana tu endapo Wakristo wataacha chuki zao, ubaguzi na uonevu wanaokuwa nao wawapo katika sehemu zao za kazi serikalini na sehemu nyingine.

Baadhi ya watu waliosoma taarifa hiyo ya Marekani kupitia vyombo vya habari wamedai kuwa upo ukweli katika taarifa hiyo juu ya ukweli kwamba serikali haitaki kutafuta ufumbuzi wa tatizo.

Tukio la serikali kumkamata Sheikh Mbukuzi badala ya kujibu hoja na tuhuma alizozieleza dhidi ya serikali; imeelezwa kama kielelezo cha msimamo huo wa serikali.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org

 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook