SHURA YA MAIMAMU DAR ES SALAAM
S.L.P. 75633, TEL: 170664, Dar es Salaam
 


MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI, Tarehe 15/09/99
MSIKITI WA MKWAJUNI, DAR ES SALAAM


 


Ndugu wanahabari,

Nikiwa Amir wa Shura ya Maimamu, Shura ambayo sina shaka ni maarufu masikioni penu, nimeona ni vyema kuongea nanyi siku ya leo, juu ya suala zito linalohusu mwenendo na mustaqbal wa nchi yetu.
 

Ndugu wanahabari, mtakuwa tayari mmesikia juu ya kilio cha waislamu kupitia vyombo mbalimbali na katika fursa mbalimbali, ya kuwa waislamu wanadhulumiwa ndani ya nchi yao na hawatendewi haki sawa na wenzao.
 

Malalamiko haya ya waislamu yamekwishafikishwa katika ngazi mbalimbali za kiutendaji za serikali ikiwa ni pamoja na Rais mwenyewe lakini bado haijaonekana nia thabiti kutoka kwa vyombo husika ya kutaka kuyafanyia kazi na kuyatafutia ufumbuzi wa hakika malalamiko hayo.
 

Kinyume chake tumeona serikali ikiongeza vitendo vya kuonesha kukidharau na kukipuuza kilio cha waislamu, na zaidi ya hapo serikali na watendaji wake kuwakejeli waislamu na kuwaendelezea vitendo vya kibabe, na pia kuwahoji waislamu eti watoe ushahidi wa 'kisayansi' juu ya hiyo dhuluma tunayodai kufanyiwa.
 

Ndugu wanahabari, katika kuipa faida serikali na watendaji wake na katika kuitakia mustaqbal mwema nchi hii, ningependa, kwa niaba ya Shura ya Maimamu na Waislamu, kwa mara nyingine tena na kwa uchache kuiweka wazi dhulma tunayofanyiwa Waislamu, kama ambavyo imeshabainishwa katika kauli zilizotangulia kutolewa huko nyuma. Pia, kutoa wito kwa Serikali na watendaji wake, kulitazama suala hili kwa uzito unaostahiki na kuchukua hatua za makusudi zenye lengo la dhati la kulitatua tatizo hili kikweli ili kuinusuru nchi hii na janga ambalo ni dhahiri litaikumba iwapo ufumbuzi wa haraka hautopatikana.

Waislamu wa nchi hii, juu ya kuwa kwa ukweli wa kihistoria, ndio tuliotoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru wa nchi hii wakati makanisa yakiwakataza waumini wao kuupiga vita utawala wa kikoloni, yaani utawala wa Waingereza, tumeambulia kuwa ni raia wa daraja la pili tukichukiza katika macho ya watawala wapya katika nchi yetu huru.
 

Ndugu wanahabari, baada ya Waislamu kwa moyo mkunjufu kuamua kushirikiana na baadhi ya raia wenzao wasiokuwa Waislamu, ili kutafuta utawala wa wenyewe katika nchi hii, wenzao hao, hususan Wakristo, wakawageuka baada ya uhuru na kuamua kujenga dola yenye kuwanufaisha wao na kuwadunisha Waislamu.

Huu ni ukweli wa kihistoria ambao hauhitaji utafiti mrefu kuuthibitisha. Lakini lililo baya zaidi hivi sasa, si yale waliyofanyiwa Waislamu huko nyuma, bali matendo ya Serikali kuendeleza udhalimu na ukandamizaji dhidi ya Waislamu hata sasa, jambo ambalo hapana shaka litawafikisha Waislamu wa nchi hii, kama raia na wananchi, kuamua kuiondoa dhulma hiyo kwa mikono yao.
 

Kwani Mtume (s.a.w) amesema kuwaambia Waislamu,nanukuu: "Yeyote miongoni mwenu atakayeuona uovu, na auondoe kwa mikono yake, ikiwa hawezi kwa mdomo wake, akiwa hawezi auchukiye; ama huko kuchukia ni udhaifu wa imani".

Pia Al-marhumu Professa Kighoma Ali Malima mara nyingi alikuwa akiukumbushia msemo wa hekima ya kuwa, nanukuu: "Haki haiombwi bali huchukuliwa."
 

Ndugu wanahabari, hapana shaka nyote mtakubali ya kuwa haimstahikii mtu kukiomba kitu chake mwenyewe. Hivyo iwapo haki ni yako, si wajibu wako kumuomba anayeizuilia, huyo ni dhalimu, yapasa apokonywe haki hiyo.
 

Ni jambo lililo wazi ya kuwa iwapo miongo ya kusubiri itazidi kuwa mirefu, na kiburi na dharau za wenye kudhulumu zitazidi, Waislamu tutafikishwa mahali pa kuamua kuichukua haki yetu na kuondoa dhulma kwa nguvu. Hapo machafuko yatatokea na janga la kumwaga damu litaikumba nchi yetu kama zilivyokumbwa nchi nyingine.
 

Mifano iko mingi ambapo waliodhulumiwa wamenyanyua mikono yao dhidi ya dhulma, kama vile kule Palestina, Bosnia, Chechnya, Kashmir, Dagestan, Afghanistan, Rwanda, Burundi, Afrika Kusini, na kwingineko. Hivyo watawala wetu wachukue mifano na wala wasifikiri hayo yanayotokea kwingine hayawezekani hapa kwetu. Kuendelea kunadi nchi yetu ni kisiwa cha amani wakati kundi moja la raia linalalamika kudhulumiwa bila kupatilizwa ni kujindanganya.
 

Na zaidi ya hivyo, Waislamu tunapenda kutoa ilani kwa namna Waislamu walivyobaguliwa katika nchi yao wenyewe, sasa Waislamu hawa wamegeuka kuwa tabaka la "wasio nacho", tabaka la "makabwela," na hali wakiwaona wenzao wa dini nyingine hususan wakristo wakineemeka na kujengeka kama tabaka la "wenye nacho".
 

Hapa, tunatanabahisha ya kuwa utabiri uliotolewa na Karl Marx, katika "The Communist Manifesto" alipotoa wito akisema, nanukuu: "Enyi makabwela duniani kote; Amkeni! Hamna cha kupoteza isipokuwa minyororo yenu." Hivi sasa imefikia hali Waislamu wa nchi hii, litakapo tokea la kutokea hawatokuwa na cha kupoteza ispokuwa kuondokewa na udhalili wao. Ikifikia hali hii, haitawawia vigumu kuamua kuangamiza kila kilicho chao, ikiwa ni pamoja na mali na roho zao, katika kupigania haki zao. Hapo inaweza kufikia tukagawana mpaka mitaa kama ilivyofikia katika nchi nyingine.
 

Lakini ni dhulma gani tunayosema tunafanyiwa? Serikali pamoja na vyombo vyake, imekuwa mstari wa mbele katika kuwadhulumu Waislamu. Serikali, ikiwa ndio mwekaji wa mipango, sera na mikakati ya uendeshaji nchi, inabeba lawama kwa kuweka mipango, sera na mikakati ya makusudi ya kuwadunisha Waislamu katika nyanja mbali mbali, badala ya mipango ya kuwaendeleza.
 

La mwanzo kabisa ni dhulma katika mgawanyo wa elimu. Tunakumbusha historia kuwa moja ya vilio vya Waislamu vilivyowapelekea kuendesha harakati za uhuru, ni kutopewa fursa sawa katika elimu. Hivyo Mwalimu Nyerere aliwaahidi Waislamu kwa kinywa chake kuwa angelirekebisha tatizo hilo baada ya uhuru na wao kutokana na ahadi hiyo, wakamuweka mbele katika harakati za uhuru. Kinyume na matarajio ya Waislamu si tu kuwa Serikali haikufanya juhudi kuwanyanyua kielimu, bali pia tumeshuhudia juhudi za makusudi za Serikali kuwakwamisha Waislamu hata katika juhudi zao wenyewe kujikwamua kielimu. Mfano suala la kuanzishwa Seminari za Kinondoni na Jumuiya, serikali ilifanya mambo matano:

(1) Ilitoa waraka wa Wizara ya Elimu kuzuia wanafunzi wa Seminari wa O'Level kuingia A'Level na Vyuo vya serikali lakini waraka huu haukuwazuia wanafunzi wa A'Level za seminari kuingia katika vyuo vya elimu ya juu vya serikali. Athari yake ilikuwa ni kuwakwamisha waliosoma Seminary wasiweze kuendelea mbele kutokana kwamba shule hizi zilikuwa hazina A'Level. Lakini Wakristo waliachiwa mlango wazi kuendelea na vyuo vya juu vya serikali kwa kutoka A'Level zao.

(2) Mwaka huu ulisitishwa kuanza kazi mpaka miaka minne baadaye wahitimu wa kwanza wa seminari hizi walipomaliza shule.

(3) Waraka huu ulifutwa mwaka seminari hizi za Waislamu zilipobadilishwa hadhi yake na kuwa sekondari za kawaida.

(4) Rais Nyerere na watendaji wengine wa serikali wa wakati huo, walitoa kauli kuwa Waislamu kuwa na seminari 2 ni kuleta udini. Hali yakuwa Wakristo walikuwa nazo seminari 29, haikuonekana kuwa ni udini.

(5) Serikali iliitisha, iligharamia, kusimamia na kukiwekea ulinzi mkali kikubwa cha BAKWATA kilichofanyika Chuo cha Ardhi Dar es Salaam ili kuwafukuza viongozi walioleta fikra ya kuanzishwa seminari hizi. Matokeo ya kikao kile, viongozi wale walifukuzwa na shule zikavuliwa hadhi ya seminari. Matokeo ya haya yote takwimu zinaonyesha kuwa shule hizi hivi sasa zinaongoza kwa kufelisha.
 

Hapa tunahoji juu ya mifumo inayotumika katika kusahihisha mitihani ya darasa la saba na kufanya uchaguzi wa wanafunzi kuingia sekondari.
 

Ni vigezo gani vinavyotumika mpaka uteuzi huu uchukuwe Waislamu wachache siku zote iwapo si upendeleo? Na ikiwa wanachaguliwa kwa kufuata viwango vya kufaulu,, je, ndio tuseme kuwa Waislamu kwa asili yao ni watu wasio na akili? Lakini mbona data zinaonyesha mwaka 1988 mitihani iliposahihishwa kwa namba, uteuzi au uchaguzi wa wanafunzi ulipofanywa kwa namba na si kwa majina idadi ya wanafunzi Waislamu walioingia kidato cha kwanza ilipanda kwa asilimia kubwa kiasi cha kushangaza? Au akili zao ziliongezeka ghafla. Na inatueleza nini kuhusu pale uchaguzi ulipofanywa kwa majina Waislamu wakawa wachache; je waliachwa makusudi.

Lakini si hivyo tu. Kwani Waislamu chini ya East African Muslim Welfare Society na Maulid Commettee tulianzisha shule nyingi tu za msingi Serikali ikazitaifisha shule zote zile kwa kisingizio kuwa elimu ya msingi itaendeshwa na Serikali. Zilitaifishwa pia baadhi ya shule za sekondari zilizokuwa "zikiendeshwa" na makanisa. Lakini shule za makanisa zilizoitwa "Seminari" ziliachwa. Pia zilitaifishwa na shule za Agha Khan na Karimjee na taasisi nyingine za Kiislamu. Lakini hivi sasa Serikali imetiliana saini mkataba wa maelewano na TEC na CCT, (Memorandum of Understanding), ili Serikali izipe taasisi hizo kubwa za Kikristo nchini shule na hospitali zake pamoja na kuzipa ruzuku za kuendeshea, kuwasomeshea wataalamu wake na kuwatafutia misaada kutoka kwa wahisani.
 

Zaidi ya hivyo, idadi ya taasisi zinazokusudia "kurejeshwa" kwa makanisa haya, inaizidi kwa kiasi kikubwa idadi ya zile zilizo chukuliwa toka mikononi mwao, ukiachilia mbali ukweli kwamba nyingi ya shule hizo zilikuwa zimeendelezwa kwa jasho letu sote toka zilipotaifishwa. Pia, nyingi ya zile zilizo "taifishwa" tangu awali hazikuwa za makanisa hayo bali makanisa yalikabidhiwa na serikali ya kikoloni kuziendesha kwa utaratibu huo wa kupewa ruzuku, kulipiwa mishahara na kusomeshewa wataalamu.
 

Dhulma ya pili kubwa ni suala la Serikali kukiuka sheria na katiba ya nchi na kuwashinikizia BAKWATA kama chombo pekee cha kusimamia mambo yote ya Waislamu bila ridhaa yao. Lakini pindi tu lengo la Serikali lilibainika kuwa ilikuwa ni kuwadhibiti Waislamu na si kuwahudumia. Matokeo yamekuwa ni kuwabana Waislamu wasiweze kuendesha jambo lolote la maendeleo.
 

Serikali pia ililazimisha taasisi zote za elimu za Kiislamu kuandikishwa chini ya BAKWATA kinyume na sheria za nchi na bila ridhaa ya Waislamu. Ufanisi wa shule na vyuo vya BAKWATA unaeleweka. Imefikia kuwafanya Waislamu kuwa kichekesho. Basi ni kwa nini Serikali iwalazimishe Waislamu kuweka taasisi zao za elimu chini ya chombo kisicho na ufanisi kiasi hicho kama si kukusudia kuwazuia Waislamu wasisome?
 

Kutokana na hali hii Waislamu tunauchungu kwa jinsi tulivyorudishwa nyuma na kukwamishwa kielimu. Na tumejikokota kuweza kuwa na shule zenye maendeleo mazuri.
 

Serikali ilipora nyumba na mali nyingi za waqfu kutoka kwa Waislamu zilipovunjwa jumuiya za East African Muslim Welfare Society na Maulid Committee na kuzikabidhi nyumba na mali hizo kwa BAKWATA kitendo ambacho kimechangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya Waislamu nchini. Na ni dhulma na ukandamizaji wa dhahiri kutokana na ukweli kwamba serikali ilifanya hivyo bila ya ridhaa ya wamiliki halali wa mali hizo.

Katika kuhakikisha ya kuwa Waislamu wamedhibitiwa kikamilifu chini ya BAKWATA wasiweze kufurukuta, chama tawala na Serikali yake vimeipa BAKWATA mamlaka mengi na makubwa juu ya Waislamu ambayo yote hayana msingi wowote kisheria na kikatiba. Kutokana na hali hiyo imefikia kuifanya BAKWATA kuwa kama idara ya serikali, shirika tanzu la CCM au kitengo cha makachero. Hapa Tunaorodhesha baadhi ya mamlaka hayo:

- Mpaka leo si ruhusa kusajili taasisi yoyote ya kiislamu, si shule, hospitali, nyumba ya mayatima, msikiti wala jumuiya ya Kiislamu, bila idhini ya BAKWATA. Hili linapingana na sheria ya vyama vya Hiyari (Societies Ordinance).

- Kwa amri ya Waziri wa Sheria BAKWATA ilikabidhiwa mamlaka ya kuunda "Mabaraza ya Usuluhishi ya masuala ya Ndoa" kwa Waislamu nchi nzima jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 na kinyume na katiba ya nchi.

- BAKWATA imefanywa kuwa kitengo cha Idara ya Uhamiaji kutokana na kwamba Muislamu hii leo hawezi kupewa hati za kusafiria iwapo hatothibitishwa uraia wake na kuidhinishwa na BAKWATA. Hili ni suala la uraia, sheria zinaeleza wazi ni mamlaka gani zinahusika kusimamia masuala haya. Ni kinyume kabisa kwa chama cha hiyari kilichoundwa na raia kukabidhiwa mamlaka hayo nyeti.

- Katika mashule yote ya Serikali, mpaka hivi karibuni kabisa, BAKWATA ilihodhishwa mamlaka ya kuteua walimu wa dini na kuendesha utoaji wa elimu ya dini ya Kiislamu, jukumu ambalo limewashinda kabisa na kusababisha watoto kukosa mafunzo muhimu ya dini yao.

- Kila ilipotokea taasisi na nchi wahisani wa Kiislamu kutoa misaada yoyote kwa ajili ya ya Waislamu na kuipitishia misaada hiyo serikalini, Serikali mara zote imeitoa misaada hiyo kwa BAKWATA ambapo uzoefu umeonesha ya kuwa mingi ya misaada hiyo kama si yote imefujwa na kuishia matumboni mwa "masheikh" na "ma-mufti". Hii inatokana na BAKWATA kuwa ni chombo kilichobebwa na Serikali na hivyo kutowajibika kwa Waislamu wenyewe.

-Yako mengi kuhusu BAKWATA lakini lalamiko la msingi ni kuwa Serikali kuendelea kuishinikiza BAKWATA juu ya Waislamu ni dhulma na ukandamizaji. Jambo hili limewachosha Waislamu na hawako tayari kuendelea kulivumilia.

Mbali na dhulma katika mambo hayo mawili tuliyotanguliza kuyaeleza, yapo mengi mengine yanayoonesha nia mbaya, chuki na dharau ya Serikali na watendaji wake dhidi ya Waislamu.Kwa mfano suala la watendaji wa Serikali kutojali hisia za Waislamu juu ya mambo yafuatayo:
 

(a) Dharau ya Serikali juu ya suala la ufugaji wa nguruwe na uuzaji nyama yake katika maeneo yenye wakazi mchanganyiko. Tunatoa tahadhari kuwa suala hili kama halitokomeshwa haraka, kwa hakika litaifikisha nchi hii mahali pabaya! Waislamu tunajivua lawama kwa lolote litakalotokea.

(b) Vitendo vinavyokithiri siku hizi vya askari kuingia misikitini tena wakiwa na viatu miguuni. Tunasema ya kuwa Waislamu wa nchi hii ni watu wa amani sana. Vinginevyo tunakumbushia matukio ya hivi karibuni ya kuuawa askari wasiopungua wanne waliokuwa na Bunduki "sub-machine guns" walipoingia msikitini kule Uganda, na lile la askari aliyeuawa katika msikiti wa Anas Bin Maalik kule Mombasa Kenya mwezi uliopita. Pia tunakumbushia tukio la askari wa kikoloni waliouawa Zanzibar katika miaka ya thelathini kwa kuvamia Misikiti.

(c) Matendo ya askari kuwapiga, kuwadhalilisha na kuwaadhibu Waislamu wawapo mikononi mwa polisi au magerezani kabla ya kutiwa hatiani na mahakama za sheria, na kufanya hivyo kinyume na mipaka ya kiutu na kisheria, yanatuuma sana Waislamu. Wapo waliodhoofika afya zao na waliopata vilema vya maisha. Na vitendo vya mahakama za nchi hii kuwanyima waislamu dhamana bila sababu za msingi hali ya kuwa dhamana ni haki ya kila mtuhumiwa suala hili pia linatuuma Waislamu. Tunatoa tahadhari kwa Serikali juu ya kuendelea na vitendo vya namna hii. Pia, Jeshi la Polisi hutumia nguvu zake kinyume na taratibu za kisheria inapokuja suala la kushughulikia Waislamu kama lile la askari kumpiga risasi ya moto kwa kumlenga shabaha mtu anayerusha jiwe kutoka umbali wa mita hamsini. Hatuelewi nini dhamira ya halisi ya polisi kama huyu. La kusikitisha na kushangaza zaidi ni juu ya mtoto Chuki Athumani kijana mdogo wa kidato cha pili, akiwa amevalia sare ya shule, ana vitabu mkononi kupigwa risasi. Aibu kubwa ni sababu iliyotolewa na polisi juu ya kwa nini alipigwa risasi. Jibu lilikuwa eti alikuwa na karatasi za uchochezi.

Ndugu wanahabari, bila shaka mtajiuliza maswali yafuatayo:

. Je, katika mazingira yale, polisi walimwona na karatasi hizo za "uchochezi" kisha ndio wakampiga risasi au walimkuta nazo baada ya kumpiga?

. Pili, hivi hukumu ya kuwa na karatasi za uchochezi ni kupigwa risasi?

Ndugu wanahabari, tunaurejea tena wito na kilio cha Waislamu kuwa nchi hii haitokuwa na salama mpaka suala la Mwembechai, hususan mauaji ya Waislamu na idhlali waliyofanyiwa wanawake waKiislamu, yatakapoundiwa tume huru kuyachunguza.

Sheikh Ponda hana kosa lolote kwa kutoa wito huu, basi Waislamu tunasema sote tuko naye na tutasimama na hili mpaka ripoti ya tume itakapotoka na kufanyiwa kazi. Tunaurejea pia wito kuwa wale walioua ni lazima wafikishwe mahakamani. Na ama kuhusu mtoto Chuki Athumani, Serikali imekuwa ikitoa kauli za uongo juu ya suala la kumtibu hali mtoto huyu anazidi kuvia na kupooza. Tunashuhudia Viongozi wa nchi wakipelekwa nje kwa matibabu wakati mtoto huyu yatima akiendelea kutaabika. Tunasema Serikali ilibebe kwa ukamilifu jukumu lake hili na zaidi ya kumtibu imlipe fidia yeye na familia yake.

(d) Juu ya suala la vazi la stara la Hijaab, bado tunaendelea kupokea taarifa juu ya walimu na wakuu wa shule jeuri wanaoikaidi amri ya Rais na nyaraka mbili za wizara ya elimu juu ya suala hili.

Kwa hivyo tunaitaka Serikali itamke bayana hatua gani itawachukulia watakaolipuuza agizo la Hijaab na suala za Ijumaa.

(e) Katika mlolongo wa madhila wanayofanyiwa Waislamu na Serikali ni pamoja na viongozi na watendaji wake kuendelea kutoa kauli zenye kuwakejeli Waislamu na Uislamu. Mfano mbaya zaidi ni wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Luteni Yusuf Makamba kutuita sisi tunaosimama kutetea haki zetu na dini yetu kuwa tu wahuni, vibaka, wavuta bangi, wachochezi, waleta vurugu, na siasa kali.

Pia Waziri Mkuu, Mhe. Frederick Sumaye ambaye mara nyingi huwaandama na kuwabeza Waislamu anapozungumza kama msemaji wa Serikali Bungeni. Wakumbuke waheshimiwa hawa kuwa yote haya yanabaki katika kumbukumbu za Waislamu.

Tunataja hapa tukio la hivi karibuni la mahakimu wa mahakama za mwanzo nao kuzikejeli na kuzikashifu sheria za Kiislamu kuwa eti zimepitwa na wakati.

Mwanafalsafa na kiongozi wa Kikomunisti wa China, Mao Tse Tung, alipata kusema, nanukuu: "No research, no right to speak".

Ndugu wanahabari, ningependa kukufahamisheni jambo moja yakuwa, kwa taarifa tulizonazo hapa nchini kwetu hakuna hata Jaji mmoja wa Mahakama Kuu wala Mahakama ya Rufaa aliyesomea sheria ya Kiislamu. Na kwamba uchambuzi wa hukumu zao juu ya masuala ya Kiislamu unaonesha wazi kiwango kikubwa wasivyoijua sheria ya Kiislamu na hivyo kupelekea kuipotosha. Bali pia chombo muhimu kama Tume ya kurekebisha Sheria, iliyojaa majaji na wasomi wa sheria wa Chuo Kikuu, imethibitika kutoijua kabisa sheria ya Kiislamu. Iwapo wakubwa hawa waliopea katika sheria hawaijui sheria ya Kiislamu, watatueleza nini mahakimu wa mahakama za mwanzo ambao kutokana na upeo wao mdogo imelazimika mahakama hizo ziwekewe taratibu maalum zilizorahisishwa ili walau waweze kutekeleza wajibu wao?

Tunarejea tena usemi wa Mao Tse Tung; "No research no right to speak". Asiyejua jambo haruhusiki kusema lolote juu ya jambo hilo.

(f) Suala la Waislamu kunyimwa uhuru wa kutangaza dini yao pia linathibitisha upendeleo dhidi ya Waislamu. Japokuwa sheria ya vibali kwa ajili ya mikutano ya hadhara ilishafutwa kuwa ni kinyume na Katiba, bwana mkubwa mmoja kwa chuki zake dhidi ya Uislamu alitoa amri kuwa mihadhara ya kidini nje ya nyumba za ibada ni lazima iombewe kibali. Tangu tangazo hilo batili Kikatiba litolewe, hajawahi hata mhadhiri mmoja wa Kiislamu kupata kibali, wahubiri wa Kikristo wametawala viwanja vya wazi wakihubiri mwaka mzima kana kwamba viwanja hivyo ni mali yao peke yao. Na tena japo tangazo lile lilihusu Mkoa wa Dar es Salaam pekee, watoa vibali wote nchi nzima wanalitekeleza bila msingi wowote wa kisheria.

Lakini kero imezidi hapo, hata Waislamu wanapo hadhiri katika viwanja vya misikiti yao, wanaandamwa kwa uchokozi, vitisho na kuwekewa masharti yenye lengo la kuwazuia wasiweze kuendesha mihadhara hiyo. Na mara nyingi wahadhiri hukamatwa, kuwekwa rumande muda mrefu bila dhamana kama walioua, na kufunguliwa kesi zisizo na kichwa wala miguu.

Mwisho na baada ya mateso na madhila kesi hizo hufutwa bila kufika mwisho. Katika matukio mengi ya namna hii wahadhiri na waumini wengine wamevamiwa na kupigwa na kuporwa vifaa na mali zao na polisi na mara nyingine vifaa na mali hizo vimetoweka mikononi mwa polisi. Hii ni fitna tunaikumbusha Serikali ya kuwa Qur-an inatuambia Waislamu, nanukuu: "Fitna ni mbaya kuliko vita!" Na kwamba Waislamu watakapozuiliwa na watawala kuitangaza dini yao, basi wana wajibu kupambana na watawala hao mpaka watakapoachwa huru kuitangaza dini. Basi Serikali yetu isitufikishe huko, sharti la kuomba vibali kwa ajili ya mihadhara lifutwe ili kuleta sahala katika nchi.

(g) Katika mlolongo wa madhila haya ya Serikali dhidi ya Waislamu ni suala zima la kuwaingilia Waislamu katika masuala yao ya sheria. Mwaka 1963, serikali ilizifuta Mahakama za Kiislamu na kukabidhi usimamizi wa sheria ya Kiislamu kwa Mahakama hizi ambazo, kama tulivyotangulia kutaja, majaji na mahakimu wake hawana ujuzi wowote wa sheria ya Kiislamu. Tafsiri yetu ni kuwa hawakuwa na dhamira nyingine ila kuipotosha na kuivuruga sheria ya Kiislamu.

Juu ya hilo na kwa kuthibitisha dhana yetu, kuanzia pale ulifuata utaratibu wa kuifuta sheria ya Kiislamu kidogo kidogo. Mwaka 1971 ikapitishwa sheria ya Ndoa ambayo iliathiri vibaya sheria ya ndoa na talaka ya Kiislamu. Moja ya hadidu za rejea ya Tume ni kutafiti mazingira ya kuleta sheria moja ya Mirathi (Uniform system of Law).

Baada ya hapo ulitengenezwa mswada wa sheria moja ya mirathi mwaka 1979. Lakini mwishoni mwa miaka ya 80, suala hili likakabidhiwa kwa Tume ya kurekebisha sheria ili hatimaye ipatikane sheria moja ya mirathi .

Kwa hivyo tunashangaa hivi leo kuwa Serikali inataka kurejesha mfumo wa mahakama za makadhi. Basi makadhi hao watafanya kazi gani iwapo sheria za Kiislamu mnataka kuzifuta?

Basi tunasema kuwa Waislamu tumechoshwa na kesi zetu kusimamiwa na mahakama hizi zisizokuwa za Kiislamu. Kwa hivyo, hapana budi kwetu kuzirejesha mahakama za makadhi. Lakini iwapo ni fikra ya Serikali kuleta mahakama hizi kwa lengo la kuwatafutia Waislamu chombo kingine cha kuwadhibiti baada ya BAKWATA kuporomoka na kutoka thamani machoni pa Waislamu, ni vyema wafute fikra yao hiyo, Mahakama za makadhi zenye hadhi halisi na uadilifu wa Kiislamu zitasimama watake wasitake. Na tunatamka pia kuwa, ni msimamo na muelekeo wa Waislamu hivi sasa kuwa watahukumiana kwa sheria zao, wala hatokuwepo wa kuifuta sheria ya Kiislamu ya mirathi, ila apende Allah (SWT) mwenyewe. Na ni kusudio letu kurekebisha upotofu ulioletwa na sheria ya Ndoa ya mwka 1971.

Hivi inafikia hali kama ilivyofikia kuhusu tatizo la mirathi ya Hayati Hajjat Aziza bint Omar kuwa mali ya Muislamu, tena aliyoitoa Waqfu arithishwe Mkristo? "The Judicature and Application of Laws Ordinance" marekebisho ya mwaka 1963 yanasema kesi ya Muislamu juu ya maswala ya mirathi itahukumiwa kwa sheria ya Kiislamu. Sheria ya Kiislamu ya mirathi inasema kuwa Muislamu hamrithi asiyekuwa Muislamu wala harithiwi na asiyekuwa Muislamu.

Kwa hivyo tunathubutu kumtaja kwa jina na kumhoji mama Natalia Kimaro, Hakimu mkazi mkuu katika mahakama ya Kisutu, na ambaye hivi sasa amepandishwa na kupewa wadhifa wa Msajili wa Mahakama Kuu, aliyesimamia shauri hili ni kwa misingi gani na kwa kufuata sheria gani alimteua Mkristo, Bwana Daniel Zakaria, kuwa "msimamizi wa mirathi na mrithi pekee" wa Bi Aziza Omar?

Kuna mengi ya kutia shaka juu ya shauri hili lakini kwa kuwa liko mahakamani hivi sasa tunazuia kauli zetu.

Kwa hivyo ndugu wanahabari, tumekufikishieni ujumbe huu mkiwa wawakilishi wa umma wa Watanzania, ili huenda haya yakiwafikia wanaohusika wakabadilisha mwenendo wao na kuwatendea iliyo haki Waislamu. Hiyo itakuwa ndio njia bora na ya pekee ya kuiepusha nchi yetu na janga ambalo ni hakika linainyemelea.
 

Ndugu wanahabari, Waislamu ni wananchi, ni raia, ni walipa kodi na wajenga nchi, na zaidi ya hivyo ndiyo waliopigania uhuru wa nchi hii; ni lazima wapate haki sawa na wengine.

Ndugu wanahabari, Waislamu walipigania uhuru wa nchi hii wakati ambapo makanisa yakiwahadharisha Wakristo wasiupige vita utawala wa kikoloni. Ni Wakristo wachache waliounga mkono harakati zile. Basi Insha-Allah, ikibidi, Waislamu hawatoshindwa kusimama tena kujikomboa.
 
 

Wabillahit-Tawfiiq.


 


--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook