AFISA Elimu wa Manispaa
ya Morogoro Bi. Ester Mwangamila amesema kuwa uvaaji wa hijabu mashuleni
ruksa kutokana na kauli ya Rais, hivyo hakuna mtu atakayenyanyaswa kutokana
na kuvaa na atakayethubutu kukiuka agizo hilo hatua kali zitachukulia dhidi
yake.
Aliyasema hayo Jumatatu wiki hii katika shule ya sekondari ya wasichana ya At-Taaun iliyopo mjini hapa wakati alipokuwa akifunga semina ya siku tatu kwa walimu wa Kiislamu wa shule za msingi Manispaa ya Morogoro.
Bi Mwangamila alisema kuwa amesikia kauli ya Rais Benjamin Mkapa akitoa agizo hilo na ni lazima iheshimiwe.
Akijibu risala ya wanasemina wapatao 120 Afisa huyo alisema kuwa ratiba ya Ijumaa mashuleni itashughulikiwa vizuri ikiwa ni pamoja na siku za mitihani na suala zima la hijab na mwalimu yeyote atakayeonekana ni kikwazo katika kufanikisha zoezi hili hatua za haraka zitachukuliwa dhidi yake.
Akizungumzia ucheleweshaji wa nyaraka mbalimbali mashuleni hususan zinazowahusu Waislamu alisema kuwa ni kweli suala hili linaleta matatizo, hivyo ataiomba ngazi ya juu kushughulikia tatizo hili haraka ili kuweza kuondoa migongano inayoweza kutokea.
Aidha, Afisa huyo aliwataka walezi, wazazi na walimu wa Kiislamu kuwahamasisha vijana wa Kiislamu kushiriki nafasi mbalimbali katika uongozi wa shule, siasa ili kuondoa manung'uniko kuwa Waislamu wanaonewa.
Awali waandalizi wa semina hiyo Islamic Propagation Centre na mdhamini wa semina hiyo Morogoro Islamic Foundation walimkabidhi Afisa huyo waraka wa serikali unaohusu uvaaji wa hijabu pamoja na kitabu cha mitaala kwa wanafunzi wa Kiislamu.
Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti kunyanyaswa baadhi ya wanafunzi wanaovaa hijab mashuleni na kutolewa kashfa mbalimbali kutoka kwa baadhi ya walimu wakuu na wale wa kawaida. Shule inayodaiwa kufanya kitendo hicho ni Kikundi na Kiwanja cha Ndege zote za mjini hapa.
Semina hiyo ya walimu wa Kiislamu wa shule za msingi Manispaa ya Morogoro ilifunguliwa Septemba 18, mwaka huu na Dk Ally Abood Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) ambaye alimwakilisha aliyetarajiwa kuwa mgeni rasmi Profesa K. Dihenga.
Maazimio kadhaa yalipitishwa na wanasemina hao ikiwa ni pamoja na kujielimisha kwa wanasemina hao kwa njia mbalimbali ikiwemo ile ya masomo kwa njia ya Posta (E.K.P) inayotolewa na Islamic Propagation Centre pamoja na kujiunga na madrasa mbalimbali. Pia walimu hao wameazimia kufundisha elimu ya Maarifa ya Kiislamu (Islamic Knowledge) mashuleni kwao.
Vile vile waliazimia kufuatilia harakati za Uislamu kwa karibu kama vile suala zima la uvaaji wa hijab kwa wanafunzi na wao wenyewe, kufuatilia habari kwa mtazamo wa Uislamu.
Azimio lingine ni kufanya kazi kwa bidii kwa lengo la kukuza vipato vyao ili kuweza kuupigania vizuri Uislamu kwa hali na mali zao.
KANDA zipatazo 51
na Redio kaseti moja mali ya muuza kanda za kidini Bw. Hassan Mwadili inasemekana
zinashikiliwa na polisi kwa takriban mwezi sasa.
Kanda zinazoshikiliwa na polisi Mtwara mjini ni pamoja na zile za Qur'an, kasida na mawaidha ya dini juu ya mada mbalimbali.
Mpashaji wetu wa habari ameeleza kuwa Bw. Hassan alikamatwa na polisi mapema mwanzoni mwa mwezi huu akituhumiwa kuuza kanda za mihadhara ya mlingano wa kidini ambazo hudaiwa na polisi kuwa ni za kashfa.
Hadi Septemba 21, Bw. Hassan Mwadili alikuwa hajafikishwa mahakamani na hulazimika kupiga ripoti polisi mara kwa mara.
Kwa muda mrefu sasa katika miaka ya hivi karibuni polisi wamekuwa wakiwakamata wanaotoa mihadhara au wanaouza kanda zinazosema kuwa Yesu si Mungu ingawa viongozi wakuu wa Makanisa wamekwisha kusema Waislamu ni haki yao kiimani na ndio maana hawajasimama mahakamani.
Mara nyingi Waislamu wamekuwa wakishangazwa kutokana na hatua za polisi za kuwakamata Waislamu wanaosema Yesu si Mungu, lakini hawachukui hatua zozote kwa waumini wa Kikristo wanaosema Yesu ni Mungu.
Wakati huyu akikamatwa na kanda zake palikuwepo muhadhara wa walokole wakisema Yesu ni Mungu katika uwanja wa Council Mtwara mjini si mbali na mahala alipokamatwa muuza kanda huyo pasipo kuhojiwa na polisi.
Haikuweza kujulikana kama kuna uhusiano wowote kati ya muhadhara na ukamatwaji wa Bwana huyo.
Juhudi za gazeti hili kuwasiliana
na Kamanda wa polisi Mtwara juu ya tukio hili hazikuweza kufanikiwa.
TABASAMU Karimu (15)
amekuwa ni alama katika alama za Mwenyezi Mungu kutokana na uwezo usio
wa kawaida alionao katika somo la hesabu.
Binti huyo ambaye hajamaliza elimu ya msingi ana uwezo wa kufanya hesabu kubwa iwe ni kutoa, kujumlisha, kuzidisha, kugawanya, vipeo na kadhalika na kutoa majibu kwa muda mfupi bila ya kuandika mahali.
Chakushangaza ni kuwa unapompa hesabu binti huyo; mfano (17)5 anachofanya ni kuchezesha mikono yake huku akishika sehemu ya kifua na kichwa na kuwa kama mtu anayetazama katika 'Screen' huku akitafakari na kutoa jawabu baada ya sekunde chache.
Chakushanagza zaidi ni kuwa akipewa hesabu za kugawanya au kutafuta 'Roots' ( V au V) atakupa jawabu mpaka desimali zote hata kama ni nyingi kiasi gani.
Akiongea na Waandishi wa gazeti hili juzi Tabasamu bint Karim alipewa hesabu zifuatazo na kutoa majibu katika muda usiozidi dakika moja kwa kila swali.
(17)3 = 4713; (74) = 2401; (13)5 = 371293; (3136)2 =9834496; 47/ 7 = 6.714285714; 563,463 x 3739 = 2106788157; (62624)2 = 3921765376; 17/ 3 = 5.6666; 39/ 4 = 9.76; 1000,000/ 350,000 = 2.857142.
Katika mahojiano hayo Tabasamu alieleza kuwa alishawahi kuongea na wataalamu wa mahesabu Chuo Kikuu katika jitihada za kutafuta watu wa kumsadia kukuza kipaji chake.
Uchunguzi zaidi wa gazeti hili umeonyesha kuwa mmoja wa Maprofesa wa hesabu Profesa Masenge katika kustaajabia uwezo wa binti huyo aliishia kusema kuwa "She is unteachable". Hata hivyo akashauri kuwa apelekwe katika kijiji cha Sayansi kinachoongozwa na Profesa Shayo.
Kilio cha Tabasamu ni kupatiwa
shule itakayokidhi haja ya uwezo alio nao.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |