JIFUNZE SHERIA
 
Mashahidi wa nyongeza kabla ya hukumu
Na Dkt. Abdallah J. Saffari
 

KATIKA haja ya kuhakikisha kuwa ushahidi wote muhimu unapatikana kabla ya hukumu kutolewa mahakama yana mamlaka ya kuita mashahidi wa nyongeza (F. 195, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Kwanza tutaangalia jinsi uamuzi huo unavyoweza kuchukuliwa katika uendeshaji wa shauri kwa mara ya kwanza. Katika hatua hiyo mahakama yanaweza kuwaita mashahidi wa nyongeza kwa namna moja kubwa. Inawezekana wakati shahidi wa upande wowote ule anapotoa ushahidi akawa anamtaja mtu mwingine ambaye hakuitwa kabisa kutoa ushahidi. Mahakama yanaweza kuona kwamba mtu huyo ambaye hakuitwa na upande unaohusika labda anaweza kutoa ushahidi muhimu kufikia uamuzi sahihi wa shauri hilo. Hata hivyo, mara nyingine sio lazima shahidi huyo awe amemtaja mtu fulani katika ushahidi wake pale mahakamani. Kumbukumbu za maelezo yake mbele ya askari au afisa yoyote yule mathalan Mlinzi wa Amani kabla ya kusikilizwa kwa shauri hilo zinaweza kuonyesha kwamba kuna mtu ambaye ametajwa, ambaye kama akiitwa mahakamani, anaweza kutoa ushahidi kugundua mtu gani anaweza kuitwa kama shahidi wa nyongeza mbali na njia hizo mbili. Hata hivyo, kinadharia, mahakama bado yana mamlaka na uwezo wa kumwita mtu yeyote yule kama shahidi ilimradi kuna imani kwamba anaweza kutoa ushahidi wa maana katika uamuzi wa shauri linalohusika (F. 142, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).

Mashahidi muhimu katika shauri wanaweza wasiitwe na pande zinazohusika bila ya kukusudia au pengne kwa makusudi kabisa. Aghalabu kila upande unakuwa na haja ya kushinda kesi kwa kila hali. Wakati mwingine, kwa nia njema kabisa, upande mmoja unaweza ukaacha kumwita shahidi wa maana pengine kwa imani tu kuwa ushahidi wake sio muhimu hata kidogo, au labda kwa dhana kuwa tayari umeshatolewa na kutomwita shahidi muhimu ikawa ni kuficha kweli. Ya kwamba iwapo shahidi huyo ataitwa mahakamani basi atasema kweli ambayo itaukandamiza upande unaohusika.

Bila ya kujali makusudi hayo mawili matokeo ya kutoitwa mashahidi hao muhimu ni mmoja: Kuathiri utoaji hukumu ya haki.

Katika shauri la R.V. Lawrent Kihwele (Shauri Maalum la Jinai Na. 50, 1977, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mbeya (Haijachapishwa) mshitakiwa, Mmasi, alishitakiwa kwa kumwua kwa makusudi kijana mdogo aliyekuwa akichunga ng'ombe wa baba yake katika shamba la mshitakiwa. Wakati wa tukio hilo mshitakiwa alikuwa na kaka yake. Jamhuri ilichelea kumwita kaka yake huyo kwa hofu kuwa asingetoa ushahidi wa kweli. Mshitakiwa alipokuwa anatoa ushahidi alikiri kuwa wakati wa tukio alikuwa na kaka yake, lakini hata hivyo hakupenda kumwita kama shahidi. Mahakama yalitumia uwezo wake kumwita shahidi huyo. Shahidi huyo alikuwa hakutoa maelezo marefu kuhusiana na mauaji yenyewe mbele ya polisi miaka kadhaa kabla ya shauri lenyewe kusikilizwa. Ushahidi wake, hata baada ya kuitwa na mahakama, ukawa hauna uzito wowote ule. Hapana shaka, hata hivyo, kuwa hatua hiyo ya mahakama ilikuwa katika kutafuta kweli - ushahidi sahihi ili kufikia uamuzi wa haki katika shauri. Hatimaye mshitakiwa alipatikana na hatia ya mauaji ya kutokusudia kutokana na ushahidi wa mazingira ingawa yeye alikana kosa kabisa kuwa hakumpiga na kumwua marehemu.

Katika shauri la Joseph Mwinuka v R. (Shauri la Jinai la Rufani Na. 159, 1979, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mbeya (haijachapishwa) ambapo mshitakiwa alikabiliwa na shitaka la wizi wa shilingi 16,483.20 upande wa mashitaka uliacha kumwita shahidi muhiju Edward Mapunda. Lakini mahakama yalimwita shahidi huyo na kumtia hatiani mshitakiwa sio kwa wizi wa shilingi 16,483.20 kama ambavyo ilidaiwa bali shilingi 9,340.15.

Wakati wa kusikiliza shauri kwa mara ya kwanza kwa kawaida mahakama huwaita mashahidi wa nyongeza mwisho kabisa wakati pande zote mbili wamemaliza kuita mashahidi wao. Lakini mahakama yanaweza kumwita shahidi wa nyongeza wakati wowote katika hatua ya kusikilizwa shauri hilo iwapo kufanya hivyo kutasababisha ufanisi. Sababu kuchelewa kumwita shahidi huyo kunaweza kuathiri mfululizo wa ushahidi, ambapo kung'ang'ania kufanya hivyo kunaweza kuchelewesha shauri hasa pale ambapo shahidi huyo hayupo mahakamani na anahitaji muda mrefu kupatikana. Kumwita shahidi huyo katikati ya shauri kunaweza kuwa na athari ya kuingilia mpango au utaratibu wa kuendesha shauri kwa upande ambao wakati huo unafanya hivyo. Shahidi wa mahakama au wa ziada huhojiwa na mahakama yenyewe. Pande zinazohusika katika shauri huweza kumhoji kwa ruhusa ya mahakama. Vinginevyo utaratibu wote wa kuhoji ni kama ule mintaarafu ya shahidi mwingine yeyote yule.

Kuita mashahidi wa ziada hakuishii tu katika hatua ya kwanza ya kusikiliza shauri. Mahakama yana mamlaka ya kufanya hivyo hata wakati wa kusikiliza rufani. Yanaporidhika kwamba ushahidi huo wa nyongeza ni lazima yataandika kuelezea sababu zake kisha yanaweza kuchukua ushahidi huo yenyewe au kuyaamuru mahakama ya chini kuchukua ushahidi huo kwa niaba yake (F. 360 (1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Iwapo yatafuata hatua ya pili mahakama ya chini yatachukua ushahidi wa shahidi anayehusika na kupeleka kumbukumbu ya ushahidi huo katika mahakama ya juu ambayo yatautilia maanani wakati wa kuandika hukumu.

Jambo hili linadhihirisha umuhimu wakuwa na ushahidi sahihi ili kufikia uamuzi wa haki. Masuala ya ushahidi yanaweza kubishaniwa katika rufani ya kwanza isipokuwa ya pili mpaka kwa ruhusa maalum ya mahakama ya rufani yanayohusika (K. 65, Kanuni za Mahakama ya Rufani Na. 15, 1979).

Kwa bahati mbaya mahakimu wengi na baadhi ya majaji hawatumii uwezo waliopewa chini ya mafungu haya ya sheria inavyopasa. Mfano mzuri ni shauri la R.v. Wilbert Mushi (Shauri la Jinai la Rufani Na. 31, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mbeya (Haijachapishwa) ambapo ilidaiwa kwamba mrufani alipokea rushwa ya shilingi 1,000 kutoka kwa mtu aliyeitwa Idd Bakari ili mrufaniwa achomoe vielelezo vya ushahidi kwenye jalada la kesi dhidi ya mtu aliyeitwa Erick Nyonyona. Wakati kesi hiyo inasikilizwa mara kwa mara jina la Erick Nyonyona lilitajwa na baadhi ya mashahidi. Hata hivyo mwisho wa kesi Erick Nyonyona mwenyewe hakuitwa na upande wa mashtaka. Mahakama hayakutumia uwezo wake kumwita shahidi huyo wa maana sana kuthibitisha kama kweli mrufani aliomba na kupokea rushwa ili amsaidie huyo Erick Nyonyona. Kwa kushindwa kufanya hivyo ushahidi huo muhimu mno ulikosekana. Badala yake mara tu baada ya mshitakiwa kumaliza kujitetea Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo aliandika hukumu kumtia hatiani mshitakiwa kama alivyoshitakiwa.

Wilbert Mushi alikata rufani katika Mahakama Kuu dhidi ya hukumu hiyo ya mahakama ya Wilaya. Katika hukumu yake ndefu kiasi Jaji Mwakibete alisema: "Hakuna shaka ushahidi unathibitisha kwamba mrufani alipokea noti zilizowekwa alama kutoka kwa Idrisa Bakari zenye thamani ya shilingi 1000. Lakini sio kitendo cha kupokea fedha pekee kinachozua kosa ambalo kwalo mrufani ameshitakiwa". Mheshimiwa Jaji huyo aliendelea kusema: "Upande wa mashitaka ulidai kuwa mrufani alimfuata Erick Nyonyona kumwomba shilingi 1000 kwa kubadilishana na vielelezo vya ushahidi wa kesi dhidi ya Erick Nyonyona. Mrufani alikana dai hilo. Inadaiwa kwamba mrufani aliomba rushwa hiyo wakati akiwa yeye na Erick Nyonyona tu. "Kwa maoni yangu inaonekana ni Erick Nyonyona pekee anayeweza kuthibitisha kweli au uongo wa madai hayo pamoja na kuyaeleza mahakama mazingira ya maombi hayo ya rushwa iwapo kweli yalifanyika". (Msisitizo ni wangu).

Kwa sababu hizo rufani ya Wilbert Mushi iliruhusiwa.

Ni kweli kwamba kama upande wowote unashindwa kumwita shahidi anayeonekana ni wa maana katika shauri linalohusika dhana ni kuwa laiti shahidi huyo angeitwa na upande huo angetoa ushahidi dhidi yake. Hivyo pengine ni sawa kusema au kufikiri kuwa upande wa mashitaka uliogopa kumwita Erick Nyonyona kwa vile angetoa ushahidi dhidi yao. Bali pamoja na hayo yote haki katika shauri hili ilihitaji Erick Nyonyona aitwe hata katika hatua hii ya rufani. Kwamba kufanya hivyo kungekuwa sawa na kuusaidia upande wa mashitaka, kwa sasa , sio lazima amwite shahidi huyo hata kama aina ya ushahidi atakaoutoa unasaidia upande wa mashitaka (Kolukuna Otim v R. (1963) E.A. 253, na kufuatiwa baadaye katika Faustin Manoni v. R (1969) H.C.D. n.29). Izingatiwe kwamba shahidi wa aina hiyo ataitwa inapolazimu tu.

Katika kesi maarufu ya hivi karibuni ya Abel Mwanga v Elisaph Lima (Shauri la Madai la Rufani Na. 4 1982, Mahakama ya Rufani Tanzania, Mwanza (Haijachapishwa) Mahakama ya Rufani ya Tanzania yalipinga hoja ya wakili wa mrufani kwamba Mahakama Kuu yaliyosikiliza shauri hilo mara ya kwanza yalistahli kumwita shahidi mmoja kwa vile mahakama hayo yaliona hakuna haja ya kufanya hivyo pale ambapo kweli imeshadhihirika. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook