Na Mwandishi Wetu
RAIS wa nchi asiwe na madaraka ya kuteua watendaji waandamizi wa serikali, ambacho angefanya ni kupendekeza majina na Bunge likatibitisha au kukataa.
Maoni hayo yalitolewa katika kipindi cha Katiba yetu kilichorushwa na kituo cha DTV wiki iliyopita.
Wakizungumza kwa pamoja katika kipindi hicho, Sheikh Abubakar Mwilima, Dk. Abdallah Safari na Sheikh Othman Matata wamesisitiza kupunguzwa kwa madaraka ya Rais katika marekebisho ya Katiba yanayokusudiwa kufanywa hivi karibuni.
Akitoa maoni yake kuhusu suala hilo, Dk. Abdallah Safari amesema kupewa madaraka ya kuteua waandamizi kunaweza kuleta dhana ya kuwepo upendeleo wa kirafiki, kichama na ukaribu mwingineo baina ya Rais na mtu anayemteua.
Alisema Rais angepewa fursa ya kupendekeza majina kisha Bunge likakaa kuyajadili majina hayo kwa kuzingatia sifa na vipaji vya wahusika.
"Rais anaweza kumteua mkuu wa majeshi au mwanasheria mkuu wakati hana sifa ya kupewa wadhifa huo", alisisitiza Dk. Safari ambaye ni mtaalam wa masuala ya sheria na mhadhiri wa vyuo mbalimbali nchini na nje ya nchi.
Akichangia suala hilo Sheikh Abubakar Mwilima alisema hata katika uteuzi wa mkurugenzi wa idara ya usalama usifanywe siri baina ya Rais na huyo anayemteua.
Sheikh Mwilima aliongeza kuwa suala hilo liwe wazi na kwamba jina la aliyependekezwa na Rais lifikishwe bungeni ili lijadiliwe kwa vigezo vya uwezo na sifa zinazotambulika.
Kuhusu suala la uchaguzi kufanywa wa gharama nafuu, watoa maoni hao walisema jambo hilo litawezekana iwapo haki itazingatiwa.
Mzee Mwilima alikuwa na maoni kwamba ila zote za udanganyifu ziondolewe, kusiwe na kumpendelea mtu wala kuzima taa wakati wa kuhesabu kura.
Aidha, alisema uchaguzi uwe wa siku moja, usirudiwe rudiwe hata kama kutakuwa na visingizio vya uchelewaji wa maboksi ya kura.
Alitoa mfano wa uchaguzi wa mwaka 1958 ambao alisema ulikuwa huru na majina ya waliopiga kura yalibandikwa katika vituo vya kupigia kura.
Hali hiyo alisema ilifanya kuwepo kwa uwazi, hivyo alipendekeza kifungu cha usajili wa wazi kuwepo katika katiba kuhusu masuala ya uchaguzi.
Kuhusiana na matokeo ya Rais, Bwana Othman Matata alisema wananchi wawe na haki ya kuhoji matokeo hayo kabla Rais hajatangazwa rasmi na kwamba matokeo hayo yathibitishwe kwanza na mahakama.
Akichangia kuhusu Tume ya Uchaguzi, Dk. Safari alisema, Tume hiyo ni uti wa mgongo wa uchaguzi, hivyo alipendekeza kushirikishwa watu kutoka vyama vyote vya siasa katika uundwaji wake.
Sheikh Othamn Matata alichangia suala la wagombea binafsi kwa kusema kwamba dhana ya kuwa mtu lazima awe mwanachama wa chama fulani ndipo achaguliwe kuwa kiongozi ni kinyume na Katiba ambayo inasema mtu anayo haki ya kuchagua na kuchaguliwa.
Akitilia mkazo suala la ugombea binafsi, Sheikh Mwilima alisema chama kinaweza kulazimisha mtu kusimama katika uchaguzi wakati wananchi hawamtaki.
"Wanaweza kukataa kupiga kura kwa sababu wanalazimishwa kula shubiri wakati wanataka halwa", alisema Sheikh huyo maarufu nchini.
Juu ya siasa ya ujamaa na kujitegemea kuingizwa katika katiba, Mzee Mwilima alisema wakati umefika wa kuondokana kabisa na "slogan" hiyo.
Alisema siasa ya ujamaa imepitwa na wakati ulimwenguni kote na kwamba hapana haja Watanzania kuiga mfumo kutoka nje kwani wana utamaduni wao wa asili wa kushirikiana na kuishi pamoja.
Katika kipindi hicho ambacho
huendeshwa na mwanahabari mkongwe Bwana Hamza Kasongo, mambo mengine yaliyotolewa
maoni ni pamoja na kuwepo kwa serikali tatu katika muundo wa muungano,
hatari iliyopo katika suala la usawa wa raia wa dini zote, uhuru wa vyombo
vikuu vitatu vinavyounda dola na kuondoshwa kifungu cha kutangaza hali
ya hatari na kuwaweka watu kizuizini kwa amri ya Rais.
--
|
|