Na Mja Dikupatile
WAHENGA walikuwa na desturi ya kufasiri ndoto, hali, tabia na matukio mbali mbali kisha kuyanasibisha na ima majanga, misiba na mikosi au neema, furaha na matumaini.
Ukiweka pembeni dosari fulani fulani, hawakuwa wakifanya hivyo zaidi ya kujenga desturi ya kuenzi na kuheshimu mila ya jamii, kuchukua hadhari, kujiepusha au kuweka matarajio.
Katika mafundisho ya dini tunawakuta manabii kadhaa wakikumbwa na hali kama hizo kulingana na mazingira yao. Nabii Yusuf mwana wa Yakobo alitoa tafsiri ya ndoto iliyohusiana na janga la njaa lililokuja kutuka baadaye. Hali kadhalika tukio la kutokuzungumza kwa muda kwa Nabii Zakaria lilikuwa ishara ya mkewe kujifunga uja uzito wa mwana aliyekuja kufahamika kama Yohana Mbatizaji (Nabii Yahya).
Mabalaa ya mafuriko, njaa na ajali yalihusishwa na baadhi ya miaka au kuonekana kwa wanyama na wadudu walio nadra zama fulani, vivyo hivyo mtu au watu kukiuka adabu, miiko na maadili ni ulaanifu uliopewa sura hiyo. Mfano mtu kukosa radhi ya wazee wake ni hali iliyopewa tafsiri nzito kiadabu, kimiiko na kimaadili.
Kwa utaratibu huu hadhari zilichukuliwa, miiko ilichungwa, wabaya walitengwa na heshima ilihifadhiwa.
Watu walikuwa makini kufuatilia matukio yasiyo ya kawaida ili kujipa matumaini ya neema fulani au kujiepusha na majanga yaliyohofiwa.
Nabii Yona (Nabii Yunus) alifikwa na mtihani huu pale alipoghafilika kutaka kuihama kaumu yake bila ya ruhusa ya Mwenyezi Mungu hatua ambayo ilipelekea atoswe baharini kwa mujibu wa desturi za zama hizo kwamba mtumwa kumkimbia bwana wake ni mwiko ulionasibishwa na mkosi unaoweza kusababisha maafa. Kufuatia kuyumba na kutaka kuzama kwa jahazi alilopanda, waongozaji na abiria wote jahazi hilo walitafakari kilichosababisha hali hiyo na kuamua kupiga kura kumtafuta mwenye mkosi ili "atoswe", kura ilimuangukia Nabii Yona(Yunus) akatoswa, jahazi likaendelea na safari. Mwenyezi Mungu alifikisha ujumbe kwa mja wake kulingana na mazingira yaliyokuwepo.
Katika kipindi cha miaka minne Watanzania mbali ya hali ngumu sana ya maisha inayotukabili, tumeshuhudia matukio mazito yaliyogusa hisia zetu. Kama kulikuweko na matukio kama haya miaka 34 (awamu mbili za mwanzo) ya uhuru iliyopita basi si katika kiwango kinachoweza kulinganishwa na miaka minne hii.
Tumo ndani ya jahazi linaloyumba, hali inayohitaji vichwa vyenye hekima vya wazee kutafakari kuweza kupata tafsiri munasibu huku tukizingatia mafunzo ya vitabu vya dini kwamba misiba na majanga mbali mbali hutokana na vitendo vyetu.
Kwa kuwa 1999 ni mwaka wa wazee vijana wangetaraji hekima zao hasa katika matatizo mazito ambayo ufumbuzi wake mara nyingi huhitaji umri wa walio kula chumvi nyingi.
Ifuatayo ni sehemu ya mlolongo wa matukio mazito yaliyolikumba taifa letu tangu kuanza awamu hii.
Desemba 2, 1995:
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilitumia askari wa Jeshi la Wananchi na polisi kusimamia zoezi la kuharibu ngano ya mfanyabiashara maarufu nchini, Bw. Said Bakhresa. Ngano hiyo inakisiwa kufikia tani 3,800. Zoezi hilo lilifanyika huku kukiwa na amri ya muda ya mahakama inayozuia kuharibiwa kwa ngano hiyo hadi kesi iliyofunguliwa na mahakamani na Bw. Bakhresa dhidi ya Jiji itakaposikilizwa.
Desemba 7, 1995:
Watu 10 wafariki, 42, wajeruhiwa baada ya basi la Shirika la Posta nchini, SU 31644 kupinduka kati ya vijiji vya Mtyangimbole na Gumbiro kilometa 40 kutoka mjini Songea katika barabara ya kwenda Njombe.
Januari 9, 1996:
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Hali ya Hewa, Dk. Mohamed Mhita atangaza Tanzania kukumbwa na ukame kutokana na kuchelewa kunyesha kwa mvua za vuli. Alisema mkondo ambao ulikuwa ukileta mvua katika ukanda wa Tanzania umebadili mwelekeo.
Januari 16, 1996:
Watu 17 wafariki kwa ajali ya basi la Abood Service lenye Na. TZB 5534 lililokuwa likitokea eneo la Bwawani, mkoani Morogoro.
Januari 30, 1996:
Mkurugenzi wa Idara ya Uslama wa Taifa, Imrani Kombe auawa akitokea mjini Moshi kwenda nyumbani kwake maili sita wilayani Hai.
Mei 21, 1996:
Watu wanaokisiwa kuwa 948 walikufa kufuatia kuzama kwa meli ya MV Bukoba waliyokuwa wakisafiria kutoka Bukoba kwenda Mwanza.
Agosti 1, 1996:
Wachimbani wa madini 12 wafukiwa wakiwa hai kwenye migodi ya Bulyamhulu, wilayani Kahama.
Desemba 27, 1996:
Watu kadhaa wafariki kufuatia ajali ya basi la Air Chalinze iliyotokea eno la Kilimanjaro Machame, Moshi.
1996:
Njaa yaikumba mikoa ya kusini hadi wananchi wa Kilwa wafikia kula majani.
Januari 9, 1997:
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Hali ya Hewa, Dk Mohamed Mhita atangaza Tanzania kukumbwa na ukame kutokana na kuchelewa kunyesha kwa mvua za vuli. Alisema mkondo ambao ulikuwa ukileta mvua katika ukanda wa Tanzania umebadili mwelekeo.
Januari 17, 1997:
Mbunge wa Morogoro Kaskazini, Prof. Nicas Mahinda auawa na majambazi nyumbani kwake Kunduchi Mtongani.
Januari 10, 1997:
Moto mkubwa wazuka na kuteketeza eneo kubwa la msitu wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA).
Januari 29, 1997:
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Brigedia Hassan Ngwilizi atangaza ugonjwa wa kipindupindu walikumba Jiji la Dar es Salaam na hadi siku hiyo watu 8 walikuwa wamefariki na watu 61 kulazwa Hospitalini.
Januari 30, 1997:
Akihutubia kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya, Rais Benjamini Mkapa akanusha watu kufukiwa Bulyanhulu na kuagiza utaratibu wa kisheria dhidi ya wote waliotoa habari hizo katika vyombo vya habari wafikishwe mahakamani.
Februari 7, 1997:
Serikali yatangaza kwamba ugonjwa wa malaria waikumba wilaya ya Korogwe, mkoa wa Tanga na kuua watu 36.
Machi 12, 1997:
Waziri Mkuu, Frederick Sumaye aagiza jeshi la polisi Jijini kukamata na kuwafungulia mashitaka watu wanaomwagilia bustani, mboga kwa kutumia maji ya bomba.
Machi, 13, 1997:
Watu saba wafariki baada ya kufukiwa na udongo kwenye mgodi wa kuchimba marumaru ulioko kijiji cha Moivaro, wilaya ya Arumeru, Arusha. Pamoja nao, pia lori tani saba aina ya Isuzu lenye Na. ARJ 583 mali ya kikosi cha kuzuia ujangili Arusha lilifukiwa kabisa bila kuonekana.
Machi 13, 1997:
Mbunge wa Ludewa, Horace Kolimba afariki katika mazingira ya kutatanisha huko Dodoma alipokuwa ameitwa na Kamati Kuu ya CCM kujieleza kuhsu kauli zake kwa CCM kuwa haina dira wala mwelekeo.
Machi 25, 1997:
Mwanzo wa mvua za maafa za El-Nino.
Agosti 13, 1997:
Watu 14 wafariki na 31 wajeruhiwa vibaya baada ya mabasi matatu kugongana katika eneo la Kingolwira, mkoani Morogoro. Mabasi hayo ni No.Challenge Na. Ta TZJ 1958, lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Singida, basi la Safina Na. TZJ 2658 na basi la Abood TZK Na. 3812.
Itaendelea toleo lijalo
--
|
|