AN-NUUR 
Na.185 Shawwal 1419, Januari 29 - Februari 4 , 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Kupokelewa kwa malalamiko ya Waislamu:
Masheikh wasubiri ukweli wa Mkapa

Kajitia kitanzi shingoni 

MASHEIKH wamemtaka Rais Benjamin William Mkapa kutimiza ahadi aliyoitoa wakati akijibu risala juu ya malalamiko ya Waislamu katika Baraza la Idd lililofanyika Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam wiki iliyopita. 

Wakizungumza na ANNUUR kwa nyakati tofauti, Masheikh hao wamesema kwamba kwa kuwa kumekuwa na ahadi nyingi zinazotolewa na serikali bila ya kutekelezwa Rais kupokea malalamiko na kuahidi kuyashughulikia hakutaondoa wasiwasi walio nao juu ya kile walichokiita "sindano nyingine ya ganzi". 

Katika hotuba yake kwenye Baraza la Idd; Rais Benjamin Mkapa aliahidi kuyachambua yeye na baraza lake malalamiko ya Waislamu kisha kuyatafutia ufumbuzi. 

Malalamiko hayo ni pamoja na upendeleo wa kidini uliopo serikalini na katika vyombo vya dola dhidi ya Waislamu, suala la mauaji yaliyofanywa Mwembechai, mahakama za kadhi, uwiano mbaya wa kidini katika vyuo na maofisi ya serikali, kiini cha kuwepo kwa idadi kubwa ya vijana wa Waislamu katika magereza na suala la OIC. 

Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili kutoka Morogoro Sheikh Ayyub MUwinge amesema yawezekana Rais kuwa na nia nzuri kwa raia wake lakini bila ya kutekeleza anachoahidi hataeleweka vyema na raia hao. 

"Ni kawaida ya viongozi wa nchi za dunia ya tatu kuahidi wasiyo yatekeleza au kupuuza shida za wananchi wao; labda nia njema aliyonayo Rais kwa Watanzania wa dini zote itathibitishwa na kutimiza alichoahidi", alisema Sheikh huyo maarufu mkoani Morogoro. 

Naye Sheikh Jabir Katura Imamu wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa Mwanza ameielezea ahadi ya Rais kama ni jambo wasilopaswa Waislamu kuliwekea matumaini ya asilimia kubwa kutokana na historia ya viongozi wa nchi hii. 

"Mwalimu Nyerere aliahidi mwaka 1962 hakutekeleza ahadi badala yake tukaundiwa Bakwata ambayo imedidimiza kabisa maendeleo kidogo tuliyokuwa nayo huko nyuma", alisema Sheikh Katura. 

Hata hivyo, Sheikh Jabir alisema kuwa ufumbuzi wa matatizo ya Waislamu ni Waislamu wenyewe kujidhatiti, kujiendeshea mambo yao kwa kuweka mipango ya kiutekelezaji. 

"Tusibweteke kutegemea misaada ya wanadamu, msaada halisi upo kwa Allah (s.w.) peke yake", alisema kwa msisitizo Sheikh Jabir Katura. 

Sheikh huyo alinukuu aya ya 118 iliyomo katika surat Alimrani na aya 120 ya surat Baqara kutilia mkazo maelezo yake kwamba wasio Waislamu hawatakuwa na nia njema kwa Waislamu katika utekelezaji wa mambo mbalimbali yenye manufaa kwa jamii. 

Aidha, alisema nusra ya Waislamu iko kwa Allah kwa sharti la kumtii yeye katika maisha yao. 

"Na bila shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayeisaidia dini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu na mwenye kushinda(22:40)", alikariri Sheikh Jabir. 

Akizungumzia maendeleo ya Waislamu yaliyokuwepo huko nyuma ambayo yalikuja kupigwa vita na aina ya viongozi wanaoorodheshewa matatizo ya Waislamu leo hii. Sheikh Jabir alitolea mfano wa mkoa wa Kagera ambao alisema ulikuwa na shule nne za msingi za Waislamu ambazo zote zilitaifishwa na serikali ya Tanzania huru. 

Alizitaja baadhi ya shule hizo kuwa ni Katoro Muslim School, Kamachumu na Kasenene. 

Alisema leo hii wakati Wakristo wamerejeshewa Nyegezi, Forodhani na nyingine, serikali haijaona haja ya kuzirejesha shule za Waislamu. 

"Ahadi ya Rais kama itatekelezwa ni vizuri kwetu lakini tusikae tukabweteka na sindano hizo za ganzi", alimalizia Sheikh Katura. 

Hata hivyo, Sheikh mmoja maarufu Jijini amesema kwamba hana wasiwasi na kauli ya Mh. Rais Mkapa. 

Akifafanua amesema kwamba kwa mwanadini na muungwana ni chukizo kubwa kusema asiyoyatenda. Amesema Rais Mkapa ni mwanadini na hivyo hana wasiwasi kwamba kauli yake ni thabiti. 

Sheikh huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini amewataka Waislamu wawe na subira wakiwa na matarajio mema kutoka serikali yao. 

Amesema kwa kufanya subra bila kubwabwaja ovyo, Waislamu hawatapoteza kitu. Ahadi ya Rais ikitimia ndio matarajio na hata isipotimia bado hawatakuwa na hasara kwani watakuwa wamepata funzo litakalowasaidia mbele ya safari. 

Kupokelewa kwa madai ya Waislamu wiki iliyopita kumezua mijadala tofauti sehemu mbalimbali nchini. 

Mijadala hiyo inatokana na kile kilichoonekana huko nyuma kuwa ni uchochezi wa kidini kuzungumzia kukandamizwa Waislamu katika masuala mbalimbali hapa nchini ambao ulinasibishwa na "Waislamu walioitwa kuwa na Siasa kali". 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 

Tahari 
Kama hakuna haki watu watachukua sheria mkononi  

Kupokelewa kwa malalamiko ya Waislamu: Masheikh wasubiri ukweli wa Mkapa  

Afariki baada ya kutokwa damu nyingi: Yadaiwa hakuwa na sh. 4,000  

Nyumba ya Wakfu iliyoporwa yarejeshwa  

Kamanda Gewe atakiwa amkamate Daniel  

Sheikh awasambaratisha walevi Liwale  

Msikiti wavamiwa na kuvunjwa milango, madirisha  

Mjue Usama bin Ladin -2  

Msikiti wa Mwinyimkuu wafanya sensa  

Njaa hakuna, tunategemea kula silaha  

Parole kwa mbinde!  

Mabaraza yawatetee Waislamu - Sheikh Bafadhil  

Hali ya Uislamu Lukulunge, Kongwa inatisha  

Waislamu Kondoa waagizwa kuyatunza magazeti ya ANNUUR  

I.P.C yatakiwa kujitangaza  

Kutoka magazeti ya zamani  

Sabato ni ya Waisraeli, Mungu alikwishaiondoa  
Na Muhibu Said  

Waislamu wachoma moto nguruwe  

Tume ya kubadili Katiba Kenya: Waislamu kuwakilishwa  

Waislamu Msonge waomba wanusuriwe  

Sayansi na Teknolojia  
[PELEKA FAX NCHI ZA NG’AMBO BURE! – (2)]  

Masomo ya Kiislam  

Barua za Wasomaji  

Mashairi  

Chakula na Lishe  
[Mwongozo wa mlo wa kila siku]  
 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita