|
|
|
KWA vile kiasi cha juma moja lijalo, wasomaji wetu wa gazeti hili ambao ni Waislamu wataanza mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani; tumeonelea ni vyema makala ya wiki hii ya chakula na lishe izungumzie dhana ya futari (kifungua kinywa), na hasa futari ya tende ambayo imesisitizwa sana na Mtume Muhammad (s.a.w.). Kwa hoja hiyo makala hii pia imewasilishwa kwa staili ya ‘kusilimishwa’ yaani imeelezwa kwa msisitizo wa Qur’an na Hadith za Mtume Muhammad (s.a.w.). Kama staili hiyo (Qur’an na Hadith) ni ‘kero’ kwa wasomaji wetu wasiokuwa Waislamu, tunaomba watuvumilie. Futari katika makala hii ni neno lenye maana kama ile iliyoelezwa katika kamusi ya Kiswahili (1981 - Dar es Salaam). Katika Kamusi hiyo, futari ni chakula cha kwanza kinacholiwa magharibi na mtu aliyefunga baada ya kumaliza saumu yake. Kwa mujibu wa sheria (Fiqh) ya dini ya Kiislamu, chakula au kinywaji chochote kile cha halali kinafaa kutumika kama futari. Kwa mfano mihogo, viazi, wali, ugali, nyama, samaki, mikate, maandazi, ndizi, maji, soda, juisi, matunda, uji, togwa, biskuti, pipi, muwa, maharage, n.k. Pamoja na sheria ya dini ya Kiislamu kutoa nafasi (ruhusa) kubwa ya aina ya vyakula vinavyoweza kutumika kama futari (au matumizi mengine), Qur’an inawafundisha waumini na wanaadamu wote kwa ujumla kufanya uchaguzi juu ya vyakula watakavyokula. Uchaguzi huo unazingatia vigezo vikubwa viwili: Uhalali na ubora (uzuri). Mafundisho hayo tunayapata katika aya kadhaa ndani ya Qur’an. Baadhi ya aya hizo ni: "Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri, wala msifuate nyayo za shetani (yale anayokuamrisheni). Bila shaka yeye kwenu ni adui dhahiri". (2:168) Na kuleni katika alivyokuruzukuni Mwenyezi Mungu vilivyo halali na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye nyinyi mnamwamini. (5:88). Enyi mlioamini! Kuleni vizuri tulivyokuruzukuni, na mumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa mnamwabudu Yeye peke yake. (2:172). Kwa kuzipitia aya za hapo juu na nyinginezo zinazohusu somo la vyakula, mtu anawza akajiuliza swali. Kufanya uchaguzi wa vyakula kwa kigezo cha halali na haramu, hikma yake iko wazi. Baadhi ya hikma ya kukatazwa kula baadhi ya vyakula ni kuwa vyakula hivyo vina madhara kwetu (walaji) kiafya, kijamii, n.k. au ni mpango (mtihani) wa Mwenyezi Mungu kuwapima waja wake - wepi wanaotii na wepi wanao asi. Lakini vile vyakula vilivyohalali kwa nini navyo tufanye uchaguzi? Jibu la swali la hapo juu tunalipata kwa kuitafakari aya ifuatayo: "Na katika ardhi muna vipande vinavyoungana (na kuzaa kwake namna mbalimbali), na muna mabustani ya mizabibu, na mimea mingine, na mitende ichipuayo katika shina moja. Vyote vinanoshelezwa (vinamiminiwa) maji yale yale; na tunavifanya bora baadhi yake vyingine katika kula. Hakika katika haya zimo ishara kwa watu wanaotia mambo akilini". (13:4) Tukazitazama futari zetu (na vyakula vingine) zimo ndani ya aya au la. Kwa maneno mengine, Muislamu (na wanaadamu wengine) wanapokwenda sokoni, dukani, shambni kwa ajili ya kulima au kununua chakula lazima wawe wanaongozwa na Qur’an. Wakati wa swala ukifika tunaswali, au Ramadhani ikifika tunafunga au nguruwe hatuli kwa nini, jibu tunaifuata Qur’an. Lakini mtu mathalan anapokwenda sokoni haizingatii Qur’an katika uchaguzi wa vyakula kwa kigezo cha ubora (virutubisho), Kwa mtazamo wangu, mwenendo kama huo ni kufuata baadhi ya aya na kukufuru (kuacha) baadhi yake, jambo ambalo limeufanya ummah wa Kiislamu leo kutawaliwa kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, n.k. Zaidi ya hayo, mwenendo huo utatuweka pabaya kesho Akhera. Vile vile ni vyema nikachukua fursa hii kuwaomba Masheikh kwamba, tafsiri na ufundishaji wa Qur’an na Hadith lazima uwe wa kina ili Waislamu waweze kuifaidi Qur’an katika kila kipengele cha maisha. Kama kuna upungufu kwa baadhi ya Masheikh kuhusu ufafanuzi wa aya kama tulivyozinakili hapo juu, hapana budi kuwa na semina na ili kukuza taaluma zetu kwa gharama nafuu. Baada ya maelezo hayo, ni wakati mzuri sasa kurudi katika kiini cha makala yetu. Katika utekelezaji wa maneno ya Mwenyezi Mungu (Qur’an) kuhusu vyakula, Mtume Muhammad (s.a.w.) amesisitiza chakula cha tende kiwe ndicho futari. Msisitizo huo tunaupata katika Hadith kadhaa, baadhi yake ni hizi: "Anas (r.a.) ameeleza kuwa: "Mtume (s.a.w.) alikuwa akifungua kwa tende mbivu kabla ya kuswali (magharibi) kama hizi hazikuwepo alifungua kwa tende kavu, na kama hizi hazikuwepo alikunywa mafundo machache ya maji". Tirmidh na Abu Daud) "Salmah bin Amir amesimulia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Mmoja wenu atakapokuwa anafuturu, na afuturu kwa tende kwa sababu ni baraka, kama hakupata tende, na afuturu kwa maji, kwa sababu yametakasika (ni twahara)". (Ibn Majah) Msisitizo mkubwa katika Hadith za hapo juu ni kuwa Waislamu wafuturu kwa tende. Makusudio ni japo tende moja na si lazima ziwe nyingi kiasi cha kushiba. Hata hivyo, mtu akipata kiasi cha kushiba si vibaya. Akili ya mwanaadamu ni ya kudadisi. Kwa hiyo, inawezekana akadadisi kwanini tende? Inawezekana sababu za Mtume (s.a.w.) kusisitiza futari ya tende ziko nyingi, lakini makala hii itachambua virutubisho (nutrients) vinavyopatikana katika tende ili iwe ni kama moja ya hikma ya mafundisho hayo ya Mtume (s.a.w.) ambayo mwalimu wake mkuu ni yule Mjuzi wa yote, yaani Mwenyezi Mungu. Tende ina vitu vingi sana vyenye faida kwa binadamu. Ina sukari (glucose) yenye kuyeyuka upesi na ikampa binadamu haraka haraka ile sukari iliyokuwa imepungua wakati wa kufunga (saumu). Vile vile tende inapunguza mtu kuona uvivu na unyong’onyi na machofu ya macho, ina vitamini nyingi zenye kusaidia kukua na kutia nguvu za kuona usiku. Baadhi ya vitamini A, B1 na B2. Zaidi ya hayo, tende ina madini ya potosium na phosphorus ambazo ni muhimu kwa maendeleo ya mwili. Tende pia zina nyuzi nyuzi (dietary fibres) ambazo ni muhimu kwa afya ya binadamu. Kwa mfano nyuzi nyuzi zinapunguza tatizo la mtu kukosa choo kikubwa na zinanyonya sumu iliyozalishwa tumboni. Tukizingatia virutubisho vinavyopatikana katika tende na pia tukizingatia aya tulizoziona mwanzoni, tunapata kanuni ya kuandaa futari bila kuathiri mazingira (upatikanaji wa chakula), mazoea na sababu nyingine zinazokubalika na sheria ya dini ya Kiislamu. Kanuni yenyewe ni kuwa, futari lazima iwe imeandaliwa na vyakula vyenye
sukari na mafuta mengi na yenye matunda matamu. Pia chakula cha baada ya
futari lazima kiwe mlo kamili kama tulivyowahi kuona katika makala zilizopita.
|
YALIYOMO
Maoni Waislamu tunakusudiwa kufanywa watumwa wa nani? Wananchi waingiwa na hofu kuhusu silaha Serikali yagwaya kwa wafugaji
nguruwe
Hakuna njama za kupindua Bakwata - Sheikh Yahya MARADHI YA KISAIKOLOJIA:: VOYEURISM
Tathmini: Miaka 37 ya uhuru wa Tanganyika
Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo:
Batendi hakumuelewa Mkomidachi
Muhammad (s.a.w.) katika
Unabii wa Isaya (a.s.)
Ijue SUA Madrasa Moro
Kiteto wakosa darsa kwa kupinga Ramli Ustadh ayeyuka na saruji ya Msikiti mjini Arusha Akina mama Muheza waungana kufanya
Daawa
Wanafunzi Waislamu Mbeya wapata
uongozi
Je, hivi tuendelee kushika amri
za Mungu tena? - 2
Njia ya uzima ni nyembamba,
waionao ni wachache - 2
Waandishi andikeni ukweli - Kamati
Sheikh Jongo aichachamalia
Uwawaru
Waamriwa kurejesha Mali ya
Mirathi
Waislamu Mlimba Moro mashakani
Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|