|
|
| Madini
ya chuma
Na Mujahid Mwinyimvua KATIKA moja ya makala zetu za chakula na lishe tuliwahi kuzungumzia dhana ya mlo kamili. Katika makala hiyo tulisema kwamba mlo kamili (balanced diet) ni chakula (mlo) wenye virutubisho vyote muhimu kwa afya ya binadamu (au viumbe wengine). Vilevile tulisema kwamba virutubisho hivyo vinaweza kuwekwa katika makundi makuu sita. Makundi hayo ni kabohaidreti (wanga, sukari, nyuzi nyuzi - dietary fibre), mafuta, protini, maji, vitamini na madini. Sawiya na hayo, pia tulisema kwamba; kwa ujumla kabohaidreti na mafuta ni virutubisho vinavyoupatia mwili nguvu na joto; protini ni virutubisho vinavyojenga mwili, vitamini ni virutubisho vinavyolinda mwili na, madini na maji ni virutubisho vinavyosaidia kazi zote za hapo juu (kutoa nguvu na joto, kujenga na kulinda mwili). Katika makala yetu ya wiki hii tutatazama chuma kama moja ya madini yanayohitajika mwilini. Madini ya chuma (Iron) ni moja ya madini iliyo muhimu watu kuijua, katika nchi zetu za Afrika Mashariki na Kati. Madini nyingine (kwa umuhimu huo) ni madini joto (iodine), ‘zinc’ na ‘fluorine’. Chuma ni madini iliyomo katika damu, imeungana na protini katika chembe chembe nyekundu za damu. Muunganiko huo unaitwa ‘haemoglobin’. Haemoglobin inabeba hewa safi (oxygen) kutoka katika mapafu (lungs) na kuipeleka sehemu mbali mbali za mwili zenye chembe chembe hai ili hewa hiyo iunguze chakula na kutoa nguvu na joto. Pia haemoglobin inabeba hewa chafu (carbon dioxide) kutoka katika chembe chembe hai (cells) na kuipeleka katika mapafu, na hatimaye kutolewa nje ya mwili. Chembe chembe za damu ambazo huwa na madini ya chuma kama tulivyoona hapo juu, huishi kwa miezi michache. Yaani hufa baada ya miezi michache. Zinapokufa, madini ya chuma kiasi kikubwa hutumika tena kutengeneza chembe chembe za damu mpya. Hata hivyo, kiasi kingine cha madini ya chuma hupotea (hutoka nje ya mwili kwa njia mbali mbali kama mkojo). Vile vile, mtu akipoteza damu kwa njia mbalimbali kama vile kujikata, wakati wa uzazi, wakati wa hedhi, kutoa damu hospitalini, n.k., madini ya chuma nayo hupotea kwa wingi. Kama mtu ana kiasi kidogo cha madini ya chuma kuliko mahitaji yake, mtu huyo anapata shida ijulikanayo kama enemia (kupungukiwa damu). Tukizingatia maelezo ya hapo juu ni wazi kuwa kila mtu anahitaji madini ya chuma ili mwili wake uweze kutengeneza damu ya kutosha. Ukweli huu uko wazi zaidi hasa katika miaka yetu ya sasa yenye gonjwa la Ukimwi, ambalo mpaka sasa halina tiba wala kinga (ya kitabibu). Ujumbe ninao kusudia kuutoa hapa ni kuwa, watu tujitahidi kuimarisha taratibu zetu za kula ili miili yetu iwe na damu ya kutosha. Hii ni kwa sababu, utakapokuwa na upungufu wa damu, siku hizi (za Ukimwi) kupata damu isiyokuwa na vijidudu vya Ukimwi ni kazi kubwa. Pia uwezekano wa kuwekewa damu yenye vijidudu hivyo upo, hasa tunapoitazama sekta ya afya hapa kwetu Tanzania. Katika taaluma (na nyanja nyingine pia) ni mwiko kusema mambo ambayo huna ushahidi nayo. Ninavyoona mimi taarifa ifuatayo inatosha kutoa picha ya sekta ya afya Tanzania, hasa katika kipengele cha tiba. Gazeti la Dar Leo (24/11/1998) likilinukuu gazeti la The African la tarehe hiyo hiyo (24/11/98), limeandika kwamba: "The African lina habari kuwa wafanyakazi wa Hospitali ya Muhimbili wamekiri mbele ya waziri jana kuwa wamekuwa wakipokea rushwa kutoka kwa wagonjwa kutokana na kukatishwa tamaa na mishahara midogo wanayopewa na kufanya kazi katika mazingira magumu. Wafanyakazi hao walimwambia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Wilson Masilingi, kuwa wamekuwa hawapati mishahara ya kutosha kuendesha maisha yao na vifaa vya Hospitali ya Muhimbili viko katika hali isiyokarabatika". Watu ambao miili yao inahitaji kutengeneza kwa wingi chembe chembe nyekundu za damu, ni lazima miili yao hiyo ipate madini ya chuma kwa wingi. Watu hao ni wanawake wanaopata hedhi (siku za mwezi), kinamama waja wazito (wenye mimba), watoto (wanaokua) na watu wenye anemia. Madini ya chuma yanapatikana kwa wingi katika vyakula vifuatavyo.:- maini, figo, nyama, maziwa, maharage, nafaka, mboga za majani za kijani kilichokolea), n.k. Vyakula kama vile kahawa, chai na nafaka isiyokobolewa zina vitu vinavyozuia
mwili kunyonya madini ya chuma kutoka katika vyakula tunavyokula. Hivyo,
ni vyema tukapunguza utumiaji wa vyakula hivyo.
|
YALIYOMO
Tahariri
Urambo wamlilia Profesa Lipumba
Sheikh aridhia Waislamu
kubatizwa
Uongozi Masjid Qadiria waitwa Polisi kuhojiwa Wakazi wa Mbagala Msalabani kuishitaki Tume ya Jiji Akhera ipo, makafiri ni wakadhibishaji
Mdahalo kati ya Waislamu na
Wakristo ni mgumu
Aina ya maudhi yaliyoharamishwa juu ya Muislamu PAROLE: Rais kasusa
au hana ubavu?
Serikali ikithamini kilimo
Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto
wadogo - 3
Madrasa Arrijalu Muswallin Damba Ijue Madrasat Fauzia - Kibondo Waislamu Kondoa waanza
kupokea misaada ya ujenzi wa Msikiti, Madrasa
Waislamu Dodoma wasali sala ya Ghaib kwa marehemu Kilima na mkewe Songea kujenga shule ya sekondari Wanafunzi wa Bihawana Dodoma wamshukuru Alhaj Ismail Dawood Mashindano ya kusoma Qur’an yafanyika Kondoa Waislamu wautazame upya mfumo wao wa elimu Ujenzi wa Chuo cha Kiislamu Shamsiya Bereko wakwama Kesi ya kushambulia kituo yaahirishwa tena Polisi waondolewa kimya kimya Mwembechai Msikiti wa Kiwanja cha Ndege wapania kujenga shule Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|