KAULI ya Mwenyekiti wa chama cha siasa
cha UDP Bw. John Cheyo aliyoitoa hivi karibuni kwamba anasikia harufu ya
udini (Uislamu) katika muungano wa CUF na CHADEMA imefanya mkutano wake
uhudhuriwe na watu wachache mjini hapa wiki iliyopita
Karibu asilimia 80 ya wakazi wa Tanga ni Waislamu ambapo baadhi ya wakazi hao walieleza kuwa walichukizwa na kauli ya John Cheyo.
Hata hivyo, katika kile kilichotafsiriwa kuwa ni kuwaweka sawa wananchi kuhusiana na madai ya udini dhidi yake, kabla ya Mwenyekiti huyo kuhutubia mkutano huo alitanguliwa na mzee wa Kiisalmu kuongea na wananchi.
Mzee huyo aliyetajwa kuwa ni Mshauri wa chama hicho Taifa aliyejitambulisha kwa jina la Idrisa Abdulrahman mzaliwa wa Makunduchi Zanzibar, aliwataka Waislamu wasiwe na ubaguzi wa kidini kwa Wakristo.
Alisema, Waislamu wasitake kujenga mfumo wa uongozi wa Kiislamu katika siasa jambo ambalo alieleza kuwa halitawezekana.
Kwa kadiri alivyoeleweka na wengi kwa kauli hiyo aliwataka kutochagua vyama kwa kuwa tu vina viongozi Waislamu.
Hata hivyo baadhi ya watu waliohudhuria mkutano huo walisikika wakijibu kuwa Waislamu hawana ubaguzi isipokuwa Bw. John Cheyo ndiye mwenye ubaguzi na Waislamu.
"Angemuelimisha Cheyo kwanza aliyesema anasikia harufu ya udini kwenye muungano wa CUF na CHADEMA", mkazi mmoja alisikika akisema.
Hata hivyo, viongozi hao walionekana kunywea kila walipopanda kwenye jukwaa na kusema UDP wakitizamia wananchi wajibu Upendo ambapo sauti zilizojibu zilitoka kwenye safu ya viongozi tu.
Katika tukio jingine, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi na kisha TLP mkoani hapa Bw. Peter Kimaro alitangaza kwenye mkutano huo kuwa aliamua kujitoa kwenye chama hicho na kujiunga na UDP baada ya kugundua kuwa wanaongozwa na shushushu wa Taifa.
"Mrema ni shushushu wa Taifa hawezi kuongoza upinzani. Ana kesi zaidi ya 15 lakini hajafungwa wala kutozwa faini hata kwa kesi moja. Ni CCM 'B'",alidai.
Alisema hata katika uongozi wake, Mrema haonekani kuwa na sera za kuwaeleza wananchi, jambo lililomfanya ashindwe kumuelewa na hivyo kujitoa kwenye chama hicho.
Tangu baadhi ya viongozi wa upinzani kuanza kudai
kuwa chama cha CUF ni cha udini kutokana na kuwa na viongozi Waislamu,
viongozi hao sasa wameanza kutembea na wapambe na Masheikh wa Kiislamu
ili kuonesha wao hawana udini wa Kikristo.
WAZEE mbalimbali mkoani Tanga wameisifu na kuipongeza hutuba ya Prof. Ibrahim Lipumba aliyoitoa juzi kwenye mkutano wa chama hicho uliofanyika mjini hapa.
Wazee hao wamesema, katika hotuba hiyo Prof. Lipumba ambaye ni mgombea Urais kupitia chama cha CUF, imeonesha utaalamu wake wa uchumi kwa jinsi alivyoyachambua masuala mbalimbali ya kichumi tangu nchi yetu ipate uhuru.
Wamesema, Prof. Lipumba amewafahamisha kwa kina jinsi uchumi wa Tanzania ulivyokuwa na jinsi unavyozidi kudidimia siku hadi siku kwa vile chama kilichopo madarakani kimekosa sera imara.
Hata hivyo wazee hao ambao waliongea na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti wamesema, hutuba ya Prof. Lipumba imewatia machungu hasa ilivyowakumbusha maisha yalivyokuwa enzi ya ujana wao na hivi sasa.
"Ni kweli mji wetu ulikuwa ni kitovu cha maendeleo. Watu walitoka miji mingine kufuata ajira hapa. Lakini leo mji wetu ni kama umekufa", alisema Mzee Bakari kwa masikitiko.
Aidha, wazee hao wamesema hutuba za Prof. Lipumba zimekuwa na tofauti kubwa na za wagombea Urais wa vyama vingine kwa vile zinayaeleza matatizo, sababu zake na kutoa ufumbuzi.
Kinyume chake, wamesema, hutuba za wagombea wengine zimekuwa zikikosoa tu sera za CCM bila kutoa ufumbuzi wa kitaalamu ni vipi watavyowaletea wananchi mabadiliko ya kiuchumi.
Mmoja wa wazee hao alitoa mfano wa mgombea Urais kupitia chama cha TLP, Bw. Augustine Mrema ambaye alisema katika hali inayoonesha kushindwa kueleza ubora wa sera zake na hata kuikosoa CCM aliamua kukishambulia chama cha CUF.
"Hii ni dalili ya kiongozi mpenda shari na asiye na uwezo na atakapopata Urais ataleta machafuko badala ya kujenga nchi", alisema.
Baadhi ya wazee hao wamelitaka gazeti hili kuziandika hutuba za Prof. Lipumba kikamilifu ili wananchi waweze kuzisoma kwa kina na kuzitafakari.
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |