Alhaj Zuberi Mwinshehe Manga Mtemvu - 2


Na Mohamed Said


MWAKA 1958 serikali ya kikoloni iliandaa uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria ambao viti vilikuwa vishindaniwe kwa misingi ya utaifa. Kulikuwa na viti kwa ajili ya Wazungu, Wahindi na Waafrika. Masharti mengine ya kumwezesha Mwafrika kupiga kura yalimtaka awe na kipato cha paundi mia nne za Kiingereza kwa mwaka, awe na kiwango cha elimu ya darasa la kumi na mbili na awe ameajiriwa katika kazi maalum. Haya yalikuwa masharti magumu na yaliyoonekana kama hayataweza kukubalika na TANU. TANU ilifanya mkutano wake mkuu wa mwaka wa 1958 mjini Tabora kuanzia tarehe 21-26 Januari kujadili miongoni mwa mambo mengine ikiwa ishiriki katika uchaguzi chini ya masharti haya ya kibaguzi yaliyowekwa au wasuse.

Mkutano ule ulitishia kuigawa TANU katika kambi mbili hasimu. Kambi moja ni ile ya wenye siasa za wastani waliopendelea kushiriki katika uchaguzi na ya pili ni ile ya wenye msimamo mkali waliotaka uchaguzi ususiwe kabisa. TANU ilinusurika na kile ambacho kingeweza kuwa mgogoro ndani ya chama ambao ungewafanya wale wenye msimamo mkali kama Sheikh Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU katika makao makuu na Zuberi Mtemvu kufanya mapinduzi ambayo yangekigawa chama katika makundi mawili. Akimwandikia Kathleen Stahl mmoja wa wanasiasa wa Kiingereza wa mlengo wa kushoto katika Fabian Colonial Bereau, Katibu Mwenezi wa TANU, mwaka wa 1956 Zuberi Mtemvu ambaye alikuwa amelichambua jambo hili aliandika:

"Katika nchi kama Tanganyika, utajiri na elimu vimo mikononi mwa wageni. Mwafrika ni maskini na hana elimu. Upigaji kura wenye masharti magumu yaliyoegemezwa kwenye mali na elimu utawaathiri Waafrika peke yao bila kuwagusa Wazungu na Waasia hata kidogo.

Hakuna kumbukumbu zozote zinazoeleza mawazo ya Nyerere katika suala la kura tatu wala hakuna nyaraka inayoweza kueleza kuwa alipata hata kuzungumza suala hili kwa faragha pale makao makuu na viongozi wenzake kama Sheikh Suleiman Takadir, Zuberi Mtemvu, Rajab Diwani, Idd Faiz, Haidar Mwainyimvua, Dossa Aziz au Bibi Titi Mohamed. Kwa ajili hii ni vigumu kuweza kujua ni kwa kiasi gani Nyerere alikuwa amejizatiti katika msimamo wa TANU kuingia katika kura tatu chini ya masharti yake. Lakini ikiwa utafanya tathmini kutokana na hali ya hewa ya siasa kama ilivyokuwa katika miezi ya mwisho ya mwaka 1958, si vigumu kuona kwa nini Nyerere ilibidi afiche msimamo wake katika suala la kura tatu kama TANU ilivyotwishwa na serikali. Nyerere alikuwa anafahamu hatari iliyokuwa ikinyemelea TANU kutokana na kura tatu.

Mtemvu alikuwa mpinzani wa kura tatu toka mwanzo na Nyerere aliufahamu msimamo wake. Katika maandalizi ya mkutano wa Tabora ilikuwa Mtemvu ndiye atakaeongoza hoja ya kupinga kura tatu. Lakini baadae Nyerere alimshawishi Mtemvu akabaki nyuma Dar es Salaam kuendesha makao makuu kwa kile achodai kuwa haitakuwa busara kwa viongozi wote kuondoka na kuiacha ofisi bila kiongozi wa juu ofisini. Nyerere alimshawishi Mtemvu akubaliane na ushauri wake na kuhusu hoja ya upinzani wa kura tatu, Nyerere alishauri hoja hiyo aachiwe Kissenge aiwasilishe kwenye mkutano Tabora. Nyerere alijua wazi ili kukinusuru chama na mgawanyiko kulikuwa na haja kubwa ya yeye kufanya uamuzi wa haraka na kwa makini kabla ya kwenda kwenye mkutano Tabora. Yaliyotokea katika mkutano wa Tabora sasa ni historia mashuhuri. Nyerere akishirikiana na Sheikh Rashid Sembe na viongozi wengine wa TANU kutoka Tanga kama Mwalimu Kihere waliweza kufanya mbinu zilizokuwa zikijongelea hila kiasi cha kwamba mkutano uliamua TANU iinge katika kura tatu.

Baada ya uamuzi huo siku iliyofuata wakati mkutano bado ukiendelea Mtemvu alituma simu ya maandishi kwa Rais wa TANU, Nyerere kupitia ofisi ya TANU Tabora, akitangaza kujiuzulu kwake kutoka TANU na kuanzishwa kwa chama chake cha upinzani - African National Congress (ANC). Chama cha Mtemvu kilikuja kujulikana kama 'Congress' neno ambalo kutokana na vyama vyote viwili jina hili lilikuja kunasibishwa na usaliti. Mtemvu akamshutumu Nyerere kwa kusaliti dhamana aliyokabidhiwa na TANU na wananchi, na Nyerere akimshutumu Mtemvu kwa kuacha mapambano na kujiunga na upinzani ili kudhoofisha TANU, na hivyo kusaliti harakati za kudai uhuru. Msimamo wa Mtemvu ulikuwa ' Afrika kwa Waafrika' hakuna mgeni atayekubaliwa kuitawala Tanganyika. Mtemvu alikuwa amelenga kwenye serikali ya Waafrika watupu ndani ya Tanganyika huru. Ujumbe wa Mtemvu ulipokelewa katika ofisi ya TANU mjini Tabora na mara moja tarishi alipanda baiskeli kupeleke ujumbe ule mkutanoni kule Parish Hall. Nyerere aliwasomea wajumbe wa mkutano mkuu ile simu kwa sauti. Ilikuwa habari za kushtusha. Hatua hii ya Mtemvu ilikuwa ya pekee katika historia fupi ya TANU. Hapakuwahi kutokea kiongozi wa chama kujiuzulu na kuanzisha chama cha upinzani.

Tanganyika waliikataa Congress na katika uchaguzi wa Rais wa mwaka 1963 Mtemvu alishindwa vibaya na Nyerere. Wakati Mtemvu akiwa katika juhudi za kuimarisha Congress, chama kilikuwa kimegubikwa na matatizo ya ugomvi kati ya viongozi wake. Chama kingine cha upinzani AMNUT kilikuwapo lakini Waislamu walikisusa ingawa katika kambi ya upinzani ilikuwepo tamaa kuwa huenda upinzani ukapata nguvu mpya. Kasanga Tumbo aliyekuwa Katibu wa Tanganyika Railway African Union (TRAU) ambaye Mwalimu Nyerere alikuwa amemteua balozi Uingereza, alikuwa amejiuzulu ubalozi akarudi Tanganyika na kuanzisha chama cha upinzani, Tanganyika Demoracy Party (TPD). (Wakati ule babu wa mwandishi, Salum Abdallah Popo alikuwa Mwenyekiti wa TRAU). Kulikuwa na mazungumzo ya kuunganisha TDP na AMNUT. Mtemvu ingawa alikuwa Muislamu hakulipenda wazo la kuunganisha TDP na chama cha siasa cha Waislamu AMNUT kama vile Ali Muhsin Al Barwani kiongozi wa Zanzibar Nationalist Party, Hizbu alivyokataa kuiunga mkono AMNUT.

Salum Abdallah Popo alikuwa mmoja wa wale Waislamu waliokuwa wakiipiga vita AMNUT. Hawa walikuwa viongozi walioweka maslahi ya taifa mbele kwanza kuliko hisia za dini zao. Je wenzao walikuwa na hisia kama zao za kuupiga vita udini? Historia imedhihirisha kuwa Mwalimu Nyerere alimshinda Mtemvu kwa kila hali katika medani ya siasa.

Kwa ajili hii basi siku za awali za uhuru kukawa na kundi kubwa la Waislamu waliodhulumiwa sana na ukoloni. Hawa ndio walikuwa wanatawala siasa Tanganyika na ndiyo waliokuwa kwa hakika wameiweka TANU madarakani. Waislam walikuwa na mategemeo makubwa kuona ile hali yao ya unyonge iliyodumu kipindi chote cha ukoloni ikitoweka. Kwa ajili hii hawakutaka kumuunga mkono Mtemvu na Congress, AMNUT wala chama cha Kassanga Tumbo TDP. Upinzani ulioanzishwa na Mtemvu ukawa hauna nguvu yoyote ya kuweza kupambana na TANU.

Mwezi Aprili 1961 miezi michache kabla ya uhuru wa Tanganyika Rais wa Congress, Zuberi Mtemvu akiwahutubia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Karl Marx mjini Leipzig, Ujerumani ya Mashariki, alibashiri kuwa kutolewa kwa uhuru wa Tanganyika kwa uongozi wa TANU, hautobadili chochote kwa kuwa wanaoingia madarakani wameamua kushirikiana na wale wale wanyonyaji wa zamani na hii itavunja nguvu za wazalendo na matumaini yao (Tanganyika Standard, 15 Aprili, 1961) Waislamu waliokuwa ndiyo walioanzisha na kuijenga TANU walipambana vikali dhidi ya siasa za kibaguzi za Zuberi Mtemvu na chama chake cha African National Congress hawakuweza kwa wakati ule kuelewa ubashiri wa Mtemvu. Iliwachukua miaka mingi sana kuja kuuona ukweli kwa dhahiri yake halisi.

Msimamo wa Zuberi Mtemvu katika kujadili kura tatu ungekuwa na athari kubwa katika historia ya uhuru wa Tanganyika kama wanahistoria wangekuwa wametafiti historia ya Tanganyika kwa ukweli. Labda leo Watanzania wasingepata tabu kuelewa tatizo la uzawa. Halidhalika wananchi wangeliweza kuelewa vipi hii leo karibu miongo minne ya uhuru Waislamu wanadai kubaguliwa kwa ajili ya dini yao na wanapambana na askari wenye silaha mitaa ya Dar es Salaam. Vipi wakati wa uhuru Misikiti ilikuwa ngome za harakati dhidi ya dhulma, leo Misikiti ivamiwe ati kwa madai ya kuficha 'siasa kali'. Hivi mzalendo mzee Mtemvu na waasisi wenzake wa TANU walipokuwa wanadai uhuru walikuwa na mawazo yao uhuru gani? Haiwezekani kwa mzalendo kama Mtemvu apiganie uhuru na kuingia katika upinzani na kwa hiyo kupoteza nafasi kubwa kwa yeye 'kula matunda ya uhuru' ili nchi hii iwe kama ilivyo hivi sasa. Hivi kweli wananchi wanajua hasa tatizo hili la udini linalotikisa misingi ya umoja wetu waasisi wake ni nani? Mzee Mtemvu kwa kufahamu hisia zangu kuhusu dhulma wanazofanyiwa Waislamu alipata kunieleza kuwa udini katika Tanzania Bara ni hatari ya kweli kabisa na unatishia uhai wa Tanzania kama taifa huru.

Katika miaka ya 1980 nilikuwa mara kwa mara nikimtembelea Mzee Mtemvu nyumbani kwake mtaa wa Uhuru tukifanya mazungumzo kuhusu historia ya TANU. Katika miaka ya mwisho wa uhai wake ikatokea akawa anaishi Masaki karibu na nyumbani kwangu. Nyakati za jioni alikuwa akitoa kiti nje ya nyumba yake kupunga upepo na mimi nilikuwa nafanya tabia ya kupita nyumbani kwake mara tu nikiteremka kutoka kwenye basi kuelekea nyumbani kwangu. . Tukiwa tumebarizi barazani kwake pale Masaki, Mzee Mtemvu alinisomesha mengi kuhusu juhudi za Watanganyika kuondoa dhuluma na fedheha ya kutawaliwa. Si hayo tu alinieleza masikitiko yake jinsi mambo yalivyokwenda kinyume cha mategemeo ya wale waliopigania uhuru ili paweko haki na usawa kwa wote. Mzee Mtemvu alisikitika jinsi historia ya uhuru ilivyopotoshwa kwa makusudi na wanasiasa waliokuwa madarakani. Nilimkiri Mzee Mtemvu kama baba yangu na yeye akanichukua kama mwanae. Pakawa hapana pazia baina yetu. Ninashukuru kuwa nilifahamiana na mmoja wa wazalendo wa Tanganyika ambao ingawa wanahistoria wamewapuuza lakini mchango wao hautafutika kirahisi hivyo. Tarehe 27 Aprili, 1985 Mwalimu Kambarage Nyerere, sasa marehemu, alitunuku jumla ya medali 3979 katika sherehe kubwa katika viwanja vya Ikulu si Zuberi Mtemvu wala wazalendo waasisi wa harakati za kudai uhuru walikuwa ndani ya orodha ile. Nilimfuata Mzee Mtemvu kumuuliza kulikoni? Kwa mshangao kwangu alicheka sana na kunidhihaki akisema, "mwanangu Mohammed wewe mtoto matata sana niache nipumzike".

Mwenyezi Mungu amghufirie Mzee wetu Zuberi Mwinshehe Manga Mtemvu.

--
JuuRUDI 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji


   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook