MAKALA
 
 
Hamkuwaelewa wazee wenu?
Sheikh Suleiman Takadir
 

YANAPOTOLEWA malalamiko juu ya hali ngumu ya maisha, miundo mbinu mibovu, mazingira machafu, upendeleo wa kidini na Waislamu kulalamika kuenguliwa kidini na kijamii, historia inarejea kile alichotuhumu na kupigia kelele mwanaharakati na mpigania uhuru maarufu wa nchi hii marehemu Sheikh Suleiman Takadir.

Mwandishi Maarufu bwana Mohamed Said aneleza wasifu wa Gwiji hili la siasa za Tanganyika

"Sheikh Suleiman Takadir alihofia kwamba mara watakaposhika madaraka hawa Wakristo walioelimishwa misheni wataendeleza sera zile zile za wakati wa ukoloni wakiwa wameegama kupokea amri za makadinali na mababa askofu wakiwa hawana lengo la kuiletea maendeleo nchi wala kuinua hali za Wananchi waliowengi hususan Waislamu.

Sheikh Takadir alikuwa kiongozi wa kwanza wa TANU kuonyesha hatari hii katika Tanganyika na hatimaye Tanzania huru.

Sheikh Haidar Mwinyimvua rafiki mkubwa wa Sheikh Suleiman Takadir, mjumbe wa Baraza la Wazee wa TANU na mjumbe wa Kamati Kuu ya TANU katika mwaka 1958, anakumbuka jinsi Sheikh Takadir alivyosimama ghafla na kuanza kuweka wazi tuhuma zake dhidi ya Nyerere na wenzake:

"Ilikuwa katika ofisi ya zamani ya TANU tulipokuwa tukisubiri kufanya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Ghafla tu Sheikh Takadir alisimama wima akishikilia bakora yake ya kutembelea na kumuelekezea Nyerere huku akisema, "Huyu mtu katu hatakuja kutujua ndugu zake. Usipoziba ufa utajenga ukuta." Sheikh Takadir alirudia maneno haya mara mbili. Sisi sote katika kile chumba cha mkutano tulishangazwa sana ama kwa maana ya maneno yale. Nilimwona Nyerere akilia. Nyerere alitugeukia sisi na kutuuliza, "Je, Sheikh Suleiman alisema maneno yale kwa niaba yenu ? Tulijibu kwa kwa pamoja hapana na ule mkutano ulivunjika papo hapo."

Sheikh Takadir alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo waliomjenga Nyerere mpaka akakubalika miongoni mwa Wazee wa kiislamu na alikuwa ameifanyia kampeni TANU kwa nguvu akihutubia mikutano juu ya jukwaa moja na Nyerere. Alikuwa amesaidia kufutilia mbali 'doa' la Ukristo toka kwa Nyerere ili kuwafanya watu mjini Dar es Salaam kuacha kumnasibisha Nyerere na Kanisa Katoliki. Wadhifa wa Sheikh Takadir mwenyewe kama mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU ulikuwa wa heshima kubwa.

Si kwamba wale wote waliokuwemo ndani ya chumba kile hawakuelewa alichodokeza Sheikh Takadir. Walielewa kila neno alilotamka na maana yake hasa kwa uongozi wa TANU.

Kile ambacho hawakufahamu, kutambua au kusadiki kilikuwa ule ukweli kwamba Nyerere, kijana wao mpendwa na kiongozi wao iko siku moja atageuka dhidi ya Waislamu. Wakati huo hili lilikuwa wazo lisilokuwa na maana kwao. TANU na mtangulizi wake, African Association, hazikuundwa kwa ajili ya masilahi ya kikundi fulani pamoja na ukweli kwamba Waislamu aghalabu ndio walioanzisha kuundwa kwao (vyama hivyo viwili) na kuchukua majukumu ya utendaji katika uongozi. Sheikh Takadir alikuwa amegusa jambo nyeti. Njia pekee ya kuzuia mgogoro huu mpya kuendelea mbele ilikuwa kwa Nyerere kuthibitisha kwamba wananchi Waislamu watatendewa vizuri na kwamba kutakuwa na haki sawa kwa wote baada ya uhuru kupatikana.

Kwa wakati ule, umoja wa watu ulikuwa muhimu kwa ajili ya harakati mbeleni. Hii ikajakuwa ndio hoja Nyerere katika hotuba zake tangu ule mkasa wa Takadir ulioelekea kwenye ule uchaguzi wa kura tatu uliochukiwa.

Kwa hiyo HKT-TANU (Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU) iliamua kuunda kamati moja ya upesi upesi bila ya matayarisho ili kwenda nyumbani kwa Sheikh Takadir katika Mtaa wa Msimbazi kumuuliza kwa nini alimtukana Nyerere.

Miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo walikuwa Idd Faiz, Mwenyekiti wa HKT-TANU (TANU-NEC), Idd Tulio na Jumbe Tambaza. Sheikh Takadir aliiambia kamati hiyo kwamba Nyerere alikuwa akitumia mwavuli wa lile sharti la elimu la uchaguzi wa kura tatu kuwaweka Wakristo wenzake madarakani kwa hoja kwamba wanazo zile sifa za lazima kuchukua majukumu ya serikali. Kisha Sheikh Takadir akarudia tena maneno yale yale aliyomwelezea Nyerere, neno kwa neno, akiongeza kwamba hana majuto yoyote kwa msimamo wake huo. Wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Idd Tulio walisimama na kuondoka kimya kimya.

Kwa hiyo Sheikh Takadir akafukuzwa toka TANU kwa kuanzisha suala la udini, ambalo lilidhaniwa, lingewagawa watu. Uenyekiti wa Baraza la Wazee ukapelekwa kwa Idd Tulio.

Kwa usiku mmoja tu Sheikh Takadir akageuka kuwa mtengwa wa kisiasa. Sheikh Takadir alikuwa dalali na alikuwa akifanya biashara yake hiyo pale nyumbani kwake.

Wakati mmoja pale mnadani kwake palikuwa mahala walipokutana wanachama wa TANU. Walikuwa wakikutana pale kunywa kahawa na kujadili matukio ya kisiasa ya siku zile. Baada ya kufukuzwa kwake toka TANU mahali hapo paliachwa na hakuna aliyekwenda pale.

Sheikh Takadir alipokwenda sokoni Kariakoo kununua chakula, hakuna mfanyabiashara aliyegusa fedha zake au hata kule kumtizama tu. Na aliposalimia watu hakuna aliyemwitikia. Sheikh Takadir alikuwa amefukuzwa katika jamii na TANU na alihisi hasa ule uzito kamili wa kutengwa. Biashara yake ikaanza kuanguka na vivyo hivyo siha yake. Akageuka kuwa mpweke sana na mwenye kufadhaika.

Zimepita zile siku alipokuwa akisoma "surat fat'ha" na kusoma dua kabla ya kumtambulisha Nyerere kwa watu wa Dar es Salaam katika mikutano ya awali ya TANU katika viwanja vya Mnazi Mmoja. Zimepita zile siku wakati Sheikh Takadir akiijenga vyema taswira ya Nyerere akimkweza na kumdadavua kufikia kiwango kisichosemeka.

Mara baadaye, Sheikh Takadir alifariki. Lakini kabla ya kufariki aliacha usia. Kikundi cha Waislamu kilikuwa kimekwenda nyumbani kumdhihaki, wakimtukana na kumcheka, wakipiga makelele huku wakiimba kwa sauti kubwa ule wimbo, "Takadir mtaka dini". Kikundi hiki kilimtembelea baada ya kutoka mkutanoni ambako Nyerere alitoa hotuba ya kumshambulia Sheikh Takadir.

Hapa ndipo Sheikh Takadir alipotoa ule usia ambao leo hii ndio kilio cha Waislamu dhidi ya Serikali ya Wakatoliki inayojitokeza kwa sura ya CCM. Mzee Takadiri alitoka nje ya nyumba yake na akawaambia wale Waislamu kwamba, "iko siku mtanikumbuka".

Gazeti la kila wiki la TANU Mwafrika, chini ya uhariri wa Heri Baghdelleh na Robert Makange, lilichapisha habari za Sheikh Suleiman Takadir katika ukurasa wa kwanza, likitangaza kufukuzwa kwake toka TANU kwa wino mzito, picha yake akiwa amevaa kanzu na kofia akikodoa macho pale gazetini.

Picha ya Sheikh Takadir iliwekwa pale ili wote wauone uso wa "msaliti" aliyetaka kuchelewesha mwenendo wa uhuru kwa kutaka Waislamu wapewe uthibitisho wa mustakabali wao kwa sababu ya mchango wao katika harakati za kudai uhuru."

***********

Huyo ndiye Sheikh Suleimana Takadiri. Mzee wa kiislamu aliyetekeleza wajibu wake wa kidini na jamii yake.

Huyo ndiye Sheikh Suleiman Takadiri ambaye kile alichokibashiri kilianza kujitokeza mwaka 1964. Masheikh walikamatwa kwa kuhusishwa na maasi ya jeshi. Baadaye mwaka 1968 EAMWS ikavunjwa . Mwaka 1969 ikaahidiwa rasmi kufanywa yale yaliyoazimiwa ambayo Waislamu leo hii ni mashahidi.

Sheikh Takadiri hakutaka kusubiri "vinono" vya baada ya uhuru huku akiona hatari inayowakabili Waislamu mbele. Alijua wazi kuwa kuamua vile wakati ule wa jazba za uhuru ni kujikaribishia huzuni, lakini alisimama kama sheikh na kama kiongozi wa Waislamu kuhoji nafasi ya wananchi Waislamu katika nchi yao.

Ni Masheikh wepi waliotayari kuipokea hali aliyokumbana nayo Sheikh Takadiri, wakaachana na mialiko ya vyakula vya madhalimu badala yake wakasimama kuhoji hatima ya Waislamu chini ya serikali ya CCM.

Abu Kalam 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook